Niliua kwa Kukusudia-12-
ILIPOISHIA :
Nikaelekea kwenye kituo cha kupanda mabasi hadi Ubungo ambako nilichukua gari la kwenda Chalinze. Niliwasili Chalinze saa tatu na nusu asubuhi. Nikapanda baiskeli hadi nyumbani.
Aiii, jamani dada, alisema Inana baada ya kuniona na kunikimbilia kwa furaha kubwa.
SASA ENDELEA...
Habari za huko jamani dada?
Nzuri, sijui wewe?
Salama jamani.
Za hapa nyumbani vipi?
Mm! Nipo nahangaika hivyohivyo, Mungu anasaidia sana.
Nilimlipa yule mwendesha baiskeli ya kukodisha ujira wake. Akaondoka na kutuacha na Inana.
Nilikukumbuka sana mdogo wangu.
Hata mimi dada, unaendeleaje huko Dar es Salaam?
Vizuri, ngoja nikikaa nitakusimulia yote. Kwa sasa ngoja nipumzike kidogo.
Hali niliyoikuta nyumbani ilinitia simanzi. Kijumba kibovu kilikuwa kimezidi kujiinamia. Nikamuangalia Inana. Moyo uliniuma mno. Hakika niliumia kupita kiasi.
Nikashindwa kuingia ndani kwanza, nikawa nakikagua kile kijumba chetu kwa macho.
Dada, Inana aliniita huku akinisogelea baada ya kupeleka ndani kifurushi nilichokuwa nimebeba.
Bee, niliitika huku nikijifuta machozi kwa kiganja cha mkono wa kushoto.
Kuna jambo nataka nikuambie, alisema Inana na kunifanya nimuangalie kwa umakini ili nisikie alichokusudia kunieleza.
Ha! Sasa mbona unalia tena dada?
Maisha mdogo wangu, maisha Inana.
Kwani hujafanikiwa kupata kazi ?
Siyo hivyo.
Sasa kumbe nini tena?
Hii hali Inana, inaniuma sana kuona tuko katika hali hii.
Mmh! Inana aliishia kuguna.
Hee, wewe Inana wewe.
Vipi dada.
Yaani siku hizi una simu? nilimuuliza Inana kwa taharuki kubwa baada ya kuona ameshikilia simu kwa mkono wa kushoto.
Mmh!, ina maana dada ndiyo umeiona sasa hivi?
Eee, nilikuwa sijaona kabisa umenunua simu! nilisema huku nikikaa kwenye mfuko wa foronya uliokuwa karibu na mahali tulipokuwa.
Mshangao na maswali yangu mengi, yakamfanya Inana asahau alichotaka kuniambia baada ya kuniita.
Inana alikuwa amenunua simu aina ya sumsung. Ilikuwa ni fupi yenye mwanga wa njano kila ikiwaka.
Nimebangaiza polepole kwa kujinyima dada, maisha ni magumu sana, alinieleza Inana akiwa anaishika simu yake.
Sasa inakusaidia nini kwa sasa, nilimuuliza huku nikimkazia macho ya udadisi mkubwa.
Inanisaidia kwa mambo mengi mno dada.
Kama yapi?
Kuna wakati vibarua huwa vya shida sana, ninalazimika kukaa nyumbani, lakini vikipatikana, watu mbalimbali wenye namba zangu hunipigia na kunitaarifu kuwa sasa vinapatikana, Inana alinijibu kwa kirefu na kunifanya nimuelewe.
Haya bwana, nimekuelewa.
Vipi huko mjini, maisha yanaendeleaje?
Mungu anasadia sana.
Aisee.
Unamkumbuka yule mwarabu aliyenigonga kwa gari wakati ule?
Ee dada.
Basi nilikutana naye.
Ha! Ikawaje sasa, Inana aliniuliza kwa shauku ya kutaka kujua kilichojiri.
Nikamweleza jinsi nilivyokutana na yule mwarabu.
Hadi jinsi alivyonisaidia kupata kazi hotelini kwake. Inana alishangaa sana kusikia nafanya kazi kwenye hoteli ya yule mwarabu.
Aisee Mungu ni wa ajabu sana, alijikuta akitamka maneno hayo na kunifanya nimwangalie tena usoni.
Moyoni nikajikuta nikipata hamu ya kununua simu.
Niliingia ndani na kukuta mazingira kama niliyoyaacha, japokuwa kuna baadhi ya vitu vichache ambavyo Inana alikuwa amevinunua kwa kuibangaiza na vibarua.
Niliendelea kuishi huko kijijini kwa muda wa juma moja, ndipo nikaamua kurejea tena Dar es Salaam.
Kwa hiyo mimi naondoka kesho.
Sawa dada, lakini mimi niko mpweke sana hapa nyumbani, alisema Inana na kunifanya nijisikie uchungu mkubwa sana moyoni. Maneno yake yalinichoma kwa hisia kali mno. Nikanyanyuka mahali nilipokuwa nimekaa na kumfuata Inana. Nikamkumbatia kwa upendo.
Tulibaki tumekumbatiana kwa muda, huku kila mmoja akisikiliza mapigo ya moyo ya mwenzake. Ulikuwa ni usiku wa maumivu mno kwetu. Kwa muda wa juma moja tulilokaa pamoja, tulizoeana sana.
Lakini sikuwa na jinsi zaidi ya kurejea kwenye kazi yangu.
Siku hiyo tukafanya agano kubwa na la ajabu mno maishani.
Inana, nilimuita mdogo wangu huku nikibubujikwa machozi yaliyolowanisha mgongo wake. Hali kadhalika kwa upande wake, naye alikuwa analia huku akinilowanisha kwa machozi mgongoni mwangu.
Na...aaamu dada, aliitika kwa sauti iliyojaa kwikwi na kigugumizi cha machungu na maumivu makali sana.
Acha niende, nakwenda kukuandalia mazingira ya kupata kazi, baadaye nitarejea kukuchukua ili tuwe pamoja Dar es Salaam kupambana na maisha, nilisema maneno hayo kabla ya kutulia kidogo.
Nitashukuru sana dada, alisema Inana kwa sauti ya utulivu.
Kitu kimoja nataka nikuambie.
Nakusikiliza dada.
Katika maisha yetu hatutakufa masikini, nilisema huku nikijinasua mikononi mwake na kubaki tumetazamana.
Nikamwambia ni lazima tufikie vilele mbalimbali vya mafanikio maishani mwetu. Kwa pamoja tukaapa kupambana na maisha kwa kiwango cha juu mno. Umasikini uliokuwa umetuzunguka ulitutia uchungu mkubwa.
Kwa muda wa saa moja na dakika kadhaa, tulibaki tumeshikana mikono na kupeana faraja ya matumaini.
Sawa dada, nimekuelewa lakini tutatumia njia gani kufanikiwa? Inana aliniuliza huku akinitazama kwa umakini mkubwa.
Ipo njia, nitakuambia kesho asubuhi, nilimjibu kwa ujasiri hali iliyomfanya ashituke.
Je, nini kiliendelea? Usikose kufuatilia leo jioni....