Niliua kwa Kukusudia - 19
ILIPOISHIA:
"Kwa hayo sina shida naye. Naamini hataniangusha," nikajibu na kumuangalia Inana.
Wakati tunaendelea na mazungumzo, shangazi alisema kitu ambacho kilitufanya mimi na Inana tushituke.
ENDELEA SASA…
Ndiyo. Mimi na Inana tulishituka sana hasa kutokana na ukweli kwamba hatukutegemea kusikia maneno kama hayo kutoka kwa mtu kama shangazi.
Alisema: "Maisha hayawezi kutafutwa kwa kuajiriwa na watu hasa weupe." Ni kauli ambayo hakika ilinikata maini. Nikamwangalia Inana kwa macho ya huruma, naye alionesha kuumizwa na kauli hiyo.
"Hata hivyo, siwakatishi tamaa, endeleeni kupambana, huenda mkafikia malengo na ndoto zenu," aliendelea kutuambia shangazi au mama Shufaa kama wengi walivyozoea kumuita licha ya mtoto wake huyo kufariki dunia miaka mingi iliyopita.
Tuliendelea kula japo si kwa hamu ya chakula bali kwa kushiba na kuondoa njaa.
Muda mfupi, niliamua kujitenga pembeni na kisha kunawa.
"Mbona mapema sana?" shangazi aliniuliza kwa sauti ya chini.
"Nimetosheka shangazi," nikamjibu.
Ukimya ukazidi kutawala. Si shangazi, Inana wala mimi aliyefunua mdomo kwa wakati huo. Baadaye Inana naye alishiba na kuungana nami mahali nilipokuwa nimejiegesha.
Shangazi alipomaliza kula, akaingia ndani na kulala bila hata ya kutusemesha tena, hali ambayo ilizidi kutuchanganya mimi na Inana. Lakini hata hivyo, hatukutumia muda mwingi sana kuwaza juu ya kitendo kile.
Mimi na Inana tukalala pamoja na kujifunika shuka moja huku tukitandika jingine. Tukaukaribisha usingizi kwa ukimya wa ajabu. Katika ndoto ya usiku ule, niliota kuwa mimi na mdogo wangu tunaishi maisha ambayo ni ya kifahari sana. Katika ndoto ile, tulikuwa tumepata karibu kila kitu tulichokikosa utotoni.
Kulipopambazuka, nilikuwa wa kwanza kuamka na kumkuta Inana bado akiwa anaufaidi usingizi wa asubuhi uliokuwa ukisindikizwa na sauti za ndege wa asubuhi. Hakika alionekana kukolea kwa usingizi.
Ilipotimu saa moja kamili, nilimuamsha ajiandae ili nimpeleke kazini akakutane na mdogo wake na bosi ili waelewane jinsi gani ataanza kazi.
"Inana," niliendelea kumuita lakini alionekana kuzidiwa kwa usingizi. Lakini kutokana na kumuita kwa nguvu, aliamka na kukaa kitako kwenye kigodoro huku akijifuta usoni kama ishara ya kuyaweka sawa macho kwa ajili ya kukabiliana na hali ya mwanzo wa siku mpya.
"Shikamoo dada," alinisabahi huku akijiandaa kuvaa.
"Marhaba, umeamka salama?"
"Salama kabisa sijui wewe?"
"Salama, basi jiandae nikupeleke ukaonane na huyo bosi anayehitaji mtumishi, sawa?"
"Sawa dada."
Kwa muda huo shangazi alikuwa akiendelea na shughuli yake ya kukaanga chapati kwa ajili ya umama ntilie. Nikaenda kumsalimia kisha nikaingia bafuni.
Baada ya kuoga, Inana naye akaenda kuoga na alipomaliza tulivaa na kumuaga shangazi kwa ajili ya kwenda kazini.
"Haya nawatakia mafanikio mema," alijibu shangazi huku akituangalia mmoja baada ya mwingine.
"Haya, ahsante sana, nawe kazi njema," Inana alijibu kwa uchangamfu, japo si kwa hali ya kujiamini kwa asilimia zote kutokana na maneno ambayo shangazi alikuwa ameyatoa jana yake.
Tukaongozana hadi kwenye kituo cha mabasi ya Mwananyamala ambapo tulipanda na kukaa siti za karibu sehemu ya nyuma kabisa.
Safari ya kuelekea Mwananyamala ikaanza huku Inana akionekana kushangaa kila mahali tulipopita kutokana na ugeni wake ndani ya Jiji la Dar es Salaam. Kutokana na foleni kubwa iliyokuwepo kwa siku hiyo, tulitumia muda mwingi sana njiani.
Tulitumia mwanya huo wa urefu wa foleni kujadili mambo mengi ikiwemo mustakabali wa maisha yetu. Hatimaye foleni ilipungua na magari yakaanza kwenda japo kwa mwendo wa taratibu sana.
Mara itembee mara isimame, hakika siku hiyo kulikuwa na foleni ndefu sana. Lakini sikushangazwa sana na jambo hilo, kwani ni kawaida kwa Jiji la Dar es Salaam kuwa na foleni ndefu ya magari hasa kwa siku kama hiyo ambayo ni Jumatatu.
"Kwani dada, kwa kuwa mimi nitakuwa naishi mahali nitakapoanza kufanya kazi, wewe utaendelea kuishi na shangazi hadi lini?" Inana aliniuliza huku akiwa amenikazia macho.
"Kwa nini umeniuliza hivyo Inana?" nilimuuliza kwa shauku kubwa.
"Jibu swali dada Tunu, kuna kitu nimekiona kwa shangazi, ndiyo maana nimekuuliza," alisema Inana kwa msisitizo.
Je, nini kitaendelea? Usikose kufuatilia baadae .....