Niliuwa kwa kukusudia-1

Niliuwa kwa kukusudia-1

Niliua kwa Kukusudia -9-

ILIPOISHIA :
"Unaitwa nani vile?"
"Tunu, kwani vipi?"
"Nilitaka tufahamiane, mimi naitwa
Hemed."

"Nashukuru kukufahamu," nilimjibu
huku nikianza kupiga hatua kuendelea na
safari yangu.

"Kuna jambo moja nataka nikuulize."
"Jambo gani tena?" Nikamuuliza kwa
sauti ya juu na ukali kidogo kutokana na
uchovu pamoja na mawazo niliyokuwa
nayo. ENDELEA SASA…


Ukali wangu ulimfanya yule kijana kunyamaza kidogo. Akakosa neno la kuongeza, nami nikaendelea na safari yangu.
Nikatembea hatua chache kabla ya kufika eneo la kupandia mabasi ya Ubungo ambapo baadaye nilitakiwa nikapande tena mabasi ya Buguruni.

Nilipofika kwenye kituo hicho, nikaungana na abiria wenzangu waliokuwa wakisubiri mabasi. Nikajitenga pembeni kidogo.
Muda mfupi baadaye, yalifika mabasi mawili ya kuelekea Ubungo. Nikapanda mojawapo na kuketi kiti cha nyuma kabisa ambapo niliendelea kuwa mkimya sana.
Mawazo yaliendelea kuisumbua akili yangu. Nikaendelea kumkumbuka sana mdogo wangu. Inana.

Niliendelea kuzama kwenye lindi la mawazo hadi niliposhtuliwa na sauti ya kondakta aliyekuwa akiomba nauli yake baada ya basi hilo kuwasili kituo cha Ubungo.
"Oyaa wewe sista, nipe changu bwana."
"Sawa jamani," nilimjibu yule kondakta huku nikimkabidhi nauli yake.
"Hayo ndiyo mambo," alisema yule kondakta lakini sikumjali zaidi ya kushuka na kuelekea kwenye kituo cha kusubiria mabasi ya kuelekea Buguruni.

Kutokana na wingi wa watu kituoni hapo, abiria wengi walikuwa wakigombania mabasi. Nami nikaungana nao nikiwa na mkoba wangu begani. Niliuangalia kwa uangalifu wa hali ya juu mno.
Baada ya pilikapilika ya kugombania mabasi, nilibahatika kupata basi moja na kukaa kwenye kiti ambapo niliendelea kuwa kimya huku msongo wa mawazo ukizidi kuniandama.

Nilifika nyumbani jioni sana kutokana na foleni ndefu iliyokuwepo kwa siku hiyo. Nilikuwa nimechoka kweli.
"Naona mwenzangu sasa mambo yameanza kukuendea sawa," shangazi aliniuliza baada ya kusalimiana na kujuliana hali tangu tuachane nyakati za asubuhi.
"Afadhali kidogo, Mungu ameanza kuonesha mwanga," nilimjibu lakini kwa sauti iliyoashira uchovu mno.
"Umeanza kazi?"

"Ndiyo shangazi."
Baada ya kubadilishana mawazo na shangazi, niliingia chumbani ambapo nilitandika jamvi langu la kulalia lililokuwa limechakaa kupindukia.
Sijui ni saa ngapi nilipitiwa na usingizi, nilishituka ikiwa tayari ni asubuhi.
Nilimsabahi shangazi aliyekuwa tayari anajiandaa kwa biashara zake za mama ntilie.

Haraka sana nikaingia bafuni. Nikaoga pamoja na kusukutua mswaki kabla ya kujiandaa kwa safari ya kurejea kazini ili niwahi majukumu ya usafi nitakayopangiwa kwa siku hiyo.
"Haya kwaheri shangazi."
"Haya basi, baadaye," shangazi alinijibu lakini kwa sauti iliyojaa utulivu mno.

Nikawahi hadi kituo cha mabasi ya Ubungo. Nikawasili na kuunganisha hadi Mwananyamala, eneo langu jipya la kazi.
Niliendelea na kazi za usafi hotelini hapo kwa siku kadhaa bila kuona dalili yoyote ya kubadilishiwa nafasi nyingine ya kazi. Hata hivyo sikukata tamaa hata kidogo. Nikaendelea kujipa matumaini huku Mungu akiendelea kuwa nguzo na tegemeo langu kuu.
Kawaida wafanyakazi wote wa hotelini hapo walikuwa na desturi ya kubadilishana siku ya kupumzika kwa siku nne mfululizo baada ya kuingia kazini kwa muda wa majuma mawili mfululizo.

Siku moja nilipokuwa naingia kazini asubuhi, nilimkuta yule Mwarabu amesimama pembeni mwa lango kuu la kuingilia hotelini hapo.
Tofauti na siku nyingine nilizokuwa nimemzoea kwa ukarimu wake, siku hiyo hakuwa mwenye furaha kabisa. Wajihi wake ulionekana kugubikwa kwa mawazo tele.
"Salama, za kwako," aliniitikia kwa sauti ya chini baada ya kumsabahi.

Nilipompita nikiwa naelekea eneo la kubadilishia nguo kabla ya kuanza kazi, nilisikia akiniita.
"Naamu," niliitikia kwa uoga kidogo.
"Njoo. Unaendeleaje na kazi," aliniuliza akiwa amenikazia sana macho.
"Vizuri tu bosi," nilimjibu kwa utulivu.
"Mbona kama…"
"Hebu njoo ofisini kwangu," aliniambia huku akipiga hatua kuelekea ofisini ambapo nami nilimfuata.


Je, nini kitafuata? Fuatilia Kesho Usiku.
 
Niliua kwa Kukusudia -10-

ILIPOISHIA

Nilipompita nikiwa naelekea eneo la kubadilishia nguo kabla ya kuanza kazi, nilisikia akiniita.
"Naam," niliitikia kwa uoga kidogo.
"Njoo. Unaendeleaje na kazi?"

Aliniuliza akiwa amenikazia sana
macho.
"Vizuri tu bosi," nilimjibu kwa utulivu.
"Mbona kama…"
"Hebu njoo ofisini kwangu," aliniambia huku akipiga hatua kuelekea ofisini ambapo nami nilimfuata.
SASA ENDELEA…


Baada ya kufika ofisini, alivua koti lake na kulitundika juu ya kiti chake kirefu kilichokuwa nyuma ya meza nzuri ya kifahari sana.
Akashika mkebe uliokuwa na sigara mezani hapo. Akachomoa moja na kuiwasha kabla ya kuanza kuivuta.
Moshi ulitapakaa chumba kizima cha ofisi hiyo. Ulipita ukimya kwa muda.

"Nimekuita asubuhi hii kwa lengo la kuzungumza na wewe," yule Mwarabu alifungua uwanja wa mazungumzo huku akiinua uso na kupumua moshi mwingi wa sigara kupitia matundu ya pua na mdomoni.
Alikohoa kabla ya kuendelea.
"Nilikuuliza unaendeleaje na kazi," alirudia swali lake la awali huku akimalizia kukaa.

"Naendelea vizuri bosi," nilimjibu na kumwangalia usoni ambapo tulikutanisha macho kwani naye alikuwa amenikazia ya kwake.
Akatulia na kuendeleza mazungumzo yake.
"Nimeambiwa na meneja kuwa unaendelea vizuri sana, lakini mara nyingi sana unaonekana mkimya na mnyonge kuliko kawaida, una tatizo gani kwani," aliniuliza kwa kuonesha hali na wajihi wa ukarimu sana.

"Niko sawa," nikajibu japo ukweli ni kwamba muda wote nilionekana kuwa mwenye msongo wa mawazo kutokana na magumu tunayoyapitia mimi na mdogo wangu Inana.
"Sikiliza."
"Ndiyo bosi."
"Hapa tuna utaratibu wa watu kupata muda wa kupumzisha akili baada ya kuhudhuria kazi kwa wiki mbili mfululizo."
Alipofika hapo akatulia tena.

"Miongoni mwa wafanyakazi tuliowateua kuwapa mapumziko ya muda wa wiki mbili ni pamoja na wewe," alisema kisha kufungua droo ambapo alichomoa bahasha fulani yenye rangi ya kaki.
Akanikabidhi bahasha hiyo na kuniambia ndani mlikuwa na kiasi fulani cha pesa ambacho kingenisaidia kwa kipindi chote cha likizo kabla ya kurudi kazini ambapo mshahara ungekuwa tayari.

Tulizungumza mengi sana ofisni kwake, lakini akanitakia mapumziko mema na kuniambia kuwa naweza kurudi nyumbani kuanzia wakati ule.
"Ahsante sana bosi," nilimjibu na kuinuka.
Nilipofika nje, nilikutana na meneja. Nikamueleza yote tuliyozungumza na bosi ambapo aliridhia vyema na kuniruhusu.

Nilipanda basi nikiwa mwenye furaha kubwa sana. Nikawa nawaza jambo moja tu, kwenda kumjulia hali mdogo wangu Inana kule kijijini.
Japo sikujua ni kiasi gani hasa kilikuwa ndani ya bahasha hiyo, moyoni nilijipa matumaini makubwa kuwa nitaweza kujikimu vyema.

"Sijui Inana atakuwa anaendeleaje na vibarua vyake kwa sasa," nilijikuta nikiwaza nikiwa nimekaa kwenye siti ya basi kuelekea Ubungo kabla ya kuunganisha hadi Buguruni yaliko makazi yangu.
"Hee, kulikoni tena mapema hii yote kurudi nyumbani mwanangu," shangazi aliniuliza kwa shauku baada ya kuwasili nyumbani nikiwa sina raha kabisa.

"Hapana shangazi, nimepewa mapumziko kwa muda wa wiki mbili ambapo ni utaratibu wa hoteli ile kwa watumishi wake."
"Haya, sasa unawaza nini?" Shangazi aliniuliza akiwa amejishika kiunoni.
"Kwa sasa nawaza kwenda kumjulia hali mdogo wangu huko kijijini, nikajue ana hali gani na anaendelea vipi na mihangaiko yake," nikamjibu kwa sauti iliyoashiria uchungu mwingi kwa ndani.

Roho ilikuwa ikiniuma sana siku hiyo. Kichwani niliitabiri vyema hali ya mihangaiko anayokabiliana nayo Inana kwa kuhangaikia vibarua ili kujikimu na maisha magumu.
Nikiwa naendelea kuwaza na kuwazua, ghafla mawazo yalinirejesha kipindi kirefu cha nyuma. Nikakumbuka jinsi tulivyoishi maisha ya furaha na wazazi wetu. Machozi yakaanza kunilengalenga. Niliumia mno moyoni.

Nikazidi kuwaza jinsi tulivyositisha masomo baada ya kufiwa na wazazi wetu, nikafikiri namna nilivyokuwa na ndoto za maisha mazuri baada ya kumaliza masomo. Machozi yakazidi kunibubujika kwa wingi.
"Wewe mbona unalia tena?" Shangazi aliniuliza baada ya kunitazama kwa umakini.
"Hapana shangazi."

"Hapana wakati naona machozi yakikumwagika?"
"Kichwa kinaniuma shangazi," nilimdanganya japo ukweli ni kwamba siku hiyo mawazo juu ya maisha yetu na mdogo wangu yaliutesa sana ubongo wangu.
"Umeshameza dawa?"
"Ndiyo shangazi."

"Basi kalale ili upate wasaa wa kupumzika."
"Sawa," nikamjibu na kunyanyuka kuelekea ndani.
Nilipofika ndani, jambo la kwanza kulifanya ilikuwa ni kufungua ile bahasha nikiwa na hamu kubwa sana ya kujua ni kiasi gani cha pesa kilikuwemo.
"Mungu wangu!" nilijikuta nikitamka kwa sauti baada ya kufunua ile bahasha na kuona kilichokuwemo.


Je, nini kitaendelea? Usikose kufuatilia Usiku wa leo......
 
Niliua kwa Kukusudia-11-

ILIPOISHIA KWENYE GAZETI LA IJUMAA WIKIENDA:
Nilipofika ndani, jambo la kwanza kulifanya ilikuwa ni kufungua ile bahasha nikiwa na hamu kubwa sana ya kujua ni kiasi gani cha pesa kilichokuwemo.
"Mungu wangu!," nilijikuta nikitamka kwa sauti baada ya kufunua ile bahasha na kuona kilichokuwemo ndani yake.
SASA ENDELEA…


Noti nyekundu zilikuwa zimejipanga kwa wingi. Haraka sana nikazichomoa na kuanza kuzihesabu.
"Nne, tano, siiita," nilitamka kwa sauti nikimalizia kuihesabu noti ya mwisho na kugundua kuwa zilikuwa ni shilingi elfu sitini. Nilipiga magoti chini na kuanza kumshukuru Mungu kwa riziki aliyokuwa amenijalia kwa siku hiyo.

"Ahsante muumba wa mbingu nchi, jina lako lihimidiwe baba," nilitamka maneno hayo huku machozi yakinitiririka kwa wingi. Ilikuwa ni kama muujiza kupata kiasi kikubwa namna hiyo cha pesa.
Nikajizoazoa na kujilaza kwenye kigodoro changu. Kichwani nilijawa na mawazo tele. Kutokana na wingi wa mawazo, nilipitiwa na usingizi hadi saa nane mchana nilipoamshwa na shangazi kwa ajili ya chakula.

"Unaendeleaje na hali kwa sasa?" Shangazi aliniuliza huku akinisogelea.
"Najisikia nafuu ila mwili hauna nguvu tu."
"Kula upate nguvu, halafu umeze dawa zako, sawa eeh."
"Sawa."

Nilienda kunawa na kujumuika mkekani na shangazi kwa ajili ya kupata chakula.
Wakati wa kula, nilitumia mwanya huo kumjuza shangazi juu ya mipango yangu ya safari ya kwenda kumjulia hali mdogo wangu Inana kule kijijini.
"Ulisema umepanga kwenda lini?"
"Kesho asubuhi."

"Utarudi lini?"
"Nitakaa kwa juma moja."
"Sawa, sina kipingamizi juu ya hilo mwanangu," shangazi aliniambia huku akiniangalia kwa macho ya huruma.
Baada ya mazungumzo hayo, sikuendelea kula. Nikanawa na kurudi ndani ambako nilijiandaa kwenda kuoga.

Nilimaliza kuoga na kubadili nguo. Nikaanza kupanga baadhi ya nguo zangu ndani ya furushi ikiwa ni maandalazi ya safari.
Niliendelea kujipumzisha hadi saa kumi ambapo shangazi aliniagiza sokoni kwenda kumnunulia mchele na baadhi ya vitu vingine vya kwenye mgahawa wake wa mama ntilie.

Nikiwa sokoni, nilimnunulia mdogo wangu nguo kadhaa zikiwemo za ndani. Nikafanya na manunuzi madogomadogo kama dawa ya meno, sabuni, mafuta ya kupaka na vitu mbalimbali vya kawaida.
Nilirejea nyumbani nikiwa mchovu sana. Nilimkabidhi shangazi vitu vyake kisha nikaingia ndani. Baadaye nilitoka na kujiegesha kwenye ukuta wa kijumba chetu kibovu. Mawazo juu ya maisha yetu na hatma yetu yaliendelea kunisumbua sana akilini mwangu. Nikiwa nawaza, sauti ya mama yangu iliyojaa upendo ilinijia akilini. Nikajikuta nikiingiwa na uchungu mkubwa mno moyoni.

Machozi yakaendelea kutuama kwenye mboni. Macho yangu yakadhoofu kwa machozi. Ulikuwa ni uchungu wa hali ya juu.
Niliendelea kukaa ukutani hapo hadi ilipojiri saa moja na nusu nilipoingia ndani. Nilala mapema huku nikiendelea kuwaza mambo mengi sana juu ya maisha. Niliendelea kumuomba Mungu atende miujiza yake.
Asubuhi nilidamka mapema na kumkuta shangazi akiwa anaendelea na shughuli zake. Nikamjulia hali.
"Mbona umeamka mapema sana."

"Nataka nijiandae kwa safari shangazi."
"Mapema yote hii jamani!"
"Ningependa nifike mapema."
Niliingia ndani na kutoka na kifurushi changu.
"Haya shangazi, ngoja nijikongoje," nilimuaga huku nikiwa nimepiga magoti kwa ishara ya heshima.
"Sawa mwanangu, nakutakia safari njema."
"Ahsante sana shangazi."

"Bahati mbaya hali yangu siyo nzuri ningekupa walau chochote kwa ajili ya Inana," alisema shangazi akiwa ameshika tama kwa masikitiko.
"Usijali shangazi," nikamtia matumaini.

Nikaelekea kwenye kituo cha kupanda mabasi hadi Ubungo ambako nilichukua gari la kwenda Chalinze. Niliwasili Chalinze saa tatu na nusu asubuhi. Nikapanda baiskeli hadi nyumbani.
"Iiiii, jamani dada," Inana alisema baada ya kuniona na kunikimbilia kwa furaha kubwa.


Nini kiliendelea? Usikose baadae...............




 
Jamani mpk kesho tena? Iongeze kidogo leo
itabidi ungojee mpaka kesho ndio upate kuisoma hadithi yangu.

Tunaomba uirefushe kidogo maana unatukatili
Acha ubahili wako hunipi (Like) Mpaka niombe?

MziziMkavu hizi episodes fupi sana mkuu
Mnalalamika Story fupi basi hata kunipa (Like) Mnashindwa? ahhhh acha uchoyo wako sio mtu mzuri.

Kifupi sana mh.
Mnalalamika Story fupi basi hata kunipa (Like) Mnashindwa? ahhhh wachoyo nyinyi sio watu wazuri.
 
itabidi ungojee mpaka kesho ndio upate kuisoma hadithi yangu.

Acha ubahili wako hunipi (Like) Mpaka niombe?

Mnalalamika Story fupi basi hata kunipa (Like) Mnashindwa? ahhhh acha uchoyo wako sio mtu mzuri.

Mnalalamika Story fupi basi hata kunipa (Like) Mnashindwa? ahhhh wachoyo nyinyi sio watu wazuri.

heshima yako mzizi mkavu
 
Back
Top Bottom