Niliua kwa Kukusudia--26-
ILIPOISHIA IJUMAA:
WAKATI dokta akijiandaa kunijibu, ghafla mlango ulifunguliwa na kutokea mtu ambaye wote tulibaki tunamwangalia kwa mshangao.
SASA ENDELEA
Alikuwa mwanamke ambaye kwa kumwangalia mara moja, ni lazima ukubaliane na akili yako kuwa hakuwa na akili timamu. Alikuwa amevalia matambara yaliyochanika na kuchakaa sana. Hakika alionesha kila dalili ya kuwa mlemavu wa akili.
Katika hali ya kushangaza, alikuja moja kwa moja hadi kitandani nilipokuwa nimelazwa. Alimsabahi kwanza dokta kisha kunigeukia na kunikazia macho huku akishindwa kusema neno.
Habari za kwako, unaendeleaje? Hatimaye alivunja ukimya kwa salamu hiyo.
Salama, nashukuru Mungu kwa kweli, nilimjibu lakini sikuacha kumshangaa kutokana na hali aliyokuwa nayo. Mimi na yule daktari tulisitisha mazungumzo kwa muda na kusubiri kuona nini alikusudia kufanya yule mwanamke.
Pole sana kwa yaliyokukuta jana, ulikuwa na hali mbaya mno, alisema yule mwanamke na kupiga magoti kitandani kwangu huku machozi yakianza kumlengalenga. Nilibaki nikimshangaa kwani sikuwahi kuonana naye hata siku moja na nikawa najiuliza maswali mengi lakini kubwa ni alinijuaje na nani alimwambia kuwa nilikuwa na hali mbaya siku iliyopita!
Nilishapoa, lakini wewe ni nani maana sina uhakika kama tunafahamiana? nikamjibu na kumtupia swali ambalo niliamini jibu lake lingenitoa gizani kujua yule mwanamke alikuwa nani hasa na alinijuaje.
Hata hivyo, moyo ulinienda mbio sana kwani sikutaka mtu yeyote tofauti na madaktari ajue kuwa nilikuwa nimeingiliwa na mwanaume bila idhini yangu. Binafsi niliamini kitendo cha kubakwa ni udhalilishaji mbaya kuliko wowote katika maisha ya mwanamke.
Mimi ni msamaria mwema niliyekuokota jana mtaroni usiku wa manane ukiwa hujitambui na damu nyingi zikikububujika kama maji ya bomba. Ulikuwa umepoteza fahamu, alisema yule mwanamke.
Uchungu nilioupata kutokana na maelezo yake ulikuwa wa kiwango cha juu mno. Hasira na chuki dhidi ya yule Mwarabu vilinijaa.
Kumbe alinibaka na kunitupa mtaroni? nilijikuta nikitamka maneno hayo kwa sauti ya juu bila kujali uwepo wa wagonjwa wengine waliokuwemo mle wodini.
Mwanamke ambaye awali nilikuwa nikimhesabu kama mwendawazimu sasa aligeuka shujaa kwangu. Ndiye aliyeniokoa na hali mbaya niliyokuwa nayo baada ya kubakwa na bosi Elhakimu, mtu ambaye nilimuamini na kumheshimu kama mwajiri wangu.
Kumbukumbu mbaya ya jinsi nilivyobakwa ikaanza kujirudia upya akilini mwangu. Kufikia hapo, moyo wangu ukatengeneza chuki isiyosimulika dhidi ya wanaume wote duniani hasa yule Mwarabu aliyejivika ngozi ya kondoo ilihali ni mbwamwitu. Sikumtofautisha na wanyama wa mwituni.
Pole sana, mimi huwa nalala kwenye mtaro huo kwa kuwa sina makazi maalum, ugumu wa maisha ndiyo ulionifikisha hapo, ufukara huu huwafanya watu wengi wadhani mimi ni mwehu, jambo ambalo si kweli, akaendelea kusema yule mwanamke.
Kuna gari la kifahari lilisimama mtaroni hapo, akashuka mwanaume wa Kiarabu na kuanza kuangaza huku na kule, muda mfupi baadaye akafungua mlango wa gari na kutoa mzigo.
Awali nilidhani ni mzigo kumbe ulikuwa wewe, akakutupa mtaroni na kuingia kwenye gari lake haraka sana na kuondoka kwa kasi ya ajabu.
Nilipokusogelea, ulikuwa hujitambui na damu zilikuwa zikikuvuja kwa wingi, nikaita watu na kwa pamoja tukakuleta hapa hospitalini, alisimulia yule mwanamke huku uso wake ukiwa umechakazwa na machozi ya huruma.
Pamoja na maadili ya taaluma yake, kukutana na matatizo mbalimbali na makubwa ya wagonjwa wengi, yule daktari ambaye kwa jina alikuwa amejitambulisha kama Dokta Masalu alishindwa kuyazuia machozi wakati yule mwanamke alipokuwa akisimulia jinsi alivyoniokota.
Ilionesha kuwa yeye hakuwepo wakati nafikishwa pale hospitalini. Nilimuona akionesha hisia za machungu na maumivu makali.
Basi ngoja nikuchome sindano kwanza, nikupe dawa fulani ndipo tuendelee na tiba nyingine, alisema Dokta Masalu na kumtaka yule mwanamke atupe muda kwani hata hivyo, muda wa kuangalia wagonjwa ulikuwa umepita kwa asubuhi ile.
Yule mwanamke aliondoka na kuahidi kurudi mchana kunijulia hali. Wakati anaondoka, macho yangu yaliganda kwake na kumuona kama shujaa wa kipekee maishani mwangu kwa wakati huo.
Bila huyu mwanamke ningefia mtaroni mimi, nilijikuta nikitamka maneno hayo huku machozi yakinitoka na kulowanisha mashuka.
Kuna jambo nitakueleza nikirudi, ila inabidi uwe na kifua, alisema yule mwanamke na kufungua mlango huku akiubamiza kwa nguvu.
Je, ni jambo gani? Usikose kufuatilia leo jioni....