SoC01 "Ni kheri kufa kuliko kuishi": Sauti ya msomi wa Tanzania

Stories of Change - 2021 Competition

BENARD SEMEN

Member
Jun 1, 2018
5
5

''NI KHERI KUFA KULIKO KUISHI‘’ SAUTI YA MSOMI WA TANZANIA

Anaanza kwa kusema,

.....Sitaisahau pindi nipo kidato cha pili, ni ngumu kuisahau siku ya jumatatu ya tarehe 6 ule mwezi wa pili mwaka 2006,ikiwa ni majira ya saa tatu asubuhi nilikua darasani najisomea, ghafla Mwalimu Mkuu aliingia akanipungia mkono ishara ya kuniita, nikamfuata kinyume nyume mpaka ofisini kwake, nafika akachukua fimbo huku ananifokea kwa hasira akisema,

“Unafikiri shule hii ni ya shemeji yako, tukikwambia leta michango huleti, leta Wazazi huleti, leo upo kidato cha pili hujalipa hata mia, pumbavu leo utanikoma”

Alinishika na akaanza kunipiga fimbo, bila huruma nilipigwa popote iwe kichani tumboni, nagaragara, nakanyagwa, nalia nafurukuta ananipiga tu. Lakini nilipopata upenyo, nilitoka “sipidi” kama risasi. Nilikimbia toka shuleni mpaka nyumbani, huku damu imenitapakaa, nafika namkuta mama, ananishangaa na kuniuliza,

“Mwanangu umekutwa na nini?” huku nalia nikamjibu,

“Sababu ni wewe” kwa wasiwasi akaniuliza,

“Mwanangu shida nini jamani? nikijifuta damu usoni nikimjibu,

“Mama ni kheri nife kuliko kuendelea kuishi, kila siku ni kipigo, shule kwangu imegeuka gereza, ona natolewa ngeo kisa ada, napambana sana lakini majukumu yamenizidia huku nalea familia huku najisomesha. Mama kwani baba yuko wapi nimwambie walau anisaidie” huku nalia akanijibu,

“Mwanangu we acha tu!”

“Nambie mama nateseka sana mwanao” chozi linamchuruzika akanambia,

“Samahani sana mwanangu, nimekaa nawe muda mrefu huku nimekuficha mengi, sikutaka kukuambia ili usiumie, lakini leo naomba nikuweke wazi. Kiukweli toka utotoni mwako hujamuona baba yako pia tunaishi maisha ya kubangaiza kama njiwa. Kama unavyofahamu, nimezaliwa Zanzibar, baba yako alinitorosha nyumbani mwaka 1985, nikiwa binti wa miaka kumi na miwili, tukaja hapa Kagera tuliaanza kuishi kama mume na mke. Kusema kweli tuliishi maisha mazuri. Baada ya miaka mitatu nilipata ujauzito. Ilikuwa wakati wa masika nikawa nimekaribia kujifungua, wakati ule siwezi kufanya kazi yoyote zaidi ya mazoezi, hali ya maisha nayo ilikuwa ngumu sana kipindi kile hatukuwa na chochote. Mume wangu alifanya vibarua ndipo tunapata kula, lakini hali ilizidi kuwa ngumu, mwishoe tukawa tunalala njaa, maisha yakazidi kuwa magumu. Hadi kuna siku tulipitisha siku mbili hatujala chochote. Nakumbuka ilikuwa siku ya kuamkia Alhamis mume wangu aliamka mida ya saa kumi na moja alfajiri akaniaga aende kutafuta, nilikaa kumsubiri kwa hamu arejee, ilipofika jioni nikainjika chungu ili pindi afikapo nisonge ugali. Wakati maji yanachemka, taratibu usingizi ukanipitia, nilikuja kuzinduka saa tisa usiku za usiku, nipo jikoni moto umezima na maji yamepoa kama barafu na pia mume hajarudi. Nilisubiri kesho yake hakutokea, ilikuwa siku, zikawa siku, ikawa miezi na hatimae miaka sijawahi mtia machoni na sijui yuko wapi. Ilinibidi kuvaa majukumu ya ubaba ilihali ni mudhoofu. Nilianza kufanya vibarua ili mkono uende kinywani. Wiki moja baada ya mume wangu kuondoka ilikuwa siku ya jumanne tarehe 06 mwezi wa 12 mwaka 1988 ikiwa ni usiku wa manane niko peke yangu, uchungu ukanishika. Mbaya zaidi sikuwa hata na senti, sina mafuta ya taa na giza nalo limetanda, nilijivuta kutoka nje walau niwaite majirani ili wanisaidie. Nilipotoa mguu wa kwanza, wa pili, nguvu zikaniishia, pale pale nikalala na uchungu ukanizidia. Kwa bahati nzuri nikajifungua, ndio wewe ukaja duniani” akilililia akazidi kunieleza,

“Mwanangu katika mazingira magumu nilipambana nikakulea na mwaka 1998 nikakupeleka shule ili usome baadae uje kukomboa maisha yangu na wadogo zako. Mwanagu sipendi uwe ulivyo ila sina namna, zaidi nakuomba ujikaze, vumilia, soma ili kesho uje kuiangaza nuru, soma mwanangu usiache shule”

Nilijikuta natokwa na machozi na kwa dhati nikaapa,

“Mama pole sana, nakwahidi kuwa nawe bega kwa bega na kamwe sitoacha shule bali nitasoma ili siku moja nikuvike taji”

Kesho yake nikarudi shuleni, Mwalimu akawa ananipiga kila siku lakini nilijikaza hadi fimbo nikazoea. Ya Mungu mengi, ilipofika mwaka 2008 nikaandika historia kwa kwa kuhitimu kidato cha nne bila kulipa hata mia. Huwezi amini matokeo yalitoka nimefaulu na tena nimepata daraja la kwanza yaani “Division one” ya point 12, mama alifurahi sana na kuniahidi kunipigania mpaka mwisho.

Safari ya Advance ikaanza, mama alijitoa mhanga ili mwanae nisome, aliuza nyumba na kiwanja tukahamua kwenye Chama (yaani jumba la mabati la Chama cha Ushirika lililojengwa enzi za Ujamaa) na akaanza kuuza gongo (pombe ya kienyeji) ili kupata hela ya chakula na kunipatia walau matumizi. Niliishika kalamu huku moyo ukichuruzikwa na damu, mwaka mbili na tisa ukaptia, mbili na kumi ukapita, ule wa mbili kumi na moja historia nyingine nikaiandika kwa kuhitimu kidato cha sita.

Baada ya shule, nikawa namsaidia mama kupika na kuuza gongo huku nikisubiri matokeo. Wakati huo nakumbuka tukio moja, sitolisahau aslani. Siku moja tulikuwa tunapika gongo, ghafla iliotokea difenda ya Polisi tulishikwa na kurushiwa nyuma ya gari kama magunia, kisha gari likaondolewa kwa fujo kuelekea kituo cha Polisi, mama wasiwasi ulimjaa, akawa anafikiri namna ya kujiokoa, huwezi amini gari ikiwa sipidi mama aliruka chini. Masikini alianguka vibaya pale pale akuvunjika miguu na kupata jeraha kubwa mdomoni. Hali hiyo ilinihuzunisha sana lakini hakuwepo hata wa kunifuta machozi. Sikuwa na namna nililibeba jukumu la kuilea familia, nilifanya kila kazi ili familia ile na mama apate walau kupona, huzuni ikanitamalaki. Ijapokuwa nilikuwa kwenye dimbwi la matatizo ghafla nilijikuta najawa na furaha, baada ya matokeo ya kidato cha sita kutoka nimefaulu vizuri, nimepata Division I ya point 4, mwaka huo huo 2011, nikachaguliwa kujiunga na chuo kikuu na nikapewa mkopo 100%, familia ikafurahi kwa kuiona nuru, hakika Mungu huwa hamtupi mja wake.

Nilipoanza chuo kikuu starehe na anasa niliziweka pembeni, muda wangu niliutumia kujisoma na hela ya mkopo maarufu “bumu” ndio ilinisaidia kuilea familia yangu. Maajabu yakatokea tena ule mwaka wa 2014, nikahitimu shahada ya awali na kuibuka kidedea kwa kupata daraja la kwanza yaani G.P.A ya 4.5 “First Class Honours” nilipiga goti kumshukuru Muumba kwani nilijua dhahiri funguo nimeipata.

Baada ya kumaliza chuo, wakati huo sina “bumu”, sina baba, mama nae mlemavu na wadogo zangu wananitegemea. Nilianza kupambana, chochote nikipata nagawana na familia, niliungojea sana mwaka 2015 niliuamini utanipa ajira, lakini ukapita kama upepo. 2016 ukapita na 2017 hivyo hivyo, 2018 nao yaleyale, matumaini yakapotea, mambo yakanielemea, nikaamua kubeba vyeti vyangu na kuzunguka maofisini.

Siku moja asubuhi nikafika ofisi moja,nilikutana na Secretary nikamwambia,

“Nina shida kuonana na Meneja” akaniuliza,

“Una appointment?”

“Hapana”

“Bila appoitment huwezi kuonana nae” huku yuko bize na kompyuta hanitazami hata usoni, nilijiondokea na kwenda ofisi ya pili, bahati nzuri nikaruhusiwa kumuona Meneja nikamweleza adhma yangu, akaniuliza kwa ukali,

“Nani alikwambia ajira zinapatikana ofisini?”

“Sijaambiwa na mtu”

“Ajira zinatangazwa kwenye website na siyo ofisini, umenielewa”

“Ndio” akanambia

“Haya wasalimie” Nilitoka moyo umesonona ila sikukata tamaa, nikaenda kwenye ofisi nyingine, nikafika nikaulizwa,

“Una uzoefu wa miaka mingapi?”

“Mimi ni fresh from school”

“Tunataka watu wenye uzoefu angalau miaka mitatu” napo nikakosa, mwaka 2019 ulipita “nahaso” bila mafanikio, 2020 nayo ikapita, 2021 nikaianza lakini hali yangu ilizidi kuwa mbaya, nikafika mahara sina hata uwezo wa kumtumia vijisenti mama, pia hela ya pango sina mwishoni baba mwenye nyumba akanichoka akaniambia,

“Kijana umekuwa mswahili sana, ni mwaka na nusu unanipiga danadana, nimekuvumilia sana lakini nimechoka na ahadi zako, hivyo kama kesho hutanipa hela, tutaongea mengine” kisha akatoka zake,

Kesho yake kama kawaida, nikaamka mapema kwenda kusaka riziki, lakini nilishangaa jua linazama sijapata hata mia, nikurudi. Kesho yake tena nikaamuka saa kumi nikatoka kwa kunyata ili mwenye nyumba asinione, nikaenda kupamaba, nilichokipata ni kheri ya jana. Hivyo hivyo nikarudi “getoni” kufika nakuta mlango umefungwa kwa kufuri, kutazama pembeni naona vitu vyangu vyote vimetupwa, nilihisi kuchanganyikiwa nikawa najisemesha,

“Sina ndugu sina msaada nyumbani ndio nategemewa, mfukoni doro, nina siku mbili sijala hata sehemu ya kulala nimekosa?” nilijikuta natokwa na machozi bila kupigwa, nikabeba virago vyangu nikaanza kuondoka bila kujua niendako.

Nikashika kitochi changu nikampigia Mheshimiwa Mbunge wangu kumwambia walau anitafutie hata kazi ya kufagia, kwa mkato akanijibu,

“Kijana kazi hakuna, cha msingi jiajiri” kisha akakata simu, niliishiwa pozi, kutazama saa yangu inasema ni saa saba za usiku nipo barabarani na sijui nalala wapi, nilitembea hatua kidogo nikafika Ubungo flyover, nikakaa chini kutafakari, nilikaa kidogo ghafla nikaweka begi la vyeti vyangu kichwani nikajilaza, taratibu usingizi ulinishika nililala pale pale. Ghafla nikashutushwa na mwito wa simu yangu, kufumbua macho ni saa moja asubuhi, kuitazama simu naona namba ngeni inanipigia, nikapokea, sauti ya mama nikaisikia, tena akiongea kwa shida,

“Hello! haujambo mwanangu? nimeazima simu nikutaarifu kuwa mimi ni mgonjwa sana yapata wiki moja siwezi hata kuinua kichwa, vilevile wadogo zako hawaendi shule hawana ada na sare, mbaya zaidi tuna siku tatu hatujaweka kitu tumboni, ndani hakuna chochote. Mwanangu! najua mimi ni wa kufa kwani hata mia ya panado sina na hali yangu si shwari. Zaidi nakuomba uje nyumbani uwalee wadogo zako, kwa kheri mwanangu’ kisha mama akakata simu, chozi lanidondoka najuta kuzaliwa naona “NI KHERI KUFA KULIKO KUISHI''.

Ni mimi Msomi wa chuo Kikuu, nipo Jijini natafuta nauli niende nyumbani nikalione KABURI LA MAMA na nikawalee wadogo zangu.

Assalam Alaikum.
 
Hayo ni ya kawaida Baba!! mie baada ya chuo! wkt natafuta kazi, tena bila kula chochote!! alikuja ndg wa Ukoo na Mkewe wakanibomolea mlango wangu wa chumba nacho lala na kuapasua pasua kila kitu pale chumbani kwangu ..wkt huo sina hata hela nyeupe!!

Nikaenda polisi! wakakimbia wakapotea km week! mbili hivi! Nikauliza kwa nini wamefanya hivi??? waka sema eti mie natembea na Mume wa Binamu yangu!! ndo maana wamenikomesha ivo!! halafu nina jidai eti Nina hela!! na kunisema eti wao ni ndg wa mbali na mimi! eti mie nasema kwa watu ivo!

Basi baada ya kuwatafuta sana na polisi bila mafanikio nikaamua kupiga kimyaa!!..........na watu waka nishauri kwa hili jifanye mjinga.... mpaka leo,..... na wao pia wakapiga kimyaa mpaka leo yapata miaka kumi sasa!!.... ila ndoa ilisambaratika na mke kawa km kichaa! wamefilisika ni hakuna mfano! walevi mbwa wana lala nje!...hawakuomba msamaha wala kuja kuniona kwa hali yeyote ile!
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom