SoC03 Ngoja mimi niendelee kuozea gerezani

Stories of Change - 2023 Competition

EDOGUN

JF-Expert Member
Jul 9, 2023
256
296
Nakumbuka kipindi chote cha miaka kumi na mitano,nilipokuwa miongoni mwa wabunge wa bunge la jamuhuri ya muungano wa Tanzania,miswada mingi ya sheria ilipokuwa ikiletwa bungeni tena mingine kwa hati ya dharura,
sikutaka kabisa kujihangaisha kuipitia kwa umakini kabla sijashiriki kuipitisha.

Hata pale wabunge wengine hasa wa vyama vya upinzani walipokuwa wakiikosoa na kupendekeza maboresho fulani kufanyika kabla ya miswada hiyo kupitishwa,mimi sikuwa na muda kabisa wa kuzisikiliza hoja zao.

Nakumbuka mara kwa mara nilijiuliza kwa nini wakati mwingine wabunge wa chama chetu huamua kushirikiana na wabunge wa vyama vya upinzani katika kutupotezea muda kuipinga miswada iliyoletwa na serikali inayoongozwa na chama chao wenyewe.

"kwa nini tusiwe tu tunaipitisha haraka haraka na kwenda kwenye mambo yetu mengine bwana."niliwaza.

Ukweli,miswada mingi kama sio yote iliyokuja bungeni,mimi sikuona namna ambavyo itaweza kuniathiri hata kama itapitishwa na kuwa sheria.Mimi,muheshimiwa mbunge,mwenye uwezo wa kuonana na rais ana kwa ana endapo nitahitaji kufanya hivyo nitishike na sheria ambazo zinakwenda kutumiwa na mahakimu wa mahakama ya kisutu.

"Nitatishwaje na kinyago nilichokichonga mwenyewe bwana."niliwaza.

Nilifikiri kuwa mbunge wa chama dola ni kuwa juu ya sheria.Mara ngapi tu nilizivunja na kuzikanyaga kanyaga sheria za nchi bila kuchukuliwa hatua na mtu yeyote.Nakumbuka kuna wakati niliweza kumtoa gerezani mpwa wangu aliyekuwa amemtwanga mjinga mmoja hivi risasi kwa kupiga simu moja tu.Yani simu yangu moja,ilifanya sheria ipindishwe pindishwe ili dogo arudi uraiani.

Kwa kila hali sikuona namna hizi sheria zitakavyoniathiri mimi au ndugu zangu.Kwa vyovyote vile hizi sheria zinakwenda kuwaumiza malofa ambao kwa kiasi kikubwa kwenye ukoo wetu sisi hawamo.

Nilijua kabisa hawa ninaowaita malofa ndio wapigakura wangu lakini sikuona umuhimu wa kuwapigania bungeni kwani hata kama ikifika kipindi cha uchaguzi wana nafasi ndogo sana ya kunizuia kurudi mjengoni.Kitu cha muhimu kwangu ni kushinda kura za maoni,mengine polisi na tume ya uchaguzi wanayamaliza.

Kwa kuwa wabunge wenzangu wengi walikuwa na fikra kama zangu na pia walikuwa na maisha ya uhakika kama yangu,miswada mingi yenye mapungufu ilikuwa inapita tu kirahisi bungeni na kuwa sheria baada ya kusainiwa na Rais.Na kama walivyozungumza baadhi ya wabunge sheria hizi ziliwaumiza sana wananchi wengi hasa wanyonge au waliokwenda kinyume na watawala.Baadhi ya vyombo vya habari vilijaribu kupiga kelele jinsi sheria hizi zinavyowaumiza wananchi.

Mimi sikujisumbua kuzisikiliza kelele hizo kwani hazikuyagusa kabisa maslahi yangu, sikuona hata ulazima wa kuzifanyia marekebisho sheria hizi.

Ikatokea siku moja ambayo siwezi kuisahau kabisa kwenye maisha yangu yote,siku nilipojikuta nimeyagusa maslahi ya mkubwa mmoja wa nchi wakati nikiwa kwenye madili yangu ya ujanja ujanja.

Kwa maagizo yake,nikapewa kesi ya uongo ya uhujumu uchumi na kutakatisha pesa.Kwa madhaifu ya sheria zile zile nilizoshiriki kuzipitisha huku nikijua zina mapungufu mengi nikapandishwa kizimbani,kwa kuwa kosa halikuwa na dhamana nikajikuta niko gerezani licha ya kuwa na makumi ya watu waliokuwa tayari kuniwekea dhamana hata kama wangehitajika kuweka mezani hati za nyumba zao.

Du! gerezani pasikie tu,huku sio pa kuja aisee,wanasema gereza ni shule lakini hii sio shule ya kumleta mwanao.

Huku hakuna maisha kabisa.Kwanza kuna msongamano mkubwa sana wa wafungwa na mahabusu,watu zaidi ya hamsini wanalala chumba kimoja,chakula kibovu hakifai hata kulishia nguruwe.

Wanasema majuto ni mjukuu,siku yangu ya majuto ikawa imewadia.Wakati niko bungeni waliibuka wabunge na kutoa hoja juu ya msongamano wa mahabusu na wafungwa,mimi sikuwa na muda hata wa kuwasikiliza.

Nakumbuka kabisa waliibuka wabunge wengi tu kulalamikia
uchelewaji wa kesi,msongamano wa mahabusu na wafungwa
,chakula kibovu,kubambikiwa kesi,ukosefu wa dawa na upungufu wa magodoro,mavazi nk.

Mimi sikujisumbua kabisa kuwaunga mkono ili kuipa msukumo serikali iongeze huduma huko magerezani,niliona changamoto za huko gerezani hazinihusu kabisa.

Niliwaona hawa wabunge kama ambao hawajawahi kuitembea Dunia kama nilivyo mimi.

"mbona magereza yetu yako vizuri mara mia kuliko yale ya Brazil ,Colombia,Honduras,Haiti nk."niliwaza.

Niliwaona hawa wabunge wanaolalamika hovyo pengine watakiwa hawaelewi maana ya gereza na wanataka labda gereza liwe kama hoteli ya nyota tano.

Sasa leo hii chakula kibovu,msongamano,huduma mbovu za afya,ni sehemu ya maisha yangu haya mapya na siwezi kuyabadilisha kwa sasa.

Lakini hivi vyote nilikuwa na uwezo wa kuvibadilisha japo kidogo kipindi niko mbunge,sijui kwa nini sikuona umuhimu wa kufanya hivyo.

Ona sasa,kama utani vile,nimemaliza miaka miwili nikiwa mahabusu,eti kuna wakati hakimu aliniambia mahakama yake haina uwezo wa kusikiliza shauri langu,hivi sheria za hivi kweli nilipokuwa nikishiriki kuzitunga nilikuwa nimelewa pombe gani jamani?

Na sasa kesi yangu imefikia kwenye hukumu,kuna kila dalili ya kuhukumiwa kifungo cha miaka si chini ya saba au faini ya mamilioni,na kwa sasa sina uwezo wa kulipa hayo mamilioni kwani akaunti zangu zote zimefungwa kwa amri kutoka juu,ndugu na marafiki zangu nao wana hofu kubwa ya kunisaidia kwani biashara zao zinaweza kuharibiwa kwa maagizo kutoka kwa wakubwa.

Ni wazi sasa lazima nitatumikia kifungo gerezani.Na kwa hali ilivyo,lazima nitapelekwa gereza la kilimo na kuna tetesi kuwa huko kama hulijulii jembe unakuwa na machaguo mawili,ama ufe kwa kipigo cha mijeredi shambani au uwe mke wa nyampara;na mpaka sasa sijajua nitachagua kipi ukizingatia toka utoto wangu sijawahi shika jembe kabisa?

Maskini sijui ni jini gani aliniingia mpaka nikajikuta nayasahau majukumu ya mbunge kwa muongo mmoja na nusu niliokuwa mbunge.

Badala ya kuwaunganisha wananchi wa jimbo langu na serikali,mimi nilijiunganisha mwenyewe kwa manufaa binafsi.

Badala ya kukusanya shida za wanachi wa jimbo langu,Mimi nilikusanya shida zangu binafsi na kuzipeleka huko bungeni.

Badala ya kushiriki kutunga sheria mpya,mimi niliishia tu kugonga gonga meza kushangilia vitu visivyokuwa na msaada kwa wapigakura wangu.

Badala ya kuisahihisha serikali ili itie juhudi zake zote kutambua hoja za wanachi,mimi niliwasifia mawaziri hata kama walichokuwa wakikizungumza hakikuwa na maslahi ya wapiga kura wangu.

Kweli majuto ni mjukuu.Acha tu ninyee debe kwa hii kesi ya kupewa.Nilijiona niko mikono salama kwa kujuana na wakubwa, kumbe hata hao wakubwa niliokuwa nikiwategemea nao wana mamia ya wakubwa wao.


Ngoja mimi niendelee kuozea gerezani.
 
Back
Top Bottom