Neema kubwa yaanza kuonekana baada ya China kufunguliwa na kulegeza kanuni za UVIKO-19

ldleo

JF-Expert Member
Jan 9, 2010
1,010
1,036
VCG111417332928.jpg


Mwaka mpya wa 2023 umekuwa mzuri na wa neema hapa nchini China kwani kuanzia tarehe 8 Januari milango yote ya China inafunguliwa na kuruhusu wageni na wenyeji kuingia na kutoka China, hii ikiwa ni hatua ya kulegeza kanuni zote za UVIKO-19, ambazo zilisababisha nchi kufungwa tangu virusi vya Corona vilipozuka mwaka 2020.

Tangu litolewe tangazo kwamba China inafungua milango yake, watu wengi wa China wamekuwa na hamasa kubwa ya kutaka kusafiri huku idadi ya wale wanaotafuta tiketi za ndege za nje ya China ikiongezeka na kuimarisha imani ya kurejesha kasi ya matumizi duniani.

Tunafahamu kuwa China ni nchi ambayo inatoa chachu kubwa katika sekta ya utalii duniani, na Wachina wanachangia mapato makubwa ya utalii duniani. Mwaka 2019 kabla ya kuzuka kwa ugonjwa UVIKO-19, idadi ya Wachina waliotalii nchi za nje ilifikia karibu milioni 155, ikiwa karibu mara tatu ya mwaka 2020. Lakini mwaka 2020, idadi hii ilipungua hadi milioni 20.3 kutokana na janga la virusi vya Corona, ambapo ilikadiriwa kuongezeka kidogo mwaka 2021.

Mbali na safari za nje ya nchi, safari za ndani pia zimeanza kushuhudia ongezeko, hasa katika kipindi cha sikukuu ya mwaka mpya wa 2023. Kwa mujibu wa makadirio ya Wizara ya Utamaduni na Utalii nchini China, watu waliosafiri ndani ya China walifikia 52,713,400, likiwa ni ongezeko la 0.44% ikilinganishwa na mwaka uliopita wakati kama huu. Safari hizi zimeshuhudiwa zikiingiza jumla ya yuan bilioni 26.517 ($3.84 billion) katika mapato ya utalii wa ndani, yakiongezeka kwa 4.0% kuliko mwaka uliopita. Hivyo katika sikukuu ya mwaka mpya wa jadi wa China, kuna matarajio makubwa kwamba mwaka huu utashuhudia ongezeko la mapato katika sekta ya usafiri, sekta ya burudani na hata sekta ya huduma.

Baada ya sera za UVIKO-19 kurekebishwa, sekta ya huduma na burudani pia zinaonekana kustawi, kwani katika mapumziko ya siku tatu ya sikukuu ya mwaka mpya wa 2023, wafanya biashara za migahawa nao pia biashara zao zimerudi kwa asilimia 70 ya viwango vya kabla ya janga la Corona hapa Beijing. Vibanda vinavyouza vyakula mitaani halikadhalika navyo pia vimeshuhudia wimbi la watu wakimiminika kwenye vibanda hivyo kununua chakula, huku mistari mirefu ya foleni ikionekana na kuashiria kwamba sasa maisha ya Wachina yanarejea katika hali ya kawaida.

Mtafiti wa Kituo cha Utafiti wa Maendeleo cha Baraza la Serikali, Liu Tao, amesema sekta ya huduma ya maisha inatarajiwa kuwa na ukuaji mkubwa na kufufuka katika mwaka 2023, na kwamba huduma za mapishi, kusafiri na nyinginezo zitakuwa na nafasi ya kukua katika mwaka huu wa 2023.

Tangu janga la UVIKO-19 lilipoanza, China imekuwa ikiweka watu kwanza na kuweka kipaumbele kwa maisha yao. Ndio maana iliweka sera kali za kudhibiti na kuzuia virusi vya Corona ili kulinda maisha ya watu. Lakini licha ya sera za maambukizi sifuri zilizokuwa zikitekelezwa hapa China, ambazo zilipelekea China kufungwa wakati huohuo ikizingatia zaidi uchumi wake, China bado iliendelea kuwa nchi ya pili kwa uchumi mkubwa duniani huku uchumi wake ukiendelea kukua vizuri.

Katika kipindi cha janga pamoja na vita vya Russia na Ukraine, nchi nyingi duniani ziliingia kwenye msukosuko wa chakula, China kwa upande wake imeendelea kujiimarisha na kupata mavuno mengi kwa mwaka wa 19 mfululizo, na kuiweka katika nafasi nzuri zaidi ya kuhakikisha usambazaji wa chakula kwa watu wake.

Kwa hiyo, kwa kuwa sasa China inafungua milango yake na kuruhusu watu kuingia na kutoka, huku wakifuata kanuni za UVIKO-19, tutarajie makubwa kwenye uchumi na mapato ya China katika mwaka huu wa 2023 na miaka inayofuata. Halikadhalika pia tutarajie mchango mkubwa zaidi wa China katika kukuza mapato ya sekta mbalimbali duniani, ikiwemo kusaidia kukuza uchumi wa dunia.
 

Attachments

  • VCG111415845138.jpg
    VCG111415845138.jpg
    164.4 KB · Views: 4
Back
Top Bottom