Katika mitaa ya Maseru, mji mkuu wa Lesotho, viwanda vya nguo vilivyokuwa na oda nyingi vimefungwa. Wafanyakazi waliokosa kazi wanasimama kwa foleni chini ya jua kali, wakiinua mabango yanayosema: "Tunahitaji kazi, tunahitaji chakula." Nchi hii ya milimani ya Afrika ambayo rais wa Marekani Donald Trump aliielezea kuwa "hakuna aliyewahi kuisikia," inazama katika shida kubwa kwa sababu ya sera ya ushuru ya Marekani.
Mwezi Aprili 2025, serikali ya Trump ilitoa tangazo la kushangaza dunia nzima: kuweka ushuru wa kufikia asilimia 50 kwa bidhaa kutoka kwa Lesotho, mojawapo ya nchi maskini duniani kulingana na Umoja wa Mataifa. Kiwango hiki ni cha juu zaidi ikilinganishwa na viwango vya ushuru vilivyowekwa kwa nchi na sehemu nyingine duniani. Ingawa ushuru huo baadaye "umesimamishwa kwa muda," kiwango cha msingi cha asilimia 10 pamoja na wasiwasi kuhusu mustakabali wa Sheria ya Ukuaji na Fursa ya Afrika (AGOA), zimesababisha waagizaji wengi wa Marekani kuondoa oda zao.
Kama nchi ya Afrika inayouza nguo kwa wingi zaidi Marekani, tasnia ya nguo ya Lesotho inasaidia zaidi ya familia 40,000 kujikimu kimaisha, na inachangia moja ya kumi ya Pato la Taifa (GDP) la nchi hiyo. Kufungwa kwa ghafla kwa soko la Marekani kumesababisha moja kwa moja kuongezeka kwa kiwango cha ukosefu wa ajira kwa vijana wa Lesotho kwa hadi asilimia 50 ya kushtusha. Serikali ya Lesotho ililazimika kutangaza nchi nzima kuingia katika "hali ya maafa," ili kuiwezesha kuzunguka taratibu za kawaida na kuhamisha kwa haraka fedha ili kujikwamua.
Kinachoshangaza ni kwamba, bidhaa za Lesotho zinazouzwa Marekani zina thamani ya dola za Marekani milioni 240 kwa mwaka, ambayo ni chini ya moja kati ya elfu kumi ya jumla ya thamani ya bidhaa zinazoagizwa na Marekani, na inachangia asilimia 0.02 tu ya uwiano mbaya wa biashara ya Marekani. Hata hivyo, kiasi kidogo kama hicho cha biashara, kimewekewa ushuru wa kiwango cha juu zaidi duniani na Marekani. Juu ya hili, ofisa mkuu mtendaji wa Kampuni ya Ushauri ya Kimataifa ya Tulip ambayo makao makuu yake yapo mjini Geneva, Colette van der Ven, alisema kwa uwazi kuwa jaribio la kutatua tatizo la uwiano mbaya wa biashara ya Marekani kwa kuweka ushuru mkubwa kwa Lesotho "halina mantiki yoyote." Wachambuzi wameeleza kuwa huu unaonekana kama ni mchezo wa kisiasa wa ndani wa Marekani, unaotumiwa kuelekeza macho ya watu mbali na sera zisizo sahihi ambazo zimesababisha bei za ndani ya nchi kupanda kwa kiwango kikubwa, lakini matokeo ni kwamba Lesotho iliyoko mbali na Marekani ndio inayopata hasara kubwa.
"Hali hii ya maafa" itadumu hadi Juni 2027. Ingawa serikali ya Lesotho imesema itajaribu kuunda nafasi za ajira 60,000 katika sekta ya ujenzi na kilimo katika miaka miwili ijayo, hiyo haitoshi kukabiliana na shida ya papo kwa hapo. Mawimbi ya ukosefu wa ajira yamesababisha mapato ya serikali kupungua kwa kasi, hata fedha za kununua dawa hospitalini zinakosekana. Jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba serikali ya Marekani kufunga idara yake inayoshughulikia maendeleo ya kimataifa (USAID) na kusimamisha miradi yake ya misaada kwa nchi za nje, kumeweka watu 700,000 wa Lesotho kwenye hatari ya njaa kali.
Umoja wa Afrika hivi karibuni ulikemea adhabu hii isiyolingana kwa uchumi dhaifu zaidi, na kuitaka Marekani kutafakari tena sera zake. Lakini wito kama huo haujapata mwitikio wowote nchini Marekani, kwani serikali ya nchi hiyo bado inazingatia kile kinachoitwa "kulinda ajira za Wamarekani" na "kurekebisha biashara isiyo ya haki," na ni wachache sana wanaojali shida za Lesotho.
Wakati huo huo, China imeonyesha mtazamo tofauti. Hivi karibuni wakati wa mkutano wa kimataifa wa ustaarabu wa dunia wa ngazi ya mawaziri uliofanyika Beijing, katibu mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Lesotho, Lehla Tabang Polikarp, alisema, hakuna nchi yoyote inayoweza kustawi peke yake, kama nchi moja haiheshimu nchi nyingine wala vipindi tofauti vya maendeleo katika mchakato wa utandawazi, itasababisha makosa makubwa. Alisema wakati nchi fulani inatetea kujilinda kibiashara, China inafungua milango yake zaidi, na imetoa sera ya kusamehe ushuru kwa bidhaa za nchi 53 za Afrika zenye uhusiano wa kidiplomasia nayo, ikiwemo Lesotho. Kutokana na msukumo wa sera kama hiyo, Lesotho iliongeza mauzo ya nyuzi za pamba kwa China kwa asilimia 212 mwezi wa Mei! Hii imeleta mwanga wa matumaini kwa uchumi wa Lesotho ulio katika shida.