“Natumai watoto wa maskini pia wawe na fursa ya kujiunga na Vyuo Vikuu bora”

Yoyo Zhou

Member
Jun 16, 2020
72
111
139195576.jpg


“Natumai watoto wa sehemu maskini pia wawe na fursa ya kujiunga na vyuo vikuu bora”

Alichosema hayo ni Zhang Guimei mwenye umri wa miaka 63. Yeye ni mwalimu mkuu wa shule ya sekondari ya juu ya wilaya ya Huaping, mjini Lijiang. Hii ni shule maalum, ambayo wanafunzi wake wote ni wasichana kutoka sehemu maskini za milimani mkoani Yunnan, kusini magharibi mwa China, na ni shule ya kwanza ya wasichana ya serikali ambayo wanafunzi hawalipi gharama yoyote. Mwezi Julai mwaka huu, mwalimu mkuu Zhang anatarajiwa kushuhudia wahitimu wa awamu ya 10 wa shule hiyo.

“Sisi hatutaji umaskini, naona kwa wasichana, umaskini ni kama jambo la kuwatweza, tunawaita wasichana kutoka sehemu za milimani.”

Shule ya sekondari ya juu ya Huaping inawaandikisha wasichana kutoka sehemu maskini za vijijini ambao wamemaliza masomo ya miaka tisa ya lazima na kushindwa kuendelea na masomo yao. Mwaka jana, shule hiyo ilipata nafasi ya kwanza mjini Lijiang kwa kufaulisha asilimia 82.37 ya wahitimu 118 katika mitihani ya kujiunga na vyuo vikuu.

Chen Mingsi ni mmoja wa wanafunzi watakaohitimu mwaka huu. Yeye anasema anapenda kujiunga na chuo kikuu kilicho mbali na maskani yake, ili kupanua upeo na uelewa wake.

“Kijijini kwetu, wasichana wa rika langu tayari wameolewa. (mwanahabari anauliza: Watafanya nini baada ya kufunga ndoa?” Wanazaa na kuanza kuishi maisha ya kufanya kazi za mashambani. (mwanahabari anauliza: Hatma kama hiyo kwa wasichana inaweza kubadilishwa vipi?) Kwa kutegemea kusoma, kwa kutegemea elimu.”

Zhang Guimei na mumewe walikuwa walimu wa shule moja mjini Dali. Mwaka 1996, mume wa Zhang Guimei aliaga dunia kutokana na saratani ya tumbo. Bibi Zhang alipata pigo kubwa kwenye mkasa huo na kuhamia na kufundisha katika shule ya kikabila wilayani Huaping mjini Lijiang, ambapo aligundua kuwa mazingira ya elimu ya mahali hapo yalikuwa magumu ikilinganishwa na yale ya mji wa Dali. Wakati ule, shule aliyofundisha ilikuwa na wanafunzi wachache wa kike, na hata kila baada ya muda fulani, kulikuwa na wasichana walioacha shule. Kisha Zhang alienda kutembelea familia za wasichana hao, na kufahamishwa kuwa wazazi walikuwa wamewaoza mabinti zao. Zhang aliwaambia wazazi hao

“Leo ni lazima nimchukue binti yako, ili akasome. Hutalipa senti hata moja, kwanini hufurahii fursa hii?”

Ili kuwafanya watoto wa darasa lake wasiache masomo, alibana matumizi yake na kufanya kila awezalo kuwasomesha watoto hao.

“Darasani kulikuwa na watoto zaidi ya 50, sikukubali mwanafunzi hata mmoja aache masomo kutokana na umaskini.”

Mwaka 2001, makazi ya yatima ya Huaping yalizinduliwa, na wafadhili walimtaka mwalimu Zhang Guimei kuwa mwalimu mkuu. Baadhi ya watoto walioasiliwa ni wasichana wadogo waliokuwa na afya nzuri ambao walitelekezwa mlangoni mwa makazi hayo, na Bibi Zhang asiyekuwa na mtoto alikuwa “mama” yao.

Mambo aliyoshuhudia katika makazi hayo na shule ya kikabila yaliibua wazo la kuzindua kwa ufadhili shule ya sekondari ya juu ya wasichana ambayo wanafunzi hawalipi ada yoyote.

Kwa familia maskini kutoka sehemu za milimani, wakati hali ya uchumi inakuwa mbaya, wazazi huwa wanachagua kuwasomesha watoto wa kiume na kutojali mabinti wao.

“Natoa mfano, nilipotembelea familia moja, mwanafunzi wangu wa kike alitakiwa kushiriki mitihani ya kujiunga na vyuo vikuu, watoto wa kiume walisoma shule ya msingi na shule ya sekondari, lakini wazazi walimfanya mwanafunzi wangu abaki nyumbani kuendelea na shughuli za kilimo na kuwapelekea watoto wa kiume kwenye masomo ya ziada mjini.

535859414.jpg
139195576.jpg
999801991.jpg
1486459661.jpg
Nilimwuliza mama, ‘hivi kweli wewe una akili? Binti yako anatakiwa kushiriki kwenye mitihani ya kujiunga na vyuo vikuu, na wewe hujampeleka kwenye masomo ya ziada, lakini umewapeleka watoto wadogo wa kiume.’ Alisema kwa sababu wao ni wavulana. Wakati ule, nilikasirika sana, kwa hivyo niliamua bila kujali ni taabu gani nitakazopata, ni uamuzi sahihi kuanzisha shule hiyo ya wasichana, na hata najitolea muhanga ni jambo linalostahiki.”

Mbali na suala la mtazamo, kwa wilaya ya Huaping, bajeti ya elimu imekuwa ndogo, na kuanzisha shule ya sekondari ya juu ya wasichana ambayo wanafunzi hawalipi ada ni wazo la ajabu. Hata hivyo, kuanzia mwaka 2002, Zhang Guimei alianza kuhangaika kutafuta pesa ili kutimiza ndoto hiyo ambayo ilichukuliwa kama ni ya kijinga.

Wakati Zhang Guimei bado akiwa mwalimu, anaamini kithabiti kuwa kuwaelimisha watoto wanaoishi sehemu maskini za milimani si jambo la watu wa kizazi kimoja tu, bali ni jambo linalohusu jamii nzima.

“Wasichana wakipata elimu, inaweza kuleta mabadiliko kwa watu wa vizazi vitatu, na mtu akiwa na elimu hawezi kumtelekeza mtoto wake.”

Ili kuanzisha shule ya sekondari ya juu ambayo wanafunzi wake hawalipi gharama yoyote, Zhang Guimei alitafuta pesa hapa na pale ambapo kuna wakati baadhi ya watu walimwelewa vibaya na kumchukulia kama mwongo. Wakati alipohangaika kutafuta ufadhili, kuna kitu kilianza kubadilika. Mwaka 2007, Bibi Zhang alikwenda Beijing kuhudhuria mkutano wa bunge akiwa mjumbe wa Bunge la 17 la Umma la China, ambapo ndoto ya kuanzisha shule hiyo iliripotiwa sana na vyombo vya habari. Kisha michango iliyotolewa na watu wa sekta mbalimbali kote nchini ilisaidia kutimiza ndoto yake. Mwezi Septemba mwaka 2008, shule ya sekondari ya juu ya wanawake ya Huaping ilifunguliwa na Zhang Guimei akawa mwalimu mkuu.

“Kwa familia nzima na hata watu wa kijiji kimoja, matarajio yao yapo kwa mtoto mmoja. Awali, wasichana hao hawakuwa na pesa kwa ajili ya elimu, lakini kwetu hawalipi ada yoyote. Nakumbuka kuna mzee mmoja aliniambia sasa anaweza kufa baada ya kuona mjukuu wake anasoma. Elimu ina uzito mkubwa mioyoni mwa watu wanaoishi katika sehemu maskini.”

Zhang Guimei amesema ili kuwawezesha watoto hao watoke milimani na kujiunga na vyuo vikuu bora, yeye na walimu wenzake wamejitolea sana.

“Nusura sisi walimu tumejitolee mihanga katika kuwafundisha wanafunzi hao.”

Zhang Guimei amepewa tuzo nyingi na idara za serikali, na kuchangia ruzuku na mishahara karibu Yuan milioni moja, sawa na dola za kimarekani 140,000 kwa watoto hao. Kila ifikapo wakati wa likizo za shuleni, aliwatembelea wazazi waishio katika sehemu maskini milimani, ili kuwapa mtazamo wa “elimu yabadilisha hatma, elimu yaondoa umaskini.” Akizungumzia thamani yake ya kimaisha, Zhang Guimei anasema,

“Kila ninaposikia alama za wanafunzi katika mitihani ya kujiunga na vyuo vikuu, na kila ninaposikia wanafunzi wangu wamepata mafanikio na kutoa mchango kwa jamii, tunaona kazi yetu ina thamani.”

“najitahidi kuokoa watu wa kikazi kimoja, bila kujali ni idadi gani, kama wanaweza kuishi maisha mazuri baada ya kuhitimu, kwangu ni faraja kubwa.”
 
Back
Top Bottom