Mimi ninachoona hapa ni kwamba CCM wanafanya michezo ya kuigiza kwa faida ya matumbo yao na wala si kwa faida ya taifa. Hii ni timu iliyoundwa mahususi si kwa ajili ya kuimarisha chama, bali ni kwasababu ya kuwarubuni watanzania kwa kuwapiga changa la macho kwamba CCM ni chama bora na kimejiboresha.
Hali hii ya kuwarubuni watz haina lengo la kuwaletea maendeleo au kuwaonyesha ni kwa kiasi gani wameendelezwa na sera za CCM, bali ni kuwashawishi kuichagua CCM mwaka 2015 bila kujali ubora wake au udhaifu wake. Na watanzania kwa jinzi tulivyo wepesi kudanganyika, usishangae mwaka huo tukaipigia CCM kura na kuipitisha kwa kishindo.
Mara baada ya kupita kwa kishindo CCM itarejea utamaduni wake uleule wa Ufisadi, Hujuma kwa uchumi wa taifa, hatimaye kuyafanya maisha ya watanzania kuwa magumu zaidi kuliko ilivyo hivi sasa. Hapo ndipo tutakapokurupuka na kuanza kulia na CCM lakini itakuwa too late.
Nasema tukiipitisha CCM 2015 yatakayotokea ni kilio na kusaga meno. Msishangae kilo ya Sukari tukaja kuinunua kwa Tsh.5000. Kuna usemi wa kichina usema, "usilaani giza, bali washa mshumaa". Ni kweli kabisa giza hata ungelilaani namna gani haisaidii kitu, ni lazima ufanye jambo.
Na sisi watanzania matatizo ya nchi hii yanayoletwa na CCM hata kama tungeyalaani mpaka wapi hayataisha kamwe mpaka siku tutakapochukua uamuzi mgumu na kufanya lisilotazamiwa, yaani kuitema CCM 2015. Vinginevyo, wimbo wetu utakuwa ni ule ule, you mark my words.