Naibu Waziri Ndejembi ataka Maeneo ya kujenga Shule yatengwe kukidhi mahitaji

Stephano Mgendanyi

JF-Expert Member
May 16, 2020
1,900
944
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Deogratius Ndejembi amesema kuna ulazima wa kutenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa shule ili kukidhi mahitaji yanayotokana na ongezeko la wanafunzi ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto wa wanafunzi kutembea umbali mrefu.

Mhe. Ndejembi ametoa wito huo akiwa mkoani Dar es Salaam, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua ujenzi wa miundombinu ya elimu inayojengwa kupitia mradi wa BOOST na SEQUIP katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.

Mhe. Ndejembi amesema maeneo hayo yakitengwa, kuna ulazima wa kujenga shule za ghorofa badala ya majengo ya chini ili kutatua changamoto ya kukosa viwanja vya michezo vya watoto ambavyo ni muhimu kwa ajili ya kujenga afya ya akili.

“Michezo ni muhimu kwa ajili ya afya ya akili na makuzi ya watoto hivyo ni lazima kuwepo na ushirikiano wa viongozi kuanzia ngazi ya mtaa, kata, halmashauri, wilaya na mkoa katika kuhakikisha shule zinajengwa kwenda juu ili kupata maeneo ya viwanja vya michezo,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Ameongeza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuboresha elimu ya msingi na sekondari, hivyo ni lazima kuendelea kutenga maeneo ya ujenzi na kuyatumia vizuri ili yawe na tija.

Aidha, Mhe. Ndejembi ameipongeza Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kwa kukamilisha ujenzi wa shule mpya na ukarabati wa miundombinu ya elimu, kupitia fedha za mradi wa BOOST na SEQUIP zilizopatikana kutokana na jitihada za Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amedhamiria kuendelea kuboresha miundombimu ya elimu nchini.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Saad Mtambule amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za ujenzi wa miundombinu ya elimu kupitia mradi ya BOOST na SEQUIP na kuahidi kuendelea kusimamia vizuri matumizi ya fedha hizo ili ziwe manufaa kwa taifa.

IMG-20230712-WA0019.jpg
 
Back
Top Bottom