Mzee Musobi Mageni hatunaye tena

[h=3]Mzee ameaga dunia akihitajika. Rafiki yangu alikuwa amepanga kufanya naye mahojiano kwa ajili ya kipindi cha TV, lakini naona kamkosa. Niliwahi kuongea naye kuhusu siasa za Vyama vya siasa, alilaani sana kusahauliwa kwa wazee katika vyama hivi. Aliwahi kusimulia pia jinsi alivyoteuliwa kuwa Waziri enzi za Nyerere, alidai alikamatwa na polisi na kusafirishwa hadi Ikulu Dar, akidhani amekosa, lakini alipofika alitaarifiwa kuteuliwa. Ilibidi ashoneshe suti kwa ajili ya kuapishwa na kazi. Alidai anamkumbuka fundi cherehani aliyemshonea suti.
RIP Mzee wetu.

-----
Hapa kwa wasifu wake, nilioudakua sehemu:

TANZIA YA ALIYEKUWA MWENYEKITI WA AWAMU YA PILI WA CUF
[/h]


TANZIA YA ALIYEKUWA MWENYEKITI WA AWAMU YA PILI WA CUF
CUF – Chama Cha Wananchi, tunasikitika kutoa taarifa ya msiba mzito wa kufiwa na aliyekuwa Mwenyekiti wetu wa Chama awamu ya pili (1995 – 1999), Musobi Mageni Musobi, aliyejiunga na chama cha wananchi CUF mwaka 1994 amefariki jana Jumatano, Mei 30, 2012 mnamo saa 2.40 usiku nyumbani kwake kijiji cha Ngudu, Wilaya ya Kwimba, mkoani Mwanza, kwa ugonjwa wa shinikizo la damu na kisukari uliokuwa ukimsumbua kwa muda mrefu.
Marehemu Musobi Mageni anetarajiwa kuzikwa nyumbani kwake Ngudu siku ya Jumatatu Juni 04, 2012 saa 7 mchana, amefariki akiwa na umri wa miaka 81, amezaliwa April 01, 1931, ameacha wajane wawili, watoto 15 (wakiwemo wanawake nane na wanaume saba), wajukuu 28 (wanawake 12 na wanaume 16) lakini pia ameacha vitukuu sita (wakiwemo wanawake wawili na wanaume wanne).
Wakati wa uhai wake alipata elimu ya Msingi katika Shule ya Kakola wilayani Kwimba, na baadae alipata elimu ya kati na Sekondari Dole iliyopo Zanzibar. Baada ya hapo 1950 alirudi wilayani Kwimba na mwaka mmoja baadae 1951 alipata kazi ya ukarani (Area Secretary) katika Halmashuri ya Maswa, na baadae 1954 akahamia Halmashauri ya Kwimba kama Muhasibu na mnamo 1957 akahamishiwa ukarani tena katika Halmashauri hiyohiyo ya Kwimba hadi 1961 alipoacha kazi na kufanya shughuli za ukulima.
Ilipofika mwaka 1965 aliamua kugombea ubunge jimbo la Mwamashimba wilaya ya Kwimba, alifanikiwa kuwa mbunge wa jimbo hilo kwa awamu mbili hadi mwaka 1975, wakati huo akiwa mbunge alifanikiwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Aridhi, Nyumba na Maendeleo Mijini mwaka 1972 na aliutumikia hadi 1975, kabla hajateuliwa kuwa mkuu wa wilaya ya Chunya mwaka 1978, wilaya ya Kahama 1983 na wilaya ya Muleba 1988 hadi 1990.
Kitaaluma, pamoja na mafunzo ya Uhasibu na Ukarani, lakini pia alibahatika kupata mafunzo ya Uandishi wa Habari katika chuo cha Cambrige University mwaka 1968 na Chuo cha Social Training Centre cha Nyegezi, mkoani Mwanza.
CUF – Chama cha Wananchi tunasisitiza tumeupokea kwa masikitiko makubwa sana msiba huu, kwani pamoja na marehemu kustaafu Uongozi, bado alikuwa na mchango mkubwa sana wa hali na mali, na alikuwa ni muhimili mkubwa sana katika wilaya ya Kwimba na majimbo yake kwa upande wa chama na wananchi wa maaneo hayo.

Imetolewa na Prof. Ibrahim H. Lipumba
Mwenyekiti, CUF Taifa,
Mei 31, 2012
 
Back
Top Bottom