Rais wa Pili wa Zanzibar, Aboud Jumbe Mwinyi amefariki dunia mbele ya familia yake, akiwa ameacha ujumbe unaokataza mazishi yake kuhusisha taratibu zinazokiuka mafundisho ya dini ya Kiislamu.
Jumbe, ambaye alivuliwa nyadhifa zote serikalini na ndani ya CCM kutokana na kutofautiana na chama hicho katika suala la muundo wa Muungano, alishika nafasi ya urais mwaka 1972 baada ya muasisi wa Zanzibar, Abeid Amaan Karume kuuawa katika jaribio la mapinduzi.
Akizungumzia kifo hicho, mtoto wa Jumbe Mustafa Jumbe amesema sababu ya kifo cha baba yake ni umri mkubwa ambao ni miaka 96.
Amesema kabla ya kuzikwa leo mwili, utaswaliwa katika msikiti wa Mwembeshauri na kuzikwa nyumbani kwake Migombani, Zanzibar.
“Marehemu ameacha wake wawili, watoto 14 na wajukuu zaidi ya 30,” amesema Mustafa.
Akataa kuzikwa kifahari
Mazishi ya kiongozi huyo aliyekaa madarakani kwa miaka 12 ikiwa ni muda mrefu kuliko marais wengine wa Zanzibar, yanaweza kutoshirikisha taratibu za kiserikali kutokana na wosia alioandika kabla ya kifo chake.
“Sitaki katika maziko yangu kutumbuizwa chochote kiendacho hata kidogo kinyume na mafundisho ya Islamu,” anaandika katika wosia huo.
“Sitaki beni (bendi), sitaki mizinga, sitaki maombolezo wala lolote jingine lenye hata chembe ya kufuru. Sitaki hivyo nikiwa hai, nitakapoondoka katika dunia. Mwenyezi Mungu anatosha kuwa shahidi wangu, duniani na akhera.”
Kwa kawaida kiongozi wa kada yake anapofariki, hupigiwa mizingi 21 na kusubiri taratibu za kiserikali ambazo wakati mwingine huchukua muda kukamilika tofauti na sheria za dini hiyo.