SEHEMU YA 66
“Tupo tayari kuwaunga mkono,” Jaji Kessy alisema akimtazama Michael.
“Ni kweli,” Michael alisema akitikisa kichwa.
Wote wakakumbatiana.
“Yatupaswa kuandaa jeshi,” Shebo aliwaambia.“Nitaanza kuwakusanya vijana taratibu na huku kwenye Kijiji cha Amani, ndiko kutakuwa mafichoni kwetu.”
“Ni kweli, lazima tuandae jeshi,” Mzee Makimbi aliiunga mkono hoja yake.
Shebo akaondoka mahali hapo na kuingia mitaani kwa tahadhali kubwa kwa ajili ya kuwatafuta vijana wa kuunganisha nao nguvu kwa ajili ya kupambana na Azra Malama na Wamarekani.
Akiwa mitaani Shebo alipigwa butwaa!
Wanajeshi wa Kimerakani walikuwa wametanda kila kona na mitutu. Shughuri za kila siku za Swadege zilikuwa hazifanyiki kama ilivyokuwa awali.
Mitaa ilikuwa tupu na kimya!
Hali hiyo aliyoiona ilizidi kumkasirisha mno Shebo. Akawa tayari kufa lakini si kushuhudia watu wa Swadege ya Rwadege wakigeuka kuwa watumwa wa Marekani.
Kwa tahadhari ya nguvu Shebo alikwenda kwenye mitaa ambayo alifahamu ni lazima atakuta watu, sehemu ambapo watu walikusanyika vita inapozuka, na kweli aliwakuta.
Akafurahi.
Akawakusanya vijana na kuwaeleza nia yake.
“Tupo tayari,” vijana walipaza sauti kwa ari kubwa.
“Lazima tupambane kwa ajili ya Swadege yetu,” Shebo aliongea kwa sauti ya juu.
“Ndiyo…” Vijana walipaza sauti.
“Hata ikigharimu uhai wetu.” Shebo aliwaambia tena.
“Ndiyo.” Vijana walikubali kuingia vitani.
Shebo akawaongoza mpaka kwenye Kijiji cha Amani, wakakutana na mzee Makimbi, Jaji Kessy na Michael ambao ndiyo wangeongoza mapambano hayo kwa ushauri na nini kifanyika.
Mipango kabambe ya vita ikaanza kupangwa! ***
“Ni lazima tumtumie Jemima!” Mzee Makimbi alitoa wazo.
“Lakini ametusaliti,” Shebo alibweka.
“Ni kweli, lakini kumbuka wanawake ni vigeugeu.”
“Nguvu ya mapenzi ni kubwa mzee Makimbi, Jemima anaweza kutuangamiza.”
“Hapana,” Mzee Makimbi alipinga. “Si mjinga kiasi hicho ashindwe kuona namna maisha yalivyobadilika Swadege. Upofu wa mapenzi ulimfunga akatenda kosa, lakini ninauhakika tunaweza kumtumia.”
”Kivipi?” Michael aliuliza.
“Yeye ndiye anaweza kutufanya tukafahamu nguvu zaidi za Azra Malama na Wamarekani.” Mzee Makimbi alifafanua.