SEHEMU YA 61
Azra alimfahamu vyema Shebo, sifa zake za mapambano amekwisha zisikia mara kadhaa akizungumziwa, alitambua anapambana na mtu hatari.
Lakini pia kitendo cha Azra kumuona Shebo mahali pale, alifahamu wazi alikuwa amepona kule msituni na alikuja kumsubiri hapo akifahamu ni lazima angekwenda mahali hapo.
“Jisalimishe,” Shebo aliyeonekana kuwa na hasira alimwambia Azra kwa sauti iliyojenga utulivu.
Azra alimtazama mfano wa mtu anayetazama sanamu.
Kitendo cha Azra kuonyesha dharau kilimkasirisha Shebo, Shebo kwa kitendo cha haraka aliruka juu na kupiga teke taa iliyokuwa inamulika mwanga kwenye chumba hicho, ikavunjikavunjika, kukawa giza ghafla.
Azra alitoa macho ili kumtazama mtu huyo yupo wapi lakini ilikuwa ni sawa amefumba macho, alikuwa anaona giza tu, na akiwa bado hajapata maamuzi ya kuchukua alishitukia kitu kizito kikimsukuma kifuani, akaruka na kujipiga ukutani.
Alikuwa amepokea teke la nguvu.
Azra akaanza kuugulia kwenye maumivu huku anajikokota chini. Akiwa hajakaa sawa pigo lingine likamfuata mahali hapo, wakati huu pigo hilo lilimuingia sawasawa mpaka akatoa sauti ya juu ya maumivu.
“Mimi ndiye Shebo, Mswadege ya Rwadege,” Shebo alianza kutamba katikati ya giza hilo akijipigapiga kifuani.
Azra Malama akiwa chini alianza kujikusanya taratibu ili kupambana na mtu huyo.
Shebo ambaye utafikiri gizani ndipo alikuwa anaona zaidi, alimfuata Azra Malama pale chini na kumuinua kisha akaanza kumpiga ngumi za nguvu za usoni.
Damu zikawa zinaruka juu.
Baada ya kumpiga ngumi kadhaa Shebo alimuachia tena Azra, kijana huyo akadondoka chini huku katepeta. Moyoni alianza kuhisi kwamba anakwisha kwani Shebo alionekana kuwa na nguvu zaidi.
Akiwa chini anajaribu kufurukuta ndipo Azra alihisi ameshika kitu chenye ncha kali, alipokishika zaidi, aligundua ni nondo iliyochongoka mbele. Azra aliichukua nondo hiyo na kuichimbia kwenye nguo zake.
Shebo akamfuata tena na kumshika nywele ili amuinue, Azra akajitepetesha na kuinuka, kumbe ilikuwa ni janja yake, Azra baada ya kuinuka juu, kabla Shebo hajamuongezea ngumi za usoni, Azra alichomoa kile chuma na kumpachika Shebo katikati ya kifua.
Shebo alilia kama hayawani akipepesuka kutokana na maumivu!