Mwandishi wa Makala – 14
ILIPOISHIA...
Nikaliona jina la Vailet Shirima kwenye kioo cha simu yangu. Huyu alikuwa ni binti mrembo ambaye alikuwa akiishi maeneo ya jirani nilipoishi na nilitokea kumpenda sana kutoka kwenye moyo wangu, ila sikujua kwanini nilikuwa naogopa kumweleza ukweli kuwa nilimpenda.
Nilishangaa sana kwa kuwa mimi na Vailet hatukuwa na mazoea ya kupigiana simu ingawa tulipeana namba za simu, hivyo nilipoona jina lake jasho jepesi likaanza kunitoka na mapigo ya moyo wangu yakaanza kwenda mbio isivyo kawaida. Sikujua kwanini hali ile ilikuwa inanitokea!
Endelea…
Nikajiuliza tena na tena, Vailet anataka nini kutoka kwangu saa hizi? Hata hivyo, kabla sijaipokea ile simu ikakatika tena na tukio lile likautowesha kabisa usingizi wangu kichwani badala yake nikabaki nikiikodolea macho ile simu kama vile nimeshika bomu la kutupa kwa mkono lililokuwa limetelekezwa na magaidi wa kundi la al-Shabab ndani ya ofisi yangu na wakati wowote lilitaka kunilipukia.
Akili yangu taratibu ikazama kwenye tafakuri nzito huku nikianza kuwaza, ni vipi Vailet anipigie simu usiku ule, alikuwa na shida gani kiasi cha kupiga simu usiku wa manane!
Kitambo kirefu cha ukimya kikapita, nikaacha kumfikiria Vailet na kukumbuka kuhusu ndoto niliyoiota ya mgeni wa ajabu aliyekuja kunitembelea ndani ya studio usiku huo. Ni ndoto ya ajabu sana! Ili kujiridhisha kuwa ile ilikuwa ni ndoto tu nikatazama pale chini ilipokuwa imeanguka ile pete. Sikuoina!
Haraka sana nikavuta droo yangu na kupeleka mkono wangu kupapasa, nikagusa kiti mfano wa pete na kuitoa ile pete ya dhahabu iliyokuwa na jiwe la zambarau ambayo niliinunua kwenye duka la vitu vya kale huko Musoma.
Niliitazama kwa makini ile pete huku nikistaajabu sana, nilijiuliza kama inawezekana ilikuwa na nguvu fulani kama ile ndoto niliyoota usiku ule, muda huohuo koo langu likakauka ghafla na nywele zangu zikanisimama kichwani kwa hofu.
Nikiwa bado naitazama ile pete kwa hofu nilianza kukata tama, mara ile simu ikaanza kuita tena mle ndani. Sikutaka ile simu iendelee kuita zaidi hivyo haraka nikaipokea na kuiweka sikioni huku nikiipa akili yangu utulivu wa hali ya juu.
Sauti ya Vailet akiongea kwa wasiwasi ikasikika upande wa pili wa ile simu. Kitendo cha kuisikia sauti adimu ya mrembo yule kikanifanya nimeze funda kubwa la mate kuutuliza mtima wangu huku nikianza kuhisi jambo lisilo la kawaida.
“Max, ni wewe?” sauti ya Vailet iliuliza kwa wasiwasi.
“Ndiyo, ni mimi! Kwani kuna tatizo lolote?” nilijibu na kumtupia swali Vailet. Lakini kabla hajajibu nilimtupia swali jingine tena. “Vipi, mbona umepiga simu usiku wote huu, kuna nini?”
Vailet hakujibu badala yake aliendelea kubaki kimya. Nilihisi alikuwa analia upande wa pili wa simu ila hakutaka nijue kama analia, na pia hakuamini kama ni mimi Max, kama alivyozoea kuniita kwa kifupi, ndie nilikuwa naongea naye kwenye simu.
“Vai?” niliita kwa wasiwasi baada ya kuona kimya kimezidi.
“Max, ni wewe kweli?” Vailet aliuliza tena kwa sauti ya wasiwasi.
“Ni mimi, kwani vipi mbona sikuelewi!?” Nilishindwa kuelewa ni kwanini alikuwa akiniuliza swali lile lile usiku huo, na kwanini anipigie simu usiku wa manane kuulizia kama nilikuwa mimi kweli! Nikahisi kuna jambo lilikuwa limemchanganya Vailet na muda huo hakuwa katika hali ya kawaida.
“Nimeota ndoto mbaya sana, nimeota…” sauti ya Vailet ilikuwa imejaa wasiwasi, alionekana kama aliyekuwa analia.
“Umeota nini?” nilimuuliza Vailet huku nikikodoa macho yangu kutazama ndani ya studio yangu. Sasa akili yangu ilikuwa inafanya kazi haraka.
Vailet aliniambia kwa sauti yenye mtetemo wa hofu kuwa alikuwa ameona watu wawili wa ajabu sana ambao hajawahi kuwaona maishani mwake waliokuwa katika maumbo ya kutisha na kuchekesha sana wakiingia ndani ya nyumba yangu kwa namna ya ajabu.
Watu hao walikuwa ni mke na mume na walikuja kudai pete yao ya dhahabu yenye jiwe la zambarau ambayo walisema nilikuwa nimeiiba kutoka kwao. Mimi nikawa mbishi na sikutaka kuwapa, nikataka kukimbia lakini nilishindwa kwa sababu walikuwa wamesimama kwenye mlango wakizuia nisiweze kutoka.
Vailet aliendelea kuniambia kuwa baadaye aliniona nikichomoka kama mkizi na kukimbilia kwenye chumba kingine cha ofisi na kujificha chini ya meza lakini wale viumbe waliniona na kunikamata. Nilitaka kulia lakini nikashindwa.
Akawashuhudia wale viumbe wakinikamata kwa nguvu na kunilaza chini, wakanifunga kamba madhubuti. Kisha yule mwanaume alinijia mbele yangu akiwa kashika kisu kikali sana na yule mwanamke akiwa na chombo cha kukingia damu.
Huku akishindwa kuficha kilio chake, Vailet alisema huku akilia kilio cha kwikwi kuwa yule mwanaume alikiweka kisu chake sambamba na shingo wakati yule mwanamke akipiga vigelegele kwa furaha ya kupata mlo. Wakaanza kuhesabu kwa sauti ya pamoja: “Moja, mbili, ta…”
Kabla hawajamalizia na kutimiza azma yao Vailet akapiga kelele na kuwashtua sana wale viumbe wa ajabu. Wakataharuki na kudondosha kisu, kisha wakakimbia.
Muda huohuo Vailet akaamka kutoka usingizini huku jasho likimtoka sana, alijaribu kutafakari juu ya ndoto hiyo lakini hakupata jibu, akaamua anipigie simu kunitahadharisha kuwa kuna jambo baya linaweza kunitokea kwani siku zote amekuwa hadharau ndoto anazoota kuaznia saa saba usiku hadi saa kumi na moja alfajiri, na mara nyingi amekuwa akipata maono kupitia ndoto endapo kuna jambo baya linakuja, ndiyo maana akasukumwa kunipigia simu ule ule.
“Na nilipokuwa napiga sana simu lakini ikawa haipokelewi, hali hiyo ilizidi kunichanganya sana!” Alimaliza kusema Vailet.
“Usihofu, hiyo ni ndoto tu,” nilimtoa shaka Vailet ingawa ndani yangu nilihisi hofu kubwa. Nilifikiria sana alivyoniambia kuhusu pete ya dhahabu yenye jiwe la zambarau jambo ambalo ni kweli ninayo pete ya aina hiyo, isitoshe mimi pia nimeota ndoto kuhusu pete hiyo hiyo, na si hivyo tu, nimewaona watu wawili, Tunu na mpenzi wake ambaye hadi wakati huo nilikuwa sijamjua jina.
Niliitazama kwa makini ile pete ya dhahabu yenye jiwe la zambarau niliyokuwa nimeishika mkononi. Wasiwasi ukazidi, nikaogopa sana na kutamani nifungue kioo cha dirisha niitupe nje.
“Ni ndoto tu, chukua maji kidogo unywe utakuwa sawa,” nilimwambia Vailet huku nikihisi kutetemeka mno, mgongo wangu ukiwa umejiegemeza kwenye kiti..
“Hapana Max, hii siyo ndoto ya kawaida kama ndoto zingine. Nina uhakika lipo jambo baya linataka kukutokea. Nisingependa likutokee jambo baya, nakupenda sana Max na sipendi kukupoteza…” Vailet alisema na kuanza kulia kilio cha kwikwi.
Nilishtuka sana. Vailet hajawahi kuonesha kunijali kiasi kile na wala hajawahi kutamka kama alikuwa ananipenda, na hata pale nilipomuonesha kwa ishara kuwa nilikuwa nampenda lakini bado aliendelea kujikausha na kujifanya haelewi kinachoendelea.
“Vai, naomba nisikilize, tulia, hutakiwi kuhuzunishwa na ndoto. Inawezekana ikawa kweli au isiwe kweli ila cha msingi ni kwamba mimi ni mzima kwa sasa,” nilijitahidi kumliwaza japo ndani yangu nilikuwa natetemeka sana.
Vailet hakunijibu. Aliendela kulia kilio cha kwikwi. Mara akanyamaza na kikazuka kimya cha dakika nzima. Nikaingiwa na wasiwasi.
“Vai?” niliita kwa wasiwasi.
“Nifungulie, nipo hapa nje ya nyumba yako.” Vailet alisema kwenye simu.
Nikashtuka sana na kuitazama saa yangu. Ilikuwa saa tisa na nusu usiku. Nikalamba midomo yangu kuilainisha huku nikikunja sura yangu na kutenegeneza matuta madogo usoni.
“Kuna nini?” niliuliza huku nikishangazwa, mtoto wa kike kuja nyumbani kwangu usiku ule kisa ndoto!
“Nifungulie tafadhali, siwezi tena kulala bila kukuona, ninataka nihakikishe kama kweli ni wewe na umzima.” Alisema Vailet na kunifanya nizidi kushangaa.
Bila hata kuwaza zaidi nilijikuta nikiinuka na kuuendea mlango wa barazani, nikaufungua na kutoka hadi kwenye geti kubwa la uwa wa nyumba yangu, nikachungulia nje kupitia upenyo uliopo kwenye geti dogo, nikamuona Vailet amesimama nje ya nyumba yangu akiwa na wasiwasi.
Kwa sekunde chache nilibaki nimesimama nikiwa nimepigwa butwaa huku nikijiuliza, hivi mtoto wa kike amewezaje kutoka nyumbani kwao katika usiku wa manane na kuja nyumbani kwangu? Nilichungulia tena kuhakikisha kama ni yeye, nikamuona akiwa na hofu akitazama huku na huko. Sikujiuliza mara mbili, nikafungua geti huku nikimtazama kwa makini.
Vailet aliponiona alinirukia na kunikumbatia kwa nguvu huku akilia kwa furaha. Nilishindwa kufanya chochote nikabaki nashangaa. Jambo moja likanijia akilini mwangu: “inawezekana hii nayo ni ndoto tu kama zingine na mara tu ningeamka kutoka usingizini na kukuta kila kitu kikiwa cha kawaida.”
Nikahisi ubaridi mwepesi ukinitambaa mwilini mwangu na kuzifanya nywele zangu kusisimka. Nikabaki hoi nisijue la kufanya!
MWISHO.