Hebo oneni haya mambo jamani, sijui jamii yetu inaelekea wapi? Halafu eti biti wa miaka 19 kidato cha kwanza!
Mwanafunzi afa akitoa mimba ya mwalimu
na Suleiman Abeid na Zuhura Waziri, Shinyanga
MWANAFUNZI mwenye umri wa miaka 19 aliyekuwa akisoma kidato cha Kwanza katika Shule ya Sekondari ya Katente wilayani Bukombe mkoani Shinyanga amekufa baada ya kutoa mimba ya miezi saba ambayo inadaiwa alipachikwa na mwalimu wa shule ya msingi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, amemtaja mwanafunzi aliyekufa kuwa ni Shukuru Edward na kwamba tukio hilo lilitokea Agosti 12, mwaka huu saa 8 usiku wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya serikali wilayani Bukombe.
Kufuatia kifo hicho, Jeshi la Polisi mkoani hapa linawashikilia wazazi wawili wa mwanafunzi huyo waliotajwa kwa majina ya Bw. Edward Shamba (52) na Bi. Anastazia Edward (48) pamoja na Bw. Anthony Edward (34) ambaye ni mwalimu anayedaiwa kumpa mimba hiyo.
Wengine waliokamatwa wakituhumiwa kusaidia utoaji wa mimba hiyo ni Bw. Robert Mashuku Bujilima (36) ambaye ni Daktari, Bw. Julius Maganga (45) mhudumu wa chumba cha maiti katika hospitali ya serikali wilayani Bukombe na Bi. Maria Andrew (26) dada wa marehemu.
Akifafanua, Kamanda Ibrahimu alisema baada ya kubainika kuwa mwanafunzi huyo ana mimba, mtuhumiwa Bw. Anthony akishirikina na Bi. Maria walijaribu kutoa mimba hiyo kwa kutumia dawa za kienyeji lakini ilishindikana na kusababisha kichanga kilichokuwa tumboni kuoza.
Hali hiyo ilimsababishia maumivu makali mwanafunzi huyo ambapo alianza kutokwa usaha katika sehemu za siri, hivyo kulazimika akimbizwe katika hospitali ya serikali Bukombe Agosti 11, mwaka huu baada ya hali kuwa mbaya zaidi.
Hata hivyo baada ya kufikishwa hospitalini hapo, mwalimu Anthony alitumia kadi yake ya Bima ya Afya kumtibia mwanafunzi huyo huku akiwa ameandika jina la uongo katika kadi za wagonjwa.
Ili kuficha ukweli wa kubainika kuwa mgonjwa huyo ni mwanafunzi, aliamua kuandikisha jina la uongo la Catherine Shamba badala ya Shukuru Edward, maarufu kwa jina la Shamba.
Kamanda Ibrahimu alisema akiwa hospitalini hapo, mwalimu Anthony alishirikiana na Daktari Mashuku kutoa kwa siri mimba hiyo lakini hata hivyo mwanafunzi huyo alifariki usiku wa Agosti 12, mwaka huu.
Baada ya kufariki mwanafunzi huyo, Dkt. Mashuku akishirikiana na watuhumiwa wengine walimfanyia upasuaji ambapo walitoa kichanga kilichokuwa tumboni chenye jinsi ya kiume kikiwa na umri wa miezi saba na kwenda kukificha katika jokofu la hospitali hiyo bila kuitaarifu Polisi kwa nia ya kuharibu ushahidi.
Hata hivyo baadhi ya raia wema walitoa taarifa Polisi ambao walifika hospitalini hapo na kukuta tayari mwili wa mwanafunzi huyo umechukuliwa na kupelekwa kijijini kwao Imalagigo kwa ajili ya maandalizi ya mazishi.
Kutokana na hali hiyo Polisi waliwahi katika kijiji hicho kabla ya mazishi na kufanikiwa kuuchukua mwili huo na kuurejesha hospitalini kwa ajili uchunguzi wa kitaalamu.
Wakiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti, walishangaa kukuta mwili wa kichanga ukiwa umefichwa katika moja ya majokofu yaliyokuwa ndani ya chumba hicho na ilipochunguzwa, ilibainika kuwa ndicho kilichotolewa tumboni mwa marehemu.
Kamanda Ibrahimu alisema baada ya uchunguzi wa kitaalamu, mwili wa mwanafunzi pamoja na kichanga chake vilikabidhiwa kwa ndugu wa marehemu kwa ajili ya mazishi.
Alisema katika mahojiano ya awali na mtuhumiwa Bw. Anthony, alikiri kumpa mimba mwanafunzi huyo ambaye sasa ni marehemu na kwamba yeye pamoja na watuhumiwa wenzake wanatarajiwa kufikishwa mahakamani hivi karibuni baada ya uchunguzi kukamilika.
SOURCE: Majira