Mwaka 2022 ulivyowanyima Usingizi Bodi ya Mikopo (HESLB)

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,377
8,121
Achana na watendaji wa Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Eklimu ya Juu (HESLB), kuitwa mbele ya Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, mwaka 2022 unaweza kuwa mwaka uliokuwa na hekaheka nyingi zilizowatoa jasho watendaji wa bodi hiyo.

Moja ya mambo ambayo yaliwapa wakati mgumu watendaji wa bodi ni kilio cha wadau wengi hasa wanafunzi wanaodai kuwapo kwa upendeleo katika utoaji wa mikopo ya elimu ya juu.

Kilio hicho kikaitikiwa na wabunge jijini Dodoma na hatimaye uongozi wa Bunge kuagiza watendaji wake kufika bungeni.

Hata hivyo, awali akionekana kuwa ana dhamira ya kufanyia kazi kilio cha wadau wa mikopo hiyo, Julai 31 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda alitangaza kuunda timu ya wataalam ya kuchunguza uhalali katika utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2017/2018 mpaka 2021/2022 ili kubaini kama kulikuwa na upendeleo kwa watu wasiokuwa na sifa.

Timu hiyo ya wataalamu wa mifumo waliobobea katika sayansi ya kompyuta na takwimu inaongozwa na Profesa Allan Mushi ambaye ni mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe Morogoro, Idd Makame kutoka Zanzibar na Dk Martin Chegeni.

Waziri alifikia uamuzi huo baada ya kupata malalamiko ya wanafunzi mbalimbali nchini ambao wamekuwa wakiyatoa kuhusu upendeleo wa utoaji mikopo kwa kupata mikopo kwa wanafunzi wasio na sifa huku wale wenye sifa stahiki wakikosa.

“Kwenye hili tunakaribisha watu watoe taarifa kwa sababu kama kuna mtoto wa Mkenda uliyesoma naye utakuwa unamjua baba yake ni nani na uwezo wake, halafu wewe unaona mtu huyo amepewa mkopo toa taarifa.Mtu yeyote ambaye ana wasiwasi na utoaji wa mikopo tunamkaribisha ili aweze kuisaidia tume kufanya kazi yake kwa kuwa na taarifa zenye usahihi wa hali ya juu kutoka kwa wanachi husika,” alisema Profesa Mkenda wakati akitangaza kuhusu timu hiyo.

Pamoja na mambo mengine Profesa Mkenda alisema timu hiyo itaangalia vigezo vilivyoainishwa ili kuona kama kuna taarifa zingine za ziada zinaweza kutumika katika utoaji wa mikopo ili fedha zinazotolewa na Serikali zikopeshwe kwa haki.

Maoni ya wadau

Akizungumzia hatua ya waziri kuunda kamati, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dk Faraja Kristomus anasema uamuzi ulikuwa sahihi, kwani ungemsaidia Waziri kuujua ukweli zaidi wa yale yanayozungumzwa kuliko kutegemea zaidi maneno ya kusikia mtandaoni.

Anasema waziri hakufanya uamuzi wa haraka kushughulikia malalamiko hayo kwa kuwa angeweza kuonekana amefanya uamuzi wa kukurupuka na baadaye akatuhumiwa kuwa na maslahi binafsi katika maamuzi hayo.

“Hata hivyo, kilichotarajiwa na wengi ni kuona hadidu za rejea za tume hiyo. Ili tuweze kuona mabadiliko kwenye bodi ya mikopo tulihitaji sana kuona hadidu za rejea kwani matokeo ya uchunguzi huo ungetusaidia kubaini kiini cha tatizo na namna ya kutatua.

“Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ina changamoto kubwa nne ambazo nyingine ni za ndani na nyingine zinatokana na Serikali. Kwanza ni mfumo wa ukusanyaji wa madeni una changamoto kwani kinachokusanywa inaonekana ni kidogo kutokana na wahitimu wengi kutokuwa na ajira rasmi na hawana mwitikio wa kurejesha mkopo,”.

Dk Kristomus anasema changamoto nyingine ni hicho kiwango kidogo kinachokusanywa hakiendi kuongeza mfuko mkuu wa bodi kwa ajili ya kuongeza wigo wa kukopesha wanafunzi na badala yake inaonekana sehemu kubwa ya fedha inatumika kuendesha shughuli za ndani ya bodi.

Mbali na hilo, anabainisha kuwa kuna changamoto katika mfumo wa kuwabaini wahitaji wa mkopo na namna ya kuwapanga kwenye makundi.

“Malalamiko mengi ni kuwa wanafunzi wengi ambao ni wahitaji halisi wa mkopo, hawapewi mkopo na wanasoma kwa shida sana vyuoni, na wengine kulazimika kuacha masomo vyuoni,” anaeleza.

Anaongeza; ‘’Pia Serikali haitoi kiasi cha kutosha kwa kadri ya bajeti na mahitaji halisi ya wanafunzi. Serikali imekuwa ikitamani Bodi ikusanye zaidi madeni lakini wakati huohuo waliowahi kunufaika na mikopo hiyo wanashindwa kurejesha ili wengine wasome. Matokeo yake tunaweza kuilaumu Bodi ya Mikopo kumbe matatizo yaliyopo ni ya kisiasa zaidi kuliko ya kiutendaji.’’

Hilo la siasa linaelezwa pia na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, (Udom) Dk Paul Loisulie, anayesema utashi wa kisiasa unahitajika katika kuhakikisha bodi inafanya kazi yake kwa ufanisi licha ya kuwepo uhitaji mkubwa wa kuundwa kwa timu hiyo kushughulikia malalamiko yaliyopo.

“Hatua ya kuunda kamati ni sahihi kwa sababu suala la mikopo limekuwa na malalamiko ya mara kwa mara, timu hii itawezesha kupata taarifa ya uchunguzi dhidi ya malalamiko yanayotolewa ili kuboresha mfumo mzima wa utoaji mikopo.

Ripoti ndiyo itakuwa zana ya kufanya maamuzi lakini inaweza isiwe na maana endapo hakutakuwa na utashi wa kisiasa katika usimamizi wake. Utashi wa kisiasa ndiyo utakaosaidia hata kwenye kuongeza bajeti ya elimu ya juu ili kuhakikisha wote wanaostahili kupata mikopo hii wanaipata bila kuwepo aina yoyote ya urasimu,”anasema Dk Loisulie.

MWANANCHI
 
Back
Top Bottom