Muulize Mobutu utamu wa Kamanyola "Cheza bila jasho"

Juma Wage

Member
Sep 8, 2023
60
201
WAPENZI wa Dansi katika miaka ya 1970 mpaka 1990, hawatosita kusimulia burudani tamu iliyokuwa ikiporomoshwa kutoka bendi ya MAQUIS du ZAIRE.

Watoto wa mjini katika kumbi za starehe walipagawa zaidi pale mwanamuziki wa bendi hiyo Mwema Mudjanga "Mzee chekecha" alipowakoga kwa kibwagizo "Cheza Kamanyola.....Kamanyola bila jasho.....cheza ukijidai…."

Hakika viti havikukalika kwani mtindo wa Kamanyola kama hutocheza kwa kiuno, basi mkono utautikisa, miguu ukipiga “step” moja mbele mwingine nyuma huku shingo ikisindikiza mdundo.

KAMANYOLA ni nini?

KAMANYOLA ni Kitongoji kilichopo Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) mpakani mwa Rwanda na Burundi.

Eneo hilo ndilo liliweka historia ndani ya moyo wa aliyekuwa Rais wa Zaire wakati huo ikijulikana, Mobutu Sese Seko Kuku Ngbendu wa Za Banga, wakati huo akiwa angali kijana akilitumikia jeshi la mkoloni (Ubeligiji).

Kwa mujibu wa Mobutu anasimulia kuwa akiwa kwenye operesheni ya kijeshi, risasi ilifyatuliwa upande wake lakini kwa kustaajabu “ilidunda” kifuani mwake. Na tangu siku hiyo alivutiwa kutumia jina la Kamanyola ikiwa ni kumbukizi ya tukio hilo.

Mobutu alipenda kujinasibu kwa jina la “Mobutu Sese Seko Kuku Ngbendu wa Za Banga" akimaanisha “Shujaa mwenye enzi aliyeshindikana.”

Miaka ya mwanzo baada ya kushika madaraka kwa njia ya mapinduzi, Mobutu aliwaalika waandishi wa habari wa kimataifa kumhoji. Wakati akiendelea kuhojiwa aliingia kwenye bwawa la kuogelea "Swimming pool" akipiga mbizi huku akijibu maswali mpaka alipomaliza kuhojiwa.

Mwaka 1974 wakati wa michuano ya kombe la Dunia yaliyofanyika Ujerumani Magharibi, Mobutu aliwakusanya waganga na wachawi nguli kuwapeleka wakasaidie timu yao ya soka.

Cha kustaajabisha, haikufaa kafara ya nazi, chale wala dawa walizooga kwani Zaire ilichakazwa bao tisa kwa nunge na timu ya taifa ya Yugoslavia.

Mobutu alikibatiza jina la KAMANYOLA kikosi kilichomlinda na pale aliponunua meli yake ya kifahari nayo aliita kwa jina hilo.

KAMANYOLA ilimstarehesha Mobutu kiasi cha kusahau kulipa mshahara wafanyakazi wa serikali na kuibuka msemo maarufu usemao "Wafanyakazi wa serikali wanaigiza kama wanaitumikia serikali ya Mobutu, wakati ambao serikali ya Mobutu ikiigiza kuwalipa mishahara wafanyakazi."

Hiyo ndiyo ladha ya KAMANYOLA, cheza bila jasho……cheza kwa step…..utamu wa rhumba lake waulize wazee wa sasa au vijana wa wazamani.

Ndimi Juma Wage
Dodoma
Septemba 10, 2023.
 
Back
Top Bottom