Mtutura: Kilio cha Uhaba wa Mbolea ya Ruzuku Nchini; Hatua za Serikali Haziondoi Tatizo

ACT Wazalendo

JF-Expert Member
May 5, 2014
610
1,540
Hali ya upatikanaji wa mbolea kwa wakulima nchini imekuwa ikilalamikiwa kwa takribani miezi minne (4) kuanzia mwezi Agosti mwaka 2022 tangu kuanza kutumika kwa mfumo wa ruzuku kwenye mbolea. Serikali ilitangaza uamuzi wa kutoa ruzuku kwenye mbolea na pembejeo kwa wakulima kufuatiwa na msukumo wa wadau kutokana na kupaa kwa bei za mbolea na pembejeo kwa msimu wa mwaka 2021/22.

Itakumbukwa, wastani wa bei za mbolea kwa msimu uliopita (2021/22) ulikuwa juu sana nchini, kwa mfano kwa baadhi mbolea kwa kilogramu hamsini (50Kgs) ziliuzwa kama ifuatavyo; UREA TShs. 110000 hadi 13,0000 sawa na 120% hadi 136% kutoka msimu wa mwaka 2021. Huku bei ya mbolea ya CAN (50Kgs) TShs. 84,000- 125,000 kutoka kwenye bei ya shilingi 50,000 mwaka 2021, ikiwa ni ongezeko la Tsh 34,000 hadi 75,000 sawa na 68% hadi 150% kwa baadhi ya maeneo. Mbolea ya DAP ilikuwa TShs.118,000 hadi 150,000, kutoka bei ya sh. 62,000 sawa na ongezeko la 90% hadi 142%. Hali ya bei ya mbolea na mbejeo za kilimo ilikuwa mbaya sana karibia kila aina ya mbolea.

Sisi ACT Wazalendo tulitoa mapendekezo kadhaa ya kukabiliana na hali ya kupanda kwa bei za pembejeo ikiwemo kuweka ruzuku ili kushusha bei kwa wakulima wetu. Uamuzi wa Serikali kuweka ruzuku kwenye mbolea kwetu ulikuwa muhimu sana na ulibeba matumaini makubwa sana kwa wakulima kwa matarajio ya kupunguziwa gharama (zilizokuwa zinaendelea kupaa) na kuhakikishiwa urahisi wa upatikanaji.

Hata hivyo, utekelezaji wa uamuzi huu umeibua malalamiko, vilio na kuvunja matumaini ya wakulima kila kona ya Nchi. Mathalani hadi sasa msimu wa kupanda umefika lakini mikoa kadhaa imekumbwa na uhaba mkubwa wa mbolea, hali inayotishia uzalishaji kwa msimu huu.

Hali halisi ya upatikanaji wa mbolea
ACT Wazalendo tumefuatilia hali ya upatikanaji na usambazaji wa mbolea kwenye mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya, Ruvuma, Rukwa, Songwe, Tabora, Kigoma, Katavi na maeneo ya Lindi na Mtwara. Hivi karibuni, tumeona ziara ya Waziri wa Kilimo Ndugu Hussein Bashe katika mikoa ya Njombe, Iringa, Mbeya, Songwe.

Tulifuatilia neno kwa neno, hotuba kwa hotuba na hatua alizozichukua, hatua zake hazijagusa kiini cha tatizo. Tunajiuliza Waziri anapataje kigugumizi kushughulikia hatima ya wakulima na Watanzania? Ndio maana bado tunaona changamoto kadhaa zimebaki kama zilivyo. Changamoto zinazowatesa wakulima ni zifuatazo;

1.Changamoto za kiusajili na ucheleweshwaji wa namba, usajili unafanyika mjini hivyo wakulima wanasafiri umbali mrefu lakini inawachukua zaidi ya siku tatu hadi tano kupata namba ya usajili ambayo inatumika kuchukulia mbolea ya ruzuku hali inaathiri pia shughuli za kiuzalishaji shambani.

Aidha, msimu wa kupanda umefika, wakulima wanatafuta mbolea lakini wanashindwa kuzipata, wengine katika baadhi ya mikoa hawajapata namba za usajili licha ya kuwa wameshajisajili.

2. Wasambazaji ni wachache sana ukilinganisha na uhitaji, mfano eneo la Lindi na Mtwara msambazaji ni mmoja aliyeko mtwara mjini, Mkoa wa Tabora, kigoma na Ruvuma ni mojawapo ya mikoa yenye wasambazaji wachache sana hivyo wakulima wanajikuta wanapaswa kusafiri umbali mrefu kufuata mbolea.

3. Baadhi ya Mawakala waliosajiliwa kwenye maeneo mbalimbali kukosa uwezo wa kusambaza (kimtaji) hadi ngazi ya chini.

4. Kuwepo kwa wasambazaji ambao wameshikilia mbolea bila kufikisha kwa mawakala na wakulima ambao ndio wahitaji.

5. Serikali kutowafuatilia kwa karibu na kuchelewesha malipo ya madai ya wasambazaji wakubwa (Makampuni) jambo linalopelekea kupunguza uwezo wa usambazaji kulinga na mahitaji ya wakulima.

Sambamba na malalamiko haya uchambuzi wetu ACT Wazalendo tumegundua kiini cha tatizo sio mfumo pekee. Mfumo wa sasa wa ruzuku unakosa Usimamizi na ufuatiliaji wa karibu kiasi cha baadhi ya Wafanyabiashara waagizaji na wasambazaji kuweka mgomo baridi unaopelekea kuwepo kwa shida ya upatikanaji na usambazaji wa mbolea. Pia, usajili wa wakulima kutumika kama vile ndio kigezo cha kupata mbolea ya ruzuku badala ya kuwa na mfumo wa kutambua mahitaji halisi.

Kutokana na hali mbaya ya upatikanaji wa mbolea inayotishia uzalishaji na uhakika wa chakula kwa nchi yetu. ACT Wazalendo tunaitaka Serikali ichukue hatua zifuatazo kunusuru kilimo na wakulima;

i) Tunatoa rai kwa Serikali kuingilia katika mfumo wa uagizaji na usambaziji kwa kuliwezesha kibajeti Kampuni ya taifa ya Mbolea (TFC) ili kushiriki kikamilifu kwenye ununuzi wa mbolea (Uagizaji nje) na usambazaji wake kwenda ngazi za chini kwaajili ya kuongeza uwezo wa usambazaji wa mbolea unaotokana na kulegalega kwa waagizaji na wasambazaji binafsi.

ii) Serikali ikishatekeleza pendekezo la kwanza, ihakikishe inaweka mfumo mzima wa usambazaji na kuhakikisha mbolea ya kutosha inafika kwa wakati kwa wakulima nchi nzima. Hili litawezekana iwapo tu Kampuni ya Mbolea ya Taifa itakuwa na uwezo wa kuleta ushindani katika Soko.

iii) Kama Serikali haiwezi kuimarisha Kampuni ya Taifa ya Mbolea (TFC) kimtaji na kimuundo (kuboresha Bodi ya Wakurugenzi yenye watu wenye weledi mkubwa na wanaojua Soko la Mbolea) basi Serikali irejeshe mfumo wa uagizaji wa pamoja wa mbolea (Bulk Procurement System) uliositishwa tangu mwaka 2021. Mfumo huu utashusha gharama za uagizaji na kudhibiti ubora wa mbolea zinazoingizwa.

iv) Aidha, kwa hatua za haraka tunatoa rai kwa Serikali kulipa kwa wakati madai ya kampuni zinazosambaza mbolea ili kuepusha ucheleweshaji unaotokana na malimbikizo ya muda mrefu ya madeni yanayopunza uwezo wa kampuni kutoa huduma hizo.

v) Serikali kuvijengea uwezo na kutoa jukumu la usambazaji wa Mbolea vyama vya ushirika ili kurahisisha upatikanaji wa haraka wa mbolea ya ruzuku vijijini.

Katika hatua za muda mrefu tunaitaka Serikali kuchukua hatua zifuatazo;

vi) Kuondoa utegemezi wa mbolea kutoka nje, kwa kuweka mazingira rafiki kwa uwekezaji ili watu waweze kujenga viwanda vya kuzalisha mbolea nchini na kuimarisha uzalishaji kwa viwanda vilivyopo.

vii) Aidha, tunatoa rai kwa Serikali kuweka mkazo wa kuimarisha mifumo ya matumizi ya mbolea mbadala (mbolea zisizo na kemikali) kutoka kwa wakulima wenyewe.

Hitimisho
ACT Wazalendo inatambua jitihada zinazofanywa na Serikali lakini bado hazigusi kiini cha tatizo lenyewe. Ni dhahiri kuwa Serikali inarudia tena makosa iliyofanya huko nyuma. Makosa ya msimu uliopita umepandisha gharama za vyakula nchini kutokana na kushuka kwa uzalishaji.

Tunaendelea kusisitiza kuwa Serikali ni lazima itimize wajibu wake wa kulinda maisha na hali za wananchi kwa kuhakikisha hakuna uhaba wa mbolea kwa wakulima, kuhakikisha kuwa mbolea husika zinapatikana katika bei ambazo watanzania wanazimudu, na zinapatikana kwa wakati.


Imetolewa na;
Ndg. Mtutura Abdallah Mtutura
Twitter: @MtuturaAbdallah
Waziri Kivuli wa Kilimo, Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi
ACT Wazalendo.
19 Januari, 2023
 
Back
Top Bottom