Msemaji Mkuu wa Serikali anazungumza kutoka Bandari Kavu ya Kwala, Mkoani Pwani, Machi 16, 2025

Msemaji Mkuu wa Serikali anazungumza kutoka Bandari Kavu ya Kwala, Mkoani Pwani, Machi 16, 2025

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Joined
Apr 18, 2017
Posts
4,783
Reaction score
14,975

Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa anazungumza na Waandishi wa Habari kutoka Bandari Kavu ya Kwala, Mkoani Pwani

Akizungumzia miradi iliyosajiliwa kati ya mwaka 2021 Machi hadi Februari 2025

"Katika kipindi cha miaka minne ya Rais Samia Suluhu Hassan, kati ya mwaka 2021 Machi hadi Februari 2025, tumefanya uwekezaji wa miradi 2099 ambayo imesajiliwa kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).Miradi hii imetuletea jumla ya ajira 539488 ambazo zimezalishwa kutokana na uwekezaji huu, sasa mitaji iliyowekezwa ndani ya nchi ina thamani ya Dola za Marekani bilioni 25.098 ambazo ni sawa na Shilingi za Kitanzania trilioni 69 ambazo zimewekezwa kwa kipindi hiki. Lakini miradi mipya ambayo imeanzishwa..tumeanzisha miradi mipya 1982, miradi ile 2099 ya kwanza niliyokutajieni ni miradi tuliyosajili. "

"Katika miradi mipya kuna miradi ya ubia, ambayo Watanzania wanashirikiana na wawekezaji kutoka maeneo mbalimbali duniani, tumeanzisha miradi ya ubia 476 lakini miradi iliyohusisha upanuzi wa maeneo na yenyewe ipo karibu 117, lakini pia miradi ya Watanzania ni 719"


Akizungumzia uwekezaji katika sekta ya viwanda

"Sekta ya viwanda ndiyo sekta inayoongoza kwa uwekezaji nchini, na katika kipindi cha kuanzia mwaka 2021 hadi Februari 2025, jumla ya miradi ya viwanda 951 imesajiliwa, miradi hii inatarajiwa kuleta ajira 124339 na kuwekeza mitaji ya Dola za Kimarekani bilioni 10.5 sawa na Shilingi trilioni 27, huo ndio uwekezaji kwenye viwanda."

"Mitaji ya viwanda imechukua asilimia 42 ya mitaji yote ya sekta iliyosajiliwa katika kipindi hicho na kufanya miradi ya viwanda kuwa sekta inayoongoza katika sekta zote za miradi, mitaji na ajira. Mfahamu kuwa eneo hili la viwanda , ukuaji wake ukilinganisha na miaka iliyopita hivi sasa tumeona umekua sana, tafsiri yake ni kwamba, pamoja na mapato ambayo tunayapata lakini tunakwenda kufanya kazi kubwa ya kuiondoa nchi yetu katika utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi. Tunapoangalia ukuaji wa uchumi wa nchi na kulinda uchumi wetu, ni lazima tupunguze kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi, sisi ndio tuzalishe kupeleka nje ya nchi"

"Tuliangalie eneo hili la uwekezaji la Kwala ambapo kuna kongani ya viwanda ya Sinotan. Kongani hii ni eneo mojawapo la miradi ya mkakati lililopo hapa Kwala mkoa wa Pwani, ukubwa wake ni ekari 2500, eneo hili lina mtaji wa uwekezaji wa Dola za Kimarekani milioni 327 sawa na Shilingi za Kitanzania bilioni 882. Mradi huu utakapokamilika utakuwa na viwanda vikubwa 200 na viwanda vidogo 300. Tutakuwa na viwanda vya kusindika chakula, vya kutengeneza vifaa, vya dawa, ujenzi, usindikaji wa viatu na nguo na viwanda vya kemikali. Kongani linatarajiwa kutoa ajira za moja kwa moja zaidi ya laki 1 na ajira zisizo za moja kwa moja laki 5."

"Tupo kwenye awamu ya kwanza, lakini jumla ya awamu zote zitakuwa 5, ujenzi wa awamu ya kwanza ulioanza mwezi Mei 2022 upo katika hatua za mwisho ambapo mpaka sasa kuna viwanda vitatu ambavyo tayari vinazalisha, na viwanda vingine vitatu vikiwa katika hatua za mwisho za kufunga mitambo huku viwanda vingine vinne vikitarajiwa kuanza ufungaji wa mitambo ifikapo mwishoni mwa Aprili. Eneo hili litakuwa na uwezo wa kuzalisha bidhaa zenye thamani ya Dola za Kimarekani bilioni 6 sawa na Shilingi trilioni 16 kwa mwaka. Serikali itakuwa ikikusanya kutoka kwenye kongani hii moja kiasi cha kodi cha Shilingi zaidi ya trilioni 1.2."


===============================

Ndugu wanahabari, naomba nitumie fursa hii kuwakaribisha kwenye mkutano wa Msemaji Mkuu wa Serikali na vyombo vya habari leo tarehe 16 Machi, 2025. Mkutano huu tumeamua kuufanyia hapa katika mradi wetu wa kimkakati wa Bandari Bandari Kavu ya Kwala katika eneo hili la Vigwaza Wilayani Kibaha-Mkoa wa Pwani ili muweze kuona utekelezaji wa Serikali. Pia tumetembelea eneo la hifadhi ya viwanda la Sino -Tan ambalo lengo la kuwaonesha Watanzania kupitia vyombo vya habari, maendeleo ya makubwa ya mradi huu na utekelezaji wa miradi mingine ya Serikali ndani ya kipindi cha miaka minne (4) ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kipekee naomba nitumie fursa hii kuwashukuru sana ninyi Wanahabari wenzangu na vyombo vyote vya habari nchini kwa kuendelea kujitokeza kwa wingi katika mikutano ya Msemaji Mkuu wa Serikali inayoendelea Jijini Dodoma na mikutano hii ambayo tumeamua kuihamishia uwandani kwenye maeneo inakotekelezwa miradi. Aidha, natumia nafasi hii kipekee kumpongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake na kazi kubwa anayoifanya ya kuwaletea maendeleo Watanzania; Sote ni mashuhuda wa miradi mikubwa iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa kwa lengo la kuboresha huduma na kuwaletea maendeleo Watanzania.

Ndugu wanahabari, Naomba nitumie fursa hii pia kuwashukuru viongozi wa Wizara ya Uchukuzi (Wakiongozwa na Mheshimiwa Waziri Prof. Makame Mbarawa Mnyaa), Kituo cha Uwekezaji Tanzania – TIC (Wakiongozwa na Mtendaji Mkuu Gilead Teri) na Mkoa wa Pwani (Wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa Bw. Aboubakar Kunenge) kwa kutupa fursa ya kufanyia mkutano wetu katika eneo hili la mradi. Aidha, nawapongeza Wahandisi na watalaam wote wanaosimamia utekelezaji wa mradi huu kwa niaba ya Watanzania.

Baada ya utangulizi huu naomba nieleze kuwa mkutano wetu wa leo utajikita katika kuzungumzia masuala mbalimbali ya maendeleo yaliyotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita katika maeneo yafuatayo;-

Shughuli za uwekezaji katika sekta ya viwanda na mafanikio yaliyopatikana kutokana na uwekezaji huo katika kipindi cha miaka minne.

⁠Maendeleo ya ujenzi wa eneo la Bandari Kavu ya Kwala, kongani ya viwanda, Bandari Kavu (ICDs) na maendeleo mengine,

⁠Matokeo ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake na Duniani 2025 (mambo makubwa yaliyojili),

Mradi wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe na sura ya Kitaifa ya utekelezaji wa miradi mingine mikubwa ya maji nchini,

Maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Dar - Chalinze – Morogoro,

Utekelezaji wa Bajeti ya Mkoa wa Pwani kwa mwaka 2024/25 na matarajio ya bajeti ya mwaka 2025/26, na miradi mikubwa iliyotekelezwa mwaka 2024/25 thamani yake na ufanisi wake.

Huduma ya utoaji wa vitambulisho vya kidigitali kwa Waandishi wa Habari (Digital Press Cards)

UWEKEZAJI KATIKA SEKTA YA VIWANDA NA MAFANIKIO YALIYOPATIKANA



Bila shaka nyote mmejionea katika ziara yetu ya leo, tulipoanza asubuhi pale Kibaha katika eneo la Viwanda. Kwa kifupi Serikali iliamua eneo hili liwe mahususi kwa ajili ya uwekezaji katika viwanda, tena viwanda vya Kimkakati. Na mpango ni kwamba tuwe na maeneo ambayo mwekezaji akija na anahitaji eneo haraka tuwe na mahali pa kumwambia weka kiwanda hapa na makubaliano yetu na wewe yatakuwa hivi.



SASA uwekezaji katika viwanda ni sehemu muhimu na kubwa iliyoleta matokeo chanya katika kampeni ya nchini yetu ya kuleta mageuzi ya kiuchumi. Na kwa ujumla wake katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan miradi ya uwekezaji na mitaji imekuwa na ongezeko kubwa nchini. Pia miradi inayomilikiwa na Watanzania imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka.



Ndugu zangu waandishi wa habari na ndugu Watanzania mnaonisikiliza HAYA SIO MANENO MATUPU, naomba nitoe takwimu chache za kuthibitisha ongezeko kubwa la uwekezaji nchini mwetu. Katika kipindi cha kuanzia Machi, 2021 hadi Februari, 2025 Tanzania imeshuhudia idadi kubwa ya usajili wa miradi mbalimbali katika sekta zote kama ifuatavyo;-



Jumla ya miradi ya uwekezaji 2,099 imesajiliwa kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC),

Jumla ya ajira 539,488 zimezalishwa,

Mitaji iliyowekezwa ndani ya nchi ina thamani ya Dola za Marekani Bilioni 25.098 (Sawa na takribani shilingi Trilioni 67),

Jumla ya miradi mipya 1,982 imeanzishwa,

Miradi ya ubia imefikia 476

Miradi ya iliyohusisha upanuzi wa maeneo ya uwekezaji ni 117

Miradi ya Watanzania ni 719

Miradi ya wageni ni 904





SEKTA YA VIWANDA

Ndugu Wanahabari;
Sekta ya viwanda ndiyo sekta inayoongoza kwa uwekezaji nchini. Katika kipindi cha kuanzia mwaka 2021 hadi kufikia Februari, 2025 jumla ya miradi ya viwanda 951 imesajiliwa. Miradi hii inatarajiwa kuleta ajira 124,339 na kuwekeza mitaji ya Dola za Marekani Bilioni 10.5 (Sawa na takribani shilingi Trilioni 27).



Miradi hii ya viwanda inachukua asilimia 45 ya miradi ya sekta zote iliyosajiliwa katika mwaka 2021 hadi 2025.

Kwa upande wa mitaji, miradi ya viwanda imechukua asilimia 42 ya mitaji ya sekta zote iliyosajiliwa katika kipindi hicho na kufanya miradi ya viwanda kuwa ndiyo sekta inayoongoza sekta zote kwa idadi ya miradi, mitaji na ajira.



Mchanganuo ufuatao unaonesha miradi ya viwandani iliyosajiliwa katika kipindi cha miaka 4 kuanzia mwaka 2021 hadi Februari 2025.



Jumla ya miradi 951 ya viwandani imesajiliwa,

Miradi mipya ya viwandani 917 imeanzishwa

Miradi 36 imehusu upanuzi wa viwanda,

Miradi 244 ya viwanda ni ya Watanzania, imesajiliwa,

Miradi ya viwandani ya wageni 501 imesajiliwa

Miradi ya ubia 206

Ajira za viwandani 124,339

Mtaji uliowekwa una thamani ya Dola za Marekani milioni 10.512.

Jambo kubwa na zuri ni kwamba takwimu zinatuonesha idadi ya viwanda imekuwa ikiongezeka kwa kasi kubwa mwaka hadi mwaka, jambo ambalo linathibitisha kuwa safari ya Tanzania ya Viwanda inakwenda vizuri na hatua ambazo Serikali yetu ikiongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inakwenda vizuri na kwa mafanikio makubwa.



Naomba nithibitishe ongezeko hili kwa takwimu kama ifuatavyo

Mwaka 2021 – Miradi 135, ajira zilizotolewa ni 20,865

Mwaka 2022 - Miradi 141, ajira zilizotolewa ni 23,341

Mwaka 2023 – Miradi 208, ajira zilizotolewa ni 26,563

Mwaka 2024 – Miradi 415, ajira zilizotolewa ni 45,883

Aidha, pamoja na takwimu hizo, katika kipindi kifupi cha kuanzia mwezi Januari hadi Februari, 2025 (miezi miwili) Sekta ya viwanda imetengeneza miradi ya viwanda 52 ambapo kati ya hiyo miradi ya Watanzania ni 14, na ya wageni ni 33. Aidha, ajira zilizotolewa ndani ya kipindi cha miezi miwili ni 7,687.



MIRADI YA UWEKEZAJI KATIKA MKOA WA PWANI

Ndugu Wanahabari;
Mkoa wa Pwani unashika nafasi ya pili katika kuvutia uwekezaji nchini ukitanguliwa na mkoa wa Dar es Salaam. Katika kipindi cha takribani miaka minne kuanzia mwaka 2021 hadi Feb 2025 Mkoa wa Pwani, umepokea miradi ya uwekezaji 369 ambapo kati ya hiyo asilimia 67 ni miradi ya viwanda ambayo jumla yake imefikia 247.

Aidha, mitaji iliyowekezwa na sekta zote kwa mkoa wa Pwani ni dola za Marekani Bilioni 4.6 (sawa na shilingi Trilioni 12.4) ambapo asilimia 61 ya mitaji hiyo inatokana na sekta ya viwanda ikiwa na mitaji ya dola za Marekani Bilioni 2.8 (sawa takribani shilingi Trilioni 7.5).



1.2. UENDELEZAJI WA ENEO LA KWALA NA KONGANI YA

VIWANDA LA SINO-TAN



Kongani ya viwanda ya SINO-TAN ni eneo la mradi wa kimkakati lililoko Kwala, Mkoa wa Pwani lenye ukubwa wa ekari 2,500. Eneo hili lina mtaji wa mwekezaji wa dola za Marekani milioni 327 (sawa na shilingi Bilioni 882). Mradi huu utakapokamilika, utakuwa na viwanda vikubwa na vya kati 200 na viwanda vidogo 300 vinavyohusiana na;-

Usindikaji wa vyakula,

Utengenezaji wa vifaa,

Viwanda vya dawa,

Vifaa vya ujenzi,

Usindikaji wa viatu na nguo na

Viwanda vya kemikali.


Sasa nini faida za kongani hii?
Kongani hii inatarajiwa kutoa ajira za moja kwa moja 100,000 na ajira zisizo za moja kwa moja 500,000 na itajengwa kwa awamu Tano. Aidha, ujenzi wa awamu ya kwanza ulianza Mei, 2022 na upo katika hatua za mwisho. Mpaka sasa kuna viwanda 3 ambavyo tayari vinazalisha na vingine 3 vipo katika hatua za mwisho za kufunga mitambo huku viwanda vingine 4 vikitarajiwa kuanza ufungaji wa mitambo ifikapo mwisho wa mwezi Aprili 2025.

Eneo hili litakuwa na uwezo wa kuzalisha bidhaa zenye thamani ya dola za Marekani bilioni 6 (sawa na shilingi Trilioni 16.2) kwa mwaka.

Serikali itakusanya kodi na ushuru kila mwaka kwa makadirio ya shilingi trilioni 1.2.


MAENDELEO YA UTEKELEZAJI WA MRADI
Tangu kuanza kwa utekelezaji wa ujenzi wa mradi huu, shughuli mbalimbali zimefanyika zikiwemo za ujenzi wa miundombinu ya awamu ya kwanza ndani ya eneo la mradi ambayo imekamilika kwa asilimia 80 ikihusisha:-

  • Mtandao wa barabara za zege zinazoweza kubeba malori ya mizigo
  • Jengo litakalohifadhi kituo cha kupambana na moto
  • Jengo la utawala litakalohifadhi ofisi za mashirika ya serikali na watoa huduma za kitaalamu ,
  • Mfumo wa maji ya mvua ,
  • Mtandao wa umeme,
  • Mtandao wa maji safi,
  • Hifadhi za viwanda za mita za mraba 26,000,
  • Lango kuu,
  • Malazi ya wafanyakazi
1.4. UWEKEZAJI WA SERIKALI KATIKA MRADI (Serikali imefanya nini katika eneo hili)

Ili kuwezesha kuanza kwa uzalishaji wa viwanda katika eneo hilo, Serikali imefanya yafuatayo ;-

  • Uunganishaji wa awali wa maji kupitia mamlaka zinazohusika, kwa ajili ya matumizi ya ujenzi. Pia Serikali inaendela na mpango wa kuiunganisha kongani hii na maji ya kutosha kwa ajili ya uzalishaji viwandani,
  • Ujenzi wa barabara za zege zinazounganisha kongani hii na Barabara ya Morogoro,
  • Kuunganisha mtandao wa nyaya za Fiber Optic (Mkongo wa Taifa),
  • Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kumalizia kazi ya kuunganisha kongani hii na umeme wa Megawati 50.
Aidha, mradi huu kwa sasa una mikataba na waendeshaji 10 wa kuanzisha shughuli katika kongani hii ambapo watatu tayari wameshaanza shughuli huku wengine watatu wakijiandaa kuanzisha shughuli na wanne waliosalia wanatarajiwa kuanza shughuli hivi karibuni.

MAENDELEO YA UJENZI WA BANDARI KAVU YA KWALA, KONGANI ZA VIWANDA NA ICDS
Serikali kupitia Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) imeamua kujenga Bandari Kavu eneo la Kwala “Quarantine” Ruvu, katika eneo la vigwaza Wilayani Kibaha - Mkoa wa Pwani, umbali wa kilomita 15.5 kutoka barabara kuu ya Morogoro na umbali wa Kilomita 90 kutoka Bandari ya Dar es Salaam.

Katika utekelezaji wa mradi huu awamu ya kwanza hekta 502 zimetwaliwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ikiwa ni sehemu ya Hekta 52,000 ya eneo linalomilikiwa na Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, ambapo kihistoria, eneo hilo lilikuwa chini ya usimamizi wa Kampuni inayoitwa “Tanzania Livestock, Marketing Company (TLMC) na baadaye kuwa chini ya Tanzania, Livestock Marketing Project (TLMP).

Eneo hili lilitolewa na Serikali kwa TPA ili kuendeleza miundombinu ya Bandari Kavu ikiwemo Yadi, Majengo, Barabara na Reli zinazounganisha bandari hiyo na reli za Shirika la Reli Tanzania (TRC) na barabara kuu ya Morogoro.

Bandari ya Kwala ipo karibu na stesheni za Msuwa na Ruvu kwa reli (SGR na MGR) za TRC. PIA iko katika eneo lenye ukubwa wa Hekta 502 ambapo kati ya hizo; hekta 120 zimesafishwa, hekta 60 tayari zimeshasawazishwa na hekta 5 tayari zimejengwa kwa kiwango cha zege. Aidha, eneo lenye jumla ya hekta 60 limewekwa uzio wenye urefu wa Kilomita 2.96 ambazo ndizo zimeanza kujengwa miundombinu ya Bandari Kavu kwa awamu ya kwanza.

SABABU ZA UJENZI WA BANDARI KAVU YA KWALA

Msongamano wa meli uliotokana na mrundikano wa shehena katika Bandari ya Dar es salaam
. Moja ya changamoto kubwa zilizokuwa zinaikabili Bandari ya Dar es Salaam kuanzia mwaka 2008 ni msongamano wa shehena bandarini. Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa kushirikiana na wadau wa Bandari ambao ni Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) ya wakati ule ambayo sasa ni Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) na Wizara ya Miundombinu kwa wakati ule (ambayo kwa sasa ni Wizara za Ujenzi na Uchukuzi) ilichukua hatua mbalimbali za kupunguza tatizo hilo kwa kuanzisha Bandari Kavu (Inland Container Depots – ICDs).

Uwezo mdogo wa bandari kavu zilizokuwepo (ICDs). Katika Jiji la DSM kulikuwa na jumla ya bandari kavu (ICDs) 11 zenye uwezo wa kuhifadhi kontena 24,300 kwa vipimo vya TEUs kwa wakati mmoja. Kati ya hizo, pia kulikuwa na Bandari Kavu (CFS) 9 zenye uwezo wa kuhifahi jumla ya magari 19,100 kwa wakati mmoja ambazo zilionekana kutokidhi mahitaji makubwa kwa wakati huo.

Sababu za kiufundi na kiuchumi, eneo la Ruvu liko karibu na miundombinu ya barabara kuu inayounganisha nchi jirani za Burundi, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Malawi, Zambia na Uganda; zinazotumia Bandari ya DSM na reli. Aidha, katika siku za usoni, eneo hili litaunganishwa na barabara ya Chalinze – Dar es Salaam “Express Highway”.

Kijamii, eneo la Kwala linamilikiwa na Serikali na hivyo halikuhitaji fidia ili kupisha mradi jambo ambalo mara nyingi huambatana na migogoro na athari mbalimbali za kijamii.

UTEKELEZAJI MRADI WA UJENZI WA BANDARI YA KWALA

Ujenzi wa mradi wa Bandari Kavu ya Kwala umefanyika kwa gharama ya shilingi Bilioni 83.246. Kazi zilizofanyika hapa

Kusafishaji eneo la hekta 60 na ujenzi wa ukuta,

Kujenga Yadi yenye ukubwa wa hekta 5 kwa kiwango cha zege ambao tayari imekamilika kwa asilimia 100 kwa gharama ya shilingi Bilioni 36.670.

Ujenzi wa reli ya mchepuko kilometa 1.3 kutoka Stesheni ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) Kwala hadi Bandari Kavu ya Kwala. Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) na Shirika la Reli Tanzania (TRC) wamekamilisha kazi hii kwa asilimia 100 kwa gharama ya shilingi Milioni 677.3

Ujenzi wa barabara yenye urefu kilometa 15.5 kwa kiwango cha zege, barabara hii ina upana wa njia mbili kutoka Vigwaza mpaka Bandari ya Kwala-Ruvu. Gharama ya mradi huu hadi kukamilika kwake shilingi Bilioni 36.432.


SHEHENA INAYOTARAJIWA KUHUDUMIWA NA BANDARI YA KWALA

Ndugu Wanahabari;
Bandari hii inatarajiwa kuhudumia shehena ya makasha 823 kwa siku yakiwemo makasha yanayokwenda nchi jirani, hivyo kuifanya Bandari hii kuhudumia hadi makasha 300,395 kwa mwaka ambayo ni sawa na asilimia 30 ya makasha yote yanayohudumiwa na Bandari ya Dar es Salaam kwa sasa.

FAIDA ZA BANDARI KAVU YA KWALA
Kuongeza ufanisi na kiasi cha shehena inayohudumiwa katika Bandari ya Dar es salaam

Kuongezeka kwa mapato ya Serikali kupitia huduma zitolewazo katika Bandari za Dar es Salaam na Kwala;

Itapunguza gharama za uendeshaji hivyo kuvutia wateja kutumia Bandari ya Dar es salaam,

Kuongeza ushindani wa Bandari ya Dar es Salaam kikanda ukizingatia uwekezaji wa Bandari za nchi jirani katika Bandari Kavu;

Kuimarisha shughuli za kiuchumi na biashara za mikoa ya Dar es salaam na Pwani kwa kupunguza msongamano wa magari uliopo sasa;

Kuimarishwa kwa usalama barabarani kwa kuwa idadi kubwa ya shehena ya Bandari ya Dar es salaam itatumia usafiri wa reli;

Maisha marefu ya miundombinu ya barabara za mikoa ya Dar es salaam na Pwani,

Utaongeza ajira kwa wakazi wanaoizunguka Bandari Kavu ya Kwala na Taifa kwa ujumla.

&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&​


3.0. MAADHIMISHO YA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI YALIYOFANYIKA MACHI 8, 2025 JIJINI ARUSHA

Machi 8, 2025, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliwaongoza Watanzania katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo nchini kwetu yalifanyika Jijini Arusha yakiongozwa na Kaulimbiu “Wanawake na Wasichana 2025: Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji”.

Maadhimisho ya mwaka huu 2025 yalibeba sura ya kipekee kwa kuwa yaliambatana na miaka 30 ya utekelezaji wa Azimio la ulingo wa Beijing (1995).

Kilele cha maadhimisho ya mwaka huu kilitatanguliwa na maadhimisho katika ngazi ya Mikoa nchi nzima ili kuwa na ushiriki wa Wanawake na jamii kwa wingi zaidi. NAOMBA KUCHUKUA NAFASI HII KWA NIABA YA SERIKALI KUWAPONGEZA WOTE WALIOSHIRIKI MAADHIMISHO YA MWAKA HUU KATIKA NGAZI MBALIMBALI.

Katika maadhimisho hayo, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alitoa mwelekeo kuhusu umuhimu wa nafasi na ushiriki wa Wanawake katika maendeleo ya nchi yetu ambapo alisisitiza yafuatayo;-
  • Tanzania tumepiga hatua kubwa kwenye sekta ya afya kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanyika wa miundombinu ya afya. Serikali imejenga miundombinu ya kisasa nchi nzima kuanzia Zahanati, Hospitali za Kata, Hospitali za Wilaya, Mikoa na Hospitali za Rufaa na kuweka vifaa tiba vya kisasa vya matibabu.

  • Tanzania tumefanikiwa kukuza ujuzi na utalaamu katika matibabu hali iliyotuwezesha kufanya matibabu mengi ambayo zamani tulikuwa hatukuna uwezo wa kuyatibu na kupeleka wagonjwa nje, sasa uwezo huo tunao, tunatoa matibabu hayo ndani ya nchi.

  • Tumeweza kupunguza vifo vya wanawake wakati wa kujifungua kutoka vifo 1,500 kwa vizazi hai 100,000 mpaka vifo 104 kwa vizazi hai 100,000. Vilevile tumepunguza vifo vya watoto kwa kiasi kikubwa na kazi hii inaendelea.

  • Kitaifa, Tanzania tumefanikiwa kujitegemea kwa chakula kwa asilimia 128, hivyo tumefanikiwa kuondoa njaa kwa asilimia 100. Kama nchi tumefikia hatua hii na kazi tunayoendelea nayo ni ya kuhimizana katika ngazi ya mtu mmoja mmoja kuhakikisha hakuna mtu anayebaki na njaa.

  • Katika sekta ya elimu, kutokana na juhudi na uwekezaji mkubwa uliyofanywa na serikali ya kujenga miundombinu na marekebisho kadhaa, sasa idadi ya wanafunzi shuleni inakwenda sawa hatua iliyotuwezesha kuwa na usawa wa kijinsia.

  • Kwa upande wa utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu tumefanikiwa kuongeza Bajeti kutoka shilingi Bilioni 450 mwaka 2021/2022 hadi Bilioni 787 kwa mwaka 2024/2025 ambayo inatolewa mpaka kwenye ngazi ya Diploma kwa programu maalum.

  • Katika kuchochea wanafunzi kupenda masomo ya Sayansi, Serikali imeanzisha ufadhili wa asilimia 100 kwa watoto wote wanaochukua masomo ya sayansi, inaitwa Samia Scholarship. Katika jitihada za kipekee tumejenga shule maalumu za wasichana kwa masomo ya sayansi, sasa hivi kila mkoa kuna shule moja ya wasichana kwa ajili ya masomo ya sayansi.

  • Kwa upande wa maji safi tumepiga hatua kubwa; Ilani ya uchaguzi ilituelekeza kwamba, kwa vijijini twende asilimia 85 na mijini tufikie asilimia 95. Mpaka Desemba mwaka jana, katika maeneo ya vijijini kwa wastani tunakaribia asilimia 80 na mijini tupo kwenye asilimia 90. Tuna miradi ya maji zaidi 1,000 ambayo ipo katika maeneo mbalimbali nchi nzima ambayo ikikamilika inakwenda kukamilisha asilimia tulizotumwa kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.

  • Kwa upande wa nishati Tanzania tumepiga hatua kubwa, Serikali imesambaza umeme vijiji vyote 12,318 sasa tunaelekea kwenye ngazi ya vitongoji na tayari vitongoji kadhaa vimewekewa umeme na kazi inaendelea.

  • Kwenye nishati safi tumefanya kazi nzuri ya kujenga Bwawa la Julius Nyerere linalotupa megawati 2,115 pamoja na bwawa hilo tuna mabwawa mengine madogo madogo sita ambayo yanatoa umeme maeneo mbalimbali ya Tanzania.

  • Kwa upande wa uwezeshaji wa mwanamke kumiliki ardhi, Serikali imeendelea kulifanyia kazi jambo hili na sasa mwanamke anaweza kufanya kazi zake katika ardhi yake mwenyewe. Pia kwa sasa wanawake na wanaume wote wanamiliki ardhi sawa, kutegemea uwezo.

  • Kwa upande wa ubunifu tumefanikiwa kujenga mazingira na kuwafanya vijana wetu kutumia miundombinu iliyopo, miundombinu ya TEHAMA kuwa wabunifu wa mambo kadhaa.

  • Kama Serikali, tumeweza kukuza sekta ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ili kuwezesha vijana wetu wa kike na wa kiume kupata ajira katika sekta hii na kujiongezea kipato.

  • Tumeendelea kuimarisha usalama na utulivu ndani ya nchi na kuendelea kuweka mifumo Madhubuti ya utoaji wa Haki jambo ambalo limeimarisha utawala bora na umoja wa kitaifa.
4.0. UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAJI KATIKA MAENEO MBALIMBALI NCHINI

4.1. Mradi wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe

Machi 9, 2025 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, alizindua mradi mkubwa wa maji wa Same – Mwanga – Korogwe unaowezesha upatikanaji wa majisafi na salama kwa wananchi wa miji ya Same na Mwanga na pia wananchi katika vijiji 38 vilivyo katika Wilaya za Same, Mwanga na Korogwe. Kati ya vijiji hivyo, vijiji 17 vipo katika Wilaya ya Mwanga, vijiji 16 Wilaya ya Same na vijiji 5 Wilaya ya Korogwe.

4.2. Uwezo wa kuzalisha na kusambaza maji (Same-Mwanga-Korogwe_
Mradi huu una uwezo wa kuzalisha maji lita milioni 103.65 ambapo lita milioni 60.2 sawa na asilimia 58 ni kwa ajili ya Wilaya ya Same, lita milioni 40.2 sawa na asilimia 38.8 ni kwa ajili ya Wilaya ya Mwanga na lita milioni 3.3 sawa na asilimia 3.2 ni kwa ajili ya vijiji 5 vilivyo katika Wilaya ya Korogwe.

4.3. Gharama za mradi
Tangu kuanza kwa awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi huu mwaka 2014, shilingi Bilioni 406 zimetumika kwa ajili ya malipo ya Wakandarasi na Wataalamu washauri.

4.3. Kazi zilizofanyika katika mradi huu

  • Ujenzi wa chanzo chenye uwezo wa kuzalisha maji lita milioni 103.65
  • Ujenzi wa mtambo wa kusafisha maji wenye uwezo wa kusafisha lita milioni 51.65.
  • Ulazaji wa bomba kuu la kusafirisha maji kilomita 81.8.
  • Ulazaji wa bomba la kusambazaji maji kilomita 306.
  • Ujenzi wa kituo cha kupooza umeme (High Tension Sub-station) chenya uwezo wa kuzalisha Megawati 16.
  • Ujenzi wa matanki saba yenye uwezo wa kuhifadhi maji kuanzia lita 300,000 hadi lita 9,000,000.
  • Ujenzi wa kituo cha kusukuma maji Kisangara.
MSISITIZO: Utekelezaji wa mradi huu katika awamu ya kwanza umekamilika na sasa wananchi wa miji ya Same na Mwanga wanapata huduma ya majisafi na salama. Aidha Vijiji tisa vya Njia Panda, Kisangara, Lembeni, Mbambua, Kiruru, Kiverenge, Mgagao, Njoro na Ishinde vimeanza kupata maji. Wizara ya Maji inaendelea na utaratibu wa kuhakikisha wanachi wa Vijiji vilivyobaki vinapata majisafi na salama.


5.0. MRADI WA UJENZI WA BWAWA LA KIDUNDA

Serikali ya Awamu ya Sita chini chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inatekeleza ujenzi wa mradi mkubwa wa maji wa Bwawa la kidunda mkoani Morogoro kwa gharama ya shilingi Bilioni 335.863 (shilingi bilioni 335,863,166,204.89) kwa lengo la kuhakikisha upatikanaji wa maji muda wote katika Mto Ruvu, hivyo kuwa na maji ya uhakika kwa Jiji la Dar es salaam, Mkoa wa Pwani na Mkoa wa Morogoro.


Mradi huu umefikia asilimia 28, ulianza rasmi tarehe 18 Juni 2023 na umepangwa kukamilika tarehe 18 Juni 2026.

Mradi huu unatarajiwa kuwa na mtambo wa uzalishaji umeme Megawati 20,

Ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme yenye urefu wa Kilomita 101 kutoka Kidunda hadi Chalinze kwenye gridi ya Taifa na;

Ujenzi wa Barabara kiwango cha changarawe yenye urefu wa kilomita 75 kutoka Ngerengere hadi Kidunda.


Utekelezaji wa mradi
Mradi unatekelezwa na Wizara ya Maji kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) na ujenzi wake utahusisha yafuatayo;

Tuta lenye urefu wa mita 870 na kina cha mita 24

Ujenzi wa njia ya kutokea maji (Spillway) utakaotumika kupitisha maji kipindi cha mvua,

Mtambo wa kufua umeme Megawati 20,

Njia ya kusafirisha umeme yenye urefu wa kilomita 101 kutoka Kidunda mpaka Chalinze kwenye gridi ya Taifa,

Barabara kilomita 75 kwa kiwango cha changarawe kutoka Ngerengere hadi Kidunda,


b) Manufaa na Mradi

Mradi utakapokamilika unatarajia Kuboresha huduma ya majisafi kwa ajili ya matumizi ya Majumbani, Kilimo na Viwanda kwa kuhakikisha upatikanaji wa muda wote katika mto Ruvu kwa kutiririsha wastani wa lita 24,000 kwa sekunde zitakazokidhi mahitaji ya maji hususani kwenye kipindi cha ukame.

Aidha, Serikali kupitia Wizara ya maji ipo katika hatua ya usanifu wa mradi ambao utawanufaisha wananchi wapatao 7,296 kufikiwa na huduma ya majisafi kwenye vijiji vinavyozunguka Bwawa la Kidunda hususani vijiji vinne (4) kwenye kata ya Mkulazi, ambavyo ni Usungura, Kidunda, Chanyumbu na Mkulazi.


6.0. UTEKELEZAJI WA MRADI WA MAJI WA MIJI 28


Katika jitihada za kuboresha huduma ya maji nchini, mwaka 2018 Serikali ilisaini mkataba wa fedha za mkopo wenye masharti nafuu baina yake na Benki ya Exim ya India, wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 500 sawa na takribani shilingi trilioni 1.172 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji Tanzania Bara (USD 465m sawa na shilingi trilioni 1.09) na Zanzibar (USD 35m).



Baada ya mkataba huo kusainiwa Wizara ya Maji ilifanya upembuzi wa awali na kuhusu kuanza utekelezaji katika miji 24 kupitia mikataba sita (6). Miji hiyo 24 inahusisha Handeni/Korogwe, Muheza, Pangani, Kilwa Masoko, Nanyumbu, Ifakara, Njombe, Rujewa, Chunya, Makambako, Wanging’ombe, Chamwino, Chemba, Manyoni, Singida, Kiomboi, Mugumu, Urambo/ Kaliua, Sikonge, Mpanda, Kasulu, Geita, Chato na Kayanga.



Aidha, Miji minne (4) inatekelezwa kwa fedha za ndani kwa gharama za shilingi za kitanzania Billioni 413 ambayo ni Makonde plateau, Mafinga, Rorya/Tarime na Songea.



Utekelezaji wa mradi huu wa miji 28 utakapokamilika takribani watu 6,934,270 watanufaika na huduma ya maji safi na salama.





UTEKELEZAJI WA MIKATABA

Mkataba wa Kwanza - Korogwe, Muheza na Pangani​

Mkataba huu unahusisha kutoa maji Mto Pangani kwenda katika miji ya Handeni/ Korogwe, Muheza na Pangani ambao unatekelezwa kwa gharama ya Dola za Marekani Milioni 81 (sawa na shilingi Bilioni 218.7), Mkataba huu ulisainiwa tarehe 6 Juni, 2022 unatekelezwa kwa kipindi cha miezi 32 kuanzia tarehe 11 Aprili, 2023 hadi 10 Disemba 2025. Mradi huu unategemewa kuhudumia wananchi wapatao 868,034. Hali ya utekelezaji hadi kufikia Februari, 2025 ni asilimia 63.

Mkataba wa Pili - Kilwa Masoko na Nanyumbu​

Mkataba wa Pili unaohusisha Miji ya Kilwa Masoko na Nanyumbu ulisainiwa tarehe 06/06/2022 kwa gharama ya Dola za Marekani 35,356,500.00 (sawa na shilingi Bilioni 95.5). Mkataba huu utakamilishwa tarehe 10 Septemba 2025. Mradi unategemewa kuhudumia wananchi wapatao 134,450. Hali ya utekelezaji hadi kufikia Februari, 2025 ni asilimia 70.



Mkataba wa Tatu - Ifakara, Njombe, Makambako, Wanging’ombe, Rujewa na Chunya.​



Mkataba wa tatu unahusisha kupeleka maji katika Miji ya Ifakara, Njombe, Makambako, Wanging’ombe, Rujewa (Mbarali) na Chunya ambao unatekelezwa kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 86.5 (sawa na shilingi Bilioni 233.5). Mkataba huu ulisainiwa tarehe 6 Juni, 2022 na unatekelezwa kwa kipindi cha miezi 30 kuanzia tarehe 11 Aprili, 2023 na kukamilika tarehe 10 Oktoba, 2025. Mradi unategemewa kuhudumia wananchi wapatao 838,260. Hali ya utekelezaji hadi Februari, 2025 ni asilimia 28.



Mkataba wa Nne – Singida, Manyoni, Kiomboi, Mugumu, Chemba na Chamwino

Mkataba wa nne unahusisha kupeleka maji katika miji ya Chamwino, Chemba, Manyoni, Singida, Kiomboi na Mugumu ambao unatekelezwa na Mkandarasi M/s Megha Engineering & Infrastructures Ltd kwa gharama ya dola za Marekani milioni 61.8 (sawa na shilingi Bilioni 167). Mkataba huu ulisainiwa tarehe 6 Juni, 2022 na unatekelezwa kwa kipindi cha miezi 24 kuanzia tarehe 11 Aprili, 2023 hadi tarehe 10 April 2025. Mradi unategemewa kuhudumia wananchi wapatao 613,840, Hali ya utekelezaji hadi Februari, 2025 ni asilimia 14.



Mkataba wa Tano - Urambo/Kaliua, Sikonge, Kasulu na Mpanda

Mkataba wa tano unahusisha kupeleka maji katika miji ya Urambo/Kaliua, Sikonge, Kasulu na Mpanda ambao unatekelezwa na Mkandarasi M/s Megha Engineering & Infrastructures Ltd kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 86.7 (sawa na shilingi Bilioni 234). Mkataba huu ulisainiwa tarehe 6 Juni, 2022 na unatekelezwa kwa kipindi cha miezi 30 kuanzia tarehe 11 Aprili, 2023 hadi tarehe 10 Oktoba, 2025. Mradi unategemewa kuhudumia wananchi wapatao 957,580. Hali ya utekelezaji Februari, 2025 ni asilimia 50.5.



Mkataba Wa Sita - Kayanga, Geita na Chato

Mkataba wa sita unahusisha kupeleka maji katika miji ya Kayanga, Geita na Chato ambao unatekelezwa na Mkandarasi M/s Afcons Infrastuctures Limited in JV with M/s Vijeta projects and Infrastructures Limited kwa gharama ya Dola za Marekani 97.9 (sawa na Shilingi Bilioni 264.4). Mkataba huu ulisainiwa tarehe 6 Juni, 2022 na unatekelezwa kwa kipindi cha miezi 32 kuanzia tarehe 11 Aprili, 2023 hadi tarehe 10 Disemba, 2025. Mradi unategemewa kuhudumia wananchi wapatao 1,182,120. Hali ya utekelezaji hadi Februari, 2025 ni asilimia 50.5.



Mkataba wa Saba - Makonde


Mkataba wa saba unahusisha kupeleka maji katika miji ya Newala, Tandahimba na Nanyamba ambao unatekelezwa na Mkandarasi M/s China Civil Engineering Construction Corporation kwa gharama ya shilingi Bilioni 84.7. Mkataba huu ulisainiwa tarehe 6 Juni, 2022 na unatekelezwa kwa kipindi cha miezi 20 kuanzia tarehe 01 Desemba, 2022 hadi tarehe 31 Julai, 2024 (Muda umeongezwa hadi 31.7.2025). Mradi unategemewa kuhudumia wananchi wapatao 1,243,150 (. Hali ya utekelezaji hadi Februari, 2025 ni asilimia 24.



Mkataba wa Nane – Mafinga


Mkataba wa nane unahusisha kupeleka maji katika mji Mafinga ambao unatekelezwa na Mkandarasi M/s Jandu Plumbers Limited kwa gharama ya shilingi Bilioni 48 (TZS 48,064,173,480.50) Mkataba huu ulisainiwa tarehe 6 Juni, 2022 na unatekelezwa kwa kipindi cha miezi 20 kuanzia tarehe 01 Desemba, 2022 hadi tarehe 31 Julai, 2024 (Muda umeongezwa hadi 31.7.2025). Mradi unategemewa kuhudumia wananchi wapatao 103,243. Hali ya utekelezaji hadi Februari, 2025 ni asilimia 16.5.



Mkataba wa Tisa – Rorya - Tarime


Mkataba wa sita unahusisha kupeleka maji katika miji ya Rorya na Tarime ambao unatekelezwa na Mkandarasi M/s China Civil Engineering Construction Corporation kwa gharama ya shilingi Bilioni 134.39. Mkataba huu ulisainiwa tarehe 01 Septemba, 2022 na unatekelezwa kwa kipindi cha miezi 30 kuanzia tarehe 23 Januari, 2023 na utakamilika tarehe 22 Julai, 2025. Mradi unategemewa kuhudumia wananchi wapatao 460,885. Hali ya utekelezaji hadi Februari, 2025 ni asilimia 12.5.


Mkataba wa Kumi - Songea

Mkataba wa sita unahusisha kupeleka maji katika Mji wa Songea ambao unatekelezwa na Mkandarasi M/s China Civil Engineering Construction Corporation kwa gharama ya Bilioni 145.7 (TZS 145,773,015,609.69). Mkataba huu ulisainiwa tarehe 10 Machi, 2023 na unatekelezwa kwa kipindi cha miezi 30 kuanzia tarehe 2 Januari, 2024 hadi tarehe 1 Julali, 2026. Mradi unategemewa kuhudumia wananchi wapatao 532,700. Hali ya utekelezaji hadi Februari, 2025 ni asilimia 5.



&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&



MRADI WA UJENZI WA BARABARA YA KIBAHA-CHALINZE EXPRESSWAY (KM 78.9)

Ndugu zangu Waandishi wa Habari,
mtakumbuka Serikali imefanya marekebisho kadhaa katika Sheria ya PPP Sura Na.103 pamoja na kanuni zake za 2020 na marekebisho ya 2023 ili kushirikisha sekta binafsi katika miradi ya maendeleo.

Tumefanya hivi kutokana na ukuaji wa mahitaji ya miundombinu ya barabara nchini, Serikali imeamua kutumia njia ya ubia kwa kushirikisha sekta ya umma na sekta binafsi (PPP) ili kuongeza wigo wa upatikanaji wa fedha za kutekeleza miradi hii.


  • Sasa katika mwaka wa fedha 2022/23, Serikali iliridhia kuanza utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya haraka ya kulipia kutoka Kibaha-Chalinze-Morogoro (km 163.8). (Maana baadhi walishaanza kusema mpango umefeli, nataka niwaambie mpango haujafeli, Serikali inafanya maandalizi ili utekelezaji wake usije kuleta changamoto nyingi baadaye)

  • Sasa utekelezaji wa mradi huu umegawanywa katika sehemu mbili ambazo ni ;-

  • Kibaha –Chalinze (km 78.9) na
  • Chalinze- Morogoro (km 84.9).

  • HATUA ZA UTEKELEZAJI
  • Barabara ya Kibaha-Chalinze (KM 78.9)

  • Mradi huu kwa sasa upo katika hatua ya ununuzi. Majadiliano baina ya Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na mbia yanaendelea ili kupata mradi unaoendana na thamani ya fedha na himilivu kwa Serikali na watumiaji.

  • . Barabara ya Chalinze - Kibaha (KM 84.9)

  • Mradi huu upo hatua za mwisho za maandalizi. Aidha, upembuzi yakinifu umekwisha kamilika na tangazo kwa ajili ya manunuzi ya kupata Wabia linatarajiwa kutolewa mwezi Mei, 2025.

  • &&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&
7.0. UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MKOA WA PWANI KWA MWAKA 2024/25, MATARAJIO YA BAJETI YA MWAKA 2025/26 NA MIRADI MIKUBWA ILIYOTEKELEZWA MWAKA 2024/25 THAMANI YAKE NA UFANISI WAKE.

Katika mwaka wa fedha 2024/25 Mkoa wa Pwani umeidhinishiwa matumizi ya Bajeti ya shilingi TZS 413,216,008,000. Kati ya kiasi hicho TZS, 344,447,365,000 ni kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu mbalimbali na Miradi ya Maendeleo.

Kipindi cha mwezi Julai, 2024 hadi Februari 2025 Mkoa wa Pwani umepokea jumla ya TZS 224,194,276,648.31 za ruzuku sawa na asilimia 65. Kati ya kiasi hicho TZS. 156,423,975,414.72 zimelipwa mishahara, TZS 22,976,478,019.00 za Matumizi Mengineyo na TZS 44,793,823,214.59 miradi ya maendeleo.

Katika Bajeti ya Mwaka 2025/26 Mkoa wa Pwani unatarajia kutumia jumla ya TZS 425,052,442,047.00. (Ndugu zangu Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Pwani, nimezungumza na Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa Kaka yangu Aboubakar Kunenge, tumekubaliana kupanga siku ambayo na mimi nitakuja na tutakuwa sote tutembelee kazi kubwa iliyofanywa na Serikali na wadau wa maendeleo katika kufanya mageuzi makubwa ya kiuchumi hapa Pwani)

7.1. UTEKELEZAJI WA MIRADI MBALIMBALI YA KIMKAKATI

A: HALMASHAURI YA BAGAMOYO
Mradi wa Jengo la Dharura (EMD)
katika Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo, ujenzi umekamilika na jengo linatoa huduma kwa wananchi wa Bagamoya na maeneo ya jirani. Gharama za mradi huu ni kiasi cha shilingi milioni 300.

Mradi wa Ujenzi wa Shule ya Msingi Kiembeni iliyopo Mapinga katika Halmashauri ya Bagamoyo umekamilika na kuanza kutumika. Thamani ya mradi ni shilingi milioni 475.

B: HALMASHAURI YA CHALINZE
Ujenzi wa miundombinu ya Hospitali ya wilaya Msoga
ambayo ilianza kujengwa tangu mwaka 2022. Ujenzi umegharimu jumla ya shilingi Bilioni 3.3.

C: HALMASHAURI YA KIBAHA DC
Ujenzi wa barabara ya kwala – Sino Tan
. Barabara hii yenye urefu wa kilometa 3.6 imejengwa kwa kiwango cha zege kwa awamu mbili kwa gharama Bilioni 9.7. Barabara hii inaunganisha bandari kavu ya Kwala na Kongani ya viwanda ya SINO TAN.

Halmashauri ya Kibaha TC.

Ujenzi wa Shule ya Sekondari viziwaziwa, ujenzi huu umetekelezwa kwa awamu tatu kwa gaharama ya shilingi Bilioni 1.099. Awamu ya kwanza imehusisha ujenzi wa madarasa 8, jengo la utawala, maabara tatu za sayansi, jengo la TEHAMA, Jengo la maktaba, vyoo na maeneo mengine muhimu kwa gharama ya shilingi Milioni 470. ⁠Awamu ya pili imehusisha ujenzi wa nyumba za walimu kwa shilingi milioni 95. ⁠Aidha, awamu ya tatu imetekelezwa katika mwaka wa fedha 2024/2025 ikihusisha ujenzi wa mabweni 4, madarasa na vyoo.

D: HALMASHAURI YA KIBITI
Mradi wa ujenzi wa shule mpya ya sekondari
kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne. Mradi huu ambao umekamilika na kuanza kutumika umejengwa kwa fedha za Sequip kwa gharama ya shilingi milioni 528,998,424.00

E: HALMASHAURI YA KISARAWE
Mradi wa Jengo la huduma za dharura katika hospitali ya Wilaya ya Kisarawe
. Ujenzi ulianza Mei 10, 2022 na kumalizika Agosti 18, 2022. Jengo hilo lilighalimu kiasi cha shilingi milioni 470, mradi umekamilika na Unatumiaka.

Mradi wa Ujenzi wa Jengo la Utawala la Halmashauri ya Wilaya Kisarawe. Ujenzi ulianza Aprili, 2022. Halmashauri ilipokea kiasi cha shilingi bilioni 3.93 (TZS 3,933,888,140.00) kwa awamu nne. Mradi huu upo katika hatua za umaliziaji.

F: HALMASHAURI YA MAFIA
Halmashauri ya wilaya ya Mafia kupitia idara ya afya ilipokea kiasi cha shilingi Milioni 550 kwa ajili ya ujenzi wa majengo mawili ya wagonjwa wa dharura na wagonjwa wanaohitaji usaidizi au uangalizi maalum kutoka Serikali kuu ambapo jumla ya shilingi Milioni 300 ni kwa ajili ya ujenzi wa jengo la wagonjwa wa dharura (EMD) na shilingi milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU).

G: HALMASHAURI YA MKURANGA
Halmshauri inatekeleza mradi wa ujenzi wa shule ya Sekondari Kilimahewa. Mradi huu upo Wilayani Mkuranga Kata ya Kimanzichana. Thamani ya mradi huu ni shilingi milioni 528 fedha kutoka Serikali kuu. Mradi huu umeondoa tatizo la wanafunzi waliokuwa wakitembea umbali wa kilometa 10 kufuata shule ya Sekondari.

G: HALMASHAURI RUFIJI
Mradi wa ujenzi wa Soko,
mradi huu umejengwa kwa gharama ya shilingi Milioni 171.63. (TZS 171, 638, 680).

Mradi wa Barabara ya kutoka Hospitali kuelekea Ofisi ya Mkurugenzi. Mradi huu umegharimu kiasi cha shilingi Bilioni. 1.4.

Mradi wa Jengo la Utawala la halmashauri ya wilaya Rufiji ambao umegharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 1.



&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&​

MFUMO WA KUTOA VITAMBULISHO VYA KIDIGITALI KWA WAANDISHI WA HABARI

Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kupitia Idara ya Habari – MAELEZO kwa kushirikiana na Wakala ya Serikali Mtandao (e-GA) inaendelea na kazi ya kukamilisha ujenzi wa mfumo wa Usajili na utoaji wa vitambulisho vya kidigitali kwa Waandishi wa Habari nchi nzima - JOURNALISTS ACCREDITATION & REGISTRATION SYSTEM (JARS).

Mfumo huu unalenga kurahisisha, kuongeza uwazi na kuimarisha utendaji kazi wa waandishi wa Habari kwa kuwapatia huduma ya usajili na utoaji wa vitambulisho vya kazi katika maeneo yao bila kulazimika kusafiri kuja Dodoma au Dar es salaam kupata huduma hii.

HUDUMA YA KUPATA VITAMBULISHO (ID CARDS) KWA WAANDISHI WA HABARI KUPITIA MFUMO (JARS)
Huduma hii ya kupata vitambulisho vya kidigitali itapatikana kwa Waandishi wa habari wote watakaokuwa wamekidhi vigezo vya kitaaluma (Taaluma ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma). Aidha, Mwandishi wa habari atapaswa kujaza taarifa zake na kufuata maelekezo yaliyoko kwenye mfumo ili aweze kujisajili.

Mfumo huu pamoja na mambo mengine utakuwa na uwezo ufuatao:-
  • Uwezo wa kusajili, kuhakiki na kuhifadhi taarifa za waandishi wa habari wote nchini,
  • Mwandishi wa habari atakuwa uwezo wa kujaza taarifa na
  • kuweka mambo muhimu kama vile picha, mahali anapofanya
  • kazi, taarifa za uraia wake n.k.
  • Mfumo utakuwa na uwezo kutoa alama za usalama ambazo
  • mtu hawezi kughushi,
  • Kupitia mfumo huu Mwandishi wa Habari atakua na uwezo wa kuomba na kupata kitambulisho chake physical ID. Mfumo uwe na uwezo wa kuonesha taarifa kwenye ukurasa wa nyuma back-end ambazo zitahakikiwa na kutumiwa na Idara ya Habari kutoa kitambulisho (Press Card) kwa njia ya mtandao.
  • Mfumo utakuwa na uwezo wa kumpatia mwandishi wa habari taarifa kabla ya muda wa kuisha matumizi ya kitambulisho chake (alert when the ID is about to expire) pia utakua na kumtumia ujumbe mfupi kupitia simu ya mkononi.
  • Mwandishi anapoomba kitambulisho mfumo utakuwa na uwezo wa kumpatia namba ya malipo “control Number” ya kulipia mtandaoni. Pia Mwandishi akishalipia malipo yake yataonekana na kupitishwa na mamlaka husika (approved).
  • Mfumo utamwezesha Mwandishi wa Habari kupakia nyaraka muhimu kama vile vyeti vya taaluma kwa ajili ya uhakiki (VERIFICATION).
  • Mfumo uwe na eneo la waombaji wa ndani na nje ya nchi pia uweke vigezo na mambo muhimu ya kupakia (Requirements) kwa waandishi wa nje.
  • Mfumo utakuwa na mwonekano wa aina mbili (madirisha) kwa ajili ya waandishi wa ndani na wa nje (International)
  • Mfumo utakuwa na uwezo wa kuhakiki taarifa za waandishi kwa kuunganishwa na mifumo mingine ya serikali kama GePG, NIDA, NECTA, Uhamiaji n.k kwa ajili ya malipo, uhakiki wa vyeti na taarifa (Verification).
  • Mfumo utakuwa na uwezo wa kuondoa wale wote waliokosa sifa/wasiohuisha taarifa zao pale wanapotakiwa kufanya hivyo.
  • Mfumo uwezeshe watumiaji kuweka sani mahali panapohusika (Digital signature)
  • Mfumo uweze kuruhusu taarifa hususani kitaaluma na eneo la kazi kupatikana kwa njia ya msimbo papo (QR CODE).
 
Back
Top Bottom