WADAU HII IMEKAAJE?
Mrema aitolea uvivu Chadema
Saturday, 25 June 2011
NA PETER ORWA, DODOMA
MBUNGE wa Vunjo, Augustino Mrema,(TLP), ameiomba serikali kuwadhibiti wanasiasa wanaochochea wananchi kuandamana, kwa kuwa kufanya hivyo hakuna tija kwa taifa.
Pia, amesema, wanasiasa wanaoendeleza maandamano na ghasia kama njia ya kutimiza malengo yao ya kisiasa, wanahatarisha usalama wa nchi, na hilo lina ushahidi duniani kote.
Ingawa Mrema hakutaja chama wala jina la mwanasiasa, Chadema imekuwa ikihamasisha maandamano, na baadhi ya viongozi wake kutoa kauli za uchochezi zenye kuashiria kuvuruga amani na utulivu nchini.
Katika mchango wake katika hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi ya waziri mkuu, iliyowasilishwa juzi bungeni na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Mrema alisema, haamini kwamba muafaka wa kijamii na kisiasa unaweza kupatikana kwa maandamano na ghasia.
Mrema alisema, athari zake hazina mipaka ya vyama, na alionya wanasiasa kwamba vitendo hivyo ni vya hatari dhidi ya amani ya nchi. Aliwasihi kuunga mkono hotuba hiyo ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliyewataka wasitumie ghasia na maandamano kwa ajili ya kutimiza malengo yao ya kisiasa.
"Nataka kumuunga mkono waziri mkuu kwa hili la amani, halina chama tawala wala upinzani. Tusichezee vurugu na hasa maandamano," alisema Mrema. Alisema, historia inaonyesha kuwa, vitendo vya maandamano mara zote vimeishia katika mikakakati ya kutaka kupindua serikali, kitendo kinachoonyesha hakina tija, zaidi ya vurugu, na wananchi wanaoandamana sio wanaotwaa madaraka.
Mrema aliwaponda wanasiasa hao bila kuwataja majina kwamba, kufurukuta kwao na kufanya vitendo vya ghasia, kumeonyesha havina tija kwani hawajawahi kufikia kupata kiwango cha asilimia 28 ya kura alizopata yeye alipogombea urais mwaka 1995 kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi.
"Nawaomba wanasiasa wa pande zote mbili, wote ni wadau. Tusitumie malengo yetu ya siasa kuchochea vurugu na hasa maandamano," alisema Mrema aliyetumia mifano ya athari za ghasia katika nchi mbalimbali zikiwemo za Kenya, Madagascar, Misri na Sudan.
Katika hatua nyingine, Mrema ameiomba serikali ianze kumlipa mshahara kama naibu waziri mkuu mstaafu, wakati wa uongozi wa serikali ya awamu ya pili. Mrema alisema, ingawa cheo hicho hakipo katika stahiki za kikatiba, lakini kwa vile ulikuwa ni uamuzi rais kumteua kushika wadhifa huo, basi ni stahili yake.
"Mbona haki yangu haipatikani? Nipatieni japo asilimia 20. Msione simba kanyeshewa mkadhani ni nyani. Ili niendelee kutetea mambo mengi ninayoyajua, naomba haki yangu," alisema na kusababisha wabunge kuangua kicheko.
Lowassa awaponda
MBUNGE wa Monduli, Edward Lowassa, ameitaka serikali kuwa jasiri kwa kufanya maamuzi magumu katika masuala yanayohusu maendeleo. Pia, Lowassa ambaye alijiuzulu nafasi ya waziri mkuu, Februari 6, 2008, amekemea watu wanaobeza mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wa serikali ya CCM katika miaka 50 ya Uhuru.
Alisema ili taifa lipate mafanikio makubwa kiuchumi, viongozi hawana budi kuthubutu katika maamuzi. "Serikali ya CCM imefanya imefanya mambo mengi tangu Uhuru," alisema Lowassa.
Alisema hayo alipochangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi ya waziri mkuu, iliyosomwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, juzi, ambapo pamoja na mambo mengine aliisifu kuwa ni nzuri.
Alianisha maeneo ambayo serikali inapaswa kuyafanyia kazi katika dhana hiyo ya kuthubutu kuwa ni kukopa fedha kutoka nje kwa kutumia dhamana ya akiba ya gesi iliyopo ukanda wa Mtwara, ili kufadhili maendeleo kitaifa.
"Eneo mojawapo la kuthubutu ni reli kati ya Dar es Salaam na Kigoma. Tunaweza na wala tusiogope," alisema.
Lowassa aliyekuwa akishangiliwa na wabunge wakati akitoa mchango wake huo, alitaja reli ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia Tanzania (TAZARA), kuwa ni sehemu nyingine muhimu ya kuhuishwa kwa fedha za mkopo ili kuboresha uchumi.
Alisema miradi itokanayo na fedha zitakazokopwa, ziwekewe utaratibu maalumu wa kuwa na manufaa kwa wananchi vijijini ambako ndiko kwenye Watanzania wengi. Pia, aliishauri ofisi ya waziri mkuu ipunguziwe majukumu, ili ifanye kazi kwa umahiri ambapo alipendekeza Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ijitegemee.
"TAMISEMI ni kubwa ni kila kitu, ipunguzwe maana ni kila kitu 'bureaucracy' (urasimu) ni kubwa katika muundo wake," alisema na kutaja idara na ofisi nyingine zilizoko chini ya ofisi ya waziri mkuu kuwa ni za maafa, baraza la uwezeshaji, na uratibu na bunge.
Lowassa aliwasifu viongozi waliotangulia katika awamu tatu zilizopita za uongozi wa nchi kwamba, wana mchango mkubwa katika kujenga msingi wa mafanikio. Alitumia fursa hiyo kuwakemea wanaobeza hatua ya maendeleo iliyopigwa kutokana na uongozi wa serikali ya CCM katika miaka 50 ya Uhuru, akiorodhesha mafanikio kama ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kwa gharama ya sh. trilioni moja, asilimia 95 ya watoto wenye umri wa kwenda shule kuhudhuruia elimu ya msingi na wingi wa sekondari za kata.
Alitaja hatua zingine za maendeleo ni mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda mkoani Shinyanga, miradi ya uchimbaji gesi Mtwara, na ukuaji wa uchumi hadi kufikia kiwango cha asilimia saba kwa sasa.
"Kwa waliokuwepo wakati huo, nakumbuka katika miaka 10 ya kwanza ya Uhuru, Mwalimu Nyerere alisema, mtu akija kwa jeuri na fedhuli, akikuuliza Tanzania mna nini, wewe mjibu kiungwana, tuna amani," alisema Lowassa. Pia, ameiomba serikali kutoa msaada wa chakula ili kuwanusuru njaa wananchi wa Monduli.
Source: UHURU