Tarehe 16/05/2011 nilisoma Tangazo kwamba serikali imepima viwanja Kinyerezi inaviuza kwa bei ya mita moja ya mraba shiringi 10,000, 15,000, 20,000, 5,000 na 8,000 kwa Viwanja vya makazi, makazi na biashara, huduma za jamii na ibada respectively, bei ambazo Watanzania wachache (hasa humu JF)wenye uelewa walilalamikia, mimi nikiwa mmoja wao, Pamoja na hayo jana nikaamua kwenda kujipinda kulipia form, leo nimeenda mahala husika(viwanja vya anautogro) na pay in slip ili kuchukua form za maombi, sijaamini nilichokiona kwasababu nimekuta kuna foleni ya watu wasiopungua miatano(500) na baadhi yao wana form zaidi ya moja mkononi na mbaya zaidi watu wanazidi kumiminika kulipia forms. Binafsi nilijua tutakuwa wachache sana tulioamua kujilipua kwa hizo bei, ndipo nikajua kumbe Watanzania wana pesa nyingi sana haiwezekani bei kubwa namna ile kukawa kuna ushindani mkubwa kiasi hicho. baada ya kudodosa dodosa nikaambiwa viwanja tunavyogombea vipo jumla 150 tu ambavyo kimsingi watapata watu 150 tu. Kwasababu mimi naamini haki itatendeka hivyo mtu wa kwanza kuviomba mpaka wa miamoja hamsini(150) ndiyo watakaopata, sisi wengine imekula kwetu sikutaka niendelee kupoteza mda wangu nikaamua kujiondokea na kuiachia serikali 20,000 ya form.
Nikiwa naondoka nilijaribu kuingizia habari za bei za viwanja kwa watu niliokuwa karibu nao wengi walionyesha hawajui bei yake na mbaya zaidi hawajui hata unaposema Mita moja ya mraba unamaanisha nini, na chakustaajabisha zaidi wengi wa watu wa namna hiyo wamelipia form za maombi ya viwanja zaidi ya kimoja.
Mtu mwingine nilipo muuliza alinijibu kwamba yeye anataka kiwanja kimoja tu cha mita 40 kwa 30 ili jumla iwe mita 70 maana ana 700,000 kwenye akaunti yake ambayo alikuwa anatafuta sana eneo la kujenga kibanda cha kujihifadhi.
Kutokana na niliyoyaona leo serikali inatakiwa inapotoa tangazo itoe kwa makusudi elimu ya ziada kwa umma maana siyo wote wanaelewa nini maana ya mita moja ya mraba, wangetoa mfano kwa kiswahili kwamba kiwanja cha 40 kwa 30 ni Milioni12 kusingekuwa na msongamano wa watu wengi kiasi kile, vinginevyo itaishia kuzikusanya elfu ishiriniishirini za Watanzania wengi ambao wana elimu duni.