Moyo Mpweke | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Moyo Mpweke

Discussion in 'Jukwaa la Lugha' started by Mzee Mwanakijiji, Oct 25, 2009.

 1. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #1
  Oct 25, 2009
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,362
  Likes Received: 6,393
  Trophy Points: 280
  MOYO MPWEKE
  Ni mti uso tunda, vivyo hivyo moyo pweke,
  Unabakia kukonda, kulikosa tunda lake,
  Tena huo umepinda, wangojea siku yake,
  Moyo ule usopenda, huo ndio moyo pweke!!
  Ndege asiye kiota, vivyo hivyo moyo pweke,
  Aenda akitafuta, wapi apaite pake,
  Mtini utamkuta, atafuta vya wenzake,
  Moyo ule usopendwa, huo ndio moyo pweke!!
  Meli isiyo nahodha, vivyo hivyo moyo pweke,
  Itaegeshwa forodha, bandarini isitoke,
  Ikasababisha adha, safarini isifike,
  Moyo ule usopenda, huo ndio moyo pweke!!
  Bahari iso samaki, vivyo hivyo moyo pweke,
  Mvuvi katahamaki, na mtumbwi ausweke,
  Amebaki kudhihaki, ndoana azitundike,
  Moyo ule usopenda, huo ndio moyo pweke!!
  Ni gari liso mafuta, vivyo hivyo moyo pweke,
  Lenda likikitakita, abiria walishuke,
  Wese wakalitafuta, waendako wakafike,
  Moyo ule usopendwa, huo ndio moyo pweke!!
  Simba asiyenguruma, vivyo hivyo moyo pweke,
  Enda akihemahema, wanyama wasishituke,
  Amekosa tamu nyama, avizia vya wenzake,
  Moyo ule usopenda, huo ndio moyo pweke!!
  Tafuta wa kumpenda, awe wako uwe wake,
  Penzi lenu mje unda, mioyo ifarijike,
  Na mola aje walinda, uwaondoke upweke,
  Moyo ule upendao, wataka nao upendwe!!

  Na. M. M. Mwanakijiji (Sauti ya Kijiji)
   
Loading...