Basi la Mohamed Trans laua 27 mkoani Tanga
na Mwandishi Wetu
ZAIDI ya watu 27 wamefariki dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa katika ajali mbaya ya barabarani, iliyotokea mkoani Tanga jana.
Habari kutoka mjini Tanga ambazo Tanzania Daima ilizipata kutoka kwa baadhi ya walioshuhudia ajali hiyo, zilisema kuwa ajali hiyo ilihusisha basi la Kampuni ya Mohamed Trans, lililokuwa likitokea mjini Mombasa, kwenda jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo mashuhuda hao walisema kuwa idadi ya watu waliofariki dunia katika ajali hiyo ilifikia 30 hadi jana saa mbili usiku na kazi ya uokoaji ilikuwa ngumu kutokana na miili mingi kungangania kwenye mabati ya basi hilo.
Akizungumza na Tanzania Daima jana kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi mkoani Tanga, Simon Sirro, alisema kuwa ajali ilitokea majira ya saa 10 alasiri katika Kijiji cha Kombo, wilayani Korogwe.
Alisema basi hilo lilipata ajali hiyo baada ya kupasuka matairi yake yote mawili ya mbele na kupoteza mwekekeo na kisha kugongana uso kwa uso na lori lililokuwa limesheheni masanduku ya bia.
Natoka eneo la tukio kwenda katika Hospitali ya Wilaya ya Korogwe, waliofariki katika eneo la tukio walifikia 27, akiwamo dereva na utingo wa lori na wengine wengi waliopoteza maisha, walikuwa ndani ya basi hilo. Ni ajali kubwa na ya kutisha kwa kweli, alisema Kamanda Sirro.
Alisema kati ya waliofariki dunia, wanaume ni 21 na wanawake sita, ambao walifariki dunia mara baada ya ajali hiyo kutokea katika eneo la tukio.
Alisema kuna uwezekano mkubwa wa idadi ya waliofariki dunia kuongezeka, kwani wapo waliofariki dunia wakati wakiwa njiani kupelekwa hospitali kwa ajili ya matibabu.
Kwa mujibu wa Kamanda Sirro, majina ya waliopoteza maisha katika ajali hiyo kubwa kutokea katika siku za hivi karibuni, yanatarajiwa kutangazwa leo.
Moja ya matukio ya kusikitisha ni pale baadhi ya wananchi wanaoishi jirani na mahali ajali hiyo ilipotokea, kupora na kuiba vitu mbalimbali kutoka kwa majeruhi na marehemu waliokuwa wakisachiwa kwenye mifuko yao.
Vitu vilivyokuwa vikiporwa ni simu za mkononi, fedha, saa, viatu na mabegi, mali ya majeruhi na watu waliopoteza maisha katika ajali hiyo.
Ajali nyingine kubwa ya aina hiyo, ilitokea mkoani Tanga Januri 12 mwaka huu ambapo watu 27 walifariki dunia baada ya basi la Kampuni ya Tashrif walilokuwa wakisafiria kutoka Dar es Salaam kwenda Tanga kuligonga lori lililokuwa limebeba shehena ya magogo.
Wengi waliokufa ni abiria waliokuwa wamesimama katikati ya basi hilo wakiwa kwenye harakati za kutaka kushuka, ambapo walijikuta wakichanwa vipande vipande na magogo hayo yaliyokuwa kwenye lori hilo lililoegeshwa kando ya barabara hiyo.
Basi la Mohamed Trans laua 27 mkoani Tanga