NADHARIA Mkojo ni dawa ya magonjwa mbalimbali

Taarifa hii ni nadharia tu, tumeitolea ufafanuzi kwa kadiri ilivyowezekana
Magonjwa mbalimbali yametufanya binadamu kubuni tiba aina mbalimbali ambazo zitatusaidia kuondokana na magonjwa hayo. Moja ya tiba iliyobuniwa na binadamu ni pamoja na mkoja wa binadamu kama tiba ya magonjwa mbalimbali.

Tena unaambiwa ukipata mkojo wa asubuhi ndio kiboko ya magonjwa kama anavyosema mdau hapa wa mtandao wa JF kuwa Mkojo wa asubuhi ni dawa murua

Shuhuda ni nyingi sana, moja ikiwa ni ya mdau huyu wa JF kutibu maumivu ya meno kwa kunywa mkojo wa asubuhi

Miaka ya 2013-2016 nchini Tanzania kulitokea kundi la wanunuaji wa mkojo wa binadamu kwa madai kuwa unaenda kutumika kama dawa.

Katika ukuaji wangu, mimi ni mmoja wa walioshawishika kutumia mkojo kwa kunywa au kupaka. Kwa kutokuzingatia suala la afya, nimewahi pia kunywa hadi mikojo ya wenzangu. Lakini pamoja na matumizi ya mkojo, sijawai kuona ufanisi wowote.

Pia ukienda Search Engine kama Google, ukiandika 'Mkojo ni Dawa" utapata mapendekezo kedekede kuhusu magonjwa yanayotibika kwa matumizi ya mkojo. Hii inaashiria kuwa kuna matumizi makubwa ya mkojo kama tiba.

Sasa hivi unaambiwa lile kojo la mwanamke linalotoka akifika mshindo ni kiboko kuliko mkojo wa kawaida.

mkojo.jpg

Mimi sina majibu ila ningependa ufafanuzi zaidi kuhusu sayansi ya mkojo kuwa dawa.
 
Tunachokijua
Mkojo ni mojawapo ya takamwili zinazotolewa na binadamu ambazo hupatikana kirahisi. Kila mtu hutoa kiasi fulani cha mkojo kwa siku. Kwa sababu ya wingi wake, tiba nyingi za watu zimehusisha mkojo kwa njia moja au nyingine ili kutibu hali mbalimbali za kiafya.

Kihistoria, mkojo umetumika kama tiba ya watu kwa hali kama vile, Pumu, Ugonjwa wa Arthritis (maungio ya mifupa), Mzio (Allergy), Saratani, Mmeng'enyo hafifu wa chakula, Kipanda uso (Migraine) na Ugumba.

Mwaka 1945, John W Armstrong, Mtaalam wa tiba Mbadala nchini Uingereza alichapisha kitabu chake kinachofafanua nguvu ya mkojo katika kutibu magonjwa.

Kitabu hicho chenye jina la "The Water of Life:A Treatise on Urine-therapy" kilidai kuwa watu walio kwenye siku za mwisho za uhai wao hawahitaji kula na kunywa chochote isipokuwa mkojo wao wenyewe. Pia, wanaweza kuutumia mkojo huo kupaka ngozi zao.

Nchini Nigeria, baadhi ya jamii hadi sasa hutumia mkojo kama mojawapo ya tiba asili za kuwasaidia watoto wenye degedege.

Aidha, watu kadhaa ikiwemo Waziri Mkuu wa Zamani wa India, Morarji Desai amewahi kutumia mkojo kama tiba.

Watu wengine pia katika nyakati kadhaaa wamewahi kukiri kutumia mkojo kutibu shida mbalimbali za kiafya na kupata majibu chanya ya shida zao.

Ukweli wa madai haya
Licha ya utajiri wa matibabu ya kienyeji, sayansi inasisitiza kuwa kwa mkojo si salama pia sio njia nzuri hata ya kuongeza maji mwilini.

Hata hivyo, Rene Javier Sotelo, MD, Daktari Bingwa wa Mfumo wa Mkojo kutoka Chuo cha Keck Medicine of USC ambaye pia hufanya upasuaji wa kutumia roboti kutibu aina mbalimbali za Saratani za mfumo wa mkojo anasema kuwa sayansi haikubaliani na madai hayo, na kwamba hakuna ushahidi wa moja kwa moja unaothibitisha ufanisi wake.

Maelezo haya yanatiliwa mkazo pia na chapisho la Makala ya BBC ya Julai 21, 2023, ilimpomhoji Dkt. Zubair Ahmad.

“Watu wengi wanaamini kwamba ikiwa huna matatizo yoyote ya figo, mkojo wako ni safi. Ni sawa maadamu uko ndani ya mwili lakini ukitoka nje unaweza kuambukizwa na bakteria. Kunywa mkojo katika hali kama hiyo kunaweza kusababisha matatizo makubwa ya kiafya.

Hakuna ushahidi wa kisayansi kwamba kunywa mkojo kuna manufaa.

Kupitia mkojo tunaondoa uchafu mwilini. Kwa hiyo hakuna msingi wa kisayansi wa kunywa mkojo taka kuwa na manufaa.”
Alisema Dkt. Zubair.

Hapa kuna muhtasari wa kwanini haupaswi kamwe kunywa mkojo:

Hatari za kunywa Mkojo
Mkojo ni mchanganyiko wenye nguvu wa chumvi na kemikali ambazo mwili wako hujaribu kuondoa.

Kemikali hizi zinaweza kusababisha shida kubwa za kiafya ikiwa utazitumia. Zaidi ya hayo, mkojo hautoi faida za ziada kiafya zisizoweza kupatikana kwa kutumia vyakula na vinywaji vingine.

Sababu ya kawaida ya kunywa mkojo ambayo huoneshwa kwenye sinema na maigizo ni kuzuia upungufu wa maji mwilini. Ikiwa mtu amepotea baharini au jangwani, wakati mwingine huoneshwa kama kunywa mkojo husaidia kukata kiu na kutunza uzito awa mwili.

Mkojo wa wastani wa mtu mzima una kiasi kikubwa cha chumvi, ambayo hujilimbikizia zaidi ikiwa mhusika atapatwa na upungufu wa maji. Watu walio na upungufu wa maji mwilini wanaweza kufikia haraka viwango vya juu vya sodiamu kwenye mkojo.

Kutumia sodiamu zaidi kunahusishwa na kuongeza kiu yako.

Viwango vya juu vya sodiamu katika mwili wako husababisha haraka kuhisi kiu. Kwa kunywa mkojo, ambao una mkusanyiko mkubwa wa sodiamu, unaweza kujiwekea kitanzi cha kiu kubwa hivyo kukufanya uhitaji kunywa maji mengi zaidi.

Kuingiliwa na Dawa
Dawa nyingi hutolewa kwenye mkojo baada ya kufanya kazi mwilini. Dawa hizi huacha mwili wako katika hali sawa na hali ambayo ziliingia kwenye mwili wako zikiwa hazijavunjwa. Dawa zinazoweza kutolewa kwa mfumo huu ni pamoja na penicillin na dawa zingine zinazochanganyikana na maji.

Kwa kunywa mkojo wenye dawa yoyote kati ya hizi, unaziingiza dawa husika kwenye mwili wako mwenyewe. Ikiwa ni dawa ambazo tayari unachukua, utaongeza dozi zaidi ya inavyopaswa kuwa.

Ikiwa unakunywa mkojo wa mtu mwingine, basi unaweza kuingiza mwilini dawa ambazo hukupaswa kuzitumia. Hii inaweza kusababisha athari hasi na matatizo makubwa ya afya.

Maambukizi
Ukusanyaji wa mkojo unaweza pia kuwa chanzo cha bakteria na virusi kutoka kwa sehemu za siri za mhusika aliye chanzo cha mkojo huo. Baadhi ya bakteria na virusi hawa wanaweza kusababisha maambukizi makubwa na hatari kwa afya.

Sumu
Mfumo wako wa mkojo hufanya kazi kubwa ya kuondoa vitu vyenye sumu mwilini. Wakati vitu hatari vinapoanza kukusanyika katika mwili wako, mkojo ni mojawapo ya njia kuu zinazotumiwa kuziondoa.

Kitu chochote ambacho figo zako huchuja kutoka kwa mwili wako huingia kwenye mkojo ili kuondolewa.

Kwa kunywa mkojo, unatumia sumu hizi ambazo mwili wako ulikusudia kuondoa. Hii inaweza kusababisha uharibifu wa figo au ugonjwa kwani viungo hivi vinahitaji kufanya kazi kwa bidii ili kushughulikia kuongezeka kwa mkusanyiko wa vitu vya sumu.

Hitimisho
Pamoja na kukosa uthibitisho wa kisayansi, JamiiForums inachukuli suala hili kama nadharia inayopaswa kufanyiwa utafiti zaidi kwa kuwa baadhi ya watu wamekiri kuwahi kupona changamoto zao za kiafya kwa kutumia mkojo.

Uwepo wa tafiti nyingi za kisasa zinazoangazia eneo hili unaweza kusaidia kutoa mwangaza mpya ambao pengine unaweza kuwa msaada mkubwa katika kutibu magonjwa.

Hata hivyo, kwa hatua ya sasa, ni muhimu kufuata masharti ya wataalam wa afya wanaosisitiza kutotumia mkojo kwani sio salama kwa afya.

Similar Discussions

1 Reactions
Reply
Back
Top Bottom