Mkasa wa kweli: Kisiwa cha harishi

Mkasa wa kweli: Kisiwa cha harishi

SEHEMU YA 24



Yasmin akanipeleka bafuni kisha akaondoka. Nilioga haraka haraka. Nilipomaliza niliondoka bafuni na kumbishia Yasmin mlango.
Yasmin alinifungulia mlango na kuniambia.
“Karibu”
Niliingia mle chumbani alimokuwa. Hamkuwa na kiti. Akaniambia.
Kaa kitandani”
Nikakaa.
“Unajisikia vizuri kidogo?” akaniuliza.
Nilijaribu kutabasamu bila kufanikiwa. Niliishia kubenua midomo tu, uso haukukunjuka.
Endelea sasa
Yasmin akaja kukaa kando yangu.
“Unajua maisha?” akaniuliza. Sikujua alikuwa na maana gani.
“Maisha ni nini?” nikamuuliza.
“Maisha ya mwanaadamu ni mtihani. Lolote linalokufika liwe zuri au baya ni mtihani kwako. Kama wewe ni muumini unatakiwa ulijue hilo”
“Ndio ninalijua”
“Mungu hashindwi kutuokoa sisi waja zake tunaomtegemea yeye ila anatupa mitihani kuona ni kwa kiasi gani tunaweza kuweka matumaini kwake na kwa jinsi gani tunaweza kumuomba kwa unyenyekevu katika siku hii ambayo mimi na wewe tunahitaji sana msaada wake”
Ndani ya moyo wangu nilikiri kuwa Yasmin alikuwa amenieleza maneno ya maana kuliko aliyowahi kunieleza wakati wowote. Nilifarijika kuona juhudi zake za kunitia moyo zilifanikiwa kwa kiasi kikubwa na kuamsha imani yangu.
Nikajiambia laiti kama ningekuwa na mke kama Yasmin nisingeshindwa kimaisha hata itokee shida ya kiasi gani
Hatimaye jua lilikuchwa. Giza lilianza kuingia. Yasmin aliwasha taa za nyumba nzima. Alikuwa ameniacha mle chumbani mwake, akanifuata na kuniuliza. “Utakula chakula?”
Nikatikisa kichwa.
“Sitakula”
“Hutakula hata kidogo”
Nikaendelea kutikisa kichwa.
“Sitakula”
Yasmin akakaa karibu yangu.
“Usiku ndio huu” akaniambia.
“Kwani Harishi atakuja muda huu?”
“Anaweza kuja wakati wowote kutoka sasa hadi alfajiri”
“Anakujaje?” nikamuuliza Yasmin huku nikiitazama ile chupa iliyokuwa juu ya kabati.
“Anakuja kama moshi. Unajaa ndani ya ile chupa kisha unatoka. Unapotoka unabadilika na kuwa jini”
“Na ni kwanini anakuja hivyo?”
Yasmin akabetua mabega yake
“Sijui lakini ondoa hofu. Mwisho wa mateso yetu utakuwa leo”
Sikusema kitu tena nikanyamaza kimya. Tulikaa kimya kwa muda mrefu. Ile shauku ya kuzungumza ilikuwa imetuishia. Tukaamua kukaa tu kusubiri muda wetu.
Tulikuwa tumekaa chini tumeelekezana migongo. Kila mmoja alielekea upande wake. Yasmin alipochoka au kuhisi kusinzia aliuegemeza mgongo wake kwenye mgongo wangu.
Kitu gani kilimfanya Yasmin asipande kitandani na kulala?
Alikuwa amejitolea kufa na mimi. Alikuwa ameamua akae na mimi pale chini hadi Harishi atakapokuja.
Ilikuwa kama saa saba usiku nywele zangu zilipoanza kunisisimka. Nikayapeleka macho yangu kwenye ile chupa ya Harishi iliyokuwa juu ya kabati. Moyo wangu ulishituka nilipoiona chupa inaingia moshi kwa ndani. Nikamgutusha Yasmin aliyekuwa anasinzia.
“Yasmin!”
“Abee!” Yasmin akaniitikia.
“Tazama ile chupa!”
Yasmin akageuza uso wake na kuitazama chupa hiyo.
“Usimuogope kiumbe aliyeghulukiwa kama wewe. Muogope aliyeghuluku” Ndilo neno aliloniambia Yasmin.
Ule moshi uliendelea kujaa ndani ya ile chupa. Kifiniko cha chupa hiyo kilikuwa pembeni. Moyo haukunipa. Mara moja nikanyanyuka na kwenda kando ya lile kabati. Niisubiri ule moshi ujae kabisa kisha nikakichukua kile kifiniko na kukifunga kwenye mdomo wa ile chupa.
Baada ya sekunde chache nilisikia sauti ya Harishi kutoka kwenye ile chupa.
“Nani amefunga kizibo?”
Sote tukanyamaza kimya.
Ile sauti ikasikika tena.
“We Yasmin si nilikwambia usifunge hiki kizibo?”
Tukaendelea kunyamaza lakini moyo wangu ulikuwa ukienda mbio.
“Fungua sasa!” ile sauti sasa ilifoka.
“Usifungue!” Yasmin akaniambia huku akinifuata.
“Ahaa! kumbe uko na hawara yako! Sasa mtanitambua”
“Sifungui!” Yasmin akasema kwa jazba.
“Nimekwambia fungua, nataka nitoke!” Sauti ikafoka.
“Toka mwenyewe!” Yasmin akajibu.
“Yasmin umechoka kuishi? Nakwambia nitakuua wewe na hawara yako!” Sauti ya Harishi iliendelea kuunguruma kwa hasira.
“Ndio tunavyotaka utuue. Tuue sasa hivi!” Yasmin aliendelea kujibu.
“Wewe kijana nani amekuruhusu ufunge hiki kizibo, hujui kuwa hii ni nyumba yangu?” Sauti ya Harishi ikaniuliza.
“Nimemruhusu mimi akifunge. Nimeshachoka na wewe. Kama unaweza kutoka toka mwenyewe utuue. Sisi tunasubiri kufa tu”
“Yasmin umeamua kunigeuka leo?” Sauti ya Harishi sasa ilukuwa imerudi chini. “Nifungulie mke wangu. Nimekuletea zawadi nzuri”
“Sitaki zawadi yako. Njoo utuue!”
“Nani amekwambia kama nataka kuwaua?”
“Si ndio kazi yako kuua watu. Watu wote wa kisiwa hiki si umewamaliza wewe!”
“He he he!” Harishi alitoa kicheko kilichoonesha wazi kuwa ni cha uongo. Kisha akauliza kwa ukali.
“Sasa utakifungua kizibo au hufungui?”
“Sifungui!” Yasmin akamjibu.
“Wewe kijana fungua kizibo hicho?’ Sauti ya Harishi ikanigeukia mimi.
“Usifungue. Mwache atoke mwenyewe. Sisi tumeshajitolea, liwalo na liwe!” Yasmin akaniambia.
Wakati wote nilikuwa najiuliza kama Harishi alikuwa hawezi kutoka mwenyewe kwenye ile chupa mpaka atuombe sisi tufungue kizibo. Nikataka kupata uhakika kama kweli Harishi alikuwa amenasa na asingeweza kutoka bila msaada wetu.
ITAENDELEA
 
SEHEMU YA 25


ILIPOISHIA...
“Wewe kijana fungua kizibo hicho?’ Sauti ya Harishi ikanigeukia mimi.
“Usifungue. Mwache atoke mwenyewe. Sisi tumeshajitolea, liwalo na liwe!” Yasmin akaniambia.
Wakati wote nilikuwa najiuliza kama Harishi alikuwa hawezi kutoka mwenyewe kwenye ile chupa mpaka atuombe sisi tufungue kizibo. Nikataka kupata uhakika kama kweli Harishi alikuwa amenasa na asingeweza kutoka bila msaada wetu.
SASA ENDELEA...
Nikamwambia Yasmin “Tusifungue hii chupa tuone nini kitatokea”
“Wewe achana naye, kama akitoka mwenyewe na atoke, potelea mbali!”
Nilikuwa nimesimama kando ya lile kabati. Yasmin alisimama karibu na kitanda. Macho yetu sote yalikuwa kwenye ile chupa.
Ingawa nilikuwa nimejikaza kiume, hofu ilikuwa ikitambaa kwenye mishipa yangu. Yasmin hakuonesha kuwa na hofu hata chembe. Nilishangaa kuona msichana ambaye siku zote nilimuona dhaifu, siku ile alikuwa amejaa ujasiri usio kifani. Hapo niliamini kweli kuwa Yasmin alikuwa amejitolea kufa kupona.
Ile sauti ya Harishi iliyokuwa ikitoka kwenye chupa ilipotea lakini ule moshi uliendelea kuonekana. Kwanza ulionekana moshi wa rangi nyeusi kisha ukabadilika na kuwa wa rangi nyeupe. Baada ya muda kidogo ulibadilika tena na kuwa wa rangi nyeusi.
Mawazo yangu yote yalikuwa kwenye kifo kibaya kilichokuwa kinatungoja.
. Nilijua kuwa Harishi angekizibua mwenyewe kile kizibo na kutoka. Hapo hasira zake zisingekuwa na kifani. Nilipata wazo la kumwambia Yasmin tukimbie lakini nikajiuliza tutakimbilia wapi usiku ule? Na ni wapi ambapo Harishi hataweza kufika?
Muda uliendelea kupita. Tuliona Harishi hatoki kwenye ile chupa kama ilivyo kawaida yake. Aliendelea kututaka tukifungue kizibo kwa sauti ya upole akiahidi kwamba hatamuua yeyote.
Nikahisi inawezekana kwamba kitendo kile cha kuwahi kukifunga kile kizibo cha cha chupa wakati Harishi yumo ndani ya chupa ile akiwa katika umbile la moshi, kilikuwa kimemzuia kutoka na hakuwa na uwezo tena wa kutoka mwenyewe.
Hapo hapo nikazikumbuka simulizi za wazee wa zamani ziizosema kwamba majini walikuwa wakifungiwa ndani ya chupa na kutoswa baharini pindi wanapofanya makosa.
Kumbe ni kitu kinachowezekana kweli, nikajiambia.
“Sisi tunaiondoa hii chupa!” nikasema kwa sauti ili kusikia Harishi atajibu nini.
“Usiiondoe. Nataka mnifungulie niende zangu” Sauti ya Harishi ikasikika kutoka kwenye ile chupa.
“Hakuna atakayekufungulia muuaji wewe”Yasmin akamwambia.
“Nifungulie nitakurudisha kwenu”
“Mbona siku zote hukunirudisha?”
“Nakwambia kweli kabisa. Ukinifungulia nitakurudisha kwenu Comoro”
“Kwenda zako, mimi si mjinga wa kukufungulia wewe.. Bora ubaki humo humo. Siku zako zimeshafika”
Yasmin akanigeukia mimi na kuniambia.
“Twende tukaizike hii chupa”
“Hapana.. hapana. Msiizike!” Sauti ya Harishi ikalalamika.
“Mimi naona tukaizike baharini” nikamwambia Yasmin.
“Hapana…hapana. Msiitose baharini!” Ilikuwa sauti ya Harishi lakini hatukuipatiliza.
“Niliwahi kusikiakule kwetu kwamba majini wanafungiwa kwenye chupa na kutoswa baharini” nikamwambia Yasmin.
“Tukiitosa baharini itaelea na kisha itarudishwa ufukweni na mawimbi”
“Labda tuifunge kamba na jiwe ili izame chini”
“Nyinyi msifanye hivyo. Mimi nimeshwambia sitawaua. Nifungulieni niende zangu” Harishi akatuambia.
“Basi tutaifunga na jiwe tizamishe” Yasmin akasema.
“Hamsikii hivi ninavyowambia. Nyinyi mnataka mfe?” Sauti ya Harishi ikasikika kutoka kwenye chupa.
“Utakufa wewe, mbona huwezi kutoka !” Yasmin akamwambia.
“Tusubiri kuche” nilimwambia Yasmin.
“Linaweza likatoka!”
“Usiku huu hatutaweza kwenda baharini”
“Basi tusubiri”
Tukasubiri. Harishi sasa alikuwa amenyamaza. Sauti yake haikusikika tena. Lakini ule moshi uliendelea kuonekana ndani ya ile chupa. Ulikuwa unabadilika rangi kila mara.
Nipoona kunaanza kupambazuka nilijaribu kuishika ile chupa. Ilikuwa nyepesi kama chupa tupu.
Yasmin alileta kapu. Akaniambia tuitie kwenye kapu.
“Tutapata wapi kamba?” nikamuuliza.
“Twende nayo, tutapata kamba huko huko”
Tukatoka nje ya lile jumba. Mimi ndiye niliyeshika lile kapu. Kulikuwa na baridi kali lakini tulijikaza hivyo hivyo. Wakati tunaelekea baharini tuliokota kipande cha kamba na jiwe tukavitia kwenye kapu.
Tulipofika ufukweni mwa bahari tuliitoa ile kamba tukaifunga kamba kisha ile kamba tukaifunga na jiwe.
Tulimsikia Harishi akisema maneno ndani ya ile chupa lakini sauti yake ilikuwa ya chini kiasi kwamba hatukuelewa anasema nini.
Mimi na Yasmin tulijitosa kwenye maji. Tukatembea kwa miguu hadi tulipofika kwenye maji mengi tukaanza kuogelea kwenda mbali zaidi tukiwa na ile chupa tuliyoifunga jiwe.
“Tuizamishe hapa hapa” Yasmin akaniambia.
Nikaiachia ile chupa, ikazama ndani ya maji taratibu. Hatukuiona tena.
“Sasa turudi. Zama za Harishi zimekwisha” Yasmin akaniambia.
Tukaogelea kurudi ufukweni. Tulipofika ufukweni nilimwambia Yasmin.
“Sidhani kama atatoka tena”
“Hawezi kutoka. Labda atokee mtu aifungue ile chupa”
“Na huyo mtu atatokea wapi?”
“Labda wavuvi”
“Wavuvi ni watu wanaojua. Wakiona chupa chini ya bahari hawaifungui. Na pia hakuna wavuvi wanaofika huku”
“Lakini ni kitu cha ajabu. Ujanja wote ule alionao ameshindwa kujitoa kwenye chupa!”
“Ndio maana tunaambiwa kiumbe hakukamilika kwa maumbile wala kwa ujuzi. Mkamilifu ni Mungu peke yake”
“Tungejua mapema tungemfungia tangu tulipofika, tungesalimika sote”
“Hatukujua. Hata mimi ningeweza kumfungia. Sasa nimeshajua sababu ya kunisisitiza kila siku kuwa niweke mbali kile kizibo na nisiifunge hata siku moja”
ITAENDELEA
 
SEHEMU YA 26



“Lakini ni kitu cha ajabu. Ujanja wote ule alionao ameshindwa kujitoa kwenye chupa!”
“Ndio maana tunaambiwa kiumbe hakukamilika kwa maumbile wala kwa ujuzi. Mkamilifu ni Mungu peke yake”
“Tungejua mapema tungemfungia tangu tulipofika, tungesalimika sote”
“Hatukujua. Hata mimi ningeweza kumfungia. Sasa nimeshajua sababu ya kunisisitiza kila siku kuwa niweke mbali kile kizibo na nisiifunge hata siku moja”
SASA ENDELEA...
“Yasmin tumeepuka kifo cha aina moja, sasa tunakabiliwa na kifo cha aina nyingine” nikamwambia Yasmin.
“Kifo gani tena?”
“Tutaondokaje kwenye kisiwa hiki?”
“Usijali. Mungu mkubwa”
Tukarudi katika lile jumba. Tulipofika tulioga maji baridi. Yasmin alinitolea “Ni kwa nguo za kiume alizokuwa akiletewa na Harishi, akaniambia nivae.
Kwa vile kulikuwa kumeshakucha alipikauji aliouchanganya na asali, tukanywa. Kwa sababu moyo wangu ulikuwa umetulia nilikunywa vikombe vitatu.
Wakati nakunywa kikombe cha tatu Yasmin akaniambia.
“Leo umekunywa uji mwingi kuliko siku zote!”
sababu nina njaa na roho yangu imetulia”
“Yasmin akacheka.
“Jana hukutaka kula kabisa!” akaniambia.
“Ni kwa sababu ya yule mshenzi, alinisababishia hofu sana”
“Sijui ulipata wapi akili ya kufunga kile kizibo?”
“Niiona tu akili yangu ikinituma nikifunge nilipoona ule moshi”
“Pengine ni kwa sababu ya zile dua ulizokuwa ukiomba tangu juzi”
“Pengine”
Wakati tunajadiliana na Yasmin tulishituka tulipoona wazungu wawili wanaume namtu mweusi mmoja wakiingia ndani ya ile nyumba.
Nguo zao zilikuwa zimeroa maji. Walionekana walikuwa wamatoka baharini.
Tukapatwa na uoga kwa vile hakukuwa na watu waliokuwa wakifika katika kisiwa kile.
Tulikuwa tumekaa pale ukumbini Yasmin akanyanyuka na kuwauliza kwa Kiswahili.
“Nyinyi ni kina nani”
“Samahani jamani. Tumekuja kuomba msaada” Yule mtu mweusiakatuambia.
“Mnatoka wapi?”
“Tunatoka Zanzibar. Chombo chetu kilipigwa na dharuba kimepinduka. Tumeogelea hadi tumetokea katika kisiwa hiki”
“Nyinyi ni kina nani” Yasmin akawauliza tena.
“Hawa wenzangu ni watalii wanatoka Ufaransa. Mimi ni Mzanzibari. Nilikuwa nawatembeza kwa boti kwenye Bahari ya Hinndi ndio tukapatwa na ajali”
“Mimi pia najua Kifaransa, ngoja niwaulize” Yasmin akasema na kuwageukia wale wazungu. Aliwauliza maswali kwa kutumia lugha ya Kifaransa. Wazungu hao walimjibu na kufurahi kuona Yasmin alikuwa akizungumza lugha yao.
“Karibuni make” Yasmin akawambia kwa Kifaransa.
Watu hao watatu wakakaa chini.
“Kwanza tunawapa pole sana kutokana na mkasa uliowafika. Mmesema kuwa mnaomba msaada, mtufahamishe mnaomba msaada gani?” Yasmin aliwauliza.
Msaada wowote tu unaostahili kwa binaadamu kwani tumezunguka sana katika kisiwa hiki hatukuona mtu yeyote. Tulichoona ni nyumba tupu na kwingine tulikuta mafuvu na mifupa ya bianaadamu” Mzanzibari alisema.
“Ni kweli” Yasmin alimjibu.
“Ni kwanini?”
“Kwanza mlitakiwa mshukuru kuwa mmefika katika kisiwa hiki katika muda mzuri, vinginevyo na nyinyi mngekuwa kama yale mafuvu mliyoyaona”
“Kwa niaba ya wenzangu nasema kuwa tumeshukuru lakini tuna shauku ya kutaka kujua kilichotokea mpaka mkabaki nyinyi peke yenu”
“Nitawaeleza”
Ndipo Yasmin alipoanza kuwaeleza kisa cha kisiwa hicho. Alianza kwa kujitambulisha kuwa yeye ni binti wa Rais wa Comoro na jina lake ni Yasmin. Akawambia kwamba alisoma elimu yake nchini Ufaransa na ndiyo sababu akawa anajua kuzungumza Kifaransa.
Akaeleza alivyoposwa na mwana wa mkuu wa majeshi nchini mwao lakini siku ile ya harusi akakumbwa na jini anayeitwa Harishi ambaye alimpeleka katika kisiwa hicho na kumgeuza mke wake.
“Sikujua nilivyofika katika kisiwa hiki. Nilijishitukia tu nikiwa ndani ya jumba hili nikiwa sijielewi” Akasema.
Watu hao watatu, wazungu wawili na Mzanzibari mmoja walishikwa na mshangao mkubwa kusikia habari ile.
Yasmin aliendelea kuwaeleza kuwa jini aliyemkumba ndiye aliyekuwa akiua watu katika kisiwa hicho kwa kuwafyonza damu na kula ubongo wao.
“Aliwamaliza watu wote waliokuwa katika kisiwa hiki na kuacha majumba yakiwa matupu. Niliishi peke yangu kwa karibu mwaka mzima” Yasmin alieleza.
Aliendelea kuwaeleza jinsi tulivyofika katika kisiwa hicho na kumkuta yeye ndani ya jumba hilo na jinsi tulivyoanza kuuawa na Harishi mmoja mmoja hadi nikabaki peke yangu.
Ni dhahiri kuwa maelezo ya Yasmin yalikuwa yamewatia hofu watu hao kwani nyuso zao zilizidi kupata fadhaa.
“Mungu ni mkubwa” Yasmin alisema kabla ya kueleza jinsi walivyofanikiwa kumfungia Harishi kwenye chupa na kwenda kuizamisha baharini asubuhi ile.
“Hiki ni kisa cha ajabu kweli kweli. Je tunaweza kwenda kuiona hiyo chupa? mzungu mmoja akauliza.
“Hatuwezi kujua tumeizamisha wapi lakini kwa sasa Harishi yuko chini ya Bahari”
“Je hao watu waliouawa tunaweza kuwaona?”
“Hao mnaweza kuwaona”
“Tunaomba mtupeleke tukawaone kama hamtajali”
Yasmin akanitazama.
“Umeridhika twende tukawaoneshe hawa wageni miili ya ndugu zako?” akaniuliza.
“Nimeridhika” nikamjibu.
Yasmin akawambia wale watu “Twendeni”
Tukaondoka sote watu wanne. Yasmin alianza kuwaonesha miili ya wenzetu waliouawa ambayo ilikuwa karibu na lile jumba. Walikuwa ni wale wenzangu waliouawa mwanzo mwanzo.
Yasmin alikuwa akieleza jinsi watu hao walivyokuwa wakiuawa kila siku mmoja baada ya mwingine.
Tukaenda mbali zaidi katika ile nyumba aliyouawa Haji. Wazungu hao pamoja na Mzanzibari waliyekuwa naye wakauona mwili wa Haji.
Mimi nilitakiwa kueleza alivyouawa Haji. Nikaeleza kwa Kiswahili huku Yasmin akitafsiri kwa kKifaransa.
Baada ya hapo tulikwenda katika nyumba aliyouawa Shazume.
Tuliwaonesha mwili wa Shazume na nikawaeleza jinsi Shazume alivyouawa.
“Hapa ndipo nilipokata tamaa kabisa. Nilijua na mimi ningeuawa leo” nilisema.
Yasmin akaeleza kuwa nay eye alikuwa ameshajitolea kufa kwa ajili yangu.
“Nilisema kama atauawa basi tuuawe sote” akasema na kuongeza.
“Niliona Hakuna haja ya kuendelea kujificha. Nilimwambia mwenzangu twende kule ninakoishi. Harishi akija atukute sote”
Wazungu hao walimsifu Yasmin kuwa alikuwa msichana jasiri na mwenye moyo.
“Kumbe na sisi tungekuja kufa!” Mzanzibari naye aling’aka.
“Ndiyo maana niliwambia mwanzo kuwa mshukuru kwa kufika katika kisiwa hiki katika kipindi cha usalama” Yasmin akawambia.
“Sasa kule nyumbani Comoro wanajua uko wapi?” Yule Mzanzibari alendelea kumuuliza Yasmin.
“Wao hawajui niko wapi na kwa sasa wanaamini kuwa nimeshakufa”
“Je wakikuona tena itakuwaje?”
“Itakuwa mshangao mkubwa. Wazazi wangu hawataamini”
“Ni mkasa wa kutisha kweli na unastahili kuandikwa katika historia ya Comoro”
“Hapo ni kama tutanusurika na nitarudi kwetu kwani kama niivyowambia mwanzo hapa hatutarajii kupata msaada wowote. Hatima yetu tumemwachia Mwenyezi Mungu”
ITAENDELEA
 
Back
Top Bottom