MKASA: Hadi Lini?

MKASA: Hadi Lini?

Bishop Hiluka

JF-Expert Member
Joined
Aug 12, 2011
Posts
7,148
Reaction score
14,716
Na Bishop Hiluka

Yalikuwa yamemfika kooni baada ya kuitafuta haki yake kila mahali na kushindikana, akafikia uamuzi wa kuwaita wazazi wa pande zote mbili ili aweke wazi kuhusu msimamo wake juu ya ndoa yake. Kama noma na iwe noma lakini asingeweza kuendelea kuvumilia, avumilie hadi lini? ...


JUMAMOSI, saa kumi na mbili na nusu jioni, kwa saa za Burundi, sauti tamu ya muziki laini wa kubembeleza ilikuwa inasikika kutoka katika spika zilizokuwa kwenye kona za ukumbi mkubwa wa kisasa wa burudani, ndani ya Hotel Club du Lac Tanganyika.

Club du Lac Tanganyika ilikuwa hoteli yenye hadhi kubwa iliyokuwa imejengwa kwenye mandhari ya kuvutia ya ufukwe wa Ziwa Tanganyika jijini Bujumbura, Burundi. Ilikuwa hoteli ya kisasa kabisa iliyokuwa imezungukwa na mazingira yenye utulivu mkubwa ufukweni mwa ziwa, ikiwa kando ya barabara ya Chausse d'Uvira iliyokuwa inaelekea katika mji mdogo wa Uvira.

Ikiwa imezungukwa na uzio madhubuti ulioifanya kuwa mahali patulivu zaidi na penye usalama wa uhakika, ilikuwa sehemu tulivu zaidi ya kwenda kujirusha kwa watu wenye ukwasi, ikiwa umbali wa kilomita tatu tu kutoka katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Bujumbura.

Pia ilikuwa sehemu muhimu sana kwa burudani na wageni wengi kutoka nje walipenda kwenda sehemu ile, hasa mwisho wa wiki, kutokana na kuwa na kumbi mbili za kisasa. Ukumbi mmoja ulitumika kwa ajili ya mikutano, ukiwa na sifa zote, na wenye viyoyozi na umeme wa uhakika saa 24, jambo linaloufanya kuvutia wageni mbalimbali. Ukumbi mwingine ulitumika zaidi kwa ajili ya burudani na matukio.

Ukumbi wa burudani ulikuwa na kila aina ya starehe, ukiwa na madirisha makubwa ya vioo yaliyofunikwa na mapazia safi marefu, na ulikuwa na kila kionjo cha daraja la kimataifa. Ndani ya ukumbi ule kulikuwa na wahudumu wazuri wa kike, warembo kwelikweli, waliokuwa wakihudumia wateja wachache waliokuwemo ukumbini muda huo wakiwa wameketi kwenye meza nzuri za mbao ya mti wa mninga na viti vifupi vyenye foronya laini.

Muda ule wa saa kumi na mbili na nusu za jioni idadi kubwa ya wateja waliokuwemo ndani ya ukumbi ule walikuwa raia wa kigeni, hasa kutoka katika nchi za Ufaransa na Marekani. Upande wa kulia wa ukumbi ule kulikuwa na mlango na dirisha dogo la jikoni, na humo ndani kulionekana wapishi waliokuwa katika mavazi yao ya kazi, wakiandaa chakula.

Katika ukumbi ule, mmoja wa wateja Waafrika walioonekana aliitwa Ibrahim Bigirimana, alikuwa mwanamume wa Kitanzania aliyekuwa na asili ya kutoka mkoa wa Kigoma, mkoa ambao uko pembezoni mwa nchi ya Tanzania katika mpaka wa Tanzania na Burundi.

Ibrahim Bigirimana alikuwa ameketi peke yake kwenye meza moja akionekana kuzama katika fikra fulani huku akiwa na shauku kubwa ya kusubiri kitu fulani muhimu sana, ambacho, ni yeye tu kati ya watu wote waliokuwemo mle ukumbini ndiye aliyekuwa akikijua.

Ibrahim alishusha pumzi za ndani kwa ndani na kutupa macho yake kuangalia nje kupitia ukuta msafi wa kioo cha dirisha, mkono wake mmoja alikuwa ameshika bilauri ndefu iliyokuwa na mvinyo mwekundu wa Kifaransa aina ya Navette de Marseille, na mkono wake wa kushoto alikuwa kauegemeza juu ya kiti alichokalia. Ibrahim akainua bilauri ya mvinyo na kupiga funda taratibu huku akionekana kuwaza mbali sana.

Alikuwa mwanamume mrefu na maji ya kunde, akiwa na sura bashasha ya kitoto iliyokuwa na muonekano uliomfanya mtu yeyote aliyemuona adhani kuwa hangeweza kuzidi miaka therathini, ingawa alishapita miaka hiyo. Akiwa na umri wa miaka arobaini na mbili, kimuonekano, Ibrahim alikuwa na umbo kakamavu la kimichezo lililofanana na maumbo ya wachezaji wa ligi ya mpira wa kikapu wa nchini Marekani.

Alikuwa mcheshi sana na mtu wa kupenda kujichanganya na watu wengine bila kujali kipato, alikuwa muongeaji mkubwa mwenye kuzimudu vyema lugha za Kiswahili, Kiingereza, Kifaransa na hata Kirundi, lugha iliyokuwa ikizungumzwa zaidi na wenyeji wa nchi ile ya Burundi, jambo ambalo liliwafanya watu wengi kudhani kuwa labda alikuwa Mrundi mwenzao, hasa kwa kuwa hata jina lake la mwisho la ‘Bigirimana’ ni jina lililokuwa linatumiwa na Warundi.

Ibrahim alikuwa Muha kutoka mkoani Kigoma, kabila lililokuwa na utamaduni ulioshabihiana kwa kiasi kikubwa sana na ule utamaduni wa Warundi. Ibrahim alikuwa ameishi jijini Bujumbura kwa takriban miaka kumi sasa. Na alikuwa akifanya kazi kama Meneja Mkuu wa CRDB Bank Burundi, benki iliyokuwa na makao yake katika barabara ya Chaussée du Prince Louis Rwagasore, ploti namba 490/A, jijini Bujumbura.

Kwa nafasi hiyo, Ibrahim alikuwa mtu mwenye mafanikio mema, ingawa alikuwa na kasoro moja iliyoonekana wazi, hakuwa na wala hakupenda kuwa na kitambi. Wengi walidhani labda Ibrahim alikuwa amebebwa hadi kufikia nafasi ile, lakaini ukweli hakufikia nafasi ya ile ya umeneja mkuu wa benki hiyo kwa bahati au kama wasemavyo Waswahili ‘zali la mentali’, bali alikuwa nazo sifa zinazostahili ikiwemo elimu ya juu na uzoefu wa kazi.

Kabla hajakuwa Meneja Mkuu wa CRDB Bank Burundi, ibrahimu alikuwa amefanya kazi kama Manager Corporate Banking na baadaye akawa Senior Relationship Manager Corporate Banking katika Benki ya Biashara ya Burundi (Commercial Bank of Burundi) iliyokuwa na makao yake katika makutano ya barabara za Avenue des USA na Chaussée P.L. Rwagasore, ikiwa mkabala na jengo la CRDB Bank Burundi, jijini Bujumbura.

Ibrahim alikuwa msomi wa Shahada ya Umahili ya Business Administration aliyoipata kutoka Chuo Kikuu cha Oxford, Uingereza, ambacho kilikuwa chuo kikongwe zaidi katika ulimwengu wa nchi zinazozungumza lugha ya Kiingereza, na Shahada ya Kwanza ya Banking and Financial Services aliyohitimu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Tanzania.

Baada ya kumaliza chuo kikuu na kabla hajaenda kufanya kazi nchini Burundi, Ibrahim alikuwa amefanya kazi kaatika Benki Kuu ya Tanzania kwa miaka miwili kisha akaacha na kwenda kuishi jijini Bujumbura ambako aliajiriwa katika benki ya biashara ya Burundi. Hii ilitokana na yeye kuamua kumfuata mke wake aliyekuwa amerudishwa nchini Burundi baada ya kukumbwa na matatizo ya uraia alipokuwa akiishi nchini Tanzania.

Alipofika Burudni na kuajiriwa Commercial Bank of Burundi Ibrahim alifanya kazi kwa miaka kadhaa, na kutokana na uwezo wake na ufanisi kazini alichukuliwa na CRDB Bank Burundi, kama mwanzilishi na Meneja Mkuu wa benki hiyo jijini humo, nafasi ambayo aliweza kudumu nayo hadi wakati huo.

Huyo ndiyo Ibrahim Bigirimana, ambaye Jumamosi hiyo alikuwa katika ukumbi wa maraha wa Hotel Club Du Lac Tanganyika akiwa mwenye shauku kubwa. Alinyanyua bilauri yake na kunywa funda dogo la mvinyo kisha akaitazama saa yake ya mkononi kwa mara nyingine tena kisha akaonekana kutikisa kichwa chake.

Alishusha pumzi za ndani kwa ndani huku akisonya kwa huzuni, ni wazi alikuwa hapo akisubiria kitu muhimu sana lakini hadi muda ule alionekana kuanza kuishiwa na uvumilivu. Aliitazama tena saa yake na kuminya midomo yake akionekana kuwaza mbali, akabaki akiikodolea macho ile saa kana kwamba ilikuwa mbovu.

Laiti kama ingelikuwa saa ya kawaida labda angeweza kusema kuwa ilikuwa na kasoro, lakini hiyo saa kama ilivyo kwa vitu vyake vingi, haikuwa ya kawaida kabisa!

ITAENDELEA...

Cc the_legend Norshad bobefu zoefu Pablo PAKAYA Ibney blackstarline Bryece Tater, Bigjahman moneytalk marybaby, nipo2, ram, kisukari, Smart911, Madame S, carbamazepine, Astelia, culture gal , Prisoner of hope, Mine eyes, kuku mweus, Thad, hearly, Shunie, moneytalk,Tumosa, Mine eyes, Kudo, swahiba92, ludist, Toyota escudo, Clkey, macson3, Thad, boga la kiangazi, macson3, LEGE, Smart911, Richard irakunda, skfull, popie, Krizy Beat, hearly nipo2 MWINDAJI HARAMU kakhulu Katavi Norami mbududa iron2012 popie Bughy Harry Kinondoni Sweetheart SUPER EMILY
 
HADI LINI! 2

Na Bishop Hiluka


Ilikuwa saa ya bei ghali aina ya Rolex Submariner, iliyokuwa imemgharimu kiasi cha Dola laki mbili na nusu za Marekani! Si haba, zilikuwa fedha nyingi sana kama angeamua kuzibadilisha kwa pesa za Burundi au hata za Tanzania.
Ibrahim alivuta pumzi ndefu na kuzishusha taratibu, kisha akainua tena bilauri ya mvinyo na kupiga funda ndefu huku akionekana kusisimkwa mwili, kisha aliitua ile bilauri juu ya meza na kugeuka kutazama nje kupitia ukuta msafi wa kioo cha dirishani, aliitazama mandhari tulivu ya kuvutia nje ya ukumbi ule kwa upande wa nyuma wa lile jengo la hoteli.
Kule nyuma zilionekana nyasi nzuri za rangi ya kijani kibichi zilizopakana na maua ya rangi tofauti ya kuvutia, na nyasi hizo zilikuwa zimepandwa kuzunguka bwawa kubwa la kuogelea ambalo kando yake kulikuwa na viti vingi vya kupumzikia kwa waogeleaji vyenye miamvuli mizuri ya kujikinga na miale ya jua.
Katika viti hivyo walionekana baadhi ya wazungu waliokuwa wameketi wakipunga upepo na wengine walikuwa wanaogelea huku wakiwa katika mavazi maalumu ya kuogelea. Kando ya bwawa lile la kuogelea kulikuwa na bustani nzuri ya miti yenye viti vya kupumzikia visivyohamishika katika mandhari tulivu.
Upande wa pili wa bustani ile kulikuwa na baa iliyokuwa kwenye mandhari nzuri yaliyovutia ya ufukwe wa Ziwa Tanganyika, naa muda ule watu kadhaa walikuwa wameketi ndani ya baa hiyo, na pembeni kabisa ya baa ile ulikuwepo uwanja wa tennis.
Muda ule ule Ibrahim alijikuta akiyahamisha macho yake kutoka kwenye uwanja wa tennis na kumtazama mwanadada mmoja mrembo aliyekuja na kusimama mbele ya meza yake huku tabasamu kabambe likivinjari usoni pake.
Alikuwa mwanadada mrembo hasa, aliyekuwa na nywele nyingi nyeusi za kibantu zisizotiwa dawa na hivyo kumfanya aonekane mzuri wa asili. Macho yake yalikuwa makubwa na meupe yaliyokuwa yamezungukwa na kope ndefu na nyeusi ambazo alikuwa amezitinda vizuri na kuzipaka rangi nyeusi ya wanja mwembamba na kuyafanya macho yale makubwa na meupe kupendeza zaidi.
Alikuwa na pua ndefu kama ya Kihabeshi, mdomo wake wa kike wenye kingo pana kiasi na lips zake laini za kike zzilikuwa imekolea vizuri rangi ya mdomo maarufu kama lipstick, na hivyo kuifanya sura yake nyembamba kiasi yenye pua ndefu izidi kupendeza. Mdomo wake ulikuwa umehifadhi meno meupe yaliyojipanga vizuri huku yakiachia kijiuwazi kidogo kwa mbele, yaani mwanya.
Yule mrembo kama angetabasamu angeacha vishimo vidogo mashavuni vilivyochomoza haraka na kuzisulubu vibaya hisia za mwanaume yeyote aliye rijali. Masikio yake madogo yasiyochusha alikuwa ameyatoga na kuyavalisha hereni kubwa za kitamaduni zenye umbo la mviringo.
Mrembo yule aliitwa Bélise Celéstine Gatete, alikuwa binti wa kabila la Kitutsi kutoka Burundi, ambaye alikuwa na umri wa miaka ishirini na nane.
Bélise alikuwa anafanya kazi katika mgahawa wa kisasa wa La Silhouette Café uliokuwa kando ya barabara ya Chaussée du Prince Louis Rwagasore, na alikuwa anaishi katika mojawapo ya nyumba za shirika la nyumba la Burundi zilizokuwa kando ya barabara ya Ave des Patriotes, nyuma ya uwanja wa mpira wa miguu wa Prince Rwegasore Stadium.
Bélise Celéstine Gatete alikuwa amevaa blauzi nyepesi ya rangi ya bluu bahari ya mikono mirefu iliyokuwa ikiyaonesha matiti yake yenye ukubwa wa wastani na chuchu nyeusi imara zilizosimama kikamilifu.
Chini alivaa sketi yake fupi ya rangi ya pinki iliyokuwa na miraba myeupe iliyoishia juu ya magoti yake na kuifichua vizuri hazina ya kupendeza yenye mvuto wa ajabu ya miguu na mapaja yake mang’avu yenye misuli imara ya rangi maridhawa ya kibantu. Bélise alikuwa na miguu mizuri iliyokuwa ikitazamika, na alivaa viatu vya ngozi vyenye vikanyagio virefu vya mchuchumio.
Sketi yake ilikuwa imenasa vyema kwenye tumbo lake lililokuwa dogo na flati na kiuno chake chembamba mithili ya dondora kilichokuwa kimeshikilia mzigo mkubwa wa makalio yake imara ambao ungeweza bila ya taabu yoyote kukondesha akaunti ya mwanaume yeyote awaye rijali.
Mkono wa kulia wa Bélise alikuwa amevaa saa ndogo nzuri ya kike aina ya Swatch, ambayo bei yake ilikuwa si haba, kwani ilikuwa inauzwa Pauni mia sita za Uingereza ambazo hazikuwa fedha ndogo endapo angeamua kuzibadilisha na kupewa fedha za Tanzania, kwani zilikuwa sawa na zaidi ya shilingi milioni moja na laki nane. Saa ile ilikuwa imetengenezwa kwa namna ya kupendeza na hivyo kuongeza ziada nyingine katika uzuri wa Bélise. Mkono mwingine wa kushoto alikuwa amevaa bangili nyingi za pembe.
Kwenye bega lake la kulia alikuwa amening’iniza mkoba mzuri wa rangi nyeusi, ambao wengine walipenda kuuita ‘kipima joto’. Huo mkoba nao ulimfanya binti yule kuvutia zaidi na zaidi. Itoshe tu kusema kuwa Bélise alikuwa mwanadada mrembo kweli kweli!
Kwa nukta kadhaa moyo wa Ibrahim ulisahahu mapigo yake, na yalipoanza alivuta pumzi ndefu, akazishusha. Alimtazama, akajikuta akiuajabia uzuri wa mwanadada yule uliokuwa mbele ya macho yake, akabaki akiwa amekodoa macho yake akiwa hana cha kusema, na bila hata kutegemea alianza kuzama kwenye bahari ya mawazo, mawazo yaliyomrudisha nyuma siku tatu kabla ya siku ile, siku alipokutana na mrembo yule kwa mara ya kwanza…
______
Ilikuwa siku ya Jumatano Ibrahim akiwa amevaa suti maridadi ya rangi ya kijivu alikuwa kasimama nje ya mlango wa chumba cha lifti katika ghorofa ya kumi ya jengo moja refu lililokuwa katika makutano ya barabara za Ave De Luxembourg na Avenue de Gréce, jirani na ubalozi wa Ufaransa.
Jengo lile halikuwa mbali sana na uwanja maarufu wa mpira wa miguu wa Prince Rwegasore Stadium. Ibrahim alikuwa amekwenda kwenye lile jengo kumuona rafiki na mshirika mwenza kibiashara, Adolf Ndilingiye ambaye pia walisoma pamoja katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Walipokuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Adolf Ndilingiye alisomea Shahada ya Kwanza ya Sanaa katika Uchumi na Takwimu (B.A. in Economics and Statistics) na Ibrahim alisomea Shahada ya Kwanza ya Banking and Financial Services.
Adolf Ndilingiye alikuwa Ofisa Mtendaji Mkuu na mwanzilishi mwenza wa kampuni ya ushauri wa masuala ya kibiashara na kiuchumi iliyoitwa Fleur économique et Business Consulting Ltd au Flower Economic And Business Consulting Ltd kwa Kiingereza.
Baada ya maongezi marefu ya kibiashara Ibrahim aliagana na Adolf, akatoka na kusimama pale nje ya chumba cha lifti akiwa peke yake, na muda wote alikuwa akiitupia jicho saa yake ya mkononi akionekana kuwa na haraka kidogo. Mara wakafika wanaume wengine wawili na kujiunga naye.
Kile chumba cha lifti kilipofika pale na milango ya lifti kufunguka, Ibrahim na wale wanaume wawili waliingia ndani kisha wale wanaume walibonyeza nambari sita, Ibrahim akabonyeza herufi G. chumba kile cha lifti kikaanza kushuka chini taratibu na kilipofika katika ghorofa ya tisa kikasimama na milango ikajifungua.
Hapo wakamuona msichana aliyeitwa Bélise ambaye aliingia haraka ndani ya kile chumba cha lifti na mara milango ya kile chumba cha lifti ikajifunga. Bélise aliziangalia zile namba na kutulia pasipo kubonyeza namba yoyote wala kusema neno lolote.

ITAENDELEA...
 
HADI LINI! 3

Na Bishop Hiluka


Bélise alikuwa amevaa suruali ya jeans ya rangi ya bluu na juu alivaa blauzi ya rangi nyekundu. Kichwani alikuwa amevaa kofia ya rangi ya bluu ya kapelo na miguuni alikuwa amevaa raba za rangi nyekundu. Begani alikuwa amening’iniza mkoba mzuri wa rangi ya bluu.
Lifti ilianza kushuka hadi ilipofika katika ghorofa ya sita ikasimama na milango ya lifti ukajifungua ukiwaruhusu wale wanaume wawili kushuka huku wakiwaacha Ibrahim na Bélise mle ndani. Milango ikajifunga na lifti ikaendelea kushuka huku wakiendelea kuwa kimya. Mara Ibrahim alijikuta akimtupia jicho yule msichana na kumuona akiitupia macho saa yake ya mkononi. Moyo ukampasuka!
“Oh Mungu wangu, ni binti mrembo hasa,” Ibrahim alijikuta akiwaza huku akimtazama yule msichana kwa makini.
Wakati wote tangu alipokuwa akija mbio hadi alipoingia ndani ya kile chumba cha lifti Ibrahim hakuwa amemchanganyia macho vizuri. Kwanza kwa sababu alikuwa ameshachoka na alitaka kuwahi mapema nyumbani akapumzike, na pili hakuwa na sababu yoyote ya kumtilia maanani yule msichana.
Kumbe alikosea sana! Msichana yule hakuwa wa kawaida kama alivyokuwa amedhani, na wala hakuwa mmoja wa wale wasichana aliozoea kupishana nao kwenye korido za mahoteli au mtaani wakijigonga gonga kwake au wale aliowaona wakijiuza kwenye madanguro!
“Hujambo bibie!” Ibrahim alimsalimia Bélise kana kwamba ndiyo alikuwa akimuona kwa mara ya kwanza.
“Sijambo,” Bélise alisema huku akigeuza uso wake nusu bila kumwangalia Ibrahim huku akionekana kuyakwepa macho ya Ibrahim baada ya kugundua kuwa alikuwa anamtazama usoni kwa makini
Ibrahim alimtazama kwa makini akijaribu kumchunguza na kugundua kuwa yule msichana alikwishamshtukia dhamira yake, kwani alikuwa anamtupia jicho laa wizi mara kwa mara kumtazama katika namna ambayo kwa kweli Ibrahim hakuweza kuielewa.
Alichogundua ni kuwa macho ya yule msichana yalijaa aibu na alikuwa hawezi kumtazama mwanamume usoni kwa sekunde tatu mfululizo bila kukwepesha macho yake na kutazama kando kwa jinsi alivyojaa haiba na aibu.
“Eh, ningependa…” Ibrahim alitaka kuongea lakini alikatizwa na mlio usio wa kawaida uliosikika mle ndani ya chumba cha lifti, kisha taa ndani ya kile chumba cha lifti zikazimika na lifti ikasimama ghafla. Mara kukatokea kiza totoro ndani ya kile chumba cha lifti.
“Mungu wangu… tunakufa!” Bélise alitoa yowe kwa sauti yake iliyoonesha kujaa hofu kubwa. Aliyakodoa macho yake kwenye kile kiza huku mapigo ya moyo wake yakibadili mwendo na kuanza kwenda kasi. Alishindwa kujizuia na kuamua kumg’ang’ania Ibrahim.
“Inaelekea tumekwama, usihofu sana, bibie!” Ibrahim alisema katika hali ya kumtoa hofu yule msichana mrembo. Alisema huku akizungusha mkono wake mmoja kwenye mabega ya Bélise na mkono wa pili ulikuwa unapapasa kwenye vibonyezo vilivyokuwa ndani ya kile chumba cha lifti.
Akabahatisha kuvipata na kubonyeza kitufe kimoja ambacho kilitoa mwanga hafifu. Kisha macho yake yalitua kwenye uso wenye hofu wa yule msichana mrembo aliyekuwa akitetemeka.
“Sasa tutafanyaje, kaka?” Bélise alimuuliza Ibrahim huku akiendelea kutetemeka kutokana na hofu kubwa aliyokuwa nayo.
“Hatuna la kufanya isipokuwa tusubiri tu, huenda msaada unakuja!” Ibrahim alimwambia kwa sauti tulivu huku akimkumbatia kwa upendo. Bélise akajitoa mikononi mwa Ibrahim na kumwangalia usoni kwa mshangao.
“Unasemaje! Utakuja vipi wakati sisi tumekwama humu ndani na hakuna anayejua? Tafadhali fanya jambo, fanya jambo!” Bélise alilalama kwa sauti laini ya kubembeleza huku machozi yakianza kumlenga lenga machoni.
Ibrahim aliachia tabasamu jepesi na kuanza kulegeza tai yake, kisha akavua koti lake na kuanza kufungua vifungo vya shati lake. Bélise alimtazama Ibrahim kwa mshangao kisha akaonekana kuhamaki.
“Unataka kufanya nini?” Bélise alimuuliza Ibrahim huku akimkazia macho kwa hofu.
“Unadhani nataka kufanya nini, huoni kama navua koti langu!” Ibrahim alimwambia huku akimtazaa kwa tabasamu.
“Ili ufanye nini?” Bélise aliuliza tena kwa hofu.
“Nipate afueni kidogo, kwani huoni kuwa joto linazidi kuwa kali!”
Bélise alimtazama Ibrahim kwa hofu akionekana kubabaika sana, hofu ilikuwa imemtawala zaidi.
“Tafadhali kaka, jaribu kufanya maarifa yoyote tutakufa humu!” Bélise alilalama kwa hofu huku akionekana kuanza kukata tamaa.
“Usijali, kimoja cha vibonyezo nilivyobonyeza ni cha tahadhari kwa hiyo wahusika wamekwishafahamu kuwa chumba hiki cha lifti kimekwama na kina watu ndani yake… usihofu tutatoka salama,” Ibrahim alimwambia Bélise kumtoa wasiwasi.
Bélise alifungua mkoba wake na kutoa leso laini, akajifuta jasho usoni lililoanza kumtoka kwa wingi. Ibrahim alimtupia jicho la matamanio, akatamani kumkumbatia na kumporomoshea mabusumfululizo. Mara akashtuka kumuona Bélise akianza kulia kilio cha kwikwi.
Kabla Ibrahim hajajua afanye nini mara wakasikia sauti za watu zilizokuwa zinasikika kwa mbali.
Ibrahim akamsogeza Bélise karibu yake na kumkumbatia kwa mikono yake yote miwili ikiwa mmoja ulikuwa umeshika koti, Bélise bila hiyari yake alijikuta akijilegeza na kujilaza kifuani kwa Ibrahim huku akikiegemeza kichwa chake juu ya kifua cha Ibrahim, lakini aliendelea kulia kilio cha kwikwi.
“Usilie, binti, tutaokolewa,” Ibrahim alimwambia Bélise huku akimpapasa kwa mahaba nyama zake za mgongo.
Kisha Ibrahim alipeleka vidole vyake vya mkono wa kulia kwenye mashavu ya Bélise na kuanza kupangusa machozi yaliyokuwa yakimtoka Bélise utadhani milizamu iliyopasuka. Wakiwa katika hali ile mara chumba kile chaa lifti kinaanza kutingishika na kuteremka chini taratibu kwa kusuasua.
Baada ya kuteremka kwa muda mara wakaona chuma kikipenyezwa katikati ya ile milango ya kile chumba cha lifti na kulazimisha kuitenganisha ile milango miwili ya chumba kile cha lifti.
Kazi ile ilifanywa kwa muda mfupi, na baada ya kupata upenyo, Ibrahim na Bélise walifanikiwa kutoka ndani ya kile chumba cha lifti huku Ibrahim akimtanguliza Bélise kutoka nje.
Ibrahim akiwa kashika koti mkononi, tai shingoni ikiwa imelegezwa na vifungo vya juu vya shati vimefunguliwa na kuachwa wazi alitoka na kumkuta Bélise akiwa kazungukwa na watu wakimpa pole huku wengine wakijitokeza kumsaidia Ibrahim, na baadhi yao, hasa wadada na wanaume wakware walionekana kuwaangalia Ibrahim na Bélise kwa hisia tofauti.
Ibrahim alimsogelea Bélise ambaye alikuwa bado ana hofu na ahakuamini kama alikuwa ametoka ndani ya kile chumba cha lifti salama, akamuuliza kwa sauti ya chini, “Sijui mwenzangu unaelekea wapi?”
“Kwa hali hii niliyo nayo, kwa vyovyote itabidi niende kwanza nyumbani,” Bélise alisema huku akijiangalia.
“Unao usafiri?” Ibrahim alimuuliza huku akimtulizia macho.
“Hapana, nitakodi teksi,” Bélise alimwambia huku akiyakwepa macho yake na kutazama kando.
“Usijali, mimi nina gari, niruhusu nikusindikize hadi nyumbani kwako iwapo hutajali,” Ibrahim alimwambia huku macho yake yakiwa hayabanduki usoni kwa Bélise.
“Sitajali kama sitakusumbua,” Bélise alisema huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani.
“Oh hapana, siwezi kusumbuka kwa hilo,” Ibrahim alisema huku akiminya midomo yake.
“Basi nisindikize kwani najisikia kizunguzungu…” Bélise alisema huku akiminya macho yake kama aliyekuwa akihisi maumivu ya kichwa.
“Na macho ya watu wengi wanaotuangalia nayo pia yanasababisha madhara, twen’zetu!” Ibrahim alisema huku akimshika mkono na kuanza kumuongoza kutoka katika eneo lile.

ITAENDELEA...
 
HADI LINI! 4

Na Bishop Hiluka


Kama aliyekumbuka kitu, Ibrahim aligeuka kuwatazama wale watu waliokuwa wamejazana eneo lile na kuwashukuru sana kwa msaada walioutoa kwao.
Kisha Ibrahim alimuongoza Bélise hadi nje kabisa ya lile jengo kwenye eneo la maegesho ya magari alikokuwa ameegesha gari lake la kifahari aina ya Toyota Landcruiser GX V8 la rangi nyeusi. Bila kujali macho ya watu waliosogea eneo lile Ibrahim alimfungulia Bélise mlango wa mbele wa upande wa kulia, kisha alikwenda upande wa kushoto, pasipo kuwajali watu akaingia.
Ibrahim aliliondoa lile gari kwa mwendo wa kasi na kuyafanya magurudumu yachimbe ardhi, akaingia katika barabara ya Ave De Luxembourg na kuelekea uelekeo wa ya uwanja wa mpira wa miguu wa Prince Rwegasore Stadium kama alivyokuwa ameelekezwa na Bélise. Aliyavuka makutano ya barabara za Ave De Luxembourg, Ave De France na Ave De Portugal akaendelea na ile barabara ya Ave De Luxembourg hadi alipoifikia barabara pana ya Boulevard de Iʾndependence, Bélise akamuelekeza kuwa akunje kushoto na kuifuata ile barabara ya Boulevard de Iʾndependence iliyokuwa ikipita mbele ya ule uwanja wa mpira wa miguu wa Prince Rwegasore Stadium.
Muda mwingi Bélise alionekana mtulivu sana huku akitafakari hili na lile. Ibrahim alimtupia jicho la matamanio mara kwa mara wakati lile gari lake likichanja mbuga kukatiza mitaa na kuipita Aroma Sambicoffee, kisha uwanda mpana uliokuwa na majengo ya Shule ya Kifaransa kulia kwao.
Baadaye wakakuta barabara pana ya Boulevard de I’Uprona iliyokuwa ikikatiza mbele yao ikitokea Ubalozi wa Ufaransa. Bélise akamwelekeza Ibrahim kuingia upande wa kulia akiiacha ile barabara ya Boulevard de Iʾndependence na kufuata barabara ya Boulevard de I’Uprona.
Ibrahim akaingia katika ile barabara ya Boulevard de I’Uprona akiendelea kuambaa kando kando ya uwanda mpana wa majengo ya Shule ya Kifaransa kulia kwake, na alipofika mwisho wa eneo la ile shule ya Kifaransa Bélise alimuelekeza tena Ibrahim kuingia kulia kwake kuifuata barabara ya Ave Muyinga.
Ibrahim aliongeza mwendo huku akiipita barabara ya Ave de lax Paix iliyokuwa inaingia upande wake wa kushoto na kwenda mbele zaidi kisha akaifikia barabara ya Ave des Patriotes, ambayo pia ilikuwa inaingia upande wake wa kushoto, kisha Bélise akamuonesha jengo moja la ghorofa lililokuwa jirani na baa ya Bunga Bunga, nyuma ya ule uwanja wa mpira wa Rwagasore.
Ibrahim akafunga breki na kuliegesha gari lake kando ya ile barabara ya Ave Muyinga huku akilitazama lile jengo kwa makini.
“Hapo ndipo ninapoishi, bwana mkubwa! Karibu ndani… karibu kwetu tafadhali” Bélise alimwambia Ibrahim kwa sauti laini na tulivu ya nyenyekevu.
Ibrahim alimtazama Bélise na kuachia tabasamu pana, “Je, ninaweza kuruhusiwa kukaribia kwako siku nyingine baada ya leo?” alimuuliza huku akiyatulizia macho yake kwenye uso wa Bélise.
Bélise alimtupia jicho la wizi akimtazama Ibrahim kwa udadisi huku akionesha wasiwasi kidogo, “Sawa… unaruhusiwa wakati wowote,” Bélise alijibu huku akishusha pumzi.
Muda ule ule Ibrahim aliteremka na kuwahi kuzunguka upande wa pili, akamfungulia Bélise mlango huku akimpisha ashuke kutoka kwenye gari. Bélise aliposhuka akanyoosha mkono wake kumpa Ibrahim huku akiachia tabasamu pana na laini lililozidi kumkoroga ibrahim, kisha akainamisha kidogo kichwa chake kwa adabu.
“Uende salama bwana mkubwa… kwa heri,” Bélise alisema kisha alianza kupiga hatua kuanza kuondoka lakini akasita na kugeuka baada ya kusikia Ibrahim akiongea.
“Naitwa Ibrahim Bigirimana…” Ibrahim alisema kwa sauti tulivu huku akimtazama Bélise kwa makini na kutoa business card moja, akanyoosha mkono wake kumpa Bélise. “Mawasiliano yangu yote yapo humo).
Bélise aliipokea ile kadi huku akimtupia jicho la wizi Ibrahim, kisha macho yake akayapeleka kwenye ile kadi aliyopewa na kuitazama kwa makini.
“Asante, bwana mkubwa, mimi naitwa Bélise Gatete, nitawasiliana nawe kwa vile umenipa namba zako… kwa heri bwana Bigirimana,” Bélise alisema huku akimtazama Ibrahim akionekana kusubiri ruhusa ya kuondoka.
“Kusema ukweli, natamani sana tufahamiane zaidi ya hivi, Ee... ninachojaribu kusema... ni... ee, kwa nini tusiwe ee ... labda tuseme marafiki?” Ibrahim alisema kwa sauti tulivu huku akimtazama Bélise kwa makini.
“Kwa hali inavyoonekana, sisi tayari tu marafiki, au ni urafiki gani unaoutaka?” Bélise alisema huku akiangalia kando na kuachia tabasamu la aibu.
“Urafiki kama ulivyo… nadhani wewe si mtoto mdogo unaelewa nikisema hivyo!” Ibrahim alisema huku akiangua kicheko hafifu.
Bélise alimmtazama Ibrahim kwa udadisi zaidi huku akishusha pumzi.
“Sawa, nadhani tutaelewana zaidi kadri tutakavyokuwa pamoja, au siyo?”
Ibrahim alishusha pumzi kwa nguvu huku akijilegeza na kuegema gari lake. Akaonekana kuwaza kidogo kwa sekunde chache huku akizungusha macho yake kuyatazama mazingira ya eneo lile.
“Unaweza kupata nafasi Jumamosi ya wiki hii? Ningependa tuonane kwa maongezi zaidi ya kufahamiana, maana ni kweli tumeshakuwa marafiki,” hatimaye Ibrahim alisema huku akiilamba midomo yake iliyoanza kukauka.
“Wapi?” Bélise alimuuliza Ibrahim baada ya kufikiria kidogo huku akimtazama kwa makini.
Hotel Club Du Lac Tanganyika, saa kumi na mbili na nusu jioni. Nadhani panafaa zaidi,” Ibrahim alisema pasipo hata kufikiri.
“Sawa…” Bélise alisema huku akibetua kichwa chake baada ya kufikiria kidogo…
______
Bwana, una matatizo gani mbona hujibu?” sauti ya Bélise ilimzindua Ibrahim kutoka kwenye mawazo pale Bélise alipoulizwa swali.. Ibrahim alimtazama Bélise na kushusha pumzi za ndani kwa ndani huku akilazimisha tabasamu.
Ah, usijali! Karibu ukae,” Ibrahim alisema huku akimuonesha Bélise sehemu ya kuketi, huku akijiweka vizuri kwenye kiti chake.
Ahsante, samahani kwa kuchelewa,” Bélise alijaribu kujitetea huku akimtumbulia macho Ibrahim.
Bila samahani,” Ibrahim alimjibu Bélise kumtoa shaka huku akiitazama saa yake ya mkononi na kuongeza, “…hukuchelewa, ni saa kumi na mbili na dakika therathini na tano tu. Bado ahadi yako ni ya Kizungu.”
Bélise aliketi kwenye kiti alichoelekezwa na ibrahim huku akijitahidi kuyakwepa macho ya Ibrahim yaliyokuwa yanamtazama kwa makini. Muda huo huo mhudumu wa ule ukumbi alifika na kusimama mbele ya meza yao huku akimtazama Bélise kwa tabasamu pana la kibiashara lililokuwa likivinjari usoni pake.
Karibu dada, sijui ungependa kuagiza nini?” yule Mhudumu alimuuliza Bélise kwa sauti tulivu huku macho yake yakiweka kituo kwenye uso wa Bélise.
Bélise alimtazama yule mhudumu kwa makini huku akizungusha macho yake kujaribu kufikiria, alivuta pumzi ndefu za ndani kwa ndani kisha akazishusha taratibu huku akiminya midomo yake yenye maki.
Niletee chipsi na nusu kuku,” hatimaye Bélise aliongea baada ya kufikiria kidogo kisha aligeuka kumtazama Ibrahim huku akiachia tabasamu la haya.
Ongeza na glasi nyingine ya Navette de Marseille,” Ibrahim alimwambia yule mhudumu kisha alimtupia jicho Bélise.
Yule mhudumu aligeuka na kuanza kuondoka eneo hilo, lakini Ibrahim alionekana kukumbuka jambo na kumwita. Yule mhudumu akarudi huku akiyatuliza macho yake kumtazama Ibrahim kwa makini.

ITAENDELEA...
 
HADI LINI! 5

Na Bishop Hiluka


Kuna kingine chochote?” yule mhudumu alimuuliza Ibrahim akiwa bado kamkazia macho yake.
Ndiyo,” Ibrahim alijibu yule mhudumu huku akimtupia jicho Bélise, kisha anaongeza, “Vitu tulivyoagiza vipeleke kwenye kile chumba maalumu, sawa?”
“Ondoa shaka,” alisema yule mhudumu huku akimtupia jicho la wizi Bélise na kuachia tabasamu pana. Kisha aligeuka na kuondoka haraka kutoka eneo lile na kuelekea kwenye kaunta ya jikoni ya ukumbi wa maakuli.
Ibrahim alishusha pumzi huku akimtupia jicho Bélise na kuachia tabasamu, “Chakula cha hapa kizuri sana,” alismema huku akiendelea kutabasamu.
* * * * *
Saa tatu usiku, kwenye chumba kizuri cha kifahari cha Hotel Club du Lac Tanganyika, taa mbili za rangi ya bluu zilikuwa zinatoa mwanga hafifu wenye mg’ao na kufanya nusu ya chumba kile kuwa kizani.
Kilikuwa chumba kikubwa chenye kitanda kikubwa cha samadari kilichokuwa katikati ya chumba, kitanda kile kilikuwa cha futi sita kwa sita, cha mbao ngumu za mninga na chenye droo mbili kila upande, na juu ya zile droo kulikuwa na zile taa mbili za rangi ya bluu.
Mbele ya kile kitanda kulikuwa na seti nzuri ya runinga pana aina ya LG ya inchi hamsini na mbili na chini ya ile runinga kulikuwa na meza nzuri nyeusi ya kioo, ambayo juu ya meza kulikuwa na simu mbili kubwa za kisasa za Smartphone na kando ya meza ile kulikuwa na briefcase nzuri nyeusi iliyokuwa imeegamishwa kwenye ukuta.
Upande wa kushoto wa kile chumba kulikuwa na jokofu la vinywaji lililokuwa kwenye kona, na hatua chache kutoka kwenye lile jokofu kulikuwa na dirisha pana la kioo lililokuwa limefunikwa kwa pazia zito na refu lenye nakshi za michoro ya maua yaliyodariziwa vizuri na kuyafanya yapendeze.
Kwa kutokea juu kwenye lile dirisha la chumba kile mtu angeweza kuona mandhari nzuri yenye nyasi nzuri za rangi ya kijani kibichi zilizopakana na maua ya rangi tofauti ya kuvutia na bwawa ambalo lilikuwa limezungukwa na nyasi zilizopandwa katika hoteli ile.
Pia mle ndani kulikuwa na kabati kubwa la kisasa la nguo ambalo hata hivyo lilikuwa limefungwa. Na pembeni ya lile kabati kulikuwa na kochi moja kubwa la sofa na meza ya kioo iliyokuwa mbele yake iliyokuwa na bilauri mbili ndefu, chupa kubwa ya mvinyo mwekundu wa Navette de Marseille na vyombo vilivyokuwa na mabaki ya chakula, vyote vikiwa juu ya ile meza.
Kando ya lile sofa kulikuwa na meza fupi ya mbao iliyokuwa na simu ya mezani na kitabu kidogo kilichokuwa ba orodha ya majina ya watu na kampuni zilizotumia huduma ya simu hiyo ya mezani. Kwenye kona ya chumba kile upande wa kulia kabisa kulikuwa na mlango wa kuelekea kwenye chumba kidogo cha maliwato na bafu.
Ukutani kulikuwa na picha mbili kubwa nzuri za kuchorwa zilizokuwa zimetundikwa sehemu mbili tofauti. Moja ilikuwa ni picha ya wanyama wa porini na picha nyingine ilikuwa ya ua zuri la rangi nyekundu na bluu lililochorwa kwa ustadi wa hali ya juu.
Picha zote mbili zilikuwa zimewekwa ndani ya fremu nzuri za kioo na kuzifanya zionekane vizuri katika hizo kuta nyeupe na safi za chumba kile. Chini sakafuni kulikuwa na zulia zuri lenye mchanganyiko wa maua ya rangi ya njano, bluu na kijani kibichi.
Hapo sakafuni zilionekana nguo za Ibrahim na Bélise zilizokuwa zimetupwa tupwa na kusambaa ovyo, na juu ya kile kitanda kikubwa cha kifahari walionekana Ibrahim na Bélise waliokuwa wamemezwa na ulimwengu wa anasa.
Muda ule Bélise alikuwa anajitahidi kumwonesha Ibrahim ufundi sanaa ya aina yake na kumfanya kutoa miguno kwa raha aliyojisikia huku akimimina ahadi nyingi ambazo aliapa kuwa angezitekeleza.
Ibrahim alimbusu mzinzi mwenzie na kumpapasa nyama za mgongo huku akihema kwa nguvu. Bélise naye alikuwa anatweta kwa mchoko lakini akionekana kuhisi faraja kubwa iliyokuwa inapenya kwenye mishipa yake ya damu, akajikuta akilia kilio kilichokosa tafsiri inayoweza kukubalika kwa haraka.
Akiwa anakaribia kumaliza safari yake ya kufika kileleni, Ibrahim alianza kutapatapa kama mtu aliyetaka kukata roho, jambo hilo likamfanya Bélise kupitisha vidole vyake laini ambavyo vilikuwa na kucha ndefu kwenye masikio ya Ibrahim. Kitendo hicho kikamfanya Ibrahim kuvunja dafu huku akilia kama mtoto mdogo.
Alitweta huku akionekana kuwa hoi na mapigo ya moyo wake yalikuwa yakimuenda mbio isivyo kawaida.
Bélise alijiinua taratibu kutoka pale kitandani na kumwacha Ibrahim akiwa bado amejilaza kwa uchovu aliokuwa nao, kisha aliingia bafuni na kujimwagia maji, na alipotoka alichukua taulo na kujifunga juu yake kupitia kifuani na kufanya lile taulo liache mapaja yake wazi, kisha alirudi tena katandani, akaketi juu ya kitanda huku akimtazama Ibrahim kwa aibu. Ibrahim alikuwa bado amejilaza huku akiwa amefumba macho yake kwa uchovu.
Mara simu ya Ibrahim ikaanza kuita na kumshtua Ibrahim. Alifumbua macho yake na kuinua kichwa chake kutazama mahali zilipo zile simu zake. Bélise aliinuka na kuichukua ile simu iliyokuwa inaita huku akipitisha macho yake kuiangalia namba ya mpigaji kabla hajampa Ibrahim.
Ibrahim aliitazama kwa makini ile namba iliyokuwa inampigia na kuguna huku akikunja sura yake. Aliipokea ile simu kwa shauku kubwa na kuiweka kwenye sikio lake la upande wa kushoto huku akiminya midomo yake.
“Hallo… unasema!” Ibrahim anamaka kwa mshtuko huku akijichomoa haraka kutoka pale kitandani.
Alimkodolea macho Bélise huku akiwa makini kusikiliza kile alichokuwa anaelezwa na mtu aliyekuwa upande wa pili wa ile simu. Akashusha pumzi ndefu huku aakiuma mdomo wake wa chini.
“Una uhakika? Okay, okay… nakuja sasa hivi…” Ibrahim alisema na kuamka kutoka pale kitandania akakimbilia bafuni bila hata kukata simu, kule bafuni alijimwagia maji chap chap na alipomaliza akaokota zile nguo zake pale sakafuni na kuanza kuvaa haraka.
Muda huo Bélise alikuwa anamtazama kwa mshangao uliokuwa umechanganyika na wivu, macho yake yalionesha wazi kumuonea Ibrahim.
Ibrahim alipomaliza kuvaa alichukua briefcase yake na kuanza kutoka nje haraka kabla hata hajamaliza kuvaa shati lake vizuri, mara akakatizwa na sauti kali ya Bélise kabla hata hajafungua mlango na kutokomea.
Mpenzi!”
Ibrahim aligeuza shingo yake kumtazama Bélise kwa mshangao, alionekana kukerwa kidogo.
“Unasemaje? Nachelewa!” Ibrahim alisema huku akimtazama Bélise kwa makini zaidi.
Bélise alikuwa amezishika mkononi zile simu mbili za Ibrahim na kumwonesha huku akimkazia macho.
Sawa, lakini umesahau simu zako,” alimwambia huku akiminya midomo yake akionesha dhahiri kuingiwa na wivu.

ITAENDELEA...
 
HADI LINI! 6

Na Bishop Hiluka


Ibrahim alionekana kushtuka na kurudi haraka hadi alipokuwa amesimama Bélise, akanyoosha mkono wake kutaka kuzichukua simu zake akionekana kuwa na haraka.
“Asante, mpenzi wangu…” Ibrahim alisema huku akiachia tabasamu laini.
Bélise akaurudisha nyuma mkono wake uliokuwa umeshika zile simu huku akimkazia macho Ibrahim, kitendo kile kikamfanya Ibrahim ashike kiuno chake huku akimtazama Bélise kwa mshangao uliochanganyika na hasira.
“Kuna shida yoyote?” Ibrahim aliuliza kwa sauti iliyokuwa imebeba hasira.
”Ndiyo, kwa nini unanifanyia hivi?” Bélise alisema huku sauti yake ikionesha kubeba hasira kidogo. Wivu wa mapenzi ulikuwa unajionesha waziwazi kwenye uso wake.
Ibrahim alimwangalia Bélise kwa kitambo kifupi akionekana kutoelewa maana yake, akakunja sura yake na kutengeneza matuta madogo usoni huku akijaribu kufikiria.
“Nimekufanyia nini, mbona sikuelewi!”
“Unaniachaje?” Bélise alimuuliza Ibrahim huku akiongea kwa hasira, alimeza funda la mate kutowesha donge kubwa la hasira lililokuwa limemnasa kooni.
Ibrahim alimwangalia Bélise kwa mshangao zaidi, akakunja sura yake huku akimsogelea taratibu lakini Bélise alibetua midomo yake huku akikunja uso wake kwa hasira na kuanza kurudi nyuma.
“Kama uliona mkeo mali, kwa nini ulinitafuta?” Bélise alisema huku akirudi nyuma.
Ibrahim akazidi kushangaa, akamkazia macho Bélise na kushusha pumzi ndefu huku akijaribu kufikiria kidogo.
“Funguka, acha kuongea kwa mafumbo.”
“Usijitie hamnazo. Kama vipi nenda na usinitafute tena uone kama nitababaika!”
“Nipe basi simu zangu niende, mbona unanifanyia hivi lakini?” Ibrahim alionekana kulalamika.
“Sikupi mpaka kieleweke,” Bélise alisema na kuketi juu ya kile kitanda huku akiendelea kumkazia macho Ibrahim..
Ibrahim alisimama akamtazama Bélise kwa makini huku akionekana kukerwa, hata hivyo, alijitahidi sana kuzuia hasira yake. Kikapita kitambo kifupi cha ukimya huku kila mmoja akijitahidi kuidhibiti vyema hasira iliyokuwa inafukuta nafsini mwake. Ibrahim akatingisha kichwa chake kwa huzuni huku akimtazama Bélise kwa utulivu kama aliyekuwa akijaribu kuyasoma mawazo yake.
“Nipe changu nikupe simu zako, ulivyokuwa unaniahidi ulidhani nini!” Bélise aliongea huku akimkazia macho Ibrahim, alionekana kumaanisha kile alichokuwa anakiongea.
Ibrahim aliiweka briefcase yake sakafuni na kujipapasa mifukoni, akatoa wallet, akaifungua na kuhesabu kitita cha fedha haraka haraka, faranga laki moja kisha akanyoosha mkono wake kumpa Bélise. Bélise alizitazama zile fedha bila kuzipokea, kisha alinyanyua mabega yake kukataa.
Ibrahim alimtazama kwa mshangao, akataka kuondoka na zile fedha lakini akasita na kunyanyua mabega yake juu huku akibetua midomo yake.
“Unataka faranga ngapi?” Ibrahim alimuuliza huku akijishika kiuno.
“Laki tatu” Bélise alijibu huku akimkazia macho Ibrahim.
Ibrahim alivuta pumzi ndefu na kuzishusha taratibu, akauma midomo yake huku akiyatuliza macho yake kwenye uso wa Bélise, alionekana kufikiria kidogo na kuitupia jicho saa yake ya mkononi kisha akasonya. Alionekana kushtuka kidogo na kuamua kuongezea faranga zingine kama laki moja kwenye kile kitita cha faranga laki mbili, kisha anazitupa juu ya kitanda.
Bélise alionekana kuzihesabu zile fedha kwa macho pasipo kuzishika kisha akanyanyua uso wake kumtazama Ibrahim kwa mshangao.
“Hazitoshi!”
“Basi kesho nitakutumia zingine.”
Bélise alionekana kufikiria kidogo kama mtu aliyekuwa akijishauri jambo, kisha akanyoosha mkono wake kumpa Ibrahim zile simu. Ibrahim alizipokea na kuondoka haraka bila hata kuaga, akaufunga ule mlango nyuma yake.
Alipotoka ndani ya kile chumba alitokea kwenye korido pana na kushika uelekeo wa upande wa kulia wa ile korido pana, akaifuata korido iliyokuwa inatazamana na milango minne na upande wa kushoto kulikuwa na mlango mkubwa uliokuwa wazi.
Akaifuata korido hiyo hadi mwisho kabisa, upande wa kushoto kulikuwa na lifti, akafika na kubonyeza kitufe kilichokuwa kando ya ule mlango akijaribu kuiita ile lifti. Alisimama hapo kusubiri kwa dakika kadhaa lakini akagundua kuwa kile chumba cha lifti kilikuwa bado kipo ghorofa ya juu zaidi na kilikuwa kimekwama huko kwa muda mrefu. Huenda labda kulikuwa na mtu aliyeamua kuizuia ile lifti.
Ibrahim alisonya na kuondoka haraka akiufuata mlango mkubwa uliokuwa wazi, hapo akanza kuziparamia ngazi za kuelekea sehemu ya chini ya lile jengo la hoteli. Aliteremka ngazi mbili mbili kwa mwendo wa mbio mbio.
Baada ya kushuka hadi ghorofa ya kwanza aliufuata mshale mdogo mweupe uliokuwa umechorwa ukutani ukielekeza upande wa kushoto na kutokea kwenye ukumbi mdogo ambao kulikuwa na milango mitatu.
Mlango mmoja ulikuwa unaelekea kwenye ukumbi wa mazoezi, na juu ya mlango ule kulikuwa na kibao cheusi kilichokuwa na maandishi meupe yaliyokuwa yameandikwa kwa lugha ya Kifaransa ‘Salle de gymnastique’ yaani Ukumbi wa mazoezi (Gym).
Kwenye mlango wa pili kulikuwa na kibao juu yake kilichokuwa na maandishi yaliyosomeka kwa lugha ya Kifaransa ‘Magasin’ yaani Stoo. Na mlango wa tatu uliokuwa wazi ukiwa umefunikwa kwa pazia zuri na jepesi ulikuwa na kibao cheusi juu yake kilichokuwa na maandishi meupe ‘Sortie’ au ‘Exit’ kwa lugha ya Kiingereza, au mlango wa kutokea kwa Kiswahili.
Ibrahim alielekea moja kwa moja kwenye ule mlango uliokuwa na maandishi ‘Sortie’ juu yake na kuzikuta ngazi, akaziparamia zile ngazi kushuka chini hadi alipoukuta mlango mwingine uliokuwa na kibao juu yake chenye maandishi ‘Sortie’.
Ibrahim aliufuata ule mlango na kuvuka, wakati alipokuwa anapita akatazama upande wake wa kulia na kuona mlango mwingine ambao juu yake kulikuwa na maandishi yakisomeka ‘Sauna’, au ‘Bafu la mvuke’ kwa Kiswahili.
Sauna kilikuwa chumba maalumu kilichobuniwa kama sehemu ya kupata joto la mvuke ambalo huipa hewa ya chumba hicho joto na kisha hewa kusambaa katika chumba na kuipasha ngozi ya mtu aliyeingia humo. Joto lake huwa linategemea mtumiaji alihitaji liwe la kiasi gani na lilitumika zaidi kwenye nchi zenye baridi.
Ibrahim aliupita ule mlango uliokuwa na maandishi ‘Sauna’ na kwenda kutokea kwenye ukumbi mwingine wa baa, akaendelea mbele akiipita kaunta ya vinywaji iliyokuwa upande wake wa kulia na kukuta mlango mkubwa uliokuwa wazi. Juu ya ule mlango kulikuwa na kibao cheusi kilichokuwa na maandishi meupe yaliyosomeka kwa lugha ya kifaransa ‘Salle à manger’ yaliyokuwa na maana ya Ukumbi wa chakula kwa lugha ya Kiswahili.
Kwenye ukumbi ule wa baa kulikuwa na seti nzuri za runinga pana zilizokuwa zimetundikwa ukutani zikirusha burudani mbalimbali. Ndani ya ukumbi ule kulikuwa na watu kadhaa waliokuwa wameketi kwa utulivu huku wakijipatia vinywaji na wakati huo huo sauti ya muziki laini ilisikika taratibu ndani ya ukumbi ule na kuzikonga vizuri nyoyo za watu waliokuwemo ndani ya ule ukumbi.

ITAENDELEA...
 
HADI LINI! 7

Na Bishop Hiluka


Katika eneo hilo kulikuwa na wazungu wengi na Waafrika wachache sana, labda kutokana na gharama za juu za huduma zilizokuwa zinatolewa humo ndani, wote hawa walikuwa wanajipatia vinywaji na vyakula huku wakiendelea na maongezi yao.
Ibrahim aliwapita bila kusema neno kama vile hajawaona japo kuna mwanamume mmoja alionekana kumwita. Ibrahim hakuitika, hakugeuka wala hakusimama bali alizidisha mwendo akijifanya hajamsikia yule mwanamume na kuwafanya watu wengine mle ukumbini kugeuka kumtazama kw mshangao, kisha wakampuuza na kuendelea na hamsini zao.
Ibrahim aliongeza mwendo wake ili kulivuka eneo lile kwani alikuwa hapendi kutazamwa Aliufikia mlango wa mbele kabisa wa Hotel Club du Lac Tanganyika na kuusukuma, akatoka nje na kujikuta akikabiliana na macho ya watu wachache, hasa madereva wa teksi waliokuwa wanaosubiri wateja ili kuwapeleka sehemu mbalimbali za mji.
Wale madereva na watu wengine wachache waliokuwa wamesimama pale nje walikuwa wakipiga soga. Mara madereva wawili kati yao wakamuona Ibrahim na kumchangamkia huku wakimwita kila aina ya majina kama “Boss”, “Tajiri”, “Afisa”, “Mkubwa” n.k. ili kumvutia apande gari zao.
Ibrahim alitingisha kichwa chake kukataa huku akiwapita bila kuwatilia maanani na kuendelea na hamsini zake.
Alitembea haraka hadi alipolifikia gari yake la kifahari aina ya Toyota Lexus RX la rangi nyeupe na kufungua mlango, akaingia ndani ya lile gari na kufunga mlango, alionekana akiwa hana muda wa kupoteza. Alivaa mkanda wa siti haraka na kuliondoa gari lake taratibu kutoka kwenye yale maegesho ya magari ya Hotel Club du Lac Tanganyika akizunguka kuelekea kwenye geti kubwa la mbele la jengo lile la Hotel Club du Lac Tanganyika.
Bélise akatokea kwenye mlango wa mbele wa Hotel Club du Lac Tanganyika na kulikimbilia gari la Ibrahim lililokuwa linalifikia geti kubwa la mbele la hoteli lakini akasita, alikuwa anampungia mkono Ibrahim kwa nguvu kumwashiria asimame lakini Ibrahim aliliondoa gari lake pasipo hata kumjali na kukata kona upande wa kulia akiingia katika barabara ya Chausse d'Uvira.
Bélise alilisindikiza lile gari kwa macho akionekana kukata tamaa, lile gari liliongeza mwendo na kupotelea mtaani. Bélise akashusha pumzi za ndani kwa ndani huku akiminya midomo yake na kushika kiuno.
Kijana mmoja mtanashati, mwembamba na mrefu aliyekuwa amevaa suti maridadi ambaye alikuwa mmoja kati ya watu wachache waliokuwa wamesimama pale nje ya Hotel Club du Lac Tanganyika alimtazama Bélise kwa makini kama aliyekuwa akimfananisha, kisha akamsogelea huku akiendelea kumtazama kwa makini. Bélise alishtuka na kugeuza shingo yake kumtazama Sylvere na kujikuta akipigwa butwaa.
“Hey, Sylvere! Bélise alimaka kwa mshangao mkubwa huku akimtazama Sylvere usoni. Sylvere aliachia tabasamu pana huku akimkazia macho Bélise kwa makini.
“Bélise, unafanya nini hapa?” Sylvere alimtupia swali Bélise huku akimtazama kwa acho ya udadisi.
Bélise alishindwa kujibu, alimtazama Sylvere kwa makini kisha akatandaza mikono yake kumkumbatia. Walikumbatiana kwa mahaba huku wakibusiana. Sylvere alizungusha mikono yake kwenye kiuno cha Bélise huku akimkazia macho kumtazama usoni.
“Mbona ulikuwa hupokei simu yangu?” Sylvere alisema huku akiendelea kumkazia macho Bélise.
“Ngoja tutaongea,” Bélise alisema huku akitazama kando kuyakwepa macho ya Sylvere.
Katika barabara ya Chausse d'Uvira Ibrahim aliendelea kuendesha gari kwa mwendo wa kasi na kuyafikia makutano ya barabara za Chausse d'Uvira na barabara ya RN 5 Boulevard du 1er Novembre iliyokuwa inatokea katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Bujumbura.
Muda ule wa usiku jiji la Bujumbura lilikuwa limemezwa na utulivu wa aina yake. Kulikuwa hakuna pilika pilika zozote zilizokuwa zinaonekana barabarani wala mitaani bali magari machache tu yaliyokuwa yakikatisha barabarani, hasa magari ya Jeshi la Serikali ya Burundi.
Ibrahim aliifuata ile barabara pana ya Boulevard du 1er Novembre akizidi kuelekea katikati ya mji akiwa bado katika mwendo wa kasi, akalivuka eneo la viwanda, na mbele akakutana na pikipiki aina ya Boxer iliyokuwa na watu wawili ikiwa katika mwendo wa kasi ikitokea mjini kwenda maeneo ya viwandani, ile pikipiki ikaonekana kuingia upande ule lilipoku gari la Ibrahim.
Ibrahim aliiona ile pikipiki akakanyaga breki kwa nguvu, gari lake likasota na kuyumba kwenye barabara hiyo pana, bahati nzuri gari halikutoka nje ya barabara. Ibrahim akasonya na kukunja ngumi huku akiinua juu kidole chake cha kati kumuonesha yule dereva wa pikipiki katika hali iliyoashiria hasira alizokuwa nazo.
Pikipiki ile liserereka kisha dereva wa pikipiki akaiweka sawa na kuongeza mwendo pasipo kusimama. Mtu aliyekuwa amepakiwa nyuma kwenye ile pikipiki aliinua juu mkono wake wa kushoto huku kidole cha kati kikining’inia hewani utadhani kilikuwa kimepigiliwa msumari katika staili ya kumzodoa Ibrahim.
Ibrahim alisonya kwa hasira na kukanyaga pedeli ya mafuta, gari likajivuta na kufanya magurudumu yake kuchimba ardhi, kisha likaondoka kwa mwendo wa kasi. Ibrahim aliendesha gari lake kwa kasi huku akiendelea kusonya kwa hasira kisha akakata kona kuingia upande wa kushoto akiingia katika barabara ya Avenue de I'OUA.
Katika ile barabara ya Avenue de I'OUA Ibrahim alipishana na magari mawili matatu likiwemo lori moja la Jeshi la Serikali ya Burundi ambalo lilikuwa limewabeba wanajeshi wengi waliokuwa wamevaa sare za jeshi na bunduki zao mikononi, wakiwa kwenye doria kuhakikisha usalama wa nchi, hasa kwa sababu kulikuwa na tishio la waasi waliotaka kufanya mapinduzi mengine ya kutaka kuing’oa madarakani Serikali ya Rais Pierre Nkurunziza.
Wanajeshi waliokuwa kwenye lile lori waligeuka kumtazama Ibrahim kwa mshangao wakati gari lake likipishana na gari la jeshi kwa mwendo wa kasi utadhani labda alikuwa kwenye mashindano ya magari, hata hivyo wale wanajeshi hawakusimama wala kumfuatilia, waliendelea na safari yao.
Ibrahim aliendesha akiwa mwingi wa mawazo, akaupita mgahawa maarufu wa Parquet de la Mairie de Bujumbura na mbele yake, kabla hajakifikia kituo cha mafuta cha ANS Station mara akakuta kizuizi cha barabarani ambacho kilikuwa kimeandikwa kwa lugha ya Kifaransa POLICE CONTROLE au POLICE CHECK POINT kwa lugha ya Kiingereza, na kwenye kizuizi hicho kulikuwa na askari polisi na wanajeshi kadhaa wa serikali ya Rais Pierre Nkurunziza.
Ibrahim alikanyaga breki na kupunguza mwendo na hatimaye kusimamisha gari lake umbali wa mita kama therathini hivi kutoka kilipokuwa kizuizi kile kando ya barabara ya Avenue de I'OUA. Alisonya huku akaiitazama saa yake ya mkononi, hakuwa na muda wa kupoteza kwani alikuwa anatakiwa awe amefika Avenue de I’Hopital ambako alipigiwa simu akitakiwa kufika haraka ndani ya dakika ishirini! Laiti angejua kuwa barabara ile ilikuwa na kizuizi cha barabarani asingepita kabisa barabara hiyo.

ITAENDELEA...
 
HADI LINI! 8

Na Bishop Hiluka


Askari wawili, Major Ferdinand Niyongabo na Koplo Diomede Sinzumusi walianza kupiga hatua zao kulisogelea gari la Ibrahim huku wakiwa wameshika vyema bunduki zao aina ya SMG wakizielekeza kwenye lile gari. Koplo Diomede Sinzumusi alilifikia lile gari na kumuuliza Ibrahim kwa sauti ya ukali.
“Unatoka wapi na unaelekea wapi saa hizi?”
“Natoka kwenye miradi yangu naelekea nyumbani… Vipi kuna tatizo lolote?” Ibrahim alimuuliza yule askari kwa kujiamini huku akimkazia macho.
Wakati huo huo Major Ferdinand Niyongabo akalifikia lile gari la Ibrahim na kuzunguka akielekea upande wa nyuma wa lile gari huku akiwa analichunguza kwa jicho la hadhari.
“Nipe leseni yako ya udereva,” Koplo Diomede Sinzumusi aliongea kwa sauti kali akimwamuru Ibrahim huku akimkazia macho yake.
Ibrahim alitoa leseni yake na kumpa Koplo Diomede Sinzumusi huku naye akimkazia macho bila kupepesa. Koplo Diomede Sinzumusi aliipokea ile leseni ya udereva ya Ibrahim na kuanza kuikagua. Kitambo kifupi cha ukimya kikapita wakati yule askari akiendelea kuikagua ile leseni ya Ibrahim na wakati akifanya hivyo Major Ferdinand Niyongabo akawa anazunguka gari na kwenda mbele kwenye mlango wa dereva.
“Umebeba nini ndani ya gari yako?” Koplo Diomede Sinzumusi alimuuliza tena Ibrahim kwa ukali akiwa bado kaishikilia mkononi ile leseni ya udereva ya Ibrahim.
Ibrahim alimtazama Koplo Diomede Sinzumusi kwa makini huku donge la hasira likianza kumkaba kooni, maana aliona kuwa alikuwa anamchelewesha kuendelea na safari yake pasipo sababu za maana. Alitafakari kidogo akitafuta jibu la kumpa yule askari lakini kabla hajajibu, Major Ferdinand Niyongabo akamfikia na kumtazama kwa makini usoni.
“Hey, Bigirimana! Mambo vipi?” Major Ferdinand Niyongabo alisema huku akiachia tabasamu pana usoni kwake.
“Salama afande, vipi kuna tatizo?” Ibrahim alijibu huku naye akiachia tabasamu pana usoni kwake.
“Ni katika kuhakikisha tu kuwa nchi na wananchi wake wanakuwa salama kabisa,” Major Ferdinand Niyongabo alisema huku akiinama kidogo na kuegesha mkono wake kwenye dirisha la mlango wa gari.
Ibrahim alibetua kichwa chake akionesha kukubaliana na Major Ferdinand Niyongabo. Muda huo huo Koplo Diomede Sinzumusi aligeuka kumtazama Major Ferdinand Niyongabo kwa makini kisha akamgeukia tena Ibrahim na kuonekana kunywea kidogo, baada ya kuona kuwa mtu aliyekuwa anataka kumkagua alikuwa anafahamiana na bosi wake.
Koplo Diomede Sinzumusi hakuna na namna nyingine isipokuwa kumrudishia Ibrahim ile leseni yake ya udereva. Ibrahim aliipokea ile leseni na kushukuru.
Major Ferdinand Niyongabo akamruhusu Ibrahim aondoke na kuwapa ishara askari wengine waliokuwa wamesimama kwenye kile kizuizi kuondoa kile kizuizi. Askari hao walitii amri ya Major Ferdinand Niyongabo na kuondoa kile kizuizi cha barabarani na kumruhusu Ibrahim kupita.
“Ukipata tatizo njiani nipigie, maana si salama sana saa hizi!” Major Ferdinand Niyongabo alimwambia Ibrahim na kumwashiria kuwa anaweza kuondoka.
Ibrahim alikubali kwa kichwa huku akimshukuru, na muda huo huo akaingiza gia na kuliondoa gari lake akiifuata barabara ile ya Avenue de I'OUA iliyompeleka hadi kwenye mzunguko (roundabout) uliokuwa unaziunganisha barabara za Avenue de I'OUA, Boulevard Mwambutsa, RN 9 na Chaussée du Peuple Murundi. Akauzunguka ule mzunguko akiingia upande wa kulia kuifuata barabara ya Chaussée du Peuple Murundi iliyopita katika kituo cha mafuta cha Top One PC Station.
Barabara ile ya Chaussée du Peuple Murundi ilikuwa barabara iliyokuwa inakatisha katikati ya makazi ya watu na ofisi kadhaa na mbele kidogo Ibrahim akalivuka daraja la mto Ntahangwa, mto wenye urefu wa kilomita 10.75 uliokuwa unapeleka maji yake katika Ziwa Tanganyika, kisha mbele kidogo akalipita Kanisa la Pentekoste, lililokuwa upande wa kulia wa barabara ile.
Baada ya kulipita lile Kanisa la Pentekoste, mlevi mmoja aliyekuwa anatembea kando kando ya ile barabara ya Chaussée du Peuple Murundi alianza kuvuka ile barabara kuelekea upande wa pili wa barabara bila kutazama kama kuna gari lililokuwa likija, huku akiyumba.
Ibrahim alimuona yule mlevi na kuliyumbisha gari lake huku na huko ili kujaaribu kumkwepa. Sauti ya msuguano wa matairi kwenye lami kutokana na breki kali ilisikika na kumfanya yule mlevi kujikunja na kuruka kurudi alikokuwa ametoka huku akiwa kafumba macho yake. Pombe yote ilionekana kumtoka kichwani!
Ibrahim alimudu kumkwepa yule mlevi, na pasipo kusimama aliendelea mbele na kuanza kupunguza mwendo kisha akachepuka na kuingia upande wake wa kulia akiifuata barabara ya Avenue de I’Hopital, iliyokuwa inapita jirani na majengo ya hospitali maarufu ya Prince Régent Charles.
Prince Régent Charles Hopital
ilikuwa moja ya hospitali tatu kubwa za umma jijini Bujumbura, ikiwa na hadhi ya hospitali ya wilaya. Mahali kulipokuwa na hospitali ile lilionekana kuwa eneo tulivu mno kwa muda ule wa usiku, ni ndege pekee waliokuwa wamejazana kwenye mti mmoja mkubwa ndio walioonekana kuendelea kulipa uhai anga lililotanda kwa mwanga hafifu uliokuwa unatokana na taa za nyumba kadhaa zilizopo jirani na eneo lile huku nyota za angani zikionekana kushindwa kufua dafu katika kuileta nuru.
Ibrahim alipunguza mwendo kisha akafunga breki na kuliegesha gari lake chini ya mti ule mmoja mkubwa ambao ulikuwa mita chache kutoka kwenye nyumba moja iliyokuwa kando ya barabara ile ya Avenue de I’Hopital.
Ibrahim alitulia akionekana kulichunguza lile eneo kwa makini huku akiitazama ile nyumba huku wasiwasi ukijionesha kwenye uso wake, alishusha pumzi na kutoa simu yake ya mkononi na kuanza kutafuta namba fulani haraka haraka, lakini kabla hajabofya namba yoyote ili kupiga, kijana mmoja mrefu alijitokeza haraka na kwenda moja kwa moja kwenye lile gari la Ibrahim.
Alisimama karibu na mlango wa gari wa dereva, kisha akampa ishara fulani Ibrahim kumuonesha kuwa kulikuwa na mtu ndani ya ile nyumba ambayo Ibrahim alikuwa akiitazama kwa wasiwasi.
Yule kijana ndiye aliyekuwa amempigia simu Ibrahim kumtaka awahi kuja kumfumania mtu aliyekuwa akiishi ndani ya ile nyumba, Jeanine Kanyameza ambaye alikuwa mpenzi wa Ibrahim. Ibrahim alikuwa amempangishia nyumba Jeanine na alikuwa akigharamia mahitaji yote ya mwanamke yule.
Jeanine alikuwa mwanamke wa miaka kati ya ishirini na nane na therathini na alikuwa na umbo kubwa la kuvutia. Alikuwa mweupe kwa asili, lakini pamoja na urembo ule wa asili bado alikuwa anajiongezea kwa mapambo mengine ya gharama yaliyomfanya kuvutia zaidi. Hakuwa mwanamke wa kumtizama mara moja tu ukamwacha kwani alikuwa anavutia sana kutokana na umbo lake lililokuwa mfano wa umbo la nyigu.
Jeanine na Ibrahim walikuwa wamefahamiana baada ya kukutana katika hospitali ya Prince Régent Charles, ambayo Jeanine alikuwa anafanya kazi ya uuguzi. Walifahamiana baada ya Ibrahim kwenda katika hospitalini ile kumjulia hali mfanyakazi mwenzake aliyekuwa amelazwa baada ya kuugua ghafla.

ITAENDELEA...
 
HADI LINI! 9

Na Bishop Hiluka


Jeanine ndiye aliyekuwa muuguzi wa zamu wa wodi ile aliyokuwa amelazwa yule mgonjwa na alijitoa kwa kila hali kumhudumia, jambo ambalo lilionesha kumvutia sana Ibrahim.
Kukutana kwao ndiyo ulikuwa mwanzo wa kufahamiana zaidi, kisha urafiki ukazaliwa na baada ya wiki chache wakawa wapenzi. Kilichofuata baada ya hapo lilikuwa penzi lililokua taratibu, na baada ya miezi michache Jeanine akawa nyumba ndogo rasmi ya Ibrahim na kuanza kupata huduma zote alizostahili kupewa mke.
Ibrahim alitokea kumpenda sana Jeanine na kumhudumia kwa kila kitu, ikafikia wakati akawa katika mchakato wa kutaka kumuoa ili awe mke wake wa pili, na hata ikibidi kumwacha mkewe ili aishi na Jeanine.
Kitu ambacho Ibrahim hakuwa akikifahamu ni kwamba, Jeanine alimhitaji Ibrahim kwa kuwa alitaka kumtumia kama chombo cha kumtoa kwenye maisha ya chini na kumpeleka hatua nyingine, lakini hakuwa mwanamke wa kutosheka na mwanamume mmoja.
Jambo ambalo Jeanine hakujua ni kwamba hakukuwa na siri duniani, taarifa zilimfikia Ibrahim ingawa Ibrahim hakutaka kuziamini kwa kuwa alikuwa akimpenda sana na kumwamini Jeanine. Hata hivyo, ilifika wakati Ibrahim aliamua kumuuliza Jeanine kuhusu taarifa zile lakini Jeanine ‘aliruka kimanga’ na kudai kuwa hizo zilikuwa njama za wabaya wake kutaka kumfitinisha naye.
Pamoja na kukataa lakini habari zile zilizidi kumuumiza sana Ibrahim na ndipo alipoamua kumtafuta mtu ambaye angekuwa mpelelezi maalumu wa kufuatilia nyendo za Jeanine na kumpa taarifa pindi angemuona akiingiza mwanamume mwingine ndani ya ile nyumba.
Alikuwa akimlipa pesa nyingi kwa ajili ya kufanya uchunguzi juu ya mwenendo wa Jeanine. Haikupita hata wiki, hatimaye Jeanine alikuwa kaingia kwenye ‘kumi na nane’ za Ibrahim, na sasa Ibrahim alikuwa amesimama nje ya ile nyumba ya Jeanine tayari kufanya fumanizi.
Ibrahim alishuka haraka kutoka kwenye gari lake na kuifuata ile nyumba huku akimwacha yule kijana aliyempa taarifa akiwa amesimama pale pale kwenye lile gari lake. Ibrahim alifika mbele ya ile nyumba na kushika kitasa cha mlango wa mbele, akakinyonga taratibu na mlango ukafunguka.
Aliusukuma ule mlango taratibu na kuingia ndani akiwa na wasiwasi kidogo kisha aliurudisha ule mlango nyuma yake taratibu na kutokea kwenye sebule nadhifu.
Taa ya pale sebuleni ilikuwa imezimwa na kuifanya ile sebule kuwa na mwanga hafifu sana, hasa kutokana na mwanga uliokuwa unapenya na kuangaza humo ndani kutoka kwenye taa za nje.
Ibrahim alisimama na kuzungusha macho yake akijaribu kulizoea giza la humo ndani, alitazama huku na huko akijaribu kusikiliza kwa makini na kuupimia utulivu wa humo ndani, huku sebule ile ikionekana kuwa tulivu mno na hakukuwa na sauti yoyote ya maongezi iliyokuwa inasikika mle ndani.
Ile sebule ilikuwa pana ikiwa na zulia zuri zuri la manyoya lililokuwa na mchanganyiko wa maua ya rangi nyeusi na nyeupe sakafuni na kulikuwa na seti moja ya makochi ya sofa yaliyokuwa yamepangiliwa vizuri upande wa kushoto wa sebule hiyo. Yale makochi yalikuwa yanatazamana na seti moja ya runinga bapa aina ya Sonny Blavia ya inchi 28 iliyokuwa imefungwa vizuri ukutani na kuunganishwa na decorder ya StarTimes yenye chaneli nyingi za kimataifa.
Upande huo huo wa kushoto wa ile sebule kwenye kona kulikuwa na meza fupi ya mapambo na jokofu kubwa. Katikati ya ile sebule kulikuwa na meza nzuri ya kioo na stuli ndogo nne zilizokuwa zimepangwa kuizunguka meza hiyo.
Ukutani kulikuwa na saa kubwa na kulikuwa na picha mbili kubwa, picha moja ilikuwa ikimuonesha mwanadada mrembo, Jeanine Kanyameza, akiwa amepozi kwa ajili ya picha katika siku ya kuhitimu mafunzo yake ya uuguzi. Picha ya pili ilikuwa inamuonesha Ibrahim akiwa kamkumbatia Jeanine katika picha aya pozi la kimahaba iliyokuwa imepigwa kwenye ufukwe wa Ziwa Tanganyika.
Upande wa kulia wa ile sebule kulikuwa na ukumbi mdogo wa chakula wenye meza kubwa ya mninga ya chakula ya umbo la yai ambayo ilikuwa imezungukwa na viti sita vya mbao ya mninga vilivyokuwa na foronya laini. Jirani na ule ukumbi wa chakula kulikuwa na mlango uliokuwa unaelekea kwenye korido iliyoelekea kwenye milango mitatu. Milango miwili ikiwa upande wa kushoto na mlango mwingine ulikuwa upande wa kulia.
Mlango wa kwanza upande wa kushoto ulikuwa mlango wa kuingia kwenye maliwato ya pamoja, mlango wa pili ulielekea kwenye chumba cha kulala wageni, na mlango mwingine uliokuwepo upande wa kulia ulikuwa mlango wa chumba kikubwa chenye maliwato ndani (master bedroom).
Ibrahim alizungusha tena macho yake akitazama pale sebuleni kwa udadisi zaidi kisha alikunja uso wake. Akaanza kupiga hatua taratibu kuuendea mlango uliokuwa unaelekea kwenye korido iliyokwenda vyumbani.
Ibrahim alikwenda moja kwa moja hadi kwenye mlango wa upande wa kulia wa korido ile na kusimama mlangoni, alikishika kitasa cha ule mlango akitaka kuufungua lakini akasita na kusimama huku akisikiliza kwa makini.
Sauti ya kilio cha mwanamke aliyekuwa akilia kwa mahaba mazito ilikuwa inasikika kutokea mle chumbani huku ikiambatana na miguno ya ajabu ajabu ya mwanaume. Ibrahim alionekana kupandwa gadhabu, akashindwa kuvumilia na kumeza funda la mate kutowesha donge kubwa la hasira lililomnasa kooni.
Ibrahim alivuta pumzi ndefu na kuzishusha taratibu, akajishauri kwa kitambo kifupi akiwaza endapo afungue ule mlango au la, kisha akaonekana kushindwa kuvumilia na kukishika kile kitasa cha mlango kwa nguvu kisha akakinyonga huku akiusukuma ule mlango lakini haukufunguka.
Sauti za kilio na miguno ndani ya kile chumba zikanyamaza ghafla na kufuatiwa na sauti ya mwanamke iliyokuwa inauliza kwa hofu kutokea chumbani, “Nani?”
Kama mtu aliyepandwa na wazimu, Ibrahim akaanza kubamiza ule mlango kwa ghadhabu akitaka kuuvunja. Hasira sasa zilikuwa zimempanda kichwani kama mbogo aliyejeruhiwa, akarudi nyuma hatua kadhaa na kuurukia ule mlango kwa teke moja la nguvu, mlango ukasalimu amri na kufunguka, nguvu aliyokuwa ameitumia ilimtupa na kumwangusha kwa kishindo katikati ya kile chumba.
Mwanadada Jeanine Kanyameza alikuwa na mwanaume kitandani, wakakurupuka kutoka pale kitandani kwa hofu, Jeanine aliinuka na kupiga magoti juu ya kitanda kwa hofu, uso wake ulikuwa umejawa hofu, jasho lilikuwa linamtiririka na macho yake alikuwa kayatoa utadhani alimuona mtoa roho. Akapiga kelele kwa hofu.

ITAENDELEA...
 
HADI LINI! 10

Na Bishop Hiluka


Yule mwanamume aliyekuwa Jeanine kitandani alisimama wima bila kutingishika pembeni mwa kitanda kama aliyekuwa amepigiliwa misumali huku akiwa ameshikilia nguo zake mkononi, uso wakeulikuwa umejawa hofu. Wote wawili walikuwa watupu kama walivyozaliwa.
Mkono wa kushoto wa Jeanine uliokuwa umevikwa bangili za rangi ya dhahabu ulikuwa umekunjwa ukishikilia upande wa kanga ili kujaribu kujisitiri sehemu ya utupu wa mbele na eneo la kifuani, huku akiacha sehemu kubwa ya mwili wake kubaki tupu na hivyo kuonesha mapaja yake yaliyonawiri vizuri na kulidhirisha umbo lake lake la nyigu.
Nywele zake ndefu zilikuwa zimesukwa kwa mtindo wa rasta na kuning’inia hadi kwenye mabega yake na mkono wake wa kulia ulikuwa umekunjwa kwenye kiwiko na kuziba mdomo wake ambao ulikuwa umemdondoka kwa hofu ungedhani alikuwa amemuona ziraili mtoa roho.
Chumba kile cha Jeanine kilikuwa kikubwa na chenye nafasi ya kutosha. Upande wa kulia kulikuwa na kitanda kikubwa cha mbao chenye godoro la foronya laini na shuka za rangi ya bluu bahari. Mashuka juu ya kitanda yalikuwa yamevurugika kutokana na purukushani iliyokuwa imefanyika hapo kitandani. Sakafu ya kile chumba ilikuwa imefunikwa kwa zulia zuri la rangi ya kijivu lenye maua mekundu.
Upande wa kushoto wa kitanda kulikuwa na kabati zuri la nguo la ukutani lililokuwa pembeni ya dirisha kubwa ambalo lilifunikwa kwa mapazia marefu na mepesi yaliyokuwa yanaruhusu hewa safi kupenya na kuingia mle ndani.
Upande wa kulia wa kile chumba kulikuwa na meza ya vipodozi (dressing table) iliyokuwa na kioo kirefu cha kujitazama na aina mbalimbali za vipodozi vikiwa juu ya meza ile, na pembeni ya meza kulikuwa na mlango wa kuelekea kwenye chumba cha maliwato.
Ibrahim akiwa hayaamini macho yake, aliinuka kutoka pale sakafuni alipokuwa amedondoka huku akimkodolea macho yule mwanamume mgoni wake na kujiandaa kumvamia, lakini hakuwa amejua kilichokuwa kikiendelea kwenye mawazo ya yule mwanaume. Hivyo likatokea jambo la ghafla ambalo hakuwa amelitarajia, yule mwanaume alichomoka kwa kasi ya ajabu na kutimka kama mkizi huku akiwa ameshika nguo zake mkononi.
Wakati alipokuwa anatoka nduki alimpiga kikumbo Ibrahim ambaye alikuwa amesimama wima na kumwangusha chini, msukumo wa nguvu ukamtupa Ibrahim chini kwa mshindo mkubwa na kumfanya kugaragara pale sakafuni mithili ya mgonjwa mwenye kifafa.
Jeanine alipiga kelele ya hofu huku akiiachia kanga yake iliyodondoka sakafuni na kumwacha akiwa mtupu kabisa.
Ibrahim hakukubali kumwachia mgoni wake aondoke kirahisi, alijinyanyua haraka kutoka hapo sakafuni na kuchomoka kwa spidi kumfuata yule mwanamume kabla hajafanikiwa kutoka nje, na alipomfikia ndipo vita kuu kati ya Ibrahim na mgoni wake ilipoibuka.
Yule mwanamume alikuwa anakukuruka kushika kitasa cha mlango wa mbele wa nyumba ili afungune mlango lakini kabla hajaufungua, Ibrahim aliruka kama mkizi na kumkumba, wote wawili wakapiga mwereka sakafuni. Ibrahim akawahi kusimama huku hasira zikiwa zimempanda kichwani kama mbogo aliyejeruhiwa.
Yule mwanamume naye alisimama akiwa mtupu na kumtupia Ibrahim mapigo mawili ya kushtukiza ya ngumi kavu za tumbo, mapigo yale yalimkuta Ibrahim akiwa bado hajakaa sawa na kumpata kisawasawa, kaguna.
Yule mwanamume alirusha teke lililompata Ibrahim sawasawa kwenye kinena na kumrusha kisha kumtupa sakafuni huku akihisi maumivu makali yasiyoelezeka.
Yule mwanamume akiwa amepandwa na hasira alipanga kumfuata Ibrahim hapo hapo sakafuni ili amfundishe adabu na kumuonesha kilichomtoa kanga manyoya ya shingoni.
Ibrahim alimuona na kuinuka haraka kisha alijipanga tayari kwa mapambano akionekana kujihami zaidi kwa kufanya mashambulizi ya nguvu. Aliruka na kumvaa yule mwanamume, akampiga kichwa kikavu kinachompata barabara katikati ya macho na pua na kumvunja mshipa wa pua, pigo hilo likafanya yule mwanaume kupepesuka.
Damu zilianza kumtoka kwenye pua yake mfano wa mrija wa maji uliokatika. Yule mwanamume alijishika pua yake na kuiminya akijaribu kuzuia damu isiendelee kumtoka, na kabla hajakaa sawa Ibrahim alimrukia tena na kumkaba kabali ya nguvu iliyomfanya kukukuruka akitaka kujitoa kwenye ile kabala, lakini Ibrahim alizidisha kabali yake na kumfanya yule mwanamume kuanza kuishiwa nguvu.
Kuona vile Jeanine akaanza kupiga kelele kwa hofu akimsihi Ibrahim kumwaachia yule mwanamume, kelele hizo ziliwavuta watu wengi kutoka katika nyumba zilizokuwa jirani na hata wapiti njia, ambao walisogea katika eneo lile kushuhudia kilichokuwa kinaendelea. Ibrahim akiwa amepandwa na gadhabu alimbeba yule mgoni wake juu juu na kumtupa sakafuni kama vile alikuwa anabwaga mzigo.
Yule mwanamume alianguka na kuunguruma kwa maumivu makali kisha akatulia tuli kama mfu. Ibrahim alimtazama kwa hasira na kugeuka kuwatazama watu waliokuwa wamejazana kwenye madrisha na mlangoni kushuhudia ule mpambano, kisha akajiandaa kumkamata tena yule mwanamume ili kumpaa adhabu zaidi.
Bila kutegemea yule mwanaume alikurupuka na kumkumba Ibrahim, akamwangusha chini na kumwacha akigaragara, yeye akatoka nduki na kukimbilia nje kwenye giza akiwa mtupu.
Ibrahim alijiinua kutoka pale sakafuni alipoangushwa huku akiwa ana hasira, akageuka kumtazama Jeanine huku donge la hasira likiwa limemkaba kooni. Jeanine alimtazama kwa hofu huku akitokwa na machozi. Ibrahim aliendelea kumtazama kwa hasira kwa kitambo kisha akamnyooshea kidole. Jeanine alikuwa anatetemeka kwa hofu huku akiwa amekunjia mikono yake kifuani kaatika hali ya kuomba msamaha.
“Nisamehe mpenzi, sitarudia tena,” Jeanine alisema huku akigeuka kuwatazama watu waliokuwa wamejazama kwenye madirisha wakishuhudia kila hatua ya ule ugomvi mle ndani.
Alikuwa anaona haya lakini hakuwa na namna nyingine ya kufanya ila kujikaza kisabuni na kuendelea kumbembeleza Ibrahim ili apewe nafasi nyingine.
“Nikusamehe! Si nilikuuliza ukakataa, msamaha upi unautaka malaya mkubwa!” Ibrahim alimfokea Jeanine kwa hasira huku akimsukuma.
“Nisamehe mume wangu!” Jeanine alisema huku akianguka na kupiga magoti kwenye sakafu miguuni kwa Ibrahim. Hata hivyo, kauli ya kumwita Ibrahim mume wake ikaonekana kuzidisha hasira za Ibrahim.
“Nani mume wako, kafilie mbali!” Ibrahim alimwambia Jeanine na kumsukuma Jeanine, kisha aligeuka na kuanza kupiga hatua akielekea nje ya ile nyumba.
Jeanine alijua wazi kuwa alikuwa amelikoroga kweli kweli, uchungu ulimpanda na donge la hasira ya kumpoteza Ibrahim likamkaba shingoni. Alijiuliza angempata wapi tena mwanamume kama yule aliyekuwa msaada mkubwa kwake na kwa familia yake?
Alisimama huku mikono ikiwa kichwani, akaanza kujihisi kujidhulumu kitu kikubwa na cha thamani na kuona kuwa alikuwa anastahili adhabu hiyo kali. Alitamani amkimbilie Ibrahim na kuanguka miguuni kwake kumwomba radhi na ikibidi kugaragara.

ITAENDELEA...
 
HADI LINI! 11

Na Bishop Hiluka


Sasa akili yake ilianza kwenda kasi, alianza kujiuliza ni shetani gani aliyekuwa amemwingia hadi kujikuta akishindwa kutosheka na mwanamume mmoja? Ni shetani gani aliyempitia kiasi cha kujikuta akitamani kila mwanaume anayekutana naye? Akahisi kizunguzungu.
Kama mtoto mdogo Jeanine aliketi na kujikunyata kisha akaanza kulia kwa uchungu mkubwa pasipo kujali watu waliokuwa wakimtazama kwa mshangao na wengine kwa huruma. Taratibu wale watu waliokuwa wamesimama akishuhudia lile tukio wakaanza kuondoka huku wengi wakimuonea huruma na wengine wakimcheka kuwa alikuwa “amejitakia” mwenyewe. Wachache hawakuficha dhihaka yao kwake, kwani walikuwa wanacheka hadharani.
Ibrahim alipotoka mle ndani alifika kwenye gari lake na kuliondoa kwa kasi ya ajabu akiwa na hasira kisha akaifuata barabara ya Avenue de I’Hopital hadi kwenye makutano ya barabara za Avenue de I’Hopital, Avenue Foreami, Avenue de la Tanzanie na Avenue du Stade, akakata na kuingia kushoto akiifuata barabara ya Avenue du Stade.
Hapo akaongeza tena kasi na kulipita soko maarufu la Congolese Market lililokuwa kushoto kwake na mbele kidogo aliyapita majengo ya Bujumbura Apartments Services.
Haraka alipunguza mwendo wa gari lake baada ya kuwaona wanajeshi wawili wa doria wakijitokeza mbele yake na kusimama katikati ya ile barabara ya Avenue du Stade huku wakimuonesha ishara kwa mkono kuwa asimame. Alipowatazama vizuri akaona kuwa mikono yao ilikuwa imekamata vyema bunduki aina ya SMG.
Eneo lile lilikuwa tulivu sana lililokuwa jirani kabisa na Uwanja mkubwa wa Golf ambao ulikuwa umezungukwa na sehemu nzuri zenye viti visivyohamishika vya kupumzika vilivyokuwa chini ya miti mikubwa na mirefu ya vivuli na kuyafanya mandhari yake kupendeza sana.
Wakati akipunguza zaidi mwendo na kujiandaa kusimama mara akawaona askari wengine wawili wakijitokeza na kujongea katikati ya ile barabara kisha wakasimama nyuma ya kizuizi kilichokuwa katikaati ya ile barabarani huku nao wakiwa wameshika vyema bunduki zao mikononi.
Ibrahim alisimamisha gari lake kando kando ya ile barabara ya Avenue du Stade, akatazama vizuri eneo lile huku roho ikimdunda kwa nguvu na kugundua kuwa mbele yake kwenye kile kizuizi cha barabarani kulikuwa na magari mengine mawili yaliyokuwa yamesimamishwa kando ya barabara yakipekuliwa na askari wengine wa doria.
Ibrahim aliitazama saa yake ya mkononi na kugundua kuwa ilikuwa imeshatimu saa tano usiku, akashusha pumzi na kutulia ndani ya gari lake akiamua kubaki ndani ya gari lile, kisha akashusha kioo cha dirishani kwake huku akijiandaa kutengeneza tabasamu la kirafiki pindi askari mmoja alipomfikia.
Askari wawili walimsogelea huku wakimnyooshea mtutu wa bunduki, kisha wakalizingira lile gari. Askari mmoja aliyekuwa na cheo cha Inspekta, Medico Nzitunga alikwenda moja kwa moja pale dirishani, akamtazama Ibrahim na kumtambua mara moja, kisha akaachia tabasamu la kirafiki.
“Oh, Bosi… kumbe ni wewe?” Inspekta Medico Nzitunga alisema kwa furaha huku akinyoosha mkono wake kumsalimia Ibrahim.
Ibrahim hakujibu neno bali alinyoosha mkono wake kumpa yule askari huku akibetua kichwa chake. Donge la hasira za kumfumania mwanamke aliyekuwa anampenda lilikuwa bado limemkaba kooni. Muda huo huo askari wengine walisogea pale kwenye gari la Ibrahim kama ambao walikuwa wanalichunguza kwa makini, lakini Inspekta Medico Nzitunga aliwampa ishara ya kumuacha Ibrahim kisha akamuashiria Ibrahim kwa kichwa kuwa aendelee na safari yake.
Ibrahim aliachia tabasamu la kirafiki na kumpungia mkono Inspekta Medico Nzitunga katika namna ya kumuaga kisha akatia moto gari lake na kuliondoka kutoka eneo lile akiwaacha wale askari wanaendelea na ukaguzi wa magari mengine.
Ibrahim aliendesha kwa kasi na baada ya dakika chache alikata kushoto akaingia katika barabara pana ya kisasa iliyokuwa na sifa zote sawa na zile barabara nyingine za kisasa za jiji lile la Bujumbura, barabara ya Boulevard du 1er Novembre. Barabara hii ilikuwa inapakana na makazi ya kisasa yenye nyumba nyingi za ghorofa na ofisi chache zenye nidhamu kiuchumi.
Ibrahim aliendelea kuendesha kwa mwendo wa kasi huku akipishana na magari machache muda ule huku akiwa bado ana donge la hasira na kuufikia mzunguko wa barabara za Chaussée P.L. Rwagasore, Chaussée du Peuple Murundi na Avenue de la Revolution, akaifuata barabara ya Chaussée P.L. Rwagasore huku akilivuka jengo la Ofisi za Taifa za Utalii Burundi (Office National du Tourisme du Burundi).
Hapo akapishana na kundi la askari kama sita wa serikali waliokuwa wakielekea kule alikouwa akitoka, hakusimama bali aliendelea mbele na kuvuka majengo mengine marefu ya ghorofa yenye ofisi za kisasa za watu binafsi na ofisi za mashirika mbalimbali ya serikali ya Burundi.
Kisha akaupita mgahawa maarufu wa La Silhouette Café uliokuwa kando ya barabara ile ya Chaussée P.L. Rwagasore, Ibrahim aliutazama kwa makini na kumkumbuka Bélise. Kisha akasonga mbele na kuuvuka mgahawa mwingine wa Tropicana Net Café ambao pia ulikuwa kando ya barabara ile ya Chaussée P.L. Rwagasore upande wa kulia na kushoto kwake kulikuwa na barabara ya Rue de la Victoire.
Ibrahim aliongeza mwendo huku akiipita barabara ya Bvd. Patrice Lumumba kisha mbele kidogo akayakuta makutano ya barabara za Chaussée P.L. Rwagasore na Avenue Du Commerce.
Akataka kuingia Avenue Du Commerce lakini akasita na kuendelea mbele huku akikosa kumgonga mtu mmoja aliyekuwa akitembea kando ya ile barabara, kisha akaanza kuyapita majumba ya kifahari yaliyokuwa yamezungukwa na miti mirefu na kuta zenye usalama wa uhakika katika barabara ile tulivu ya Chaussée P.L. Rwagasore.
Eneo lile lote lilikuwa eneo ambalo limezungukwa na makazi ya kisasa kabisa ya viongozi wa kitaifa na wa kimataifa walioishi jijini Bujumbura. Vitongoji vyake vilikuwa vimeunganishwa kwa barabara nzuri za lami zenye taa za barabarani.
Ibrahim akaanza kupunguza mwendo huku akiwa na mawazo mengi, alianza kuendesha taratibu katika ile barabara ya Chaussée du Prince Louis Rwagasore iliyokuwa tulivu mno huku ikimulikwa na taa nzuri zenye mwanga mkali. Mtaa ule ulikuwa kimya sana katika nyakati zile za usiku, isipokuwa sauti kali za mbwa waliokuwa wanabweka katika nyumba za jirani kwa mbali.
Ibrahim akazidi kupunguza mwendo huku akiyavuka makutano ya barabara za Chaussée du Prince Louis Rwagasore na Avenue de L'Enseignemen. Kuanzia pale, hakwenda mbali sana mara akaifikia anaifikia nyumba nzuri ya kifahari iliyokuwa imezungukwa na miti mizuri ya vivuli na sehemu za wazi zenye bustani nzuri ya maua na nyasi za kijani kibichi zilizokatwa vizuri.

ITAENDELEA...
 
HADI LINI! 12

Na Bishop Hiluka


Ukuta wa ile nyumba kuizunguka ulikuwa mrefu uliokuwa umefungwa mfumo maalumu wa umeme wa kuzuia wezi juu yake usiomwezesha mtu kuona ndani. Ilikuwa moja ya majumba makubwa ya kisasa ya watu wakwasi yaliyokuwa yamezungushwa uzio na mageti makubwa yenye vifaa vyote vya usalama vya kuwahakikishia wakazi wake usalama wa hali ya juu.
Hapo ndipo ambapo Ibrahim alikuwa akiishia akiwa amepangishiwa na benki ya CRDB Burundi. Ibrahim alifika mbele ya geti kubwa jeusi la nyumba ile na kupiga honi mara mbili. Mlango mdogo wa geti ukafunguliwa kidogo, kisha mlinzi mmoja kutoka kampuni ya ulinzi ya KK Security Burundi ya jijini Bujumbura akatoa kichwa chake kuchungulia nje na kumuona Ibrahim.
Akaachia tabasamu na kulifunga lile geti dogo, kisha akalifungua lile geti kubwa na kuliruhusu gari la Ibrahim kuingia ndani ya ule uzio wa nyumba. Ibrahim aliliingiza gari lake ndani ya ule uzio wa nyumba na kuliegesha sehemu maalumu ya maegesho ya magari, jirani na gari jingine aina ya Landcruiser GX V8 lililokuwa na rangi nyeusi.
Baada ya kuunguruma kwa kitambo fulani Ibrahim alilizima gari lake na kuteremka kisha akachukua ile briefcase yake na simu zake mbili na kushika mkononi. Akafunga vizuri milango ya lile gari na kutupa macho yake kuangalia huku na huko. Mara mbwa mkubwa aina ya Rottweiler akamkimbilia na kumrukia huku akirusharusha mkia wake mfupi.
Ibrahim alampungia mkono yule mlinzi wa getini, mlinzi naye akapunga mkono huku akiwa kasimama kikakamavu kwenye kibanda maalumu cha mlinzi ambacho kilikuwa kimejengwa kando ya lile geti kubwa la nyumba hiyo. Kisha Ibrahim akaanza kupiga hatua zake kuelekea ndani ya ile nyumba huku akipiga mluzi kwa kujiamini zaidi.
Yule mlinzi wa getini alimtazama Ibrahim kwa wasiwasi mkubwa, kama aliyekuwa akijishauri akaanza kunyoosha mkono wake akitaka kumwita Ibrahim ili amwambie jambo lakini akasita na kushusha pumzi huku akitingisha kichwa chake kwa masikitiko.
Ibrahim aliendelea kupiga hatu zake taratibu pasipo kuelewa kile kilichokuwa kinaendelea kwenye mawazo ya yule mlinzi na kuisogea baraza ya nyumba yake ambayo ilikuwa kubwa ya kisasa, katika ile nyumba ya ghorofa moja.
Nyumba hiyo ilikuwa na madirisha makubwa ya kisasa na baraza kubwa mbele yake iliyopangwa seti moja ya makochi ya sofa. Nje ya ile nyumba upande wa kushoto kulikuwa na banda la wazi la kuegeshea magari.
Sehemu nyingine ya mandhari ya ile nyumba ilikuwa imezungukwa na miti mirefu na mikubwa ya kivuli, huku sehemu ya mbele ya ile nyumba ikiwa imezungukwa na bustani nzuri ya maua ya kupendeza na katikati ya bustani hiyo kulikuwa kumetengenezwa njia nzuri ya kutembea kwa miguu kwa vitofali vidogo vilivyokuwa vinavutia.
Kwa upande wa kulia wa ile nyumba kulikuwa na bwawa kubwa la kuogelea lililokuwa limezungukwa na vitanda vizuri vya kujipumzisha chini ya miamvuli mikubwa ya kivuli. Nyuma ya nyumba ile kulikuwa na tenki kubwa la maji na kando yake kulikuwa na karo kubwa la kuoshea vyombo na kufulia.
Ibrahim aliifikia ile baraza ya nyumba hiyo na kuacha kupiga mluzi, badala yake akaanza kuimba kwa sauti ya kawaida wimbo ule ule ambao mwanzoni aliuimba kwa kupiga mluzi, tena aliimba kwa kujiamini mno. Alikuwa akiimba kibwagizo kutoka katika wimbo wa Les Mangelepa, “Utakuja nitafuta mashariki na magharibi, utakujalia aah, kisha mama usinione… utaliaa, utalia aah, usionionee…”
Aliendelea kuimba maneno yale huku akikung’uta viatu vyake kwenye zulia dogo lililokuwepo pale mlangoni kwa kupigapiga miguu yake, kisha akashika kitasa cha mlango na kukinyonga, akausukuma ule mlango ambao ulisalimu amri na kufunguka.
Ibrahim alisimama pale akishangaa ilikuwaje hadi muda ule ule mlango wa nyumba ulikuwa haujafungwa kwa funguo? Aliinua mkono wake na kuitazama saa yake ya mkononi, ikamuonesha kuwa ilikuwa imeshatimia saa tano na dakika therathini na tano za usiku!
“Hii si kawaida!” Ibrahim aliwaza huku akikunja sura yake kwa hasira. Aliona kuwa alikuwa amepata sababu ya kumgombeza mkewe, hivyo alitulia kidogo pale barazani huku akiyatembeza macho yake kuangalia mazingira ya ile nyumba.
Yule mbwa mkubwa alikuwa bado anamfuata na kumrukia. Ibrahim alimfukuza yule mbwa na kuingia ndani huku akiendelea kuimba wimbo kwa kujiamini zaidi, akatokea kwenye sebule kubwa yenye samani zote muhimu za kisasa.
Ile sebule ilikuwa imepambwa kwa seti mbili za makochi ya sofa ya kifahari yaliyokuwa yamepangwa katika mtindo wa kuizunguka. Sakafuni kulikuwa na zulia zuri la rangi nyekundu huku katikati ya ile sebule kukiwa na meza nzuri ya kioo iliyokuwa na umbo la yai ikizungukwa na stuli ndogo nne za sofa.
Upande wa kulia wa ile sebule kwenye kona kulikuwa na runinga pana aina ya Samsung iliyofungwa ukutani na chini yake kulikuwa na meza fupi nyeusi yenye sistimu ya muziki, decorder na deki moja ya Dvd.
Ukutani kulikuwa na picha mbalimbali zilizokuwa zinamuonesha Ibrahim akiwa na familia yake, na picha zingine za kuchorwa zilizokuwa zinavutia sana. Upande wa kushoto wa ile sebule kwenye kona nyingine kulikuwa na meza fupi ya mapambo na jokofu. Pembeni ya meza ile kulikuwa na rafu kubwa iliyopangwa vitabu na majarida mengi na juu ya rafu hiyo kulikuwa na vinyago vya Kiafrika vilivyopangwa kwa ustadi wa hali ya juu.
Upande wa kushoto kulikuwa na ngazi zilizokuwa zinaelekea juu na upande mwingine kulikuwa na ukumbi mdogo wa chakula wenye meza kubwa ya chakula yenye umbo la yai iliyozungukwa na viti sita nadhifu vyenye foronya laini. Jirani na ule ukumbi wa chakula kulikuwa na mlango mwingine upande wa nyuma wa ile sebule uliokuwa unaelekea kwenye vyumba viwili vya chini vya ile nyumba.
Ibrahim alishtuka sana na kusimama ghafla, aliacha kuimba na kubaki mdomo wazi huku macho yake yakimtoka pima kwa mduwao. Akili yake ilikuwa kama iliyopigwa shoti kali ya umeme hatari wenye nguvu nyingi, na hivyo kuzifanya shughuli za mwili wake kusimama kwa ghafla kama aliyekuwa amepigwa kumbo na ugonjwa hatari wa kiharusi.
Alibaki amesimama pale pale jirani na mlango akiwa ameduwaa, kilichokuwa kimemshtua sana ni kuona ugeni mzito ndani ya nyumba yake ambao hakuwa ameutarajia kabisa na wala hakuelezwa kama wangefika siku ile. Alipatwa na hisia mbaya kuwa kwa vyovyote ugeni ule haukuwa umekuja pale kwa ajili ya kusalimia, bali kulikuwa na jambo zito lililokuwa limetokea!
Ibrahim akawaza haraka haraka huku akiwa ametahayari sana. Aliwakodolea macho wazazi wake na wazazi wa mke wake ambao walikuwa wameketi kwenye makochi ya sofa huku wakimtazama kwa makini.

ITAENDELEA...
 
HADI LINI! 13

Na Bishop Hiluka


ILIPOISHIA...

Ibrahim alishtuka sana na kusimama ghafla, aliacha kuimba na kubaki mdomo wazi huku macho yake yakimtoka pima kwa mduwao. Akili yake ilikuwa kama iliyopigwa shoti kali ya umeme hatari wenye nguvu nyingi, na hivyo kuzifanya shughuli za mwili wake kusimama kwa ghafla kama aliyekuwa amepigwa kumbo na ugonjwa hatari wa kiharusi.
Alibaki amesimama pale pale jirani na mlango akiwa ameduwaa, kilichokuwa kimemshtua sana ni kuona ugeni mzito ndani ya nyumba yake ambao hakuwa ameutarajia kabisa na wala hakuelezwa kama wangefika siku ile. Alipatwa na hisia mbaya kuwa kwa vyovyote ugeni ule haukuwa umekuja pale kwa ajili ya kusalimia, bali kulikuwa na jambo zito lililokuwa limetokea!
Ibrahim akawaza haraka haraka huku akiwa ametahayari sana. Aliwakodolea macho wazazi wake na wazazi wa mke wake ambao walikuwa wameketi kwenye makochi ya sofa huku wakimtazama kwa makini.

ENDELEA...

Baba yake, Mzee Hussein Bigirimana alikuwa ameketi kwenye sofa kubwa, aliinua mkono wake na kutazama saa yake ya mkononi kisha akainua uso wake na kumkazia macho Ibrahim yaliyokuwa na maswali lukuki, pembeni yake alikuwa ameketi mke wake, Mama Mariam Bigirimana, wote walikuwa wakimtazama Ibrahim kwa makini.
Ibrahim aliwakodolea macho na kuhisi kijasho chembamba kikimtoka mwilini. Akafungua mdomo wake kutaka kusema neno lakini maneno hayakutoka, mdomo wake ulimdondoka kwa hofu utadhani alikuwa amezingirwa na wanamgambo wa al-Shabab waliokuwa tayari kujilipua wakati wowote.
Ibrahim akayahamisha macho yake kutoka kwa wazazi wake hadi kwa wazazi wa mke wake, Mzee Diomede Tugiramahoro na Mama Ninziza Bernice, ambao walikuwa wameketi kwenye sofa jingine kubwa, nao pia walikuwa wanamwangalia Ibrahim kwa makini.
Ibrahim akaona kama vile macho yote yaliyokuwa yakimwangalia pale sebuleni yalikuwa yanamsuta, akavuta pumzi ndefu za ndani kwa ndani na kuzishusha taratibu huku akijipa ujasiri, akalazimisha tabasamu na kuyahamisha macho yake kutoka kwa wakwe zake hadi kwa watoto wake wawili, Nduwimana, mtoto wa kiume aliyekuwa na umri wa miaka 10, na Samantha, mtoto wa kike aliyekuwa na umri wa miaka 7.
Nduwimana na Samantha walikuwa wameketi kwenye meza kubwa ya chakula, nao walikuwa wakimtazmana baba yao kwa wasiwasi.
Ibrahim akaangalia saa yake ya mkononi na kuwatupia tena jicho wazazi, akalazimisha tabasamu huku akijaribu kujiamini zaidi. Aliwasalimia wazazi wake na wazazi wa mke wake kwa unyenyekevu. Na wote bila hiyana waliitikia salamu yake huku wakiendelea kumtazama kwa makini.
Ibrahim akapiga hatua kuwasogelea watoto wake Nduwimana na Samantha huku akiwaangalia kwa upole.
“Nyinyi, mbona hamjalala mpaka saa hizi saa tano na ushee? Kalaleni tafadhali,” Ibrahim alisema huku akiwashika kichwani kwa upole. Kisha aligeuka kuwatazama tena wazazi wake haraka haraka na kuanza kuziendea ngazi za kuelekea juu ya ile nyumba, lakini kabla hajaanza kupanda zile ngazi Mzee Bigirimana akawahi kumsemesha.
“Bwana mdogo, ukipumzika kidogo nina mazungumzo na wewe,” Mzee Bigirimana alisema huku akijiweka sawa pale kwenye sofa alipokuwa ameketi.
“Mazungumzo usiku huu!” Ibrahim alimuuliza baba yake kwa mshangao huku akiitazama saa yake ya mkononi.
“Ndiyo, usiku huu maana raha ya mchuzi uunywe ukiwa bado wa moto.”
Ibrahim alitaka kusema neno lakini akasita, alimtazama baba yake huku akionesha uso wa mashaka, akaitazama tena saa yake ya mkononi na kushusha pumzi.
“Sawa, baba!” hatimaye alisema huku akabetua kichwa chake kukubali, kwani hakuwa na namna nyingine yoyote ya kufanya isipokuwa kukubali.
Alishusha pumzi za ndani kwa ndani huku akiuma mdomo wake wa chini na kuanza kupiga hatua kuelekea ghorofani. Akaanza kuzipanda zile ngazi haraka haraka hadi ghorofani na kutokea kwenye korido pana iliyokuwa inatazamana na milango miwili.
Pia kulikuwa na milango mingine miwili katika korido nyingine fupi iliyokuwa kushoto na upande wa kulia uliokuwa mwisho kabisa wa ile korido.
Ibrahim hakusimama bali alikwenda moja kwa moja hadi kwenye mlango wa mwisho kabisa wa ile korido fupi, akafika na kushika kitasa cha mlango, akakinyonga na kuusukuma ule mlango. Mlango ukafunguka na kumruhusu kuingia mle chumbani.
Ibrahim akajitoma chumbani na kusimama katikati ya kile chumba huku akimtazama mke wake, Pamela Tugiramahoro, ambaye alikuwa kasimama kwenye mlango wa kuelekea kwenye kibaraza kidogo cha ghorofani (balcony) huku akiangalia juu kwa unyonge, sura yake alikuwa kaikunja na kutengeneza matuta madogo usoni. Ibrahim alimtazama kwa kitambo kifupi na kuachia tabasamu la kebehi.
Pamela alikuwa mwanamke mwenye umri wa miaka therathini na nane. Alikuwa msomi aliyehitimu Shahada ya Sanaa katika Sosholojia (B.A. in Sociology) kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Alikuwa amepata nafasi ya kusoma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa ufadhili maalumu wa Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), wakati huo yeye na familia yake walikuwa wakiishi nchini Tanzania na kufuatia machafuko yaliyokuwa yakiendelea nchini Burundi.
Pamela alikuwa Mrundi halisi, kwa baba na mama yake, akiwa mtoto wa kwanza kati ya watoto saba, watatu walikuwa wa kike na wanne walikuwa wa kiume. Paamela alikuwa na umbo kubwa lililokuwa linavutia sana, likiwa limesheheni vema na kunesanesa, likifanya kila jicho lililokuwa linamuona kumtazama mara mbili mbili pasipo kukinai.
Alikuwa mrefu wa wastani na mweupe kwa rangi ya ngozi yake, lakini haaukuwa ule weupe wa kujichubua bali weupe wa asili. Rangi yake ilikuwa na mng’aro wa aina yake na ilipendeza sana, ikiwa na mvuto wa pekee kiasi cha kumfanya kuonekana alikuwa bado msichana mdogo tofauti na umri wake. Pia hakuwa akihitaji kabisa vikorombwezo vya aina yoyote kuinakshi ngozi yake.
Ukiangalia macho yake, hmm… yalikuwa ni yale macho yanayoita kwa mng’aro sadifu, yakiambatana na kope nyingi nyeusi ambazo ziliachia nafasi kwa nyusi ili zipate kujidai.
Midomo yake ilikuwa minene yenye kingo nyepesi na mikunjo midogo midogo. Sauti yake ilikuwa ya upole kila alipoongea, na kikubwa zaidi kilichokuwa kinakamilisha uzuri na mvuto wake ilikuwa upole wake. Kwa kweli Pamela hakuwa mwanamke wa kumtizama mara moja tu ukamwacha.
Urafiki wa Pamela na Ibrahim ulianzia ufukweni mwa Bahari ya Hindi, jijini Dar es Salaam, katika ufukwe wa Cine Club, maarufu kama Mikocheni kwa Warioba, ambako Pamela akiwa na rafiki zake aliokuwa anasoma nao Chuo Kikuu cha Dar es Salaam walikuwa wakichezea mchanga uliokuwa kandokando ya bahari, walikuwa mara warushiane mchanga mara waangushane kwenye maji.
Mchezo ulipowanogea Pamela akachota mchanga ili kumwagia mwanachuo mwenzake, bahati mbaya kusudio lake likashindikana baada ya mchanga ule kukwepwa na mlengwa, kisha akammwagia mwanamume mmoja aliyekuwa amekaa jirani kabisa na eneo lile.
Kuona vile Pamela akaduwaa na kujiziba mdomo wake kwa hofu kubwa. Bila kufikiria mara mbili mbili yule mwanamume aliinuka na kumkabili Pamela ambaye bado alikuwa ameduwaa, akamfikia na kuanza kumporomoshea matusi ya nguoni pasipo hata kumpa nafasi ya kujitetea. Kama hiyo haitoshi alimkwida akitaka kumpiga.
Pamela aliingiwa woga mkubwa na kutetemeka asijue la kufanya huku wale rafiki zake wakijikunyata kwa woga wasijue la kufanya. Kijana mmoja mtanashati aliyekuwa akipita eneo lile akajongea mahali hapo haraka na kumshika yule mwanamume kwa nguvu, akamvuta kumuachanisha na Pamela na kumsukuma kando huku akimkazia macho.
“Kaka, siyo vizuri kugombana na watoto wa kike…”
“We umeona jinsi alivyonifanyia lakini, au unasema tu?” yule mwanamume alisema huku akiwa amekasirika.
“Wewe ni mwanamume na hawa ni watoto wa kike, utajitia matatani bure, mpotezee!” yule kijana mtananshati alimweleza na kumgeukia Pamela.
“Dada’angu, waambie wenzako kama ni michezo mkafanyie mbali, si unaona hapa kuna watu wamekaa!” yule kijana alisema kwa upole akimwambia Pamela.

ITAENDELEA...
 
HADI LINI! 14

Na Bishop Hiluka


Wakati huo yule mwanamume ambaye alishapandwa na hasira alipiga kite cha hasira na kushika kiuno huku akimtazama Pamela kwa makini. “Bahati yako!” alisema kwa hasira na kuondoka kabisa eneo lile huku akijifuta mchanga.
Pamela na rafiki zake walimshukuru yule kijana mtanashati na kuondoka eneo lile kisha wakasogea mbele kidogo, lakini si kwa ajili ya kuendelea kucheza bali walianza kuvaa nguo zao. Walishaona kuwa tayari ufukwe ule ulikuwa umeingia nuksi!
Walivaa nguo zao na kuanza kuondoka kutoka eneo lile, na wakati wakielekea barabarani Pamela akamwona tena yule kijana mtanashati aliyekuwa amemuokoa asipate kichapo akitembea taratibu mbele yao akielekea upande ule ule waliokuwa wanaelekea.
“Asante sana kaka, maana bila wewe sijui ingekuwaje leo kwa yule jamaa!” Pamela alimwambia yule kijana baada ya kumfikia.
“Usijali, dada’angu, hapa mjini kila mtu ana stress zake,” yule kijana mtanashati alijibu huku akiachia tabasamu.
Pamela alijikuta akivutiwa sana na ustaarabu wa yule kijana, hivyo alipunguza mwendo. Yakafuata mazungumzo kidogo ya kufahamiana, ndipo yule kijana mtanashati alipojitambulisha kwa Pamela kuwa aliitwa Ibrahim Bigirimana na alikuwa anafanya kazi Benki Kuu ya Tanzania.
Waliongea kwa kitambo kifupi na wakati walipokuwa wanaagana kwa kushikana mikono, Ibrahim alimpa Pamela kitu fulani mkononi. Pamela alikipokea kile kitu na kuufunga mkono wake vyema, kisha akawakimbilia rafiki zake waliokuwa wametangulia mbele bila kukitazama.
Walipofika kwenye kituo cha daladala cha Kwa Warioba Pamela aliufungua mkono wake kuangalia na kuiona ‘business card’ iliyokuwa na jina, cheo, anwani, mawasiliano na eneo la ofisi alizokuwa anapatikana Ibrahim.
Siku chache baadaye Ibrahim alipokea ujumbe mfupi kutoka kwa Pamela wa kumjulia hali, na yeye akaamua kupiga simu, na hapo ndipo urafiki ukazaliwa, baadaye ukawa mwanzo wa ukaribu wao uliofuatiwa na uchumba.
Baada ya Pamela kumaliza chuo, taratibu zingine zilifuatwa na hatimaye yeye na Ibrahim walioana kwa ndoa iliyofungwa kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, kisha sherehe kubwa ya harusi ikafanyika nyumbani kwao Ibrahim, kwenye ukumbi wa hoteli ya kitalii iliyopo kwenye mandhali ya kuvutia ya ufukwe wa Ziwa Tanganyika mjini Kigoma, Kigoma Hilltop Hotel.
Ndoa hiyo ilikuwa imeridhiwa na kupata baraka kutoka pande zote mbili bila kinyongo chochote. Baada ya pale Ibrahim na Pamela wakaanza maisha mapya ya ndoa. Baada ya mwaka mmoja wa ndoa yao wakapata mtoto wa kiume, ambaye Pamela aliamua kumpa jina la Nduwimana, lilikouwa na maana ya “Nipo kwenye mikono salama ya Mungu” kwa lugha ya Kirundi.
Kupatikana kwa mtoto Nduwimana kulizidisha furaha ya ndoa. Lakini ni katika kipindi hicho hicho Pamela akakumbwa na msukosuko baada ya yeye na jamaa zake kutakiwa kurudi kwao, Burundi, katika kile kilichoitwa operesheni ya kuwarudisha wahamiaji haramu. Pamela aliporudi Burundi aliamua kutafuta kazi na hakuchukua muda akapata kazi katika taasisi ya kimataifa ya World Vision International Burundi.
Kwa kuwa Ibrahim alimpenda sana Pamela, aliamua kufanya utaratibu wa kuacha kazi Benki Kuu ya Tanzania na kumfuata Pamela nchini kwao Burundi, kwani muda mrefu alikuwa akivutiwa kuishi jijini Bujumbura.
Kwa kuwa alikuwa na elimu nzuri na uzoefu wa miaka kadhaa alioupata kutoka Benki Kikuu ya Tanzania, ikawa rahisi sana kwake kupata kazi, hakuchelewa, akapata kazi katika Benki ya Biashara ya Burundi (Commercial Bank of Burundi).
Miaka miwili baadaye wakapata mtoto wa pili wa kike, wakampa jina la Samantha ambalo ni jina maarufu sana la mtoto wa kike miongoni mwa wazazi nchini Burundi, na mara nyingi waliwachukulia watoto wa kike wenye jina hilo kama wasichana wa daraja la juu, waliozaliwa katika neema.
Ni wakati huo Ibrahim alimtaka Pamela kuacha kazi ili apate nafasi ya kulea watoto wake, kwa kuwa hakupenda watoto wake walelewe na msichana wa kazi. Ibrahim aliahidi kumpenda zaidi Pamela na kumtunza yeye na wazazi wake, kama ambavyo alivyokuwa akiwatunza wazazi wake.
Aliahidi pia kumvumilia mkewe mpaka mwisho wa maisha yao, maneno ambayo yalimpa faraja kubwa Pamela na hakuwahi kufikiria kabisa kuwa mambo yangekuja kugeuka!
Furaha katika familia ile ilizidi baada ya mwaka mmoja, maana Ibrahim aliacha kazi Commercial Bank of Burundi na kuchukuliwa na CRDB Bank Burundi, baada ya benki hiyo kuanzishwa nchini Burundi, na yeye akawa Meneja Mkuu wa benki hiyo, nafasi iliyomfanya kuwa mmoja wa watu wenye mafanikio makubwa jijini humo na kuzidi kumuongezea marafiki kutoka kila kona.
Miaka ikaanza kusonga, na taratibu Ibrahim akaanza kubadilika, upendo wake kwa Pamela ukaanza kupooza kwa sababu sasa alianza kupata mialiko mbalimbali iliyomkutanisha na warembo wengi waliokuwa wanamlilia. Pia kutokana na kipato chake kuwa kikubwa alijikuta akianza kuingia kwenye maisha ya anasa na starehe za kila aina.
Akaanza kuchelewa kurudi nyumbani, wakati mwingine hadi usiku wa manane, na siku moja ilionekana kama alichelewa sana kurudi basi Pamela alilala pale sebuleni kumsubiri kwa saa nyingi lakini hakurejea kabisa. Hata Ibrahim aliporejea siku iliyofuata Pamela alipomkabili kumuuliza alilala wapi, alionekana kubezwa na hakuweza kujibiwa.
Pamela akajitahidi sana kuvumilia akiamini kuwa huo ulikuwa ni upepo mbaya tu uliokuwa ukipita na muda si mrefu maisha yangeendelea. Kutahamaki miaka miwili ikawa imepita na mienendo mibovu ya Ibrahim ikaendelea kuchukua hatamu, ikafikia kipindi Pamela akaanza kujiuliza: ina maana Ibrahim alikuwa hatambui tena umuhimu wake!
Ni kweli Ibrahim alikuwa ameanza tabia za kuchelewa kurudi nyumbani lakini siku zilivyozidi kwenda hali ilizidi kuwa mbaya zaidi. Usiku Pamela hakupata usingizi, muda wote alikuwa anawaza kuhusu hatma ya ndoa yake na Ibrahim. Akawa analia usiku kucha, donge la hasira lilimkaba kooni na hakuweza kulihimili mpaka atoe kilio. Akajiuliza, hali ile ingeendelea hadi lini?
Alitamani kuikimbia nyumba yake lakini hakuweza kuondoka na kurudi kwao bila kupewa talaka, kwa sababu baba yake mzazi alikuwa mkali mno na kama angeenda kwao basi angeishia kufukuzwa nyumbani kama mbwa koko. Pamela akatamani kuiomba talaka yake lakini kibaya zaidi Ibrahim hakuwa amewahi kumtamkia kuhusu talaka hata siku moja. Jambo hilo kwake likawa tatizo kubwa, hivyo akawa anavumilia tu huku akiishi utumwani katika nyumba yake.

ITAENDELEA...
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom