( Makala hii imechapwa na RAI juma hili)
Ben Mkapa Na Awamu Yake (1)
Na maggid mjengwa
ZAIDI ya mwaka mmoja umepita tangu Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Mh. Benjamin William Mkapa aondoke madarakani. Kuna mengi yanasemwa juu yake. Hii ichukuliwe kama tathmini ya utendaji wake alipokuwa madarakani.
Bado nina kiu ya kuona mijadala ya kina yenye kutathmini utendaji wa Serikali ya Awamu ya Tatu. Bahati mbaya, baadhi yetu wameishia kwenye kujadili mkopo aliokopa Rais Mstaafu na kufungua kampuni yake. Binafsi ningependa kuona tunainua kiwango cha mijadala, tuzame zaidi ya hapo, kwani, fedha anazodaiwa Mkapa kukopa amezikopa, hakwenda kuiba benki.
Tuna mfano wa Rais Mobutu wa Zaire ya zamani aliyekuwa akmwita gavana wake wa Benki Kuu na kumwamuru aende kuchota fedha benki. Hoja ya msingi hapa ingekuwa ni kwanini tunawaandalia marais wetu mazingira yenye kuwafanya walazimike kukopa na kufanya shughuli binafsi wakiwa madarakani. Kama tunaona mapungufu ya kimaadili kwa Rais aliye madarakani kukopa na kufanya biashara, basi, jambo hili lisiishie kwenye kudhani, kuwa kila rahisi atazingatia maadili ya uongozi hata yale yasiyoandikwa popote. Tukikubaliana kuwa ni mapungufu, basi, hayo na mengineyo yawekwe wazi katika Katiba yetu.
Lakini, katika maisha, binadamu tunapenda sana tuache kumbukumbu nyuma yetu ( Legacy). Kwamba hata siku tukiondoka hapa duniani, tuwe na mambo ambayo jamii inayotuzunguka tungependa wayakumbuke na kutuhusianisha nayo. Na hapa ndipo ilipolala hoja yangu ya msingi. Kwamba ni kwa yepi tunataka tuukumbuke utawala wa Awamu ya Tatu wa Rais Mkapa? Na, je Mkapa mwenyewe alipenda akumbukwe vipi?.
Naam! Historia n mwalimu mzuri, na ili tuyaelewe yanayotokea sasa na kesho hatuna budi kuitazama historia. Itakumbukwa, kuwa safari ya Mkapa kwenda Ikulu ilianzia Mei 8, 1995, mara ile alipotangaza rasmi azma yake ya kuwania kuteuliwa kugombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi.
Mkapa aliyekuwa Waziri wa Sayansi na Elimu ya Juu hakufahamika vema kwa Watanzania wengi. Hakupewa nafasi kubwa hata na vyombo vya habari; Mkapa naye achukua fomu, ilikuwa ni moja ya vichwa vya habari katika moja ya magazeti yetu. Neno naye limetumika kuonyesha mtu huyo Mkapa hakuwemo katika waliofikiriwa kuchukua fomu.
Miaka kumi na moja iliyopita, umaarufu wa mwanasiasa Ben Mkapa ambao haukuzidi ule wa mwanasoka Kenny Mkapa wa Yanga, ukaja kuvuka mipaka ya Tanzania na bara hili la Afrika. Kutoka Afrika Kusini hadi Asia na Marekani ya Kusini. Kama ni darasani, Mkapa aliwakuta wenzake akina Museveni, Kagame, Thabo Mbeki , Obasanjo na wengine wakiwa wanashika nafasi za mbele. Katika ukanda wa Maziwa Makuu, Museveni ndiye aliyekuwa Kiranja Mkuu. Haikuchua muda kabla ya Mkapa kuonyesha kuwa alikuwa Hodari Darasani. Kimsingi, Mkapa akaja kuchukua nafasi ya Ukiranja kutoka kwa Museveni.
Mkapa yule Benjamin akaonekana kwenye majukwaa mengi ya kimataifa, aliitangaza Tanzania na aliifanyika kazi Afrika. Pamoja na mapungufu yake ya kibinadamu, katika kipindi chake cha miaka kumi ya utumishi wa umma, Mkapa ametoa mchango mkubwa kwa watu wa nchi hii, bara hili na dunia kwa ujumla.
Maishani, binadamu hutenda mazuri na mabaya, lakini lengo hasa ni kutenda yaliyo mema na ya kimaadili. Mara nyingi anayemaliza kwa mazuri hufuta mabaya yake mengi aliyoyafanya nyuma. Na swali Je, Mkapa angependa akumbukwe kwa lipi alipata kuulizwa Mkapa mwenyewe na mwandishi David Martin miaka kumi na mbili iliyopita. Ilikuwa ni muda mfupi kabla ya kuingia madarakani. Mwandishi alimwuliza; Mwisho, ukiangalia mbele miaka mitano au labda kumi, ungependa historia ikukumbuke kwa namna gani?
Mkapa anajibu; Ningependa nikumbukwe kama mtu niliyeongoza Utawala ambao kwa vitendo umepiga vita rushwa na umeimarisha aina ya uongozi, utumishi wa umma, thamani na wajibu uliokuza utawala bora. Kwamba katika utawala wangu nimeongoza juhudi za kuimarisha nidhamu katika mchakato wa utawala, nidhamu kwa maana ya sheria, kanuni na taratibu, lakini ndani yake zikiwa na misingi ya uhuru. Hivyo basi, kukuza misingi ya huru na maendeleo ya haraka, lakini katika mtazamo wa sheria na taratibu, hivyo basi nidhamu.
Kwamba nimehamasisha ajenda ya vyama vyingi, mfumo wa vyama vingi, bila kuharibu. Lakini zaidi kwa dhamira ya wazi ya kujenga utaifa katika Jamhuri hii ya Muungano wa Tanzania. Nitatumaini kuwa itasemwa kuwa, nimejaribu kwa bidii zangu zote kufikia matoeo hayo bila kujidai ambako mara nyingi kiujumla uhusishwa na ofisi kuu ya nchi, lakini zaidi, kinyume chake, kuyafanya hayo kwa heshima na unyenyekevu mkubwa.
Hapa ni kwa Mkapa mwenyewe na jamii kwa jumla kufanya tathimini ya kile alichokieleza na alichokitenda. Kabla ya kumhukumu kwa matendo yake, kumtendea haki Mkapa ni kujaribu kumwelewa alichokisema na alichokitenda na katika mazingira aliyoyakuta na kuanza kuyafanyia kazi aliyosema. Na wenye kupitisha hukumu tusome hukumu zao kwa kuyaangalia mazingira ambayo chama cha mapinduzi kiko nayo sasa.
Ni vema pia tukafikiri kwa bidii. Tucambue kwa kina na kujiuliza. Mkapa alisema alikuwa na nia ya kuimarisha ajenda ya vyama vingi vya kisiasa. Je, ni nani wa kumlaumu leo kama ajenda hiyo inaelekea kukosa mwelekeo na pengine kuwa kinyume chake? Na, je, shutuma anazobebeshwa Mkapa sasa zinalenga kwenye kulinda maslahi ya nchi au ya kikundi cha wachache?
Muhimu katika jamii yeyote ile ni kwa wanajamii kuaminiana. Kuwepo kwa moyo wa utaifa na uzalendo miongoni mwa wanajamii. Si jambo jema kuanza kuingiwa na hofu juu ya dhamira halisi za baadhi yetu. Ni muhimu kwa waongozwa kuwaamini viongozi wao, na viongozi kuwaamini wanaowaongoza. Imani huchangia katika kujenga misingi ya amani na utulivu katika jamii. Kwani, msingi mkuu wa amani ni imani.
Unayemwamini utakuwa na amani naye. Kutoaminiana kidhamira, kutiliana mashaka ni chachu za kukosekana kwa amani katika jamii yeyote. Hata katika siasa za upinzani watu huaminiana. Ndivyo wanavyofanya wenzetu walioendelea katika demokrasia. Kutofautiana kifikra, kiitikadi, kimitazamo hakuna maana ya uadui. Kwenye kulinda maslahi ya taifa kuna wenzetu katika chama na wenzetu katika upinzani. Katika siasa hata upinzani una umuhimu mkubwa katika kujenga taifa. Hakuna Hawa wenzetu na Wale si wenzetu. Hilo la mwisho linatoa tafsiri ya ubaguzi. Itaendelea juma lijalo. Kwa makala zaidi, maoni na picha, tembelea;
http://mjengwa.blogspot.com