Zawadi nono mnayoweza kutupa ni Katiba mpya
Maggid Mjengwa
Oktoba 6, 2010
KWENYE moja ya matangazo ya uchaguzi kwenye luninga anaonekana bwana anayewauliza wapiga kura kama watakwenda kupiga kura. Kila mmoja anatoa sababu za kutokwenda kupiga kura. Kisha bwana yule anahitimisha kwa kusema: Na matokeo yakitangazwa msilalamike kuwa kura zimebwa! Nadhani tangazo lile lina walakini; maana kilichopaswa kutafutiwa jibu ni swali la kwa nini watu hawataki kwenda kupiga kura. Stalin wa Urusi aliwahi kutamka: "Anayepiga kura hana anachoamua, anayehesabu kura ndiye anayeamua kila kitu".
Na hapa lipo tatizo la msingi. Watu kukosa imani na wenye kusimamia uhesabuji wa kura zenyewe. Kuna wanaojisikia kuwa kura zao hazina umuhimu; kwani, mwisho wa yote, kura zitaibwa.
Katika nchi zetu hizi, kukosa imani na wenye kusimamia mchakato wa uchaguzi hadi kuhesabu kura ndio chanzo cha vurugu na uvunjifu wa amani. Tumeona hayo kwa jirani zetu kule Kenya.
Wakenya walishiriki mchakato wa kujiandikisha na hata kupiga kura bila matatizo makubwa. Kazi ikaja kwenye kuhesabu kura. Ndipo hapo hesabu zikaanza kuwa ngumu. Kukawa na kufuta hapa na pale. Kukawa na kushinikizana na kadhalika. Hatimaye damu ikamwagika.
Kila mwenye kufikiri alielewa kuwa kiini cha vurugu za Kenya ni Tume ya Uchaguzi ambayo haikuwa huru. Wakenya wale leo wana Katiba mpya. Katiba ya watu wa Kenya.
Hivyo basi, dawa ya kuepuka au kupunguza shari kama iliyotokea Kenya ni kwa nchi zetu hizi kuangalia upya Katiba zetu hizi na hususan inapohusu uchaguzi na Tume ya Uchaguzi.
Nasi kama taifa, tuanze sasa kuangalia uwezekano wa kuanzisha mchakato wa kuandika Katiba mpya. Zawadi kubwa kwetu Watanzania tukaposherehekea miaka hamsini ya uhuru wetu iwe ni kwa viongozi wetu kutuanzishia mchakato huo. Na huo ndio utakuwa urithi muhimu na wa maana kubwa tutakaoviachia vizazi vijavyo.
Kwamba siasa ni jambo jema na la kuvutia tunalishuhudia katika nchi za wenzetu zenye kuzingatia utawala wa sheria na zenye katiba zenye kulinda maslahi ya nchi zao.
Kwa mfano, tunaona jinsi mchakato wa kutafuta wagombea urais nchini Marekani unavyofanyika. Ndani ya chama kimoja watu wanashindana kwa hoja.
Kule Marekani tuliona Hillary Clinton na Barrack Obama wa chama cha Democrat wakichuana kwa karibu kutafuta nafasi ya kuchaguliwa kugombea urais kupitia chama chao.
Hillary na Obama hawakuwa na chuki binafsi kati yao. Walishindana kwa hoja. Ikifika siku mmoja wao akachaguliwa na mwingine akashindwa. Ustaarabu kwao ikawa ni kupongezana kwa kushikana mikono na baadae kushirikiana katika kufanikisha ushindi wa chama chao.
Na hata Obama aliposhinda Urais, akamfanya Hillary Clinton kuwa Waziri wake wa Mambo ya Nje.
Kama ni mitandao, wenzetu yao huisha siku ile mshindi anapotangazwa. Hakuna kutafutana na kufanyiana hila baada ya hapo. Hiyo ndio maana halisi ya ushindani. Hiyo ndio siasa, si mchezo mchafu.
Ikumbukwe kuwa kila matokeo ya uchaguzi yana tafsiri zake. Kama ni uchaguzi huru na wa haki kuna mawili; kushinda au kushindwa. Katika hilo la mwisho, kiongozi au chama kinashindwa uchaguzi, kuna kusikitika, lakini wakati huo huo kuwepo na furaha kuona demokrasia inafanya kazi yake.
Mgombea au chama kikubali kuwa wapiga kura wamewakataa, hamkuwafanyia mengi waliotarajia, au hawaamini kuwa mtawatekelezea wanayotarajia, hivyo basi, wamewachagua wengine. Mkubali kuchukua nafasi ya wapinzani, mwangalie kasoro zenu, mjipange upya. Siasa haiishii kwenye uchaguzi, kila siku ni siasa, kuna uchaguzi mwingine unakuja.
Katika nchi zetu hizi tunaona ni jinsi gani hilo la kukubali kushindwa linakuwa gumu kwa baadhi ya wanasiasa. Ukweli tu kuwa katika nchi zetu hizi Tume Huru za Uchaguzi hukataliwa na walio madarakani unathibitisha dalili za kutokuwa na utayari wa kuendesha ushindani wa kisiasa katika mazingira ya tambarare kwa pande zote zinazoshindana.
Lakini, ushindani wa kisiasa mara nyingi unahusu vyama. Tatizo kuna wanaoingia katika ushindani wa kisiasa kupitia vyama na bila kujua dhana ya chama ina maana gani.
Na tuanze kwa kujiuliza: Je, chama cha siasa ni nini? Katika harakati za kisiasa kuna aina mbili za vyama; Chama cha Ukombozi na Chama cha Uongozi. TANU, FRELIMO, ANC ni mifano ya vyama vya ukombozi vilivyokuja kugeuka kuwa vyama vya uongozi. CCM, CUF, CHADEMA ni mifano michache ya vyama vya uongozi.
Chama imara cha ukombozi kinatakiwa kijenge uwezo wa kuwa chama cha uongozi mara ile kitapotwaa madaraka. Hufanya hivyo kwa kuweka mkazo juu ya mafunzo kwa makada wake. TANU, FRELIMO na ANC viliweza kujenga uwezo huo.
Kielelezo cha nguvu na umakini wa chama cha kisiasa ni uwingi na ubora wa makada wake. Chama ni makada kwa vile chama ni itikadi, malengo na shabaha na wala si nasaba na umaarufu wa mtu mmoja mmoja ndani ya chama.
Chama chenye makada wengi wenye kuielewa itikadi, malengo na shabaha ya chama, huwa hakimtegemei mtu mmoja katika kuwepo kwake. Hakimtegemei mtu mmoja katika kufanikisha ushindi wa chama. Hakimtegemei mtu mmoja katika kuhamasisha wanachama au umma.
Chama hicho hujiamini. Edward Mondlane, kiongozi wa kwanza wa Frelimo alipouawa kwa bomu la barua, Frelimo walijua watafanya nini, walijua mchakato gani utumike katika kumpata mrithi wake. Na hata Samora Machel, alipotoweka ghafla kwa ajali ya ndege, FRELIMO walijua watafanya nini.
Na kama Nyerere angekufa wakati wa TANU, bila shaka, TANU walikuwa wamejiandaa vema na cha kufanya. TANU haikuwa na ukame wa jeshi la makada. Nguvu ya Frelimo kama ilivyokuwa kwa TANU zilikuwa ni makada wake.
Na ieleweke, kuwa makada ni roho ya chama. Chama kikianza kupungukiwa na idadi ya makada wake wakereketwa, basi, chama hicho hakina mustakabali ulio salama, kitayumba na pengine kuangukia kaburini.
Tuangalie basi mfano wa chama kisichokuwa na nguvu ya makada. Wakati John Garang wa SPLM alipokufa kwa ajali ya ndege, hakuna ndani ya SPLM aliyekuwa na hakika ya nini kifanyike.
Kwamba ni mke na mtoto wa John Garang waliosimama mbele ya kamera za waandishi wa kimataifa kujaribu kuelekeza nini John Garang angependa kifanyike kilidhihirisha udhaifu wa SPLM. Kwamba SPLM ni John Garang na kinyume chake. SPLM ilikuwa ni chama mtu.