Na Mwinyi Sadallah
Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, Profesa Issa Shivji
Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, Profesa Issa Shivji, amesema suala la mafuta na gesi asilia liliingizwa katika orodha ya mambo ya Muungano na Rais wa Kwanza wa Zanzibar marehemu Abeid Amani Karume Mwaka 1968.
Alisema hayo katika maadhimisho ya mkutano wa siku ya Demokrasia Duniani uliotayarishwa na Baraza la wawakilishi Zanzibar (BLW) na kuhudhuriwa na wananfunzi wa vyuo vikuu na asasi za kiraia Zanzibar jana.
Profesa Shivji alisema suala la mafuta na gesi ya asilia lilingizwa katika orodha ya Muungano kwa kufuatwa taratibu zote za kisheria baada ya kupitishwa na wabunge kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
Hata hivyo, alisema kwamba baada ya wabunge kupitisha sheria hiyo rais wa Jamhuri ya Muungano wakati huo, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere hakuwepo nchini na kaimu rais alikuwa ni Rais wa Zanzibar.
Alisema kwa msingi huo sheria hiyo ilisainiwa na Rais Karume baada ya sheria kupitishwa na Bunge la Muungano akiwa kaimu rais wa Muungano mwaka 1968 na ndipo suala hilo la mafuta na gesi asilia likaingizwa rasmi katika orodha ya mambo ya Muungano.
Hata hivyo, alisema kwamba wakati huu si wa kushindana kwa mambo yasiyokuwa na manufaa jambo la msingi mjadala wa katiba mpya ufanyike kwa uwazi na wananchi washirikishwe.
Alisema kwamba ni kweli mambo ya Muungano yalikuwa 11 lakini sasa yameongezeka na kufikia 23 lakini alisema kwamba mambo hayo yalikuwa yakiongezwa kwa kufuata taratibu za kisheria na makubaliano ya pande mbili za viongozi Zanzibar na Muungano.
Hata hivyo, alisema kwamba suala la mafuta linahitaji hekima na busara katika kulitafutia ufumbuzi wake na kutoa mfano yapo mataifa yaliingia kwenye matatizo chimbuko likiwa mafuta kama vile Angola, Nigeria na Ghana.
Alisema kwamba mambo mengine ambayo yaliingizwa kwa makubaliano ya pande zote mbili ambayo hayakuwemo katika orodha ya mambo ya Muungano ni pamoja na suala la sarafu na benki, mambo ambayo yaliingizwa mwaka 1965.
Aidha aliwataka wanafunzi wa vyuo vikuu kufanya utafiti kuhusu mambo ya Muungano kabla ya kuzungumza kwa sababu hatuahiyo itasaidia wananchi wengi kupokea taarifa zilizo sahihi na kufahamu mambo ya msingi ya Muungano.
Kuhusu uhalali wa Muungano alisema kumbukumbu zinaonyesha muungano huo umekuja kwa makubaliano ya pande zote mbili zamuungano akiwemo Rais wa kwanza wa Zanzibar marehemu Abeid Amani Karume na Rais wa kwanza wa Tanganyika Hayati Mwalimu Nyerere.
Alisema kwamba baada ya kufikiwa muungano huo, nyaraka zilipelekwa Umoja wa Mataifa na picha za viongozi hao zipo wakisaini nyaraka za Muungano na kuchanganya udongo wa Zanzibar na Tanganyika kabla ya kutangazwa kuwa taifa moja la Tanzania.
Hata hivyo, alisema kwamba wananchi watumie mjadala mpya wa katiba kushauri Serikali mambo ambayo yanaonekana kuwa ni kerokatika muungano ili yaweze kupatiwa ufumbuzi.
Akiwasilisha mada kuhusu demokrasia Profesa Shivji alisema kiongozi bora ni yule ambaye hataki kuwa kiongozi asiyekua na tama ya uongozi .Hata hivyo, alisema bahati mbaya hivi sasa nafasi za uongozi watu wanazitafuta kwa malengo ya kuchuma badala ya kutumikia wananchi na taifa.
Profesa Shivji alisema hivi sasa wafanyabiashara wengi wanazitafuta nafasi za kwenda bungeni kwa malengo ya kulinda maslahi yao binafsi na kutafuta njia ya kufanikisha miradi yao jambo ambalo alisema halina maslahi kwa wananchi na Taifa.
Aidha, alisema kwamba pamoja na Zanzibar kufikia kuwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), bado kambi ya upinzani ina umuhimu mkubwa katika mabaraza ya kutunga sheria kwa vile ndio chombo chenye uwezo wa kuikosoa Serikali na kutetea kero za wananchi kwa nguvu moja.
Profesa Shivji alisema kwamba wakati umefika vijana kuwa na ajenda wanapokabiliana na tatizo la umasikini kuvunja ukimya na badala yake kuunganisha hoja na kujadili matatizo yanayowakabili kwa uwazi. "Huwezi kupata uhuru wa kujadili bila ya kupigania uhuru huo," alisema Profesa Shivji.
Alisema wakati Tanzania inaadhimisha miaka 50 ya uhuru vijana wengi wapo mitaani wakiwa hawana ajira, wamekuwa machinga na wapiga debe, mambo ambayo alisema yanahitaji kujadiliwa na vijana wenyewe katika kujitafutia maendeleo yao.
Alisema kwamba miaka 50 ya uhuru elimu ya chuo kikuu inatakiwa iwe ya lazima kwa vijana ili kuweza kukabiliana na matatizo ya umasikini na hatua hiyo ingesaidia vyema kuondokana nao.
Awali wanafunzi hao walishangazwa na orodha ya mambo ya Muungano kuongezeka kutoka 11 hadi 23 na kuhoji kwa nini suala la muafaka na gesi asilia halijaondolewa katika orodha ya Muungano licha ya SMZ kuondoa suala hilo mwaka 2009.
Akiwasilisha mada kuhusu Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar na demokrasia kwenye Baraza la wawakilishi, Katibu wa Baraza hilo, Ibrahim Mzee Ibrahim, alisema kuwa muundo huo umewapa uhuru wajumbe katika kukosoa Serikali na kuweka kando misimammo ya vyama vyao.
Alisema kwamba tangu kuanza baraza lenye mawaziri kutoka CCM na CUF wajumbe wamekuwa wakijadili hoja zaidi kinyume na miaka ya nyuma ambapo walionekana kushikamana zaidi ya vyama badala ya kuweka mbele maslahi yao.
"Vyama vya siasa vilidhibiti uhuru wa wajumbe kwa utaratibu wa nidhamu ya vyama, muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa umepunguza makali ya udhibiti huo," alisema Katibu huyo.
Alisema wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamepewa uhuru kupitia kifungu cha 86 na sheria namba nne ya mwaka 2007. lakini wanatakiwa kuzingatia maoni binafsi ya mjumbe, maslahi ya jimbo lake na maslahi ya taifa wanapotekeleza majukumu yao.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI