Mitazamo Hasi juu ya Elimu chanzo cha Utoro Shuleni

Mitazamo Hasi juu ya Elimu chanzo cha Utoro Shuleni

UTPC

Journalists' Union
Joined
Apr 17, 2026
Posts
30
Reaction score
25
Kutokana na kukithiri kwa tatizo la wazazi kutelekeza watoto wao na kwenda kwenye makambi ya kilimo wilayani Kasulu Mkoa wa Kigoma, uchunguzi umeonyesha kuwepo kwa mtazamo hasi kwa elimu.

Awali ilibainika kuwa zaidi ya watoto 2,000 huacha masomo kila mwaka katika wilaya ya Kasulu, mkoani Kigoma, kutokana na sababu zinazochochewa na shughuli za kilimo, ikiwemo wazazi kuweka makambi mashambani na kuwaacha watoto bila uangalizi.

Mitazamo hiyo ya jamii inakwenda kinyume na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025–2050, inayolenga kujenga mfumo bora wa elimu unaozalisha wahitimu wenye maarifa na stadi zitakazowawezesha kujiajiri au kuajiriwa katika sekta mbalimbali za uzalishaji.

Mitazamo ya Jamii
Katika ukusanyaji wa taarifa wilayani humo, ilibainika kuwa, kati ya wazazi 15 waliohojiwa na mwandishi kutoka kata mbili za halmashauri hiyo, 12 walisema hawana imani na elimu kama njia ya kuwakomboa kimaisha, huku wakitoa mifano ya watu waliosoma na kuishia kukosa ajira.

Esta Lazaro, mkazi wa Kanazi, anasema jamii imekuwa ikishuhudia watoto wengi wanasoma hadi vyuo vikuu lakini hawaoni matokeo ya moja kwa moja katika maisha ya wahitimu kwamba hali hiyo huwafanya wazazi kuona hakuna tija ya watoto kusoma.

“Tumeona watoto katika familia nyingi wanasoma hadi vyuo vikuu lakini wanarudi kuendesha bodaboda au kufanya vibarua ili waishi, haina maana yoyote kusoma cha msingi mtoto ajue kusoma, kuandika na kuhesabu, basi inatosha,” anasema Lazaro.

Kauli hiyo inaungwa mkono na Adolf Ezekia ambaye anasema alifanikiwa kusomesha watoto wake watatu hadi ngazi ya chuo kikuu kwa fedha za kilimo, lakini hakuna hata mmoja aliyepata ajira.

“Niliwekeza fedha zangu zote ili wasome wapate kazi wanirudishie. Leo mimi ndiye bado ninawahudumia, faida ya elimu ipo wapi? ni bora niwekeze kwenye shughuli ninazozifahamu,” analalamika Ezekia.

Kwa upande wake, Ndikumana Goodlucky anasema mume wake amekuwa akiwazuia watoto kufanya mitihani ya darasa la saba kwa madai kuwa hata wakifaulu hatawasomesha kwakuwa hata wakimaliza hawatapata kazi.

“Mara nyingine anawaambia wafanye mtihani vibaya ili wafeli, anawaambia kusoma muda mrefu ni kupoteza muda na fedha ni bora baada ya kumaliza la saba waanze kujishughulisha na biashara, kilimo au hata wapate ujuzi kutoka Veta,” anasema Goodlucky.

Yusta Bukuru, mkazi wa Nyamyusi, anasema mitazamo hiyo inaonekana zaidi katika baadhi ya jamii za kifugaji, ambapo wazazi huwazuia watoto kufanya mitihani wakidai hata wakifaulu hakuna wanakokwenda.

Sababu za Kiuchumi na Miundombinu
Licha ya mitazamo hasi ya jamii, changamoto za kiuchumi na miundombinu zimeonekana kuchangia kwa kiasi kikubwa utoro wa wanafunzi, ikiwemo uhaba wa vyumba vya madarasa na uhaba wa walimu.

ELESTINA (1).jpg

Ofisa elimu wa Wilaya ya Kasulu, Elestina Chanafi

Ofisa elimu wa Wilaya ya Kasulu, Elestina Chanafi, anaeleza kuwa wilaya hiyo ina upungufu wa miundombinu ya elimu ikiwemo vyumba vya madarasa 1,349 kati ya 2,080 vinavyohitajika

Kwa mujibu wa takwimu za ofisa huyo, wilaya ina vyumba 731 pekee kwa wanafunzi 85,862 waliopo katika shule za msingi 89, hali inayosababisha mlundikano mkubwa wa wanafunzi darasani na kushuka kwa ubora wa ufundishaji.

Hata hivyo, Chanafi anaeleza kuwa mikakati ya halmashauri hiyo katika kukabiliana na changamoto hiyo ni kuendelea kushirikiana na wadau wa elimu na kutumia fedha za mapato ya ndani na serikali kuu kwa ajili ya kuboresha miundombinu hiyo akidai kuwa fedha zinazotengwa kila mwaka kwa miundombinu ya elimu haziendani na hali halisi ya ongezeko watu katika wilaya hiyo inayokuwa kwa kasi.

“Halmashauri yetu ni mpya ambayo bado inajengwa, na inahitaji rasiliamli fedha nyingi ili kuweza kukabiliana na changamoto zilizopo katika kila sekta, zipo juhudi mahususi ikiwemo mikutano na wazazi, na wadau wa maendeleo za kukabiliana na changamoto za kielimu zinaendelea,” anasema Chanafi.

Aidha Chanafi anaeleza kuwa kuna vijiji vinavyoibuka maeneo ya maporini bila mipango rasmi, hali inayowafanya wanafunzi kutembea umbali mrefu kufika shuleni na kwamba wamekuwa wakijitahidi kuanzisha shule katika maeneo hayo na kuagiza walimu japo changamoto huwa namna ya kupata huduma nyingine za msingi za kijamii kwa walimu hao.

Kwa upande wake meneja mradi wa Wezesha Binti unaondeshwa na shirika la Enabel katika wilaya tano za mkoa wa Kigoma ikiwemo Kasulu, Christine Karungi, anasema miongoni mwa sababu za utoro ni umbali wa kutembea kufika ambapo baadhi ya wanafunzi hutembea umbali mrefu takribani kilomita 20 kufika.

Anataja sababu nyingine kuwa ni mazingira ya kujihifadhi kwa watoto wa kike wanapokuwa katika siku za hedhi akitaja kuwa kupitia mradi huo watasimama watatoa vifaa vya hedhi ili kunusuru hali iliyopo.

Vilevile meneja mradi kutoka shirika la World Vision Kanda ya Magharibi, Jackline Kaihura, anasema miundombinu ya vyoo pia ni sababu inayochangia wanafunzi kuwa na mdondoko kwakuwa katika shule nyingi za mkoa wa Kigoma hazina vyoo vizuri kwa watoto na hasa watoto wenye ulemvu akitaja kuwa kama wada wamekuwa wakipambana kujenga vyoo na madarasa ili kupunguza ukubwa wa tatizo.

Udhaifu wa sheria
Licha ya kuwepo kwa kifungu cha 35 cha Sheria ya Elimu ya mwaka 1978 na Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009, utekelezaji wake katika Wilaya ya Kasulu umekuwa dhaifu.

Wakili Hamis Ramadhan wa Shira Advocates anaeleza kuwa tatizo si sheria, bali hakuna mfumo thabiti wa ufuatiliaji katika ngazi ya jamii, shule na mamlaka za serikali akitaja pengo la elimu ya sheria kwa watekelezaji wa sheria hiyo wakiwemo walimu, wazazi na viongozi wa vijiji.

“Sheria imekuwepo kwa zaidi ya miongo minne, lakini haina mfumo wa haraka wa kuingilia mtoto anapotoroka shule. Waraka unaoruhusu mwanafunzi kufukuzwa baada ya siku 90 za utoro unatoa mianya kwa wazazi wasiothamini elimu,” anasema Ramadhan.

Anaongeza kuwa sheria hiyo ilitungwa bila kuzingatia kikamilifu mazingira ya vijijini, ambako changamoto za umbali, hali ya hewa na uchumi zinaweza kumfanya mtoto kutoroka shule kwa muda.

Uwajibikaji wa kiutawala ngazi ya chini
Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyakitonto, January Falasi, anasema kesi nyingi za utoro na ujauzito wa wanafunzi hufa zinapofika ngazi za juu kama polisi au mahakamani.

“Sisi kama viongozi wa kijiji tunapambana kufuatilia, lakini jamii inatuona kama watu wa kuingilia mambo yasiyotuhusu wazazi wanakaa pembeni, kesi zinafutwa,” anasema.

Kwa mtazamo wa Jennifer Cornel, anasema tatizo kubwa ni kukosekana kwa mfumo wa kisheria unaoweka uwajibikaji wa wazi kwa wadau wote katika sekta ya elimu akisema kuwa walimu na viongozi wanapaswa kuwa na mamlaka ya kisheria ya kuwabana wazazi wanaosababisha watoto kutoroka shule.

“Pale kutakapokuwa na mfumo wa kuwabana walimu, wazazi na viongozi kwa pamoja, ndipo utoro utaanza kupungua,” anasema Cornel.

Katika makala haya, uchunguzi umebaini kuwa jamii inawalaumu walimu kuwa chanzo cha utoro, huku walimu wakiwalaumu wazazi kuwa chanzo kikuu huku sheria ikilaumiwa kwa kuacha mapengo katika utekelezaji wake.


ANDIKO LA: Adela Madyane – Kigoma
Makala imeandaliwa na Mwandishi anayeshiriki katika programu maalum ya kukuza uandishi wa maslahi kwa umma (Public Interest Journalism Fellowship) inayoratibiwa na UTPC kwa kushirikiana na IMS.
 
Back
Top Bottom