UTPC
Journalists' Union
- Apr 17, 2026
- 30
- 25
Kasulu. Licha ya kilimo kuwa shughuli kuu ya uchumi kwa wakazi wa Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, ikiwahakikishia usalama wa chakula na kipato kwa kuuza mazao, shughuli hiyo sasa inatishia hatima ya elimu kwa baadhi ya watoto wilayani huyo.
Hiyo ni kutokana na baadhi ya wazazi kutelekeza watoto wao na kuhamia mashambani na hivyo kusababisha watoto hao kushindwa kwenda shule.
Uchunguzi umebaini kuwa wastani wa watoto zaidi ya 2,000 huacha masomo kila mwaka katika halmashauri ya wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma kutokana na kushiriki shughuli za kilimo au kubeba majukumu ya familia wakati wazazi wao wakiweka kambi mashambani kwa kipindi hadi cha miezi sita
Baadhi ya wazazi huwabeba watoto na kwenda nao mashambani kwa msimu mzima wa kilimo, huku wengine wakiwaacha watoto peke yao bila uangalizi, chakula cha kutosha wala msaada wa karibu hali ambayo kwa namna zote mbili huwafanya watoto washindwe kuendelea na masomo.
Hatua hiyo inawanyima haki ya elimu watoto kinyume na Kifungu cha 35(2) na (3) cha Sheria ya Elimu ya mwaka 1978, mamlaka za elimu zina wajibu wa kuhakikisha kila mtoto aliyeandikishwa shule anahudhuria na kumaliza masomo.
Vilevile, Kanuni za Elimu ya Msingi za mwaka 2022 zinaelekeza hatua za kuchukua dhidi ya utoro wa wanafunzi na wazazi wasiotimiza wajibu wao.
Hata hivyo, ukweli kwamba maelfu ya watoto wanaendelea kuacha shule utekelezaji wake unaonekana kuwa dhaifu, hali inayozua maswali kuhusu uwajibikaji wa mamlaka za elimu, viongozi wa vijiji na kata katika kudhibiti utoro.
Mwenyekiti wa Nyakitonto
Simulizi watoto kubebeshwa majukumu ya wazazi
Katika Kijiji cha Nyakitonto kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, uchunguzi wa Nipashe unakutana na kisa cha binti mwenye umri wa miaka 15, mwanafunzi wa kidato cha tatu, aliyelazimika kubeba jukumu la kulea wadogo zake watano baada ya wazazi wake kuondoka na kuweka kambi mashambani kwa miezi sita mfululizo, wakati wa msimu wa kilimo wa mwaka 2025.
Akieleza kisa hicho, mjomba wa binti huyo, Yusto Ntakihemba (jina moja limebadilishwa kulinda usiri wa mtoto) anasema binti aliachiwa debe mbili za mahindi, dagaa kwenye kopo la Kimbo moja pamoja na maharage bakuli tatu zenye ujazo wa kilo moja na nusu, akiahidiwa na wazazi wake kuwa wangerudi mapema ili kuwajulia hali na kuwaachia chakula kingine.
“Bahati mbaya wazazi wake hawakurudi. Baada ya kuishiwa chakula, mtoto alianza kuomba msaada kwetu na kwa ndugu wengine ambao nao walimchoka. tulipiga simu mashambani bila mafanikio. M wishowe binti aliacha shule na kuanza kulima vibarua ili kupata chakula cha kuwalisha wadogo zake,” anaeleza Ntakihemba.
Anafafanua zaidi kuwa kutokana na mazingira hayo, binti huyo aliingia kwenye mahusiano ya kimapenzi na kijana aliyemsaidia mahitaji ya msingi, hali iliyoishia kumpa ujauzito.
“Hatuwezi kumlaumu kijana aliyempatia ujauzito binti huyu kwa sababu ni kweli alimsaidia yeye na wadogo zake, alichukua jukumu la baba kwenye familia hiyo,” walisikika wakinong’ona baadhi ya watu waliokuwepo ambako mwandishi alifanya mahojiano na mjomba wa binti
Ntakihemba anaeleza kuwa wazazi wa binti walirudi mwanzoni mwa Desemba 2025 na kumkuta binti akiwa tayari mjamzito, ambapo wazazi wake walianza kusumbua kwa maneno makali hali iliyomfanya binti huyo kuondoka na kwenda kuishi na kijana aliyempatia ujauzito.
Baada ya siku kadhaa walijua alipo binti ndipo wlipofuatana na polisi ambapo waliwakamata, na hatua nyingine za kisheria kufuata.
Mpaka wakati wa kufuatilia habari hii katika kijiji hicho, binti alikuwa chini ya uangalizi wa ustawi wa jamii akiwa na ujauzito wa taribani miezi minee huku kijana akiwa ameshikiliwa sero akisubiri hatma yake kisheria, jambo ambalo nalo linaibua maswali ya uwajibikaji.
“Huu ni uonevu, sheria inapaswa kuangalia pande zote, kwa sababu kosa la awali lilifanywa na wazazi walioshindwa kutekeleza wajibu wao wa malezi,” anasema Ntakihemba kwa huzuni.
Simulizi ya binti huyo ilitanguliwa na na kijana Rashid Shaban (20) mkazi wa Nyakitonto, ambaye aliacha shule akiwa darasa la nne baada ya kuachiwa wadogo zake sita.
“Niliachiwa debe moja la mahindi na maharage kidogo, baba alisema chakula kikiisha niuze mbogamboga sokoni, ndoto ya kuwa daktari iliishia hapo,” anasema.
Kwa mujibu wa Shaban, watoto wengi wilayani humo hujikuta katika hali kama yake bila msaada wa mamlaka yoyote, hali inayowafanya kuingia kwenye ajira za utotoni na kuacha kabisa masomo.
Ukubwa wa tatizo
Kwa mujibu wa ofisa elimu msingi wa wilaya ya Kasulu, Elestina Chanafi, kwa msimu wa kilimo wa 2024/2025 jumla ya wanafunzi 2,317 waliripotiwa kuacha shule, wakiwemo wavulana 890 na wasichana 1,427.
Takwimu hizi zinafanana na zile zilizotolewa ofisa elimu wa wilaya hiyo, Joseph Maiga kwa msimu wa kilimo 2022/2023 ambapo wanafunzi 2,000 waliripotiwa kutoroka shule ikiwa ni ongezeko la asilimia zaidi ya 50 kutoka utoro ulioripotiwa msimu wa mwaka 2020/2021 ambapo wanafunzi 800 walitoroka.
Chanafi anataja sababu kuu, kuwa ni ushiriki wa wanafunzi katika shughuli za kilimo na biashara wakati wa msimu wa mavuno, huku kata zilizoathirika zaidi zikitajwa kuwa Kagerankanda, Asante Nyerere, Herushingo na Kitanga.
Anaongeza kuwa wengi wanaotoroka au kuacha shule ni wale wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK) ambao hutoka kwenye kata zenye watu wengi.
Mkurugenzi wa Amenity Charity Organization, Obadia Binguye, aliwahi kueleza kuwa zaidi ya watoto 300 waliishi mtaani Kasulu mwaka 2019, idadi inayodhaniwa kuongezeka zaidi kwa sasa.
Taarifa ya vyombo vya habari na taasisi za kiserikali
Kwa mujibu wa tovuti ya Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Aprili 18, 2023 Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Titus Mghuha aliagiza viongozi wa kata na kijiji kuwasaka wanafunzi waliopo katika mpango wa elimu ya msingi kuripoti shuleni baaada ya kuwa shule zimefunguliwa lakini hakuna wanafunzi.
Taarifa hiyo ilifafanua kuwa zaidi ya waafunzi 30,000 walitakiwa kujiunga na Mpango wa Elimu ya Msingi Kwa Waliokosa (MEMKWA) kutokana na kuacha shule kabla ya kuhitimu huku wakiwa hawajui kusoma, kuandika na kuhesabu.
Ripoti ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ya Machi 2025, inaeleza kuwa zaidi ya asilimia 70 ya watoto mkoani Kigoma wanakosa malezi sahihi kutoka kwa wazazi wao na kusababisha wengine kuacha shule na kukimbilia mtaani au kwenda katika miji mikubwa ili kujitafutia riziki.
Kwa nini makambi ya kilimo yanaendelea?
Venance John anadai kuwa, umaskini ndio chanzo kikuu cha wazazi kuwatelekeza watoto kwakuwa wanakosa namna ya kugawa rasilimali walizonazo kwakuwa wengi wao huishi kilimo cha mkono.
Ofisa kilimo wa wilaya ya Kasulu, Ntegwa Luziro, anaeleza kuwa wazazi huweka kambi kwa sababu ya umbali mrefu kutoka makazi yao wakitafuta maeneo makubwa ya kulima huku akieleza kuwa maeneo ya karibu na makazi ni madogo na wakulima hawavuni kiwango cha mazao kinachostahili kuhudumia familia zao.
Vilevile anaeleza kuwa wakulima wengi huenda mbali na makazi wakitafuta ardhi yenye rutuba itakayowawezesha kupata mazao mengi wanayohitaji.
Kwa upande wake, afisa elimu Chanafi anakiri kuwa baadhi ya wazazi hawathamini elimu, lakini anakiri pia kuwa wanendelea kushirikiana na sekta za kilimo, ustawi wa jamii na maendeleo ya jamii ili kuondoa udhaifu katika halmashauri hiyo.
Inaendelea….
ANDIKO LA: Adela Madyane – Kigoma
Makala imeandaliwa na Mwandishi anayeshiriki katika programu maalum ya kukuza uandishi wa maslahi kwa umma (Public Interest Journalism Fellowship) inayoratibiwa na UTPC kwa kushirikiana na IMS.