Labda sasa wanashtuka na kuchukua hatua...wakiendelea hivi watatutia moyo...
Pia hongera waziri kwa "kupunguza" mgogoro huko Kahama kwa kuruhusu kijiji kiendelee kuwepo sanjari na mgodi wa dhahabu.
Serikali yaachana na Alex Stewart
Na Midraji Ibrahim
WIZARA ya Nishati na Madini, imesema haitaongeza mkataba wa ukaguzi wa madini na Kampuni ya Alex Stewart (Assayers) badala yake, itatumia wataalam wake wa ukaguzi.
Akiwasilisha taarifa ya serikali katika Kamati ya Bunge ya Biashara na Uwekezaji jana, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, alisema wizara itahakikisha inajenga uwezo wa wataalam wake kufanya kazi hiyo.
"Baada ya mkataba wa Alex Stewart (Asseyers) kumalizika mwaka huu, hatutakuwa na ulazima wa kuendelea na makataba huo. Mchakato wa kuendeleza ukaguzi kama huo kwa wataalam wetu umeishaanza," alisema Ngeleja.
Kutokana na utekelezaji wa shughuli za ukaguzi kwenda kama ilivyopaangwa katika awamu ya pili ya mkataba, Ngeleja alisema, kuna matarajio sehemu kubwa ya kazi itakuwa imekamilika ifikapo mwishoni mwa kipindi cha mkataba huo.
Kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wabunge na wananchi juu ya kuibiwa kwa dhahabu inayozalishwa na kampuni kubwa za kigeni kwa sababu ya kutokuwepo kwa usimamizi na udhibiti wa uchimbaji na biashara ya madini hayo.
Juni 14,2003, serikali kupitia Benki Kuu (BoT) iliingia mkataba wa miaka miwili na Kampuni ya ASAGBC wa kufanya ukaguzi wa dhahabu katika migodi mikubwa ya dhahabu nchini; Bulyanhulu, Geita, North Mara, Goldenen Pride na Buhemba.
Ngeleja alisema, kulingana na mkataba huo, majukumu makuu ya ukaguzi yalikuwa ni kuchambua na kupitia utaratibu unaotumika katika uzalishaji, usafirishaji wa madini nje ya nchi na uendeshaji wa shughuli za madini nchini.
Majukumu mengine ni kuhakiki dhahabu inayozalishwa na kusafirishwa nje ya nchi na kampuni kubwa, ili kubaini usahihi wa ulipaji wa kodi na mrabaha kwa serikali unaofanywa na kampuni hizo;
Kuhakiki gharama za uwekezaji na uendeshaji wa migodi kama ilivyoainishwa katika mipango ya biashara ya migodi hiyo na kukagua na kuhakiki shughuli za utunzaji wa mazingira na gharama zake.
Hata hivyo, Ngeleja alisema kazi ya kuchambua na kupitia kanuni na taratibu zinazotumika katika uzalishaji, usafirishaji madini nje ya nchi na uendeshaji, haikukamilika kutokana na mkaguzi kuwasilisha taarifa yenye upungufu.
Ngeleja alisema, kutokana na kutokamilika kwa shughuli za mkaguzi kama ilivyoainishwa kwenye mkataba, Mei 28, 2005, BoT iliongeza mkataba wa kuongeza muda wa miaka mingine miwili.
Alisema kazi ya uhakiki imekuwa ikiendelea vizuri na taarifa za kila mwezi zinaonyesha kuwa takwimu zinazotolewa na kampuni hazitofautiana na za ukaguzi, hivyo kudhihirisha kuwa hakuna udanganyifu unaofanywa na kampuni za madini.
Kazi ya ukaguzi wa gharama za uwekezaji, uendeshaji na mazingira zimekamilika katika migodi ya Geita, North Mara, Golden Pride na Bulyanhulu na kwamba, kazi ya uchambuzi serikalini itaanza baada ya kukamilika kwa kazi hiyo kwenye migodi mingine ya Tulawaka na Buhemba.
Kumekuwepo na malalamiko kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), John Cheyo kwamba hesabu za kampuni hiyo hazijakaguliwa tangu ipewe kazi na hivi karibuni alinukuliwa akimtuhumu Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi kuwa anatetea kitu ambacho hakijui.
Hatua nyingine ambayo imekuwa ikilalamikiwa ni ile ya Waziri wa Fedha, Basil Mramba (wakati huo) kwa niaba ya serikali alisamehe kampuni huo kutotoa kodi ya mapato (withholding tax).
Katika mahojiano maalum na gazeti dada na Mwananchi, The Citizen, Desemba mwaka jana, Rais na Mtendaji Mkuu wa Alex Stewart (Asseyers), Dk Enrique Segura, alikanusha kampuni yake kulipwa kamisheni na Tanzania kwa kutumia mrabaha, bali mapato yatokanayo na dhahabu inayozalishwa na kuuzwa soko la dunia.
Mojawapo ya vifungo vya mkataba huo kinasema," Benki itamlipa mkaguzi ada ya mwezi ya asilimia 1.9 ya mauzo ya dhahabu na serikali kubaki na asilimia 1.1.
Ada inayokadiriwa kutolewa tangu Agosti 2003 kwa kipindi cha miezi 24 ni dola za Marekani 751,267.90. Kiwango ambacho kilikadiriwa mwaka 2003, lakini hakihusu kupanda kwa dhahabu kwenye soko la dunia tangu mwaka juzi.
SOURCE: Mwananchi 26 Machi, 2007