Cheyo alia na madini
na Mwandishi Wetu
WAKATI serikali ipo kwenye mjadala na wawekezaji wakubwa wa madini nchini, Kamati ya Hesabu za Serikali ya Bunge, imeanza kuhoji matumizi ya fedha zinazopatikana kupitia sekta hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za Bunge Dar es Salaam, jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha, John Cheyo, alisema kamati yake inahitaji kufahamu kiasi cha mrahaba kinachopatikana kutoka kwenye madini na matumizi yake.
Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, sekta ya madini huchangia kiasi cha asilimia 40 ya pato la taifa litokanalo na fedha za kigeni.
Hoja ya Cheyo, ambaye ni Mbunge wa Bariadi Mashariki (UDP), alijikita katika kutaka kufahamu jinsi serikali inavyotumia asilimia 40 ya fedha za kigeni nchini zinazotoka kwenye sekta ya madini.
Alisema, inashangaza kuona kuwa, wakati mapato kupitia sekta hiyo yamekuwa yakiongezeka, hali za maisha ya wananchi wanaoishi katika maeneo ya migodi, zimeendelea kuwa duni.
Cheyo alisema, ni vyema Bunge likaelezwa kuwa serikali inapata au inakosa nini kutoka kwenye madini, na kwa misingi ipi, ili kupata ufumbuzi wa tatizo hilo.
Cheyo alisema, kamati imedhamiria kumwita Mkaguzi Mkuu wa Serikali ili kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu pato halisi la fedha kutoka katika sekta ya madini.
Tunataka kukutana na wenye migodi tuwape nafasi nao waseme waonavyo na watuambie wana mchango gani kwa serikali juu ya madini.
Kamati inataka kufahamu kutoka serikalini kuwa, tunapata au kukosa nini katika makusanyo ya fedha zitokanazo na madini, hivyo tumepanga kuzungumza na mkaguzi mkuu wa serikali afafanue, na wenye machimbo nao waseme ili wananchi waelewe.
Tunaambiwa kuhusu ajira kwa Watanzania, lakini kila kukicha bado walioajiriwa kwenye migodi hiyo wanalia shida, hii inaonyesha kwamba hakuna kitu huko
sasa hoja za uendeshaji wa madini na mrahaba ndio kitu kikubwa ambacho kamati inahitaji kujua, alisema Cheyo.
Aidha, ameonya mvurugano katika sekta hiyo kwa kuwa ipo hatari ya kukosa wawekezaji, na hata fedha kidogo zinazoingia serikalini zitakwama ikiwa migogoro itaendelea.
Hakuna haja ya kutajana majina kuwa huyu nani, anafanya nini, wote tunajua kuwa, wachimbaji wa kawaida wapo chini ya Alex Stewart, lakini hakuna haja ya kugombana, tushirikiane ili tuongeze kipato, alisema.
Kamati hiyo ilikutana na wawakilishi kutoka taasisi mbalimbali zikiwamo Benki Kuu, Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya Fedha na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).