Date::11/12/2008
Wanafunzi sasa wamtaka Kikwete
Na Waandishi Wetu
Mwandishi
WANAFUNZI wa Chuo Kikuu, eneo la Mlimani, sasa wanamtaka Rais Jakaya Kikwete aende chuoni kuzungumzia mpango wa serikali yake kutatua tatizo la sera ya uchangiaji elimu ambayo wanaipinga kwa kutoingia madarasani.
Hatua hiyo ilifikiwa baada ya mwakilishi kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kushindwa kutokea kwenye Ukumbi wa Nkrumah, ambako wanafunzi hao walikuwa wamekusanyika kuzungumzia mgomo wao.
Rais wa serikali ya wanafunzi chuoni hapo, Anthony Machibya, alikuwa amewataarifu wanafunzi hao jana kuwa, baada ya Waziri Jumanne Maghembe kukutana na viongozi wa vyuo saba vya serikali, aliahidi kutuma mwakilishi wa wizara chuoni hapo ili awaeleze wanafunzi hatua ambazo serikali itachukua kumaliza mgomo ulioanza juzi kupinga sera hiyo ya uchangiaji.
Baada ya wanafunzi hao kumsubiri kwa muda mrefu mwakilishi huyo, rais huyo aliingia tena kwenye ukumbi huo wa Nkrumah na kuwataarifu wanafunzi kuwa, mwakilishi huyo asingeweza kufika kwa kuwa amekwenda kukutana na Rais Jakaya Kikwete kujadili suala hilo.
"Baada ya kwenda kwa makamu mkuu wa chuo, Profesa Rwekaza Mukandala, nilitaarifiwa kuwa makamu huyo akiwa na baadhi ya wasaidizi wake wameitwa Ikulu na Rais Kikwete kuzungumzia madai yetu pamoja na Waziri wa Elimu, Profesa Jamanne Maghembe," alisema Machibya.
Taarifa hiyo iliwafanya wanafunzi kulipuka kwa furaha za shangwe.
Baadaye mmoja wa wanafunzi hao alipewa kipaza sauti na kupendekeza kuwa, kwa kuwa viongozi wengine wamekuwa wakitoa majibu ambayo yanaonekana kuwa ni ya kusumbua, ni afadhali wakutane na rais, pendekezo ambalo lilipitishwa na wanafunzi wote, waliokuwa wakipiga kelele wakidai kuwa wamechoka kuzungushwa kwa hadi zisizotekelezeka.
Wanafunzi hao wanapinga sera ya uchangiaji gharama za elimu ambayo inataka wazazi walipie sehemu ya gharama hizo na walianza mgomo wao juzi bila ya vurugu kubwa.
Chini ya utaratibu huo, wanafunzi hutakiwa kujaza fomu zinazoeleza mintaarafu ya maisha yao na wazazi wao, ikiwa ni pamoja maelezo ya shule walizopitia na baadaye taarifa hizo huingizwa kwenye kompyuta ambayo hufanya mchanganuo na kuamua muombaji mkopo wa elimu apewe fedha kwa kiwango gani.
Kwa mujibu wa takwimu za Bodi ya Mikopo, asilimia kubwa ya wanafunzi huangukia kwenye kuchangia asilimia 20 ya gharama za masomo ya vyuo vya elimu ya juu, wakati ni wachache sana ambao hupata asilimia 100.
Wakati wanafunzi wakikubaliana kuwa Rais Kikwete ndiye suluhisho la matatizo yao, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Prof Jumanne Maghembe aliwaambia waandishi wa habari kuwa, wanafunzi wote hawana budi kuingia madarasani leo, kusubiri suala lao kushughulikiwa na serikali.
Profesa Maghembe alisema kutokana na wanafunzi kutaka sera hiyo ifutwe, serikali ilikutana na viongozi wa wanafunzi juzi na kukubaliana na viongozi wa wanavyuo hao kuwa leo waingie darasani huku mchakato wa kuiangalia sera hiyo ukifanywa na serikali.
"Kama waziri mwenye dhamana, niliwasisitiza viongozi kuwa matatizo yaliyojitokeza katika utekelezaji wa sera hiyo, yatatafutiwa ufumbuzi na tukakubaliana katika kikao hicho cha pamoja cha Oktoba 23, 2008," alisema Maghembe.
Prof Maghembe aliongeza kutokana na hali ya uchangiaji elimu kuanzia mwaka 2005/06 hadi Juni 2008 wanafunzi 145,970 wamenufaika na mikopo hiyo na kiasi cha Sh254 bilioni kimetumika na kwa mwaka 2008/09 mpango huo unatarajiwa kunufaisha wanafunzi 60,000.
Pia tamko hilo la Serikali limewataka wanafunzi wote waliogoma kurejea madarasani leo saa 1.00 asubuhi na wawe wamesitisha mgomo wao wakati serikali ikiendelea kushughulikia matatizo ya sera hiyo.
Hali ilikuwa mbaya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, eneo la Mlimani, ambako wanafunzi waliogoma walifanikiwa kukwamisha takriban mitihani mitatu, ukiwemo wa Historia uliokuwa ufanywe jana asubuhi na mwingine wa 264 CO, uliokuwa ufanyike kwenye kafteria ya Yombo chuoni hapo jana saa 8:00 mchana.
Wanafunzi hao waliunda kikundi walichokiita cha 'task force' ambacho kilizunguka kwenye madarasa na maktaba ya chuo hicho na kuwatoa nje wanafunzi waliokuwa wakijisomea, kitendo ambacho kilisababisha mgogoro kati yao na kulazimu maktaba hiyo kufungwa.
"Tunachotaka ni ninyi kuondoka hapa darasani mkasomee huko mabwenini kwenu kwa sababu mnapofanya hivyo mna maana hiki tunachokifanya sisi hakina maana na ninyi ndiyo mnaopenda kusoma sana," alisema mwanafunzi mmoja wa kikosi hicho.
Kitendo hicho kililalamikiwa na baadhi ya wanafunzi hasa walio mwaka wa mwisho, wakidai kuwa kinawanyima haki ya kujisomea wanafunzi wasiotaka kujihusisha na mgomo huo.
"Kwa kawaida wanafunzi wanaomaliza siku zote kunapotokea mgomo hawataki kujihusisha. Hii ni kwa sababu wengi wanakuwa wako makini sana na kusoma na wanaogopa wakigoma wanaweza wakaathirika na kupoteza miaka yote waliyokaa chuoni," alisema Fakih Othman, ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu.
"Suala la kuwazuia wengine wasisome halipendezi kwa sababu linawanyima uhuru wao wa kusoma."
Fakih aliongeza kusema: "Ninaunga mkono mgomo huu kwa kuwa umesababisha baadhi ya wanafunzi kushindwa kuendelea na masomo na wengine kuishi maisha ya tabu, lakini njia zinazotumika kufanya mgomo huo haziwashirikishi wanafunzi wote ndiyo maana baadhi ya wabunge waliupinga katika vikao vya Bunge vilivyopita."
Afisa Uhusiano wa UDSM, Isdory Jackson alikataa kuzungumzia kitendo hicho akisema si msemaji wa chuo.
Habari hii imeandikwa na Hussein Kauli, Mussa Mkama na Festo Polea.