SEHEMU YA 77
“Mchungaji! Mimi ni mkosaji! Nimekuja kutubu dhambi zangu! Nimekuwa nikimtumikia shetani kwa kipindi kirefu katika maisha yangu. Nimemtenda Mungu wangu dhambi! Nimekuja kutubu mchungaji,” alisikika mtu mmoja akimwambia padri aliyekuwa kwenye chumba kidogo cha kuungama dhambi.
“Umefanya nini mtoto wa Mungu?” aliuliza padri huyo.
“Nimezini kwa kipindi chote cha maisha yangu, nimekuwa na tamaa ya fedha, nimekuwa nikimtumikia shetani kwa kila aina ya uchafu. Nimechoka, ninataka kuokoka mchungaji, sitaki kumtumikia tena shetani,” alisikika mtu huyo akizungumza na padri huyo ambaye muda wote alikuwa akionyesha ishara ya msalaba.
“Mungu atakusamehe dhambi zako. Amesema kwamba hata kama dhambi zako zinakuwa nyekundu kama damu, atazisafisha na kuwa nyeupe kama theluji,” alisema padri huyo.
****
“What is wrong with her?” (nini kimemtokea?)
“Asthma.” (pumu)
“Where is her inhler?” (kifaa chake cha kuwekea dawa ya pumu kipo wapi?) alisikika mwanamke mmoja akiuliza.
“Here it is but there is nothing in it!” (hiki hapa lakini ndani hakuna kitu) alisikika msichana mmoja akijibu.
“What?” (nini?)
Kila mmoja ndani ya nyumba alichanganyikiwa, mtoto Kyle alikuwa amebanwa na pumu ambayo ilikuwa ikimsumbua kila siku. Mama yake na mfanyakazi wa ndani walichanganyikiwa, walijaribu kuangalia dawa ya kumpa iliyokuwa kwenye kifaa kidogo kinachojulikana kama inhler ambacho alitakiwa kuivuta kwa mdomo dawa hiyo lakini kitu cha kushangaza kabisa, kifaa hicho hakikuwa na dawa yoyote ile.
Waliuona mwisho wa Kyle, alikuwa akilalamika, alikipandisha kifua chake juu kama mtu aliyetaka kukata roho, alipumua juu juu kwa tabu sana kiasi kwamba kila mmoja alikuwa na uhakika kwamba binti yao angekufa usiku huo.
Mama yake hakutaka kuchelewa, haraka sana akachukua simu yake na kumpigia mume wake, Dk. Watson ambaye alikuwa ni daktari kwa lengo la kumwambia kile kilichokuwa kikiendelea kwa mtoto wao, Kyle.
“Unasemaje?” alisikika daktari huyo akiuliza kutoka upande wa pili wa simu.
“Kyle anakufa! Njoo na dawa haraka sana.”
“Dawa zake zipo wapi?”