Michirizi ya Damu

Michirizi ya Damu

SEHEMU YA 33

Bilionea Keith hakuamini, alimwangalia vizuri Fareed, ilikuwa vigumu kufahamu kama mtu huyo alikuwa mwanaume, alionekana kukamilika kama mwanamke kamili. Hakutaka kumganda sana, akaendelea kufanya mambo yake na usiku wa siku iliyofauata, sherehe ikaanza kufanyika katika ukumbi wa Hoteli hiyo.

Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa wawili hao kuonana, wakabadilishana namba za simu na kuanza kuwasiliana. Bilionea Keith hakuwa na hofu na Fareed, kwake alikuwa rafiki yake mkubwa, alimsaidia kama rafiki yake na wakati mwingine alimuita mpaka Marekani kwa ajili ya kumtembelea.

Hakufanya naye kitu, kila alipokuwa akimuhoji kwa lengo la kutaka kujua mambo mengi zaidi, hasa kuhusu uhusiano, mwanaume huyo hakumficha, alimwambia kwamba alikuwa kwenye uhusiano na mwanaume mwingine aliyeitwa kwa jina la Godfrey.

“Ni mwanaume mwenye bahati sana,” alisema Keith.
“Kwa nini?”
“Kumpata mrembo kama wewe.”
“Kwani mimi mrembo?”
“Hujioni? Nenda kachukue kioo halafu jiangalie,” alisema Keith huku akimwangalia Fareed.

“Hapana!”
“Niamini!”
Safari zake za kutafuta wanaume hazikuisha, aliendelea kuizunguka dunia, kila alipoambiwa na wakala wake kwamba kulikuwa na mwanaume aliyekuwa akimtaka, alikwenda huko, alizunguka sehemu mbalimbali na hakutaka kabisa Godfrey ajue kile kilichokuwa kikiendelea katika maisha yake.

“Upo wapi Fareed,” aliuliza Keith kupitia ujumbe mfupi kwenye Mtandao wa WhatsApp.
“Ubelgiji!”
“Nahitaji nikuone.”
“Lini?”
“Hata kesho!”
“Mh! Mbona haraka hivyo?”

“Kwa sbabu nimekumisi.”
“Basi naomba tufanye wiki ijayo. Nitakuja tu rafiki yangu,” alisema Fareed.
“Basi sawa. Nakusubiri kwa hamu!”
“Kuna nini lakini?”

“Hakuna kitu! Nataka nikuone tu.”
“Mmh! Sawa,” alisema Fareed na kukata simu, hakuamini kama kulikuwa na kitu cha kawaida, alijua kabisa kwamba kulikuwa na kitu mwanaume huyo alikuwa akikihitaji kutoka kwake. Hivyo akajiandaa.
 
SEHEMU YA 34

Bilionea Keith alikuwa nyumbani kwake ametulia, aliyafikiria maisha yake, tangu siku alipopata ufahamu mpaka hapo alipofika. Alipitia mengi, alipata matatizo makubwa lakini yote hayo baadaye yakageuka na kuwa changamoto katika maisha yake.

Alifanya ushenzi wa kila aina kupitia fedha zake. Alitembea na wanawake wa kila aina, alifanya ujinga wote mpaka kuona kwamba hakukuwa na ujinga ambao hakuwahi kuufanya katika maisha yake mpaka sasa.

Aliyatathmini maisha yake na mwisho kugundua kwamba kwenye ushenzi wote aliokuwa ameufanya, kulikuwa na ushenzi mmoja tu ambao hakuwa ameufanya na ndiyo ambao ulimfanya kumpigia simu Fareed na kuomba kuonana naye.
Mwili wake ulimsisimka, hakutaka kuona kitu kingine tena zaidi ya kutembea na Fareed ambaye kwa muonekano wake tu ulimtamanisha kupita kawaida.

Siku iliyofuata akampigia simu na kutaka kuonana naye kitu ambacho hakikuwa kigumu kwa Fareed, akamwambia kwamba wiki inayofuata angeonana naye na kutaka kusikia kile alichokuwa amemuitia.

Kuanzia siku hiyo, Keith akawa na mawazo mengi, moyo wake haukutulia, ilikuwa ni kama Fareed alikuwa na majini kwani kipindi cha nyuma alimuona kuwa mtu wa kawaida lakini muda huo alibadilika, alianza kupata nguvu sana moyoni mwake.

Mwanaume tata huyo kila siku akawa akiwasiliana naye na kumuuliza ni kitu gani hicho alitaka kumwambia lakini Keith hakutaka kufumbua mdomo wake na kumwambia zaidi ya kumpa taarifa kwamba angemwambia kama angekwenda nchini Marekani.

“Jamani! Unaniweka kwenye presha mwenzako!” alisema Fareed kwenye simu kwa sauti yake ya kike.
“Usijali! Utakuja na kuona tu,” alisema Keith.

Siku zikakatika na hatimaye siku ya kwenda nchini Marekani ikawadia. Njiani, Fareed alikuwa na mawazo mengi, hakufikiria kitu kuhusiana na mapenzi, alimwamini mwanaume huyo na kwake alikuwa mmoja wa marafiki zake wakubwa.

Ndege hiyo ilichukua saa zaidi ya ishirini ndipo wakafika nchini Marekani, gari la kifahari lilimfuata, likamchukua na kuelekea katika jumba jingine la Keith ambapo huko aliambiwa asubiri na mwanaume huyo angefika siku hiyo.
 
SEHEMU YA 35

Lilikuwa jumba kubwa mno, alizunguka katika kila chumba lakini hakuweza kulimaliza, kila chumba alichoingia kilikuwa kikubwa, alitembea mpaka kuchoka hivyo akaamua kwenda kupumzika katika bwawa la kuogelea.

Walinzi waliokuwa humo walikuwa wakimwangalia Fareed. Hawakuelewa kama huyo waliyekuwa wakimwangalia alikuwa mwanaume au mwanamke. Wengi wakahisi kwamba alikuwa mwanamke, kwa jinsi alivyokuwa mzuri na mikogo yake lakini kitu cha ajabu kabisa, kifuani hakukuwa kama mwanamke, kifua chake kilinyooka kama mwanaume.

“Is he a girl?” (ni mwanamke?) aliuliza jamaa mmoja huku akiwa amemtumbulia macho Fareed.
“I don’t know!” (sifahamu) alijibu jamaa mwingine, yeye mwenyewe alivyomwangalia Fareed, hakumuelewa hata kidogo.

Baada ya kukaa kwa saa tatu ndipo Keith akafika nyumbani hapo. Kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kwenda katika chumba alichompangia Fareed na kumkuta huko.
Mapigo yake ya moyo yalikuwa juu, alimwangalia mwanaume huyo, mwili wake ulikuwa ukisisimka kupita kawaida, alijishangaa kwani kipindi cha nyuma hakuwa hivyo, japokuwa alikuwa mwanaume tata lakini kwake bado aliendelea kuwa mwanaume ila kwa siku hiyo alikuwa hoi kabisa.

Akamsogelea na kumkumbatia, mapigo yake ya moyo yalizidi kudunda kwa nguvu kiasi kwamba mpaka Fareed akashtuka kwani haikuwa kawaida kwa mwanaume huyo kuwa katika hali hiyo.
“What the hell wrong with you?” (una nini jamani?) aliuliza Fareed huku akimwangalia Keith.

“I got nothing!” (hakuna chochote)
“No! Tell me the truth!” (Hapana! Niambie kweli)
“That’s the truth! I got nothing. I just missed you,” (huo ndiyo ukweli! Sina kitu, nilikukumbuka tu) alijibu mwanaume huyo huku kwa mbali kijasho chembamba kikianza kumtoka.

Walikaa na kuzungumza mambo mengi, muda mwingi alikuwa akimwangalia Fareed, mapigo yake ya moyo hayakuacha kudunda na kwa jinsi Fareed alivyokuwa na makusudi, akaanza kukaa mikao ya hasarahasara pale kwenye kochi.

Moyo wake ulikuwa kwenye maombi mazito, kila alipomwangalia Fareed jinsi alivyokaa pale kwenye kochi, aliona kabisa shetani alikuwa akimzidi nguvu, tena kwa kasi kubwa.
 
Ngoja tusubiri maana mvumilivu hula mbivu
 
Back
Top Bottom