SEHEMU YA 32
Fareed alifurahi, kwa kipindi kirefu alitamani kufika nchini Marekani, kitendo cha kuambiwa kwamba alitakiwa kwenda huko, moyo wake ukarukaruka na siku hiyo ilipofika, wakaondoka kuelekea huko.
Baada ya saa zaidi ya ishirini, ndege ikaanza kutuka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa LAX uliokuwa hapohapo Los Angeles. Walipoteremka, tayari kulikuwa na gari lililokuwa likiwasubiria ambapo moja kwa moja wakaingia na kuanza kupelekwa katika hoteli waliyotakiwa kufikia.
Njiani, Fareed alikuwa na furaha tele, hakuamini kama kweli alifika Marekani. Aliangalia nje, jinsi jiji hilo lilivyokuwa limejengeka, lilipendeza machoni mwake na kila alipokuwa akiliangalia, alijiona kama yupo katika pepo ndogo.
Hawakuchukua muda mrefu wakafika hotelini. Wakateremka na kuelekea ndani, huko, wakatulia vyumbani na kuagiza chakula ambapo wakaletewa kwani kila kitu kililipiwa na Bilionea Keith.
“Vipi? Mmekwishafika?” aliuliza bilionea huyo.
“Yeah! Ndiyo tumeingia!”
“Nakuja!”
Wala hazikupita dakika nyingi bilionea huyo akafika hotelini humo na moja kwa moja kuelekea katika chumba hicho. Alipofika katika korido ya iliyokuwa na chumba kile akaingia ndani. Macho yake yakatua kwa watu waliokuwa humo ndani, walikuwa wasichana wazuri, aliwapenda lakini mbali na wasichana hao, alipomwangalia Fareed, akashtuka sana, hakuamini kama kulikuwa na msichana mwingine mzuri namna hiyo.
“Ooh! Ni wasichana wazuri! Naona umeniongezea wa tatu kabisa,” alisema Bilionea Keith huku akitoa tabasamu pana.
Asteria hakujibu, akamvutia pembeni na kuanza kuzungumza naye kuhusu Fareed kwamba hakuwa msichana kama alivyohisi bali alikuwa mwanaume tata maneno yaliyomfanya bilionea huyo kushangaa.
Hakuamini kama kulikuwa na mwanaume aliyekuwa mrembo kama Fareed.
Aliwafahamu wanaume tata waliokuwa nchini Marekani, hawakuwa na uzuri mkubwa lakini kwa Fareed alionekana kuwa tofauti, alikuwa na muonekano wa kike na hata maringo yake, jinsi alivyokuwa akiuweka mwili wake, alionekana kama msichana.
“Ni mwanaume?”
“Ndiyo!”
“Unanitania!”
“Siwezi kukutania!”
“Mbona kama mwanamke mrembo?”
“Ndiyo hivyo! Ni mwanaume huyo.”