SEHEMU YA 28
Muda ulizidi kusogea, ilikuwa asubuhi, mchana ukaingia, alasiri nayo ikasogea na kukatika, jioni ikaondoka, ilipofika usiku wa saa 2:03 akasimama dirishani, kwa kule juu, akaona teksi ikiingia na kwa mbali akamuona Fareed akiteremka huku akiwa na mkoba wake alioubeba kama mwanamke.
Godfrey akapandwa na hasira zaidi, akavua suruali yake, akachomoa mkanda, usiku huo, hakutaka kusikia kitu chochote, moyo wake uliwaka kwa hasira, akasimama huku akitetemeka, mkanda mkononi, mara Fareed akaufungua mlango na kuingia ndani ya chumba hicho. Hali aliyomkuta nayo Godfrey ilimshtua, akakiona kifo mbele yake.
*** Fareed alibaki akimwangalia Godfrey, aliogopa, jinsi mwanaume huyo alivyovimba ilionyesha dhahiri kwamba angeweza kumpiga hapo chumbani. Alibaki akitetemeka lakini akajipa moyo kwamba angeweza kufanya lolote liwezekanalo kuupoza moyo wa mwanaume huyo uliokuwa na hasira kali.
“Bebi kuna nini?” aliuliza Fareed kwa sauti ndogo, sauti ya kike ambayo ilipenya moja kwa moja mpaka moyoni mwa Godfrey na kuutetemesha mtima wa moyo wake.
Wakati akiwa ameuliza swali hilo, Fareed alimsogelea Godfrey na kisha kuushika mkono wake, hakuridhika, akauweka mkono wake mwingine katika kifua cha mwanaume huyo.
Hasira zote alizokuwa nazo Godfrey zikaanza kupotea, hakuamini kama kweli Fareed angeweza kuzimaliza hasira kali alizokuwa nazo kirahisi namna hiyo. Moyo wake ukarudi ndani ya penzi zito, kila alipomwangalia akahisi kabisa kuwa na mapenzi mazito na Fareed hivyo kujikuta mkono wake ukilainika na kuudondosha mkanda aliokuwa ameushika.
“Kuna nini my love jamani! Mbona unanitisha?” aliuliza Fareed huku akiuhamishia mkono wake na kuanza kukishikashika kidevu chake.
“Umetoka wapi jamani?” aliuliza Godfrey, alilainika kirahisi sana kiasi kwamba hata yeye mwenyewe hakutegemea.
“Nilikuwa nimekwenda kutembea!”
“Ndiyo mpaka usiku!”
“Naomba unisamehe baba watoto,” alisema Fareed kwa sauti iliyoutetemesha moyo wa Godfrey kupita kawaida.