Mzee Mwanakijiji
Platinum Member
- Mar 10, 2006
- 33,742
- 40,872
Nawasalimu watani, wa mbali na wanyumbani,
Nina swali mawazoni, mnijibu asilani,
Yakikukuta jamani, utafanya jambo gani?
Ukikuta nyoka ndani, utaita seremala?
Wewe umepata nyumba, mtani ukahamia,
Si nyumba hiyo ni jumba, machoni linavutia,
Bustani zimepamba, ndege wazishangilia,
Ukikuta nyoka ndani, utaita injinia?
Ulipoingia ndani, jumba ukafurahia,
Ukamuomba Manani, ulinzi kukujalia,
Jalali wetu Rabbani, kwake ukajiachia,
Ukikuta nyoka ndani, utawaita polisi?
Ndipo ukakaa chini, mke na watoto pia,
Mmetulia sebuleni, na nne mmekunjia,
Kuangalia ukutani, kuna ufa wapitia,
Ukikuta nyoka ndani, utaita daktari?
Kuangalia darini, kumbe dari linavuja!
Jikoni mpaka vyumbani, dalili haiko moja,
Furaha yako mtani, kumbe jumba ni kihoja,
Ukikuta nyoka ndani, utamtafuta nani?
Kuliinua zulia, kumbe sakafu ya vumbi!
Kichwa kinazungukia, kama mlewa ugimbi,
Hamaki imeingia, mpaka mawazo ya dhambi,
Ukikuta nyoka ndani, utawaita wakwezi?
Kabla hujatulia, kelele unasikia,
Mama Chanya Analia, “kuna nyoka kaingia!”
Mbio ukakimbilia, kuokoa familia,
Ukikuta nyoka ndani, utafanya jambo gani?
Pale mlipohamia, nyoka alishahamia,
Mayai kajitagia, tena ni mayai mia,
Hivyo ni vinyoka mia, ni moja mia sikia,
Ukikuta nyoka ndani, utafanya nini kwanza?
Patashika imekua, pumzi inakutoka,
Hao nyoka utaua, au utachekacheka?
Uamuzi waujua, ni jasiri kuushika?
Ukikuta nyoka ndani, utaanza kulaumu?
Utasema ni mfumo, nyoka ameutumia,
Nyoka kaingia humo, mfumo umeachia,
Utaanza toa somo, mfumo kuangalia?
Ukikuta nyoka ndani, utaziba nyufa kwanza?
Utaita seremala, waliangalie paa?
Ati nyoka wamelala, mzima una kichaa?
Utafanya masihala, ulale mzime taa?
Ukikuta nyoka ndani, utaanza piga maombi?
Nyoka muondoe nyoka, kabla kugeuka joka,
Mkirembesha hakika, mtageuka mahoka,
Mazuri unayotaka, mpaka nyoka katoka,
Ukikuta nyoka ndani, utaanza kulaumu?
Beti zangu nazifunga, kusema nimeshasema,
Anayetaka kupinga, apinge hii hekima,
Kama hajui kutunga, mashairi si lazima,
Ukikuta nyoka ndani, wewe utafanya nini?
Na. M. M. Mwanakijiji (Sauti ya Kijiji)
Aprili 11, 2016