Jeshi hili ni la nani, mimi nauliza nini,
La nini tena kwanini, mwenye kujibu ni nani
Nauliza kwa makini, mtanipa jibu gani,
Siri hizi ni za nini, za nani, tena kwanini?
Meremeta ni ya nani, Mkuu tuelezeni,
Twataka mtangazeni, tujue wazi kwanini,
Mnachotuficha nini, mnamuogopa nani,
Siri hizi ni za nini, za nani, tena kwanini?
Mnatuzuga kwanini, kwa majibu yalo duni, (mbadala- "ya kihuni")
"Tusiseme hadharani", mwatung'akia Bungeni,
Hivi nyinyi kina nani, mnatuona wageni,
Siri hizi ni za nini, za nani, tena kwa nini?
Ati wabunge "nyamazeni, serikali ni makini,
Mambo haya ya sirini, hatutawajulisheni,
Mengine yajadilini, Meremeta iacheni,"
Siri hizi ni za nini, za nani, tena kwa nini?
Si kura tuliwapeni, mtuwakilishe Bungeni,
Kimya chenu ni cha nini, mnaburuzwa na nani,
Mbona mwagwaya kwanini, vigugumizi vya nini,
Siri hizi ni za nini, za nani, tena kwa nini?
Mwamunyange ndiye nani, Jeshi lake ndiyo gani,
Sumari yeye ni nani, Jeshi ni la nchi gani,
Walipa kodi ni nani, Jeshi linaitwa nini,
Siri hizi ni za nini, za nani, tena kwa nini?
Walioiba kina nani, wakijificha jeshini,
Ni usalama wa nani, mbona hatuambiani,
Na usalama wa nini, nawauliza semeni,
Siri hizi ni za nini, za nani, tena kwanini?
Nasema nyinyi kubalini, Meremeta ni uhuni,
Uchafu umilikini, na bora jisafisheni,
Mtatuficha mpaka lini, hamtaweza jamani,
Siri hizi ni za nini, zanani, tena kwanini?
Kagoda nayo ninini, Dipu girini magirini,
Mwanchi goldi ya nani, Tanigolidi ya nini,
Haya yote mpaka lini, nauliza kijiweni,
Siri hizi ni za nini, zanani, tena kwa nini?
Mtakula mpaka lini, mtavimbiwa jamani,
Kula huku kula gani, ni njaa namna gani,
Bila kunawa watani, hadi ndotoni kwanini,
Siri hizi ni za nini, za nani, tena kwanini?
Watoto waje kula nini, na mnakomba chunguni,
vidole mwavilambani, njaa haiwaisheni,
Uraiani na jeshini, mwamega na kumegani,
Siri hizi ni za nini, za nani, tena kwanini?
Jembe ninaweka chini, wamenikera mtimani,
Dharau yao ya nini, mipasho nayo ya nini,
Watapeta mpaka lini, atawazuia nani,
Siri hizi ni zanini, za nani, tena kwa nini?
Na. M. M. Mwanakijiji (Sauti ya Kijiji)