Meli ya MV. Mbeya II Yarejesha Safari kwa Kishindo

Stephano Mgendanyi

JF-Expert Member
May 16, 2020
1,661
837

MELI YA MV. MBEYA II YAREJESHA SAFARI KWA KISHINDO

Naibu Waziri wa Uchukuzi Mhe. David Kihenzile amefanya ziara katika Bandari ya Kiwira (zamani Itunge) Wilayani Kyela ambapo ameshuhudia kuanza tena kwa safari za meli ya MV. Mbeya II ambayo ilikuwa imekwama kufanya safari zake kwa miaka kadhaa kutokana na ubovu sasa imeanza kusafirisha abiria na mizigo kati ya Kyela hadi Mbamba-Bay mkoani Ruvuma na maeneo mengine.

Akizungumza bandarini hapo Mhe. Kihenzile amesema Serikali ya awamu ya sita imeamua kurejesha furaha ya wananchi hasa wasafiri waliokuwa wakitegeme usafiri huo kwa kuifufua Meli hiyo ambayo ina uwezo wa kubeba watu wengi pamoja na mizigo hadi tani miambili.

Amesema usafiri huo ni gharama rafiki kwa mwananchi pamoja na kusafirisha mazao na mizigo mbalimbali ikiwemo ya biashara kwa wingi tofauti na kutumia usafiri wa ardhini.

Kihenzile amesema kusudi la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuboresha uendeshaji kwenye Bandari na sekta ya Uchukuzi kwa ujumla ili wananchi wapate tija zaidi.

"Ndugu zangu wa Kajunjumele Kyela na maeneo yote hasa mikoa mitatu (Mbeya, Njombe na Ruvuma) inayonufaika na bandari hii (Kiwira Kyela) Rais wetu Mhe. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuleta mageuzi kwenye bandari na ndio maana tunaboresha bandari zetu kwa kukaribisha wawekezaji, pale Dar es Salaam zaidi ya siku saba meli zinakaa majini hapa Kyela siku hadi nne tano, sisi (Tanzania) uwezo mdogo Teknolojia hamna sasa si bora tukaribishe wawekezaji ili tunufaike zaidi", Mhe. David Kihenzile, Naibu Waziri wa Uchukuzi.

Hata hivyo amezitaka mamlaka husika kuongeza jitihada ikiwemo kufanya marekebisho/matengenezo ya mara kwa mara kwenye meli ili kuendelea kuwasaidia wananchi wanaotegemea usafiri huo.

Amesema Serikali imeamua kufufua usafiri huo ambao utakuwa unafanyika mara moja kwa kila juma kati ya Mbeya na Ruvuma.

Mkuu wa Wilaya ya Kyela amesema kuanza kwa safari za Meli ya Mv. Mbeya II katika Wilaya yake kutachochea uchumi na kurahisisha maisha ya wananchi ambao wamekuwa wakitumia gharama kubwa hasa kwenye usafirishaji mizigo.

Naye Mbunge wa Jimbo la Kyela Ally Jumbe (Kinanasi) ameishukuru Serikali kwa kurejesha usafiri huo ambao anasema ni msaada kwa wananchi wengi hasa wa Jimbo lake.

Kinanasi amewahakikishia wananchi na kuwaondoa hofu juu ya maneno ya baadhi ya watu kuwa bandari imeuzwa au kubinafsishwa akisema ndio maana kwa bandari ya Kyela inasimamiwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania TPA pamoja na watu wa Meli chini ya Wizara ya Uchukuzi.
 

Attachments

 • WhatsApp Video 2023-10-28 at 07.05.48.mp4
  14.3 MB
 • F9cv3YmX0AEweHp.jpg
  F9cv3YmX0AEweHp.jpg
  287.5 KB · Views: 7
 • F9cv3YcXwAAnxi1.jpg
  F9cv3YcXwAAnxi1.jpg
  279.1 KB · Views: 9
 • F9cv3YfXsAAbYY5.jpg
  F9cv3YfXsAAbYY5.jpg
  202.2 KB · Views: 7
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom