Mchakato wa katiba mpya unapaswa kuanzia hatuza za awali.

PSPA Pure'12 udsm

JF-Expert Member
Jan 11, 2013
829
443
Sababu kubwa inayotolewa ya kwanini tunahitaji katiba mpya na si kufanya marekebisho kwenye katiba ya sasa, ni kwamba Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 haikushirikisha wananchi. Kama ni mapungufu yangefanyika marekebisho na kukidhi mahitaji ya sasa kama ambavyo Katiba ya JMT imeshafanyiwa marekebisho mara 14 tangu 1977 hadi 2005 yalipofanyika marekebisho ya mwisho.

Kwa kuzingatia haja hiyo, Rais Kikwete alianzisha mchakato wa kuandika katiba mpya mwaka 2011. Rais aliteua Tume ya Mabadiliko ya Katiba ikiongozwa na Jaji na Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Joseph Sinde Warioba ili kukusanya maoni ya wananchi na kuandaa Rasimu ya katiba mpya ambapo mchakato ulikamilika june 2013 na baadaye bunge la katiba kuundwa na mwisho nao walitoka na katiba pendekezwa octoba 2014. Hapa ndipo kama taifa tulikwamia kuelekea kupata katiba mpya.

Ni mhimu kwanza kuelewa, mchakato huu uliongozwa na sharia kubwa mbili. Mosi ni sheria ya mabadiliko ya katiba ya mwaka 2011 na sheria ya maoni ya mwaka 2013 ambazo kwa ujumla wake zilikoma matumizi yake na hivyo kukosa nguvu na mamlaka ya kisheria kutumika kuendelea na mchakato wa kupata katiba mpya.

Rais Samia Suluhu Hassan ameweka Mchakato wa Katiba Mpya kama kipaumbele kikubwa cha serikali ya awamu ya Sita na ametangaza kuwa Taifa linarejea katika ukamilishaji wa Katiba Mpya kwa kuanza na hatua ya Kamati ya Wataalam watakaopitia na kufanya uhuishaji (harmonization) wa Rasimu ya Katiba iliyotokana na Maoni ya Wananchi yaliyokusanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba pamoja na Katiba Inayopendekezwa iliyotokana na Bunge Maalum la Katiba ili kuandaa Rasimu Jumuishi (Harminised Proposed Constitution) ambayo itapelekwa kwenye kura ya Maoni (referendum).

Licha ya nia njema ya Mheshimiwa Rais ya kupatikana kwa katiba mpya.Na kwa dhati ka bisa naunga mkono. Lakini ni maoni yangu kwamba mchakato ukaanzia hatua za awali yaani kutunga sheria ya kuanzisha mchakato wa katiba mpya, kuunda Tume ya kukusanya maoni, Bunge la katiba mpya na mwisho kura ya maoni. Nitaeleza kwanini.

Mosi, Ni mabadiliko ya kidemografia. Mwaka 2012 nchi ilifanya sensa ya idadi ya watu ambapo Tanzania ilikua na jumla ya watu 44,929,542 kote bara na visiwani. Wakati nchi ikifanya sensa, ni kipindi hicho hicho pia Tume ya Kukusanya maoni ya katiba mpya ya Jaji Warioba ilikua kazini ikiendelea kukusanya kukusanya maoni kwa makundi watu, Taasisi na makundi wakilishi ya kanda mbalimbali. Kwa lugha rahisi tunaweza kusema Rasimu ya Warioba na Rasimu pendekezwa ya Bunge zote kwa ujumla wao ni zao la maoni ya watu takribani milioni 45. Mwaka 2022 kama ulivyo utaratibu wa nchi yetu kufanya sensa kila baada ya miaka10, ilifanyaika sensa ya watu na makazi ambapo matokeo yanaonesha tupo watanzania 61,741, 120. Kuna ongezeko la watu takribani milioni 16. Hatuwezi kupuuza idadi kubwa kama hii kupata maoni yao juu ya Rasilimali za nchi,mifumo ya utawala na mgawanyo wa mamlaka pamoja uchumi wetu kuelekea kupatikana kwa katiba mpya. Ni ukweli usiopingika kwamba mahitaji, matakwa na matarajio yao sio yale yale ya 2012. Hata kama ni yale yale basi yatakuwa ni jumuishi (inclusive). Sasa ikiwa serikali inashindwa kutumia taarifa na takwimu za idadi ya watu za miaka 10 iliyopita ya katika mipango yake ya maendeleo, kwamba hazikidhi mahitaji ya sasa, vipi ituletee katiba mpya ambayo inatokana na maoni ya muongo mmoja uliopita?

Pili, Rasimu zote mbili kutotambua vijana kama kundi maalumu na la kipaumbele. Matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, yanaonesha 70% ya watanzania ni vijana. Sera ya Taifa ya vijana ya mwaka 2007, inamtambua kijana kama ni mtu mwenye umri kuanzia miaka 15-35, wakati Umoja wa mataifa (UN) ikimtambua kijana kama mtu mwenye miaka 13 -24. Hii ina maana kwamba kwa mujibu wa sera ya Kimataifa, ikiwa tutaendelea na mchakato wa katiba mpya pale ulipokwamia kundi la vijana ambalo kimsingi ndio kundi la wengi litakuwa limeachwa nje kabisa ya katiba mpya. Hata kama sera ya Taifa ya vijana itazingatiwa, ni wazi kwamba ni chini ya 16% tu ya kundi la vijana ambao walikua wamefikisha miaka 18, hivyo kuwa na sifa za kushiriki mchakato wa ukusanyaji wa maoni ya katiba mpya 2011.

Wastani wa umri wa Raia wetu ni miaka 18, Bara la Afrika ni miaka 20 na Jumuiya ya Ulaya ni miaka 42. Wazungu wanasema “Number counts”, kwa lugha rahisi tunakubaliana kwamba Taifa letu ni la vijana. Kama nchi tunakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo umasikini, Ukosefu wa Ajira, Uongozi mbaya, mabadiliko ya tabia ya nchi nk.yote haya kwa ujumla wake yanamuangukia kijana moja kwa moja na majawabu yake yatatokana na kijana mwenyewe kwa kujumuishwa kwenye vyombo vya maamuzi kama mabaraza ya vijiji/mitaa, mabaraza ya madiwani, bunge na baraza la mawaziri.

Taasisi ya vijana ya Tanzania Youth Vision Association (TYVA) imebainisha kasoro kadhaa zilizopo kwenye Rasimu zote mbili za katiba mpya zitazomnyima kijana kuzifikia fursa kwenye mgawanyo wa keki ya taifa kwa wote. Kutokuwepo kwa kipengele kinachotaja idadi ya vijana kwenye nafasi za vyombo vya maamzi na uwakilishi toka ngazi ya msingi mpaka kitaifa, nafasi za uteuzi Rais, uwepo wa ibara zinazomzuia kijana kugombea urais na spika wa bunge ni miongoni wa machache.

Pamoja na ukweli kwamba katiba ni mchakato wa kisiasa zaidi ambapo kila kundi lenye maslahi litapoteza baadhi ya maslahi na matakwa yao na kupata kiasi, lakini kwa nchi yetu kundi la vijana haliepukiki. Bila kuanza upya mchakato, matokeo yake hayawezi kuakisi matarajio, matakwa na mahitaji halisi ya vijana ambao ndiyo kundi kubwa katika nchi yetu.
 
Back
Top Bottom