nngu007
JF-Expert Member
- Aug 2, 2010
- 15,862
- 5,797
Tuesday, 03 May 2011 19:21 newsroom
* Wafuasi wake wawapopoa polisi mawe, risasi zarindima
na chibura makorongo, meatu
MBUNGE wa Jimbo la Meatu mkoani Shinyanga, Meshack Oporukwa (CHADEMA), ametiwa mbaroni na kisha kutupwa mahabusu kwa tuhuma za kuvunja sheria. Hata hivyo, vurugu kubwa zilizuka wakati Polisi walipokuwa wakimtia mbaroni mbunge huyo, baada ya watu wanaodaiwa kuwa wafuasi wake kuwazuia wana usalama hao kutekeleza majukumu yao. Kufuatia hali hiyo polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wafuasi hao waliojaribu kukizingira Kituo cha Polisi cha Meatu, wakitaka kuachiwa kwa mbunge huyo na viongozi wawili wa Chadema. Tukio hilo lilitokea jana saa 5.10 asubuhi baada ya Oporukwa na viongozi wawili kutiwa mbaroni akidaiwa kuendesha mkutano wa hadhara kinyume cha taratibu.
Ilielezwa kuwa Oporukwa alifanya mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Nkoma wilayani hapa, lakini alishindwa kufuata taratibu na kuvusha muda uliopangwa kisheria. Polisi walilazimika kumtia mbaroni kwa mahojiano kutokana na kushindwa kufuata sheria na kusababisha adha kwa wananchi wengine wanaoshi maeneo jirani na uwanja wa mkutano. Mkutano huo wa Oporukwa ulikuwa na lengo la kuwashukuru wananchi kwa kumchagua kuongoza jimbo hilo. Habari zaidi zinaeleza kuwa Oporukwa alitiwa mbaroni wakati akitazama mpira wa miguu, ambapo alialikwa kuwa mgeni rasmi.
Polisi walifika uwanjani hapo wakiwa na gari lenye namba za usajili PT 1802, wakiongozwa na Mkuu wa Polisi Wilaya, Julius Mjengi na kuamuru mchezo kusimamishwa kwa muda ili kupata fursa ya kumhoji mbunge huyo. Hata hivyo, baadhi ya wananchi walikataa pendekezo hilo na kutishia kuwashambulia askari kwa silaha za jadi, ikiwemo mapanga na mikuki kupinga kitendo hicho.
Katika kuhakikisha amani inakuwepo Polisi waliondoa amri ya kusimamisha mchezo na kumhoji Oporukwa, ambapo mchezo uliendelea na kufuatiwa na burudani nyingine usiku wa siku hiyo, ikiwemo kuangalia filamu. OCD Mjengi alituma ujumbe kwa askari wake kumtaka Oporukwa kufika katika Kituo cha Polisi Meatu, siku iliyofuata kwa ajili ya mahojiano kufahamu chanzo cha kuvunja sheria.
Saa 9.00 usiku mbunge huyo alifika kituoni hapo, huku akiwa ameongozana na Mwenyekiti wa CHADEMA wilayani hapa, John Kwili na Katibu wake, Gogeveni Malegeza, ambapo aliwahoji kisha kuwaweka chini ya ulinzi baada ya kutakiwa kukutana na Kamanda wa Polisi Mkoa Shinyanga, Diwani Athumani.
Hata hivyo, wakati wakienda kituoni hapo walikuwa na wafuasi wa Chadema, ambao walipinga kitendo hicho na kuanza kuwashambulia askari kwa mawe kabla ya polisi kuamua kujibu mapigo kwa kuwatawanya kwa mabomu ya machozi.
Vurugu hizo zilidumu kwa saa 1.30 hadi ilipofika saa 6.32 mchana, ambapo Polisi walifanikiwa kuwasafirisha watuhumiwa hao kwenda Shinyanga kwa mahojiano zaidi.
Akizungumza na Uhuru kwa njia ya simu jana, Kamanda Athumani alisema tuhuma za Oporukwa zinaendelea kuchunguzwa na ikibainika amekiuka atafikishwa mahakamani.
Kwa sasa ameletwa hapa mkoani kwa mahojiano zaidi, ikibainika amevunja sheria atapanda kizimbani, alisema Kamanda Athuman.