Mawaziri wa Nishati Tanzania na Zambia wajadili ujenzi wa bomba jipya la mafuta

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,812
11,987

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko pamoja na Waziri wa Masuala ya Nishati wa Zambia, Peter Kapala, leo Januari 29, 2024 wamefanya kikao kilicholenga kujadili nia ya Serikali ya Tanzania na Zambia kuanza ujenzi wa bomba la inchi 24 la kusafirisha mafuta safi kutoka Tanzania kwenda Zambia.

Kikao hicho kimefanyika Jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, Makatibu Wakuu wa Wizara za Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, (Tanzania) na Dkt. Chisangano Zyambo (Zambia) pamoja na watendaji mbalimbali kutoka Wizara hizo na Mashirika yanayosimamia Mafuta.

11.jpeg

12.jpeg

1123.jpeg

Dkt. Biteko amesema, majadiliano hayo ya Mawaziri yanatokana na ziara ya Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoifanya nchini Zambia mwezi Oktoba mwaka 2023 ambapo katika mazungumzo yake na Rais wa Zambia, Mhe. Hakainde Hichilema walijadiliana kuhusu kuongeza uwekezaji kwenye Bomba la Mafuta la TAZAMA kwani bomba hilo kwa sasa halikidhi mahitaji kutokana na kuwa na ukubwa wa inchi 12.

“Kulingana na maendeleo makubwa katika nchi zetu mbili, mahitaji ya mafuta yamekuwa makubwa ndio maana inabidi kujenga bomba jingine jipya kubwa ambalo litasafirisha mafuta kutoka Tanzania kwani kuna Bandari, bomba hili litakalojengwa pembeni ya Bomba la Mafuta la TAZAMA litasafirisha mafuta pia kwenda mikoa ya kusini mwa Tanzania na hivyo kupunguza gharama za usafirishaji na kuwapatia wananchi mafuta ya gharama nafuu,” amesema Dkt. Biteko.

Ameeleza kuwa, bomba hilo litakuwa na urefu wa kilometa 1,710 na uwekezaji wa Dola za Marekani Bilioni 2.5 na kusisitiza kuwa, kwa uwekezaji huo kunahitajika umakini kwenye utekelezaji wake na bila kuuchelewesha.

Ameongeza kuwa, bomba litakuwa na matoleo ya Mafuta katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Morogoro, Makambako, Mbeya na Songwe na kupunguza suala la mikoa hiyo kutegemea kupakua mafuta jijini Dar es salaam pekee.

Dkt. Biteko amesema kuwa, Timu ya Wataalam wa majadiliano inaanza kazi leo na hii ikiwa ni msukumo ambao Marais wa nchi zote mbili wamekuwa wakiutoa ili kutekeleza mradi huo.
 
Back
Top Bottom