Mauaji yaliyojaa utata

Thanks

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Hii riwaya kila nikisoma natamani episode isifike mwisho. Thanks anyway Madame
 
NYEMO CHILONGANI
MAUAJI YALIYOJAA UTATA
Sehemu ya Ishirini na Moja.
Moyo wa Bwana Seppy ulikuwa mweupe kabisa, alichokuwa akitaka kukiona ni kuwa peke yake katika penzi la msichana Maria, kuua, kwake hakukuwa na tatizo lolote lile, kitu pekee alichokitaka ni kuwa na furaha kipindi chote.
Alipata taarifa kutoka kwa watu wengine kwamba yule mchezaji wa mpira wa kikapu aliyekuwa akitamba sana kipindi hicho, Paul alikuwa amekufa chumbani katika hoteli moja huko Los Angeles, hakutaka kujali sana kwani yeye ndiye aliyekuwa nyuma ya mpango wake.
Hakutaka kumuuliza Maria kuhusu Paul, alijua kwamba msichana huyo alikuwa na hofu kubwa kwa kuhisi kwamba angejua, akamuacha na uzuri ni kwamba kila taarifa iliyokuwa ikiandikwa, hakutajwa msichana, ilitajwa kwamba kama kawaida Benjamin alikuwa amekwenda chumbani humo na kumuua kijana huyo.
“Hakikisheni huyo msichana anakuwa huru, si mnajua kwamba huyo ni msichana wangu?” alizungumza Bwana Seppy katika simu, alikuwa akizungumza na polisi.
“Ndiyo mkuu!”
“Basi fanyeni hivyo!”
Hela zilikuwa kila kitu, alikuwa miongoni mwa matajiri wakubwa, aliheshimika kila kona, polisi wengi waliokuwa na tamaa ya fedha walikuwa chini yake na ndiyo maana wakati mwingine alikuwa huru kufanya kitu chochote alichotaka kukifanya kwa kuwa alijua hakukuwa na mtu aliyekuwa akimbabaisha hata mara moja.
Polisi walipewa maelekezo juu ya nini cha kufanya na wao walitakiwa kufanya vilevile, harakaharaka wakamuita Maria katika chumba cha mahojiano, wakaanza kuzungumza naye, hawakuchukua muda mrefu wakaamua kumwachia huku wakimwambia kwamba angehitajika kituoni hapo mara kwa mara.
Hilo ndilo alilolitaka Bwana Seppy, akawasiliana na Maria ambaye alimwambia kwamba yupo nyumbani, akamwambia kuwa alitaka kumuona wiki hiyo lakini msichana huyo akasema kwamba hakujisikia vizuri, alihitaji muda wa kupumzika.
“Si utakuja kupumzika huku mpenzi!” alisema Bwana Seppy.
“Hapana mpenzi! Naomba wiki moja ya mapumziko!”
“Sawa. Upo poa lakini?”
“Ndiyo! Najisikia kuchoka tu,” alisema Maria.
Bwana Seppy aliusoma mchezo, alijua fika kwamba msichana huyo alikuwa katika kipindi cha majonzi, alimpenda sana Paul na hakuona kama kungekuwa na mtu ambaye angelivuruga penzi lake, hata mapenzi aliyokuwa nayo juu ya Bwana Seppyy alipungua kwa kiasi kikubwa kwani hata kama fedha, Paul alikuwa nazo japokuwa hazikuwa nyingi kama za Bwana Seppy.
Siku zikaendelea kukatika, wiki ikakatika lakini msichana Maria hakufika nchini Marekani, kila alipopigiwa simu, alisema kwamba alikuwa kwenye kipindi kigumu, matatizo ya kifamilia yalikuwa yakimwandama hivyo asingeweza kabisa kwenda nchini Marekani.
Kwake, hayo yalikuwa majibu makali, yaliyouumiza moyo wake kupita kawaida, hakutaka kuona akishindwa, alichokifanya ni kuondoka Marekani na kuelekea nchini Mexico kwa kuamini kwamba uwepo wake mbele ya msichana huyo ungeweza kubadilisha kila kitu.
“Kisa nini Maria?” aliuliza Bwana Seppy huku akimwangalia msichana huyo usoni.
“Sipo vizuri kiafya,” alisema.
“Najua na ndiyo maana naona umekonda sana. Tafadhali mpenzi, kama kuna tatizo, naomba uniambie.”
“Hakuna tatizo lolote lile.”
“Kweli?”
“Hakika!”
Siku hiyo Bwana Seppy alitumia muda wake wote kuwa chumbani na msichana Maria, hata walipofanya mapenzi, haikuwa kama kipindi cha nyuma, hakupewa ushirikiano kama ilivyokuwa kipindi kingine. Moyoni mwake aliumia lakini hakuwa na jinsi, alimpenda msichana Maria na kama kuzunguka, alizunguka sehemu nyingi, aliwaona wasichana wengi lakini alikiri kwamba hakuwahi kumuona msichana kama Maria kwa jinsi alivyokuwa mzuri.
“Hii yote ni kwa sababu nakupenda Maria?” aliuliza Bwana Seppy ilipofika asubuhi.
“Kivipi?”
“Kwa unavyonifanyia!”
“Kwani nimekufanyaje mpenzi?”
“Sawa. Si umesema una matatizo ya kifamilia, ngoja nikuache uendelee nayo,” alisema Bwana Seppy.
Moyo wake ulikasirika, alimfahamu Maria, hakuwa namna ile, alijua kwamba kulikuwa na kitu kilichokuwa kikimuuma, kitendo cha mwanaume aliyekuwa akimpenda kuuawa, ndicho kilichomfanya kuwa katika hali ile.
Alikasirika kwa kuwa yeye kama yeye alikuwa na nafasi yake lakini pia hakutakiwa kukasirikiwa au kuonyeshewa hali yoyote ya kutokujali kwa sababu yeye ndiye aliyekuwa akimuweka mjini msichana huyo.
Uamuzi wa mwisho kabisa kuupanga ulikuwa ni kuondoka mahali hapo, hakutaka kurudi tena, kama kuumia, aliumia vya kutosha na huo ulikuwa muda wa kuulizwa moyo wake huku akijitahidi kutafuta msichana mzuri ambaye angempenda kama alivyokuwa akimpenda Maria.
****
Hakukuwa na aliyeamini kama Stacie alikuwa amembwaga Angelica katika kinyang’anyiro cha kumtafuta Miss World ambacho kilifanyika nchini Marekani katika jiji la Texas.
Ukumbi mzima ulipiga makofi, watu wengine walibaki midomo wazi, wapo wengine waliocheza kamari na kubashiri kwamba msichana Angelica angeibuka mshindi kutokana na kunyakua taji hilo.
Stacie alikuwa na furaha kubwa moyoni mwake, alipita huku na kule akiwapungia watu mikono, ndoto yake aliyokuwa nayo tangu kipindi cha nyuma hatimaye Mungu aliifanikisha na kuwa kweli.
Machozi ya furaha yalimbubujika, kuna kipindi hakuwa akiamini, alihisi kwamba alikuwa katika moja ya ndoto yenye msisimko ambapo baada ya kipindi fulani angeamka na kujikuta akiwa kutandani kitu ambacho hakikuwa kweli, kila kitu kilichokuwa kikitokea, kilikuwa katika maisha halisi.
Jina lake siku hiyo likapata umaarufu, waandishi wa habari wakampiga sana picha na wengine kuiweka habari yake katika mitandao ya kijamii, jina lake, yaani kwa kipindi cha dakika kadhaa, lilikuwa maarufu mno.
Uzuri wake uliendelea kuwatetemesha wanaume wengi, hawakuwa wakiamini kama kweli duniani kulikuwa na msichana aliyekuwa na sura nzuri kama alivyokuwa Stacie, wanaume wenye fedha wakajipanga, kila mtu alihitaji kuwa na msichana huyo, hawakujua kama angekubaliana nao au la, kitu walichokihitaji ni kuwa naye kimapenzi, yaani hata kama ni kutumia fedha, watumie lakini mwisho wa siku wampate msichana huyo.
Siku hiyo Stacie akapelekwa katika hoteli kubwa ya nyota saba na kukaa huko. Usiku mzima alikuwa na furaha tele, hakuamini kama kweli angefanikiwa kunyakua taji hilo lililokuwa na heshima kubwa duniani katika masuala ya urembo.
Siku iliyofuata akawasiliana na rafiki yake wa kipindi kirefu, Robert Steph ili awe meneja wake kwani mbele yake aliyaona mafanikio makubwa hasa ya kuingia mikataba minono.
Kama alivyohisi ndivyo ilivyotokea, siku hiyihiyo akapigiwa simu na watu wa Jarida kubwa la Forbes ambao walitaka kuonana naye na kuzungumza naye kuhusu masuala ya kibiashara, hilo wala halikuwa tatizo, alichoangalia kwanza ni kupiga pesa tu.
****
Fedha zikaanza kunukia kwa msichana Stacie, hakukuwa na kitu alichokiona mbele yake zaidi ya mafanikio makubwa, alijiona akiwa mtu mkubwa, mwenye fedha na heshima kubwa.
Kitendo cha kunyakua tuzo na kuwa mrembo wa dunia kilimpa uhakika wa kuishi maisha ya kuwa na fedha mpaka anakufa, kupitia uzuri wake, alishinda tuzo hiyo na hivyo kumshukuru Mungu kila siku kwa kile alichokuwa amempa.
Baada ya kusaini mkataba na Jarida la Forbes na kulipwa kiasi cha dola milioni mbili ambazo zilikuwa zaidi ya bilioni nne za Kitanzania, makampuni mengi yakamfuata, hakuwa na hiyana, alichokifanya ni kuendelea kukusanya fedha kama kawaida.
Jina lake halikushuka, liliendelea kuwa juu na kwa sababu tayari alikuwa na jina, aliona kuwa na umuhimu wa kuwa na mbunifu wake wa mavazi. Kulikuwa na watu wengi walioomba nafasi hiyo, kila siku alipokea barua pepe, watu walikuwa wakimuomba nafasi ya kuwa mbunifu wake wa mavazi kiasi kwamba akachanganyikiwa amchukue yupi kwani kila mmoja alionekana kuwa mtaalamu kwa kazi hiyo.
“Kwa hiyo utamchukua nani?” aliuliza Robert.
“Labda huyu Muitaliano, Alejandro Petrescu,” alijibu Stacie.
Alichokifanya ni kuwasiliana na mbunifu huyo wa mavazi na kumtaka kufika nchini Marekani haraka iwezekanavyo, alimtumia tiketi ya ndege, gharama za kukaa hotelini lakini mwisho wa siku walitaka kuona kila kitu kinakuwa kama kinavyotakiwa.
Tangu achukue taji hilo alikwenda nyumbani kwao Australia mara mbili tu, baada ya hapo, maisha yake yakaendelea kuwa nchini Marekani ambapo aliishi kwa kuheshimika kupita kawaida.
Alejandro ndiye aliyemfanya Stacie kupendeza zaidi, kila siku alikuwa mtu wa kumbunia mavazi mbalimbali, na kila alipovaa, alivutia kiasi kwamba wanaume wengi wakazidi kumpenda.
Jina lake lilikuwa kubwa, ni ndani ya miezi sita tu tayari aliingiza kiasi kikubwa cha fedha kwa sababu tu alikuwa mrembo na hata mastaa wa filamu walitamani kuigiza naye kitu kilichowafanya kuwaomba waongozaji wafanye kitu.
“Hakuna tatizo, nitamuita kwenye hii filamu!”
Muongozaji kutoka katika Kampuni ya Filamu ya Marvel alikuwa akizungumza na muigizaji wake mwenye jina kubwa, Tom Hardy ambaye alikuwa akihitaji kuigiza na msichana Stacie.
Hilo wala halikuwa tatizo, kwa sababu wao wenyewe walikuwa wakitafuta fedha, waliamini kuwa kama wangemruhusu msichana huyo ashiriki katika muvi yao hakika wangepata kiasi kikubwa cha fedha, hivyo bila ubishi, wakawasiliana naye na kumuita.
Stacie hakuamini, hakuwahi kufikiria hata mara moja kwamba ingetokea siku angepokea simu kutoka kwa mmoja wa waongozaji katika kampuni hiyo na kumtaka kuigiza filamu, hakukataa, kwa kuwa naye alizitaka hizo fedha na kuwa maarufu zaidi, akakubaliana nao.
Baada ya siku kadhaa, wakaanza kuigiza filamu mpya ya Black Panther. Japokuwa alikuwa muigizaji mchanga lakini alifanya vizuri sana kitu kilichoonyesha kwamba angekuwa muigizaji mkubwa sana hapo baadaye.
Hayo ndiyo yalikuwa mwanzo wa mafanikio makubwa aliyoanza kuyapata. Kila siku akawa mtu wa kuingiza fedha, uzuri wake uliwachanganya watu wengi na hivyo kuanza kumfutailia bila mafanikio makubwa.
Miongoni mwa watu wengi waliokuwa wakimfuatilia alikuwa Bwana Seppy. Mzee huyu alimpigia simu Stacie na kumwambia kwamba alitaka kuonana naye kwa kuwa kulikuwa na mambo mengi ya kuzungumza.
Jina la Bwana Seppy halikuwa geni, alimfahamu mzee huyo, alikuwa miongoni mwa watu wenye fedha ambao waliitetemesha Marekani kipindi hicho. Kwake ilikuwa furaha tele hivyo kupanga mipango ya kuonana.
Siku mbili zilizofuata, walikuwa katika Mgahawa wa SamSam ambapo hapo Bwana Seppy alikuwa na walinzi wake waliokuwa kimya kila wakati.
Bwana Seppy alibaki akimwangalia msichana huyo, alikuwa mrembo sana, tangu aachane na mpenzi wake, Maria miezi kadhaa iliyopita hakupata mtu ambaye angeziba pengo kubwa lililoachwa na msichana Maria.
Alimtafuta msichana wa kuziba pengo hilo ila kwa kipindi chote hicho, hakufanikiwa kabisa. Kila alipomwangalia Stacie, aliona kabisa kwamba msichana huyo alikuwa akielekea katika kuliziba pengo hilo lililomtesa kwa kipindi kirefu.
Kuhusu kutumia fedha, kwake halikuwa na tatizo lolote lile, kitu pekee alichokihitaji kilikuwa ni mapenzi kutoka kwa msichana huyo tu. Macho yake tu yalionyesha kila kitu, mapenzi aliyokuwa nayo moyoni hayakubaki huko bali yalizunguka mpaka machoni mwake.
Alitaka kumwambia ukweli lakini hakujua mahali pa kuanzia, alivuta pumzi huku akiagiza kahawa, kipindi chote hicho msichana Stacie alikuwa akimwangalia tu machoni mwake.
“Nashukuru sana kwa kuitikia wito wangu,” alisema mzee huyo huku akimwangalia msichana huyo.
“Usijali...”
“Nimekuita kwa jambo moja...”
“Lipi hilo? Biashara?”
“Ndiyo! Lakini sidhani kama la biashara linatakiwa kuzungumzwa leo, nadhani leo tunatakiwa kuzungumzia jambo jingine kabisa,” alisema mzee huyo.
“Lipi hilo?”
Bwana Seppy akashusha pumzi ndefu na kuangalia pembeni kama kulikuwa na watu waliokuwa wakiyafuatilia mazungumzo yao, alipoona hakukuwa na mtu aliyekuwa akifanya hivyo, hapo ndipo alipoamua kutumbua jipu.
Hakutaka kuteseka moyoni mwake, ilikuwa ni vigumu mno kuendelea kuumia, kuwa na mawazo na wakati alikuwa na uwezo mkubwa wa kumwambia msichana huyo kila kitu kilichokuwa kikiendelea.
Hakutaka kuficha, kama ni siri, aliamua kuitoa na hivyo kumwambia jinsi alivyokuwa akimpenda. Muda wote msichana Stacie alikuwa kimya, alibaki akimwangalia mzee huyo usoni, uso wa Stacie ulikuwa kwenye tabasamu pana ambalo lilimpa matumaini mzee huyo kwamba angefanikiwa kile alichokuwa akikitaka.
“Umemaliza?” aliuliza Stacie baada ya kumsikiliza mzee huyo kwa dakika tatu.
“Ndiyo!”
“Haitowezekana!” alijibu kwa kifupi.
“Kwa nini tena jamani?”
“Jua kwamba haitowezekana, hakuna sababu, jua tu kwamba haitowezekana,” alisema Stacie na hapohapo kusimama, hakutaka kusubiri, japokuwa mzee huyo alionyesha muonekano uliomtia huruma, hakutaka kujali, akachukua kila kilicho chake na kuondoka zake huku Bwana Seppy akiishia kula kwa macho tu.
Je, nini kitaendelea?
 
Baada ya mauaji ya Stacie, Benjamin atakamatwa, siku za bwana sappy zinahesabika
 
Thanks again

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…