Matumizi sanifu na fasaha ya mofimu "kwa"

Oct 4, 2023
6
12
Nimekuwa nikishuhudia baadhi ya ndugu zetu wa nchi jirani wakitumia mofimu "kwa" katika namna ambayo siyo sahihi kwa mjibu wa Kiswahili sanifu na fasaha. Ninaelewa kuwa kuna utofauti wa kilahaja na matumizi ya Kishengi lakini napenda kukumbusha juu ya matumizi sanifu na fasaha ya mofimu hiyo "kwa". Lengo ni kuendelea kuboresha, kukipamba Kiswahili chetu na kukieneza duniani kote kwani sote tunajenga nyumba moja.

Utasikia sentensi kama hizi:
a) Nimeenda kwa shamba
b) Ameenda kwa nyumba
c) Ninaishi kwa nyumba yangu

Ukichunguza sentensi kama hizo huenda ni Kiswahili fasaha lakini siyo Kiswahili sanifu. Hebu tujikumbushe kidogo matumizi ya mofimu "kwa"

MATUMIZI YA MOFIMU "KWA"

1. Kuonesha umiliki wa mahali


Mama amekwenda kwa mjomba.

Hamisi amelala kwa baba.

Dada amepeleka maji kwa kaka.

2. Kueleza sababu

Amepigwa kwa kuchezea simu

Amehukumiwa kwenda jela miaka mitano kwa ubakaji.

Amekufa kwa kujinyonga.

Kuonesha sehemu ya kitu kizima au uwiano

Amepata tano kwa mia moja.

Yahaya ana jitahidi, amepata saba kwa tisa.

Walihudhuria wazee kwa vijana

4. Kuonesha muda uliotumiwa na tendo fulani

Tulimsubiri kwa saa tisa.

Walishauriana kwa saa saba.

Walikesha kwa siku mbili wakila nyama na kucheza mziki.

5. Kulinganisha

Timu ya taifa ilishinda mbili kwa moja.

Simba ilifungwa tano kwa nne.

Horoya imefungwa tatu kwa sifuri.

6. Kuelezea kifaa kinachotumika

Analima kwa jembe la mkono.

Anavuna karanga kwa koleo.

Msichana anachota maji kwa ndoo.

7. Kueleza jinsi, namna au mbinu

Anna alipata pesa kwa kufanya kazi kwa bidii.

Mwakinyo alikimbia kwa nguvu.

Joti anacheza kwa madaha.

Anatembea kwa maringo.

Haya ni baadhi ya matumizi ya msingi ya mifimu "kwa" .
Kwa hivyo, usahihi wa sentensi zilizooneshwa mwanzo zinapaswa kuwa;
a) Nimeenda kwa shamba - Nimeenda shambani
b) Ameenda kwa nyumba - Ameenda nyumbani
c) Ninaishi kwa nyumba yangu - Ninaishi nyumbani kwangu.

Zacharia Emanuel - Swahili Linguist and Translator
WhatsApp+255755350165.
 
Back
Top Bottom