Matukio ya Ukatili wa Kijinsia yaripotiwa kuongezeka Visiwani Zanzibar

Lady Whistledown

JF-Expert Member
Aug 2, 2021
1,024
1,618
Vitendo vya ukatili wa kijinsia vimeripotiwa kuendelea kuongezeka visiwani hapa ambapo Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali inaonesha matukio hayo yakiongezeka kutoka matukio 1,222 mwaka 2021 hadi matukio 1,360 mwaka 2022, ongezeko ambalo ni la matukio 138.

Takwimu hizi zilitolewa hapo Januari 17, 2023, wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Takwimu House, Mazizini, mjini Unguja. Wadau mbalimbali wa haki za wanawake na watoto walihudhuria mkutano huo.

Takwimu hizo zinaonesha kwamba kwenye matukio 1,361 yaliyotokea mwaka 2022, matukio 1,173 yalijumuisha watoto, 185 yalihusu wanawake na matatu yalihusu wanaume. Kwenye matukio 1,173 ya watoto, 889 walikuwa ni wasichana, huku 284 walikuwa ni wavulana.

Miongoni mwa wanawake 185 waliofanyiwa ukatili na udhalilishaji wa kijinsia, wanawake waliobakwa walikuwa ni 66 na walioingiliwa kinyume na maumbile ni watano.

Kati ya matukio hayo 1,360 ya udhalilishaji yaliyoripotiwa, jumla ya matukio 941 yametokea nyumbani huku matukio 419 yakiripotiwa kutokea sehemu nyengine mbalimbali.

Kati ya matukio 1,360 yaliyoripotiwa ni matukio 534 tu ndiyo yapo kwenye upelelezi wa polisi, huku matukio mawili yakiwa katika Ofisi ya Mwendesha Mashtaka na matukio 421 yakiwa mahakamani.

Matukio mengine 181 yameamuliwa mahakamani, huku matukio 139 yakihusisha washtakiwa kuachiwa, 19 hakukua na mtuhumiwa na 64 hakuna aliyechukuliwa hatua.

Akiongea wakati wa mkutano huo na waandishi wa habari, Mkaguzi wa Jeshi la Polisi Kitengo cha Takwimu Said Ali Said alisema kwa upande wa matukio ya ubakaji jumla ya matukio 651 yalirekodiwa kwa mwaka 2022.

Said alisema udhalilishaji ni suala ambalo linasikitisha akitaka nguvu zaidi ziwekezwe kwenye kuyatokomeza.
“Lazima wazazi tuweke nguvu kwenye kuwalinda watoto wetu, matukio yanatokea mitaani kwetu, tunapaswa tuchukue jitihada kwenye hili na kuhakikisha kwamba matukio haya yanakomeshwa,” alisema Said.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, Wilaya ya Magharibi ‘B’ inaongoza kwa kuwa na matukio mengi ukilinganisha na wilaya nyingine kwa kuwa na matukio 288 ikifuatiwa na wilaya ya Mjini yenye matukio 279. Kwa upande wake, Wilaya ya Micheweni kisiwani Pemba imeripotiwa kuwa na idadi ndogo zaidi ya matukio kuliko wilaya zote ikiwa na matukio 39 tu.

Hata hivyo, wadau wanabainisha kwamba hali hii inatokana na watu wilayani humo kutokuripoti matukio hayo na siyo kwamba matukio ya udhalilishaji hayatokei. Mohammed Khamis ni Afisa Uhusiano kutoka Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA) – Zanzibar aliyeieleza The Chanzo kwenye mahojiano naye kwamba wakazi wa Micheweni ni wagumu kwenye kutoa taarifa za matukio ya udhalilishaji.

“Takwimu za Micheweni ni ndogo kwa sababu wanamaliza masuala ya udhalilishaji kifamilia na pia yanafichwa,” Khamis alisema kwenye mahojiano hayo. “Hivyo, siyo kwamba vitendo hivyo havipo ila muamko wa kutoa taarifa ni mdogo kwa wanajamii.”

Khatibu Sheha, Afisa kutoka Wizara ya Elimu Kitengo cha Mrajisi wa Elimu Zanzibar amesema kutokana na hali hiyo ni vyema Serikali ikaongeza uwepo wa madawati ya kijinsia karibu zaidi kwa wananchi ili kuongeza kasi ya utoaji wa taarifa. “Madawati ya kijinsia mengine yako mbali, wakati mwengine jamii inaona shida kusafiri umbali mrefu kutoa taarifa sehemu husika,” alisema Sheha. “Serikali iliangalie suala hili na waongeze madawati ya jinsia.”

Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Siti Abasi Ali amesema matukio ya ukatili wa kijinsia kwa watoto yanaongezeka kutokana na malezi kuegemea upande mmoja wa mama. “Suala la talaka linasababisha matukio haya kuendelea kuongezeka kwa sababu ya wazazi kutengena na wanawake kubeba majukumu makubwa ya kushughulia familia, watoto na kipato pia,” alisema Siti.

Chanzo: The Chanzo
 
Back
Top Bottom