Wahusika wa mitaala na mitihani ya kidato cha nne na sita,kuanzia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi hadi Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA),wanapaswa kujipongeza. Lengo limetimia. Katika matokeo ya kidato cha sita yaliyotangazwa leo, asilimia zaidi ya 90 ya watahiniwa wamefaulu. Matokeo makubwa sasa!
Daraja la kwanza ingawa limepunguzwa kutoka 3-9 hadi 3-7 limesheheni;daraja la pili lipo la kutosha;daraja la tatu limejaa;la nne lina watu bwerere na sifuri zimepungua mno (si zaidi ya 650). Jipongezeni kwa matokeo haya kwakuwa mmetimiza lengo. Hongereni!
Furahini mkijua kuwa elimu yetu ndiyo inazidi kuvurugika. Kuanzia wanafunzi wenyewe,wazazi/walezi na washika dau wengine hawajui hata kukokotoa madaraja na hata alama. Hawajui kwanini daraja la kwanza limeishia alama 7 na si 9.Hawajui kwanini kuna A-D za General Studies. Hawajui kama kwenye daraja husika kama kumehesabiwa General Studies na BAM au la.Lakini,wanasheherekea matokeo.
Vyuo navyo vitawekwa njia panda. Itabidi uundwe utaratibu mpya wa 'cut-off points' ili kuendana na matokeo haya. Yote haya yanafanyika ili ionekane kuwa elimu yetu inapaa kwa kuwa na ufaulu wa juu: zaidi ya asilimia 90. Lengo kubwa ni kuonyesha umma wa watanzania na dunia kwa ujumla kuwa elimu yetu na watahiniwa wetu sasa ni moto wa kuotea mbali. Safari hii hamtapigiwa kelele wala kuundwa Kamati. Mmefaulisha vyema sasa.
Lakini,mambo ni tofauti. Wahusika mjipongeze huku mkijiuliza kama kweli mko sahihi kuichora elimu ya nchi hii hivi mnavyofanya.....